Rais Samia Suluhu Hassan Anakwenda Tunakotaka Kwenda?
- Rev. Godwin Chilewa
- 5 days ago
- 3 min read

Katika siasa za kimataifa, maamuzi ya kiongozi hayapimwi kwa nia bali kwa athari zake. Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imezua mjadala mpana kuhusu mwelekeo wa sera ya nje ya Tanzania. Hii ni katika wakati ambapo mataifa mengi ya Magharibi ikiwa pamoja na Marekani, nchi za Umoja wa Ulaya, na Canada yamechukua msimamo mkali dhidi ya Urusi kufuatia vita vya Ukraine.
Swali la msingi linabaki: je, Tanzania inaelekea wapi kisiasa na kiuchumi? Je, kujenga ukaribu na Urusi katika mazingira haya ni uamuzi wa kimkakati au ni hatari inayoweza kugharimu taifa kidiplomasia na kiuchumi?
Kwa miaka mingi, Tanzania imekuwa ikinufaika kwa kiasi kikubwa na misaada, uwekezaji, na ushirikiano wa kiuchumi kutoka nchi za Magharibi. Hatua ya kuonekana kupunguza ukaribu huo huku ikiimarisha mahusiano na Urusi inaweza kutafsiriwa kama mabadiliko makubwa ya sera ya nje lakini bila maelezo ya wazi kwa wananchi.
Zaidi ya hapo, hali hii inaibua maswali mazito kuhusu washauri wa Rais katika diplomasia. Je, wanadiplomasia wanaomzunguka wana dira sahihi ya kulinda maslahi ya taifa, au wanamsukuma katika mwelekeo usio na uwiano? Na je, Waziri wa Mambo ya Nje Mahmoud Thabit Kombo ana weledi na uzoefu wa kutosha kusimamia nyakati hizi nyeti za mahusiano ya kimataifa?
Katika dunia ya leo, diplomasia si mchezo wa majaribio. Makosa madogo yanaweza kuwa na athari kubwa kuanzia kupungua kwa misaada hadi kuporomoka kwa uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni. Tanzania haiwezi kumudu gharama ya kufanya maamuzi ya nje bila mizani sahihi.
Si hivyo tu, ndani ya nchi, hali si shwari. Baada ya matukio ya Oktoba 29, 2025, matarajio ya wananchi yalikuwa kuona uongozi unaojirekebisha na kusimamia misingi ya haki na uwajibikaji. Badala yake, matukio ya hivi karibuni yanaonyesha picha tofauti.
Mpaka sasa bado watu waliotekwa nyara au kupotea ikiwa pamoja na Mhe. Balozi Polepole hawajapatikana hali inayofanya wengi waendelee kuwa na hofu. Hilo linaenda sambamba na kuendelea kuwekwa mahabusu kwa mwenyekiti wa CHADEMA mheshimiwa Tundu Lisu anayeshitakiwa kwa makosa ya uhaini, kesi inayoiumbua Tanzania kimataifa.
Kauli ya Waziri Paulo Makonda kwamba “mtu anayekemea rushwa hajakaa jikoni” ilizua mjadala mkubwa. Katika taifa linalopambana na rushwa kama adui wa maendeleo, kauli hiyo ilihitaji msimamo mkali wa Rais. Ukimya wake umeacha maswali mengi kuliko majibu. Je, kauli ya waziri huyo inaakisi maono ya Rais, au mheshimiwa Rais anasita kumchukulia hatua waziri wake?
Kadhalika, mbunge kutoka Zanzibar Mhe. Simai Mohammed Said alipotoa kauli tata Bungeni na kumuita (kwa mafumbo) Makamu wa Rais “Yuda msaliti,” hakuna hatua zozote za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi yake. Hili limeibua wasiwasi juu ya kudorora kwa nidhamu ya kisiasa na heshima kwa taasisi za dola.
Huko Zanzibar, nako kauli za kibaguzi dhidi ya Watanganyika zimepamba moto. Hoja za kuwanyima ajira na huduma Watanganyika kwa kisingizio chochote kile zinaashiria hatari kwa Muungano. Kukosekana kwa ukemeaji kutoka kwa kiongozi mkuu wa nchi kunazidisha tafsiri kwamba kauli hizi zinavumiliwa au zinaasisiwa na kiongozi mwenyewe.
Kwa mtu asiye na taarifa za kina angeweza kuhisi kwamba Rais Samia Suluhu hana tabia au kawaida ya kuwawajibisha wasaidizi wake kwa sababu ya matamshi ya kisiasa. Hata hivyo, dhana hiyo inapingwa na tukio lililotokea miezi michache iliyopita ambapo aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. George Simbachawene aliondolewa madarakani baada ya kutoa kauli ya kupinga matumizi ya nguvu kupita kiasi na unyanyasaji wa jeshi la polisi dhidi ya raia.
Ingawa kauli hiyo ilikuwa ya haki na ilielekea kumsafisha Rais, ilimghalimu Simbachawene uwaziri wakati viongozi wengine wanaotoa kauli tata wanaendelea kubaki madarakani bila hatua zinazoonekana. Hii inajenga taswira ya uongozi usio na usawa katika maamuzi, na kuibua hofu kwamba ukosoaji wa kujenga unadhibitiwa badala ya kuhimizwa, na au wako wenye kibali cha kusema watakalo.
Mkusanyiko wa matukio haya yote, ya ndani na nje ya nchi una athari kubwa kwa taswira ya Rais. Ukimya wake katika nyakati nyeti unatafsiriwa kama udhaifu, na maamuzi ya kimataifa yasiyoeleweka huonekana kama kukosa dira. Matokeo yake ni pamoja na Kuendelea kudorola kwa imani ya wananchi, kuongezeka kwa mgawanyiko wa kisiasa, kudhofika kwa vita dhidi ya rushwa na hatari ya kupungua kwa ushirikiano wa kimataifa
Ili kurejesha imani na heshima, Rais anapaswa kutoa mwelekeo wazi wa sera ya nje na kueleza wananchi sababu za maamuzi ya kidiplomasia. Kauli kwamba nchi yetu “haifungamani na upande wowote” ilikuwa na nguvu nyakati za vita baridi lakini si ya kuiendekeza katika vita vya kiuchumi. Ni lazima kutanguliza naslahi ya kiuchumi mbele.
Ni vyema pia kusimamia nidhamu kwa viongozi wote bila upendeleo. Kukemea vikali na kwa wazi kauli za kibaguzi na kulinda Muungano. Kuimarisha vita dhidi ya rushwa kwa vitendo, si kauli. Kuhakikisha uwiano kati ya mahusiano ya Mashariki na Magharibi.
Ni dhahiri kwamba uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan uko katika njia panda. Maamuzi ya sasa yataamua si tu mustakabali wake wa kisiasa bali pia mwelekeo wa taifa. Historia haitahukumu kwa nia njema bali kwa matokeo halisi. Swali linabaki: je, hatua zitachukuliwa kabla ya gharama kuwa kubwa zaidi?
Rev. Godwin Chilewa






Comments