top of page

CHANZO CHA WANANCHI KUKOSA HAKI KISHERIA: Mfumo wa Utawala Usio na Uwajibikaji (Systemic Failure)

Updated: May 2


Wiki hii kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu idadi kubwa ya watu wasio na hatia waliotupwa katika magereza mbalimbali nchini. Mahabusu hao pamoja na wafungwa wengi waliohukumiwa kwa kesi za kubambikiza unaifanya Tanzania ionekane mojavya nchi zisizojali kabisa utawala wa sheria, jambo ambalo ni fedheha kubwa kwa watanzania.


Idadi kubwa ya watu waliosikika wakichangia mjadala huu wamelitupia lawama nyingi jeshi la polisi kwa kuamini ndiyo chanzo cha tatizo hili. Baadhi yao wamependekeza jeshi la polisi kupunguziwa kazi ya upelelezi na badala yake iundwe taasisi mpya ya uchunguzi inayojitegemea kama (kama FBI ya Marekani) ili kufanikisha uchunguzi wa kesi za jinai. Wanaopendekeza hilo wanaamini taasisi hiyo ikiundwa na kupewa mamlaka ya kisheria itaweza kufanya kazi kwa ufanisi.


Ingawa pendekezo hili linaonekana la kuvutia, ni vyema kila mtu ajiulize kama kuundwa kwa taasisi mpya ya uchunguzi (TBI) kutatatua tatizo la ukosefu wa haki au kutaongeza matumizi ya pesa za serikali na mlolongo wa ulaji kwa wateule tu? Je taasisi mpya zilizoundwa au kubatizwa hivi karibuni zimetimiza wajibu wake kama wananchi walivyofikiri? Tusipokuwa na jibu sahihi kwa swali hili tunaweza kujikuta tukibadilisha jina la chombo au idara lakini utendaji wake ukabaki vilevile kama ilivyotokea kwa TUME HURU YA UCHAGUZI.


Tatizo ni Mfumo, Siyo Tu Taasisi


Kimsingi, tatizo la dhuluma ya haki nchini Tanzania si la mtu mmoja, taasisi moja, au tukio moja. Ni matokeo ya mfumo mbovu wa utoaji haki usio na uwajibikaji, usioheshimu mgawanyo wa madaraka, na unaowaruhusu wachache kutumia sheria kama silaha ya kulinda maslahi yao binafsi. Mfumo huu una kasoro zifuatazo:


  1. Ukosefu wa uwajibikaji katika taasisi za haki – Polisi wanaweza kumweka raia ndani kwa siku nyingi bila kufikishwa mahakamani. Mahakimu wanaahirisha kesi bila sababu, na hakuna anayewawajibisha.

  2. Mwingiliano usiofaa kati ya mihimili ya dola – Mahakama, badala ya kuwa huru, mara kadhaa huonekana kufuata maelekezo ya kisiasa. Uteuzi wa majaji unaingiliwa na utashi wa chama tawala.

  3. Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) yenye mamlaka yasiyo na ukomo – DPP anaweza kufuta kesi yoyote bila kutoa sababu ya wazi kwa umma, jambo linalotumika vibaya kuficha ukweli na kuwalinda wahusika wenye nguvu.

  4. Upungufu wa rasilimali na wataalamu – Mahakama hazina majaji wa kutosha, polisi hawana vifaa vya kisasa vya upelelezi, na magereza yamejaa watu ambao hawajahukumiwa.

  5. Kutosikilizwa kwa Idara ya Usalama wa Taifa. Idara hii imekuwa ikiionya serikali na kuishauri kutatua kelo za wananchi katika ngazi zote. Idara imekuwa kiifahamisha serikali uvunjifu wa sheria na ukiukwaji wa haki katika mahakama na magereza . Hata hivyo serikalinimekuwa ikiziba masikio.

  6. Utamaduni wa ukimya na woga miongoni mwa wananchi – Wananchi wanaogopa kulalamika kwa hofu ya visasi au kwa kutokuamini taasisi zilizopo.


Ukiangalia kwa kina mlolongo wa mauzauza haya bila shaka utajua hata taasisi mpya ya uchunguzi ikiundwa hakuna haki itakayotendeka. Kama wakuu wa Wilaya, wakuu wa Mikoa, Mawaziri na au Rais wataendelea kuwa na uwezo au hulka ya kuingilia mihimili mingine au kutoa maagizo kwa majaji na mahakimu suala la haki litaendelea kuwa ndoto kwa watanzania.


Ili kurekebisha hali hii, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anahitaji kuchukua hatua za kina na za kimfumo. Mchakato wa mabadiliko yoyote unahitaji moyo mweupe unaojali maslahi ya nchi badala ya vipaumbele vya walioko madarakani. Ni muhimu sana mheshimiwa Rais aongoze mabadiliko haya kwa lengo la kuliponya Taifa bila kujali maskahi yake binafsi au ya chama tawala. Hii ni kumbukumbu njema atakayojiwekea kwa vizazi vyote.


  1. Kuundwa kwa Tume ya Kitaifa ya Mageuzi ya Haki.


Iundwe tume huru itakayochunguza kwa kina mfumo wa haki—kuanzia upelelezi, uendeshaji wa mashtaka, hadi mahakama—na kupendekeza mabadiliko ya kisheria na kitaasisi. Tume hii isiwe ya watu wa serikalini pekee, bali ijumuishe wanasheria huru, wanaharakati wa haki za binadamu, na viongozi wa dini.


Pamoja na hili iundwe tume nyingine ya kuchunguza malalamiko ya mahabusu na wafungwa walioko nagerezani kwa kuonewa. Wako watu wengi waliofungwa kifungo cha maisha au miaka zaidi ya ishirini kwa kesi za kubambikizwa au kwa kulinda maslahi ya watu fulani . Ni muhimu mheshimiwa Rais achukue hatua hii bila kujali nani aliyefanya makosa.


Wakati wa utawala wake Rais Jakaya Kikwete aliunda tume huru iliyofanya uchunguzi wa dhuluma na mauaji yaliyofanywa na Polisi (Wakiongozwa na Zombe) dhidi ya wafanya biashara wa Kilombelo. Tume hii ilifanya kazi vizuri na kutoa taarifa ya haki iliyofanya askari wasiokuwa na nidhamu washighulikiwe kwa mujibu wa sheria. Mfano huu unaonesha umuhimu wa Rais kutenda haki bila kujali dhuluma imefanywa na nani.


  1. Kuunda Idara Huru ya Upelelezi


Ni vyema iundwe taasisi huru ya uchunguzi inayojitegemea (Tanzania Criminal Investigations Services - TCIS) itakayofanya uchunguzi kwa uhuru, kitaalamu na kisasa, bila kushinikizwa na wanasiasa au viongozi wa serikali. Taasisi hii iwe na uwajibikaji kwa Bunge, si kwa wizara au rais moja kwa moja. Zingatia kwamba Rais tayari ana chombo kinachowajibika kwake ambacho ni Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).


  1. Kubadili Sheria Inayompa DPP Mamlaka Yasiyodhibitiwa


Sheria ya DPP ifanyiwe marekebisho ili kuhakikisha kwamba maamuzi ya kufuta kesi au kuendelea nayo yanapaswa kuidhinishwa na chombo huru cha uangalizi. Hivi sasa DPP ana mamlaka makubwa mno, anayoweza kuyatumia vibaya kama tulivyoona wakati wa Rais John Pombe Magufuli.


  1. Kuundwa Katiba Mpya ili Kuhakikisha Uhuru wa Mahakama


Katiba iliyopo sasa inatoa mwanya kwa Rais kuwaburuza majaji kwani yeye ndiye mwenye uwezo wa kuwaweka na kuwaondoa madarakani apendavyo. Ni muhimu katiba mpya au itakayofanyiwa marekebisho itamke uteuzi wa majaji na mahakimu upitie mchakato wa wazi unaoshirikisha Bunge na Tume Huru ya Mahakama. Pia, mhimili wa mahakama upewe bajeti inayojitegemea ili kuondoa utegemezi wa serikali kuu.


  1. Kuweka Muda wa Kisheria wa Kesi Kusikilizwa


Sheria iweke kikomo cha muda kwa mahabusu kusubiri kesi. Kwa mfano, kesi za jinai zisizokuwa za mauaji zisikilizwe ndani ya miezi 6, vinginevyo mshtakiwa aachiwe kwa dhamana au afutiwe kesi na kukamatwa upya uchunguzi utakapokuwa umekamilika.


  1. Wananchi Wafanye Nini?


Mabadiliko makubwa kama haya hayawezi kuja kwa hisani ya watawala tu. Wananchi wana jukumu la kihistoria kuhakikisha haki inapatikana kwa wote:


  • Kujifunza na kufundisha haki za kikatiba – Elimu ya uraia ihamasishwe kupitia shule, makanisa, misikiti na vyombo vya habari.

  • Kushiriki katika mijadala ya umma – Wananchi wazungumze kwa ujasiri kuhusu matatizo ya haki, waandike barua kwa wabunge, na kushiriki katika majukwaa ya kiraia.

  • Kuishinikiza serikali kupitia vyombo vya habari na asasi za kiraia – Wananchi waunge mkono kampeni za mabadiliko ya sheria, waandamane kwa amani pale inapobidi, na kutumia nguvu ya kura kuwawajibisha viongozi wazembe.

  • Kuunda mashirika ya kiraia yenye lengo la kufuatilia utoaji wa haki – Vuguvugu la kijamii linaweza kuwa chombo muhimu cha kuhamasisha uwajibikaji.


Haki isipotendeka kwa mtu mmoja leo, hakuna atakayekuwa salama kesho. Tanzania haiwezi kujenga taifa la haki, usawa, na maendeleo ikiwa mfumo wake wa haki ni chombo cha ukandamizaji badala ya kuwa kinga ya wanyonge. Rais anayo nafasi ya kihistoria kusimamia mageuzi ya kimuundo yatakayojenga imani mpya kwa wananchi. Lakini bila shinikizo la wananchi, historia imetufundisha kwamba hakuna kiongozi anayejirekebisha mwenyewe kwa hiari.


Rev. Godwin Chilewa.

 
 
 

Comments


bottom of page