top of page

Onyo kwa Bunge la JMT


Mauaji ya halaiki ya Rwanda hayakuanza kwa mapanga. Yalianza kwa kauli—mzaha wa kisiasa, dharau kwa wapingaji, na lugha ya kibaguzi. Pale walipoanza kuwaita wenzao “mende,” walikuwa wakipanda mbegu ya chuki ambayo ilizaa maafa makubwa. Waswahili husema “Atakaye kumuua mbwa wake huanza kwa kumpa jina baya”


Leo hii, ndani ya Bunge la Tanzania, tunashuhudia wabunge wanaothubutu kuikosoa serikali wakibaguliwa, kudhalilishwa, na kutengwa huku wananchi waliowapigia kura wabunge walioko enzini wakiitwa “kenge.” Hii si siasa ya afya—ni ishara ya kuanguka kwa demokrasia na uchanga wa kisiasa. Bunge letu badala ya kukua na kukomaa linarudi nyuma kwa kasi, kiutendaji.


Bunge halikuundwa kumtetea Rais, liliundwa kuisimamia serikali. Tena Bunge halikuundwa kulinda maslahi au wadhifa wa mtu au kikundi cha watu, limeundwa kulinda maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla. Kumbe ni haki na wajibu wa Bunge kumshauri Rais kwa ukweli na uwazi.

Ukakasi wa Bunge katika kuishauri serikali kwa haki na kukemea maovu ndiko kulikomsukuma mhe. Askofu Josephat Gwajima kuchukua hatua ya kukemea hadharani vitendo vya utekaji nyara vinavyoendelea nchini. Gwajima amezungumza kama raia wa kawaida ili kufikisha ujumbe; Yamkini mhe. Gwajima amelazimika kufanya hivyo baada ya spika wa Bunge kuzima hoja za baadhi ya wabunge waliohoji kuhusu utekaji nyara unaoendelea. Kwa bahati mbaya hoja hiyo sasa inaonekana kama uhaini.


Mbaya zaidi ni unyanyasaji alioanza kufanyiwa kiongozi huyu aliyechaguliwa na wananchi na mwenye dhamana ya kuliongoza kanisa lenye maelfu ya waumini. Licha ya vitisho vya maneno toka kwa viongozi mbalimbali wa kitaifa, serikali imefikia hatua ya kufunga kanisa ambalo ni taasisi inayojitegemea ili tu kumkomoa kiongozi huyo. Serikali imefanya hivyo bila kujali mustakabali wa maaskofu wengine, wachungaji, na maelfu ya waumini wa kanisa hilo jambo linaloweza kutafsiliwa (vibaya) kama ubaguzi wa kidini.


Ni muhimu Bunge lijitambue. Ni muhimu wabunge wanaojielewa watoe tamko la kuitahadhalisha serikali kuhusu athari za yanayoendelea. Ulianza ubaguzi kwa wapinzani, ukajengwa kiasi cha kumfanya kila mwanachama wa chama cha upinzani kuwa adui. Sasa tunakoelekea kila mkweli, atakayeihoji serikali kwa wema au kutoa ushauri wenye maslahi ya taifa pia ataonekana mchochezi. Yamkini huku ni kujenga taifa la watu wanafiki na wasioitakia mema nchi yao.

Nitoe wito kwa wabunge, na viongozi wote wa vyama vya siasa kuamka kabla ya kwenda kuomba kura. Unafiki na kujipendekeza kunakoendelea hakulisaidii taifa wala kumsaidia rais. Uungwana ni kuishauri serikali kwa ukweli na uwazi kwa manufaa ya taifa. Uungwana ni kumshauri na kumuonesha njia sahihi mheshimiwa rais pasipo hofu ya kudondosha tonge.


Wahenga husema ukiikalia kimya dhuluma leo, usilalamike kesho itakapobisha hodi nyumbani kwako. Mauaji ya kimbali nchini Rwanda yangeweza kuzuilika kama ukweli, busara ya watawala, hekima na hofu ya Mungu ingetumika mapema.


Historia huwaandama waliokaa kimya. Usihesabiwe miongoni mwao.


Rev. Godwin Chilewa

 
 
 

Comments


bottom of page