Hapana! Tusikubali Iddi Amin Dada Kuwa ‘Role Model’ Wetu.
- Rev. Godwin Chilewa
- Dec 1, 2024
- 4 min read

Wakati wa utawala wa Iddi Amin (1971–1979), Uganda ilishuhudia mateso na ukandamizaji mkubwa. Iddi Amin aliwachukia wanasiasa, wataalam, viongozi wa dini, na hata raia wa kawaida walioonesha dalili za kutokubaliana naye. Makumi elfu ya watu walitekwa, kuteswa, na kuuawa kwa njia za kikatili. Inasadikiwa katika utawala wake waganda zaidi ya nusu milioni waliuawa. Hali kama hiyo pia ilitokea Afrika ya Kati chini ya utawala wa Jean-Bédel Bokassa na Equatorial Guinea wakati wa Francisco Macías Nguema. Madikteta hawa , wote walitawala kwa mkono wa chuma, wakitumia hofu na unyanyasaji kudhibiti wananchi na kuhakikisha wanadumisha madaraka yao.
Tanzania ya wakati huo ilikuwa tofauti sana. Amani na utulivu ulitamalaki kila mahali. Rais wetu mwalimu Nyerere (Mungu amrehemu) alichukia unyonyaji, ubaguzi wa aina zote, na zaidi sana ukiukaji wa haki za binadamu. Hiki ndicho kilichofanya aongoze mapambano ya kuwaondoa makaburu wa Afrika ya kusini, na kukataa kuhudhuria mkutano wa OAU wakati Iddi Amin alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa mkutano huo. Nyerere alisema hakuwa tayari kukaa meza moja na muuaji.
Ndiyo maana leo hii najiuliza, nani anayetaka kumfanya Iddi Amin kuwa ‘Role Model’ wetu? Yaani Iddi Amin ndiye mfano wa kuigwa kwa uongozi uliotukuka!? Iddi Amin Dada huyu aliyeua waganda laki tano ndiye awe mfano wa kuigwa kwetu!? Hapana kabisa. Tutafute ‘role model’ mwingine, sio huyu. Iddi Amin hafai kuigwa, hana la maana la kutufundisha. Kiongozi muuaji hafai kuigwa hata kidogo.
Napinga kiongozi yeyote wa Tanzania au Afrika kufuata nyayo za Iddi Amin. Naam, alianza kwa kuua mtu mmoja tu, akaongeza wakawa wawili, baada ya muda wakafika laki tano. Waswahili husema safari ndefu huanza na hatua moja. Na ndivyo ilivyo, hata mauaji ya kimbali huanza na roho ya mtu mmoja. Nyerere aliwahi kusema mtu akishaonja (kula) nyama ya mtu hawezi kuacha. Ndiyo, shetani anajua kuwaenzi watu wake, na kuwapa bidii ya kazi.
Tanzania tulikuwa tumetulia. Majeshi yetu yamekuwa yakienziwa miaka na mikaka kwa nidhamu bora, utii na ushirikiano na wananchi. Majeshi yetu hayakuwahi kufananishwa hata kidogo na majeshi ya tuliyemuita mwendawazimu, nduli Iddi Amin Dada. Lakini sasa nasi tunaelekea pabaya. Vitendo tulivyokuwa tukivisikia kwa Iddi Amin vinaanza kuzoeleka nchini kwetu. Watu wanatekwa, wanateswa, wanauawa na hakuna anayekamatwa. Alipopotea Azori Gwanda ilikuwa kama mzaha, akapigwa risasi Tundu Lisu watu wakaanza kujiuliza kulikoni. Mpaka hapo tulidhani hilo ni jinamizi tu, litapita.
Ajabu hali inazidi kuwa mbaya. Sasa wahanga wamekuwa wengi mpaka kuwataja kwa majina inakuwa ngumu. Tena acha waliopotea, wapo kina Tundu Lisu, Roma Mkatoliki, Sativa na Mdude Nyangali walionusulika kuuawa na wakawataja wahusika waliowateka na kuwatesa vibaya, lakini hakuna aliyekamatwa au kushitakiwa kwa utekaji huo. Mzee Ali Kibao alitekwa hadharani, na watu waliojitambulisha kuwa polisi na baadae mzee huyo akakutwa ameuawa. Pia hakuna aliyekamatwa. Wananchi wamekuwa wakiituhumu serikali kuhusika na utekaji. Nayo serikali imekuwa ikikanusha na kusisitiza kuwa hizo ni propaganda tu. Tatizo ni kuwa hata Iddi Amin, naye alikuwa akitumia lugha hiyo hiyo kukanusha mauaji aliyoyafanya.
Kwa ujumla vitendo hivi vya kikatili vina athari kubwa kwa jamii:
1. Kudhoofisha Demokrasia:
Utekaji na unyanyasaji wa wanasiasa wa upinzani huvuruga mifumo ya kidemokrasia. Wananchi hupoteza imani kwa vyombo vya dola, hali inayofanya uchaguzi kuwa wa kinafiki na serikali kuendelea kuwa na uhalali wa kutiliwa shaka. Wananchi wanaweza kujenga chuki kwa viongozi na mfumo wa utawala.
2. Kuchochea Hofu na Ukosefu wa Usalama:
Hofu inayosababishwa na vitendo hivi haibaki kwa wanasiasa pekee bali huenea kwa umma mzima. Raia wanapojua kwamba haki zao hazitalindwa, wanakuwa waoga wa kushiriki mijadala ya kisiasa au hata kutoa maoni ya wazi kuhusu masuala ya kitaifa. Hali hii hupunguza uzalendo wa wananchi na kuwafanya waweze kutumiwa na maadui wa ndani na nje.
3. Kuzuia Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi:
Utawala wa kiimla unaozuia uhuru wa kisiasa huchochea migogoro ya ndani, uhamaji wa wataalamu (brain drain), na kuzuia uwekezaji wa ndani na wa nje. Matokeo yake ni kuzorota kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Wawekezaji wakubwa huona shaka kuhamishia mitaji yao kwenye nchi yenye migogoro. Amani ni dhahabu.
4. Kupoteza Uhai na Maadili ya Kibinadamu:
Utekaji, mateso, na mauaji yanaondoa maisha ya watu wenye mchango muhimu katika jamii, kama viongozi wa upinzani, wanaharakati wa kijamii, na waandishi wa habari. Vifo vyao ni pigo kwa maendeleo ya kitaifa na kizazi kijacho. Sambamba na hilo utekaji na mateso huwafanya watu kuwa sugu na kujenga roho ya kisasi. Hili ndilo linalofanya viongozi madikteta kuendelea kuua watu wengi zaidi na zaidi. Kadri unavyomwaga damu ndivyo unavyoongeza upinzani, na kulazimika kumwaga damu zaidi.
Ni muhimu sana kila mmoja wetu akumbuke kuwa haki za binadamu ni msingi wa jamii yenye amani na maendeleo. Ni wajibu wa serikali yetu kuimarisha demokrasia, kuheshimu haki za raia, na kuhakikisha uwajibikaji kwa matendo yoyote ya ukiukwaji wa haki. Vyombo vya sheria vinapaswa kufanya kazi bila upendeleo, na vyombo vya usalama vinafaa kuwa walinzi wa raia, si mawakala wa hofu.
Zaidi ya hayo, jumuiya za kimataifa zinapaswa kuongeza shinikizo kwa serikali zinazokiuka haki za binadamu. Jumuiya za kikanda kama Umoja wa Afrika (AU) zina jukumu la kuanzisha miongozo madhubuti dhidi ya viongozi wenye mwelekeo wa kidikteta.
Hitimisho
Utekaji nyara na unyanyasaji wa wanasiasa ni dosari kubwa kwa mustakabali wa Afrika. Kufumbia macho vitendo hivi ni kuendeleza hali ya hofu na ukandamizaji ambayo imesababisha mateso kwa mamilioni ya watu. Ni wakati wa Afrika kuachana na historia hii ya giza kwa kukuza utawala bora, kuheshimu haki za binadamu, na kuimarisha mifumo ya haki ili kuhakikisha kuwa sauti zote zinaheshimiwa, na maisha ya kila mmoja yanalindwa. Tusikubali kumfanya nduli Iddi Amin kuwa role model wetu.
Comments