top of page

Bunge Lisifanye Mzaha Kwenye Mambo ya Msingi


Bunge ni chombo muhimu katika kuwakilisha wananchi, kutunga sheria, na kusimamia serikali. Hivyo basi, linapaswa kuwa sauti ya ukweli, ulinzi wa haki, na dira ya utawala bora. Kwa bahati mbaya Bunge letu linaonekana kuzidi kupoteza muelekeo.


Hivi karibuni, Bunge la Ulaya lilijadili hali ya kisiasa nchini Tanzania likibainisha ukiukwaji wa haki za binadamu, kuteswa kwa wapinzani, na matumizi mabaya ya sheria kama njia ya kuwakandamiza viongozi wa upinzani, akiwemo Tundu Lissu. Hili lilipaswa kuwa fursa kwa Bunge la Tanzania kutathmini ukweli wa mambo na kuchukua hatua kulinda katiba, badala ya kujihami kwa kejeli na kuhamisha mjadala toka ajenda kuu na kusimamia hoja ya ushoga.


Ni kweli kwamba ushoga ni dhambi ya sodoma na kinyume cha maadili ya kiafrika. Hata hivyo badala ya kukiri changamoto na kushughulikia madai ya ukandamizaji wa vyama vya upinzani, utekaji nyara, na kesi onevu ya Tundulisu, wabunge wetu kwa makududi walilihamishia mjadala kwenye hoja ya ushoga, na kulifanya kuwa ajenda kuu ya majibu yao. Jambo hili lilifanywa makusudi ikiwa njia ya kupotosha umma na kufunika hoja nzito za kisiasa zinazohusu demokrasia, uhuru wa maoni, na haki ya kuchagua viongozi bila vitisho. Huu ni uhuni na usaliti kwa wananchi.


Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua haki za binadamu, uhuru wa kisiasa, na uwajibikaji wa serikali kwa wananchi. Bunge linapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha haki hizi zinalindwa bila upendeleo wala itikadi. Kukwepa hoja za msingi kwa kutumia mihemko ya kisiasa ni usaliti kwa wananchi.


Ni wakati sasa kwa Bunge la Tanzania kusimama juu ya misingi ya ukweli na haki. Wabunge wanapaswa kutumia nafasi yao kuhimiza utawala wa sheria, kuheshimu katiba, na kutetea uhuru wa vyama vyote vya siasa. Kupinga ukandamizaji si sawa na kupokea maagizo ya kigeni; ni kutimiza wajibu wa kizalendo kwa mustakabali bora wa taifa.

 
 
 

コメント


bottom of page