Serikali Inashindwa Kubuni Vyanzo Vipya vya Mapato?
- Rev. Godwin Chilewa
- Nov 1, 2024
- 6 min read

Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikitegemea kwa kiasi kikubwa kodi na tozo kama vyanzo vikuu vya mapato ya serikali. Ingawa kuna haja ya serikali kukusanya kodi na ushuru ili kugharamia huduma za umma, mfumo wa sasa wa kodi na tozo unawalemea wananchi wa kawaida na sekta binafsi. Kwa ujumla mfumo wa uchumi unaotegemea kodi na tozo , badala ya kujikita kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma zinazoweza kuuzwa nje ya nchi kunazuia uchumi kukua kwa kasi inayohitajika, na kuifanya serikali kuwa ombaomba.
Nifafanue hapa kwa kusema kwamba hakuna serikali yoyote duniani isiyotoza kodi. Hata hivyo utozaji wa kodi unapaswa kwenda sambamba na pato la wananchi. Kodi na tozo zinapokuwa nyingi na kubwa kuliko uwezo hugeuka kuwa mzigo mkubwa kwa wananchi wa kawaida. Na hili ndilo tatizo linaloikabili Tanzania. Kila huduma sasa imegeuzwa kuwa pato la serikali kiasi kwamba wananchi wanashindwa kujua kodi na tozo wanazolipa zinagharimia huduma gani ukizingatia kuwa miradi yote mikubwa ya ujenzi wa miundombinu inajengwa kwa mikopo au fedha za wafadhili.
Kimsingi kodi na tozo zinakuwa na maana zinapofanya kazi ya kuboresha maisha ya wananchi. Lakini zinapokuwa nyingi au kuvwa kupita kiasi zinaleta matokeo hasi kwa wananchi. Kodi zisizo na uwiano na pato la wajasiliamali zimefanya biashara nyingi kufungwa au kukosa uwezo wa kupanuka. Matokeo yake, wananchi wanashindwa kuzalisha zaidi, na hali ya kiuchumi inabaki kuwa duni. Ndiyo maana nchi zilizoendelea huwarudishia wananchi na makampuni ya biashara sehemu ya kodi waliyotoa katika kipindi (mwaka) ili kuongeza mzunguko wa fedha na kuwapa nafuu wananchi. Tax cuts hutumika kama kichocheo cha uchumi.
2. Udhaifu wa Kuzalisha na Kuuza Nje
Tanzania inayo maliasili nyingi—ardhi yenye rutuba, madini, misitu, na mbuga za wanyama—lakini bado haijafanikiwa kuzalisha bidhaa na huduma za kutosha kuuza nje. Kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi bado kinategemea mbinu za jadi na miundombinu duni, jambo linalosababisha uzalishaji mdogo na kuifanya Tanzania kutegemea bidhaa za nje.
Kushindwa kukuza viwanda vya ndani kunazidi kufanya Tanzania kuwa taifa tegemezi. Bidhaa nyingi muhimu kama vile mafuta, sukari, nguo, na vifaa vya kielektroniki zinaagizwa kutoka nje, na hivyo pesa nyingi hutumika kuagiza bidhaa badala ya kujenga viwanda vya kuzalisha bidhaa hizi nchini. Hii inaathiri akiba ya fedha za kigeni na kudhoofisha shilingi, na pia inazuia fursa za ajira kwa wananchi.
3. Kujali Ustawi wa Viongozi na Kusahau Wananchi wa Kawaida
Ni wazi kwamba, kuna pengo kubwa kati ya ustawi wa viongozi na hali ya maisha ya wananchi wa kawaida. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya serikali yasiyo ya lazima na yanayohusu ustawi wa viongozi kama vile ununuzi wa magari ya kifahari, posho za juu, na nyumba za gharama kubwa za serikali. Wakati huo huo, huduma muhimu kama vile afya, elimu, na maji safi zimekuwa zikikabiliwa na changamoto nyingi kwa wananchi wa kawaida.
Badala ya kuweka kipaumbele kwenye mahitaji ya msingi ya wananchi, serikali inajikita zaidi katika kuboresha maisha na mazingira ya viongozi, hali inayoongeza hasira na kutoridhika miongoni mwa wananchi. Fedha zinazopaswa kuimarisha huduma za umma hutumika kwa manufaa binafsi ya wachache, huku wananchi wengi wakikosa huduma za msingi. Hii ni dhambi na ukatili wa kiwango cha juu.
4. Athari za Mfumo Huu kwa Maendeleo ya Watu na Ustawi wa Tanzania
Matokeo ya utegemezi wa kodi na tozo, kutokujali uzalishaji wa bidhaa za kuuza nje, na matumizi ya kupindukia ya viongozi, yanaathiri sana maendeleo ya Tanzania. Hali ya uchumi inaendelea kuwa duni, na nafasi za ajira zinazidi kuwa chache. Wananchi wanakosa uwezo wa kujikwamua kiuchumi, na hata wale wanaojaribu kuanzisha biashara wanashindwa kutokana na mzigo wa kodi na tozo.
Utaratibu huu pia unaathiri kiwango cha uwekezaji kutoka nje, kwani wawekezaji hawana uhakika wa mazingira ya kibiashara yanayoweza kubadilika ghafla kutokana na tozo na kodi mpya. Hali hii inafanya kuwa vigumu kwa Tanzania kuingia kwenye ushindani wa kimataifa, na kuendeleza uchumi unaotegemea matumizi ya ndani badala ya kuongeza thamani kwenye malighafi na kuzalisha bidhaa zinazoweza kuuzwa nje.
SULUHISHO:
Ili kupunguza maumivu ya kodi na tozo kwa wananchi wanyonge, serikali inapaswa kuchukua hatua zifuataxo:
1. Kuongeza Uzalishaji wa Ndani:
Serikali inapaswa kuwekeza katika miundombinu ya kilimo na viwanda ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa za ndani na kujenga uwezo wa kuuza nje bidhaa hizo. Hii inaweza kufanywa kwa kuanzisha sera na mazingira bora kwa sekta binafsi na kubuni vyanzo vipya vya mapato vinavoweza kuvutia watu wa ndani na nje. Mfano wa vyanzo vya mapato ambavyo serikali inaweza kuanzisha ni hivi vifuatavyo:
(a) Makumbusho ya Jeshi na Kumbukumbu za Vita vya Kagera.
Hapo panaweza kuwa sehemu ya maonesho ya silaha na kumbukumbu za historia ya jeshi la Tanzania. Silaha zilizotumika kwenye vita vya Kagera zinaweza kutumiwa kama kivutio cha utalii huku wanajeshi waliofindishws wakieleza, mbinu za vita zilivyoiwezesha Tanzania kupata ushindi.
Pamoja na silaha pia picha na historia za makamanda au wapiganaji mashujaa walioshiriki vita hivyo zinaweza kubandikwa au kuuzwa ili kuongezea uhai wa makumbusho hayo. Watu Wanaotembelea kituo hiki wanaweza kutozwa kiingilio kuongeza mapato ya serikali huku kituo kikielimisha wananchi kuhusu historia ya nchi na kujenga uzalendo.
(b) Bustani za Maua na Mimea ya Asili
Tanzania inajivunia wingi wa mimea na maua ya asili. Serikali inaweza kuhamasisha wananchi kuanzisha bustani za maua, ambazo zingeweza kutumika kama kivutio cha utalii. Bustani hizi, zikiwa chini ya uangalizi wa serikali au sekta binafsi, zinaweza kuchangia mapato kupitia ada za kiingilio na hata uuzaji wa mimea na maua adimu kwa wageni. Aidha, bustani hizi pia zitasaidia kutunza mazingira, kukuza elimu kuhusu mimea ya asili, na kuleta fursa za ajira kwa jamii.
(c) Makumbusho ya Tiba na Maonesho ya Afya na Sayansi ya Mwili
Serikali kupitia Kitivo cha Sayansi ya Tiba katika Chuo Kikuu cha Muhimbili kinaweza kuanzisha makumbusho ya tiba na afya. Makumbusho haya yangetoa fursa kwa wanafunzi, wataalamu wa afya, na wananchi kwa ujumla kujifunza kuhusu maajabu ya mwili wa mwanadamu na historia ya tiba nchini. Maonesho haya yangeweza kujumuisha vifaa vya zamani vya tiba, historia ya magonjwa na matibabu, pamoja na mifumo ya kisasa ya afya. Kutembelea makumbusho haya kungeweza kutozwa ada ndogo ambayo ingesaidia kitivo hicho kujitegemea kifedha na kusaidia katika tafiti za afya.. Badala ya watu kuwaona wataalam wa tiba kama Dr. Janabi kwenye luninga, watapata nafasi ya kukutana nao hapo na kuelimishwa. Pia wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo watapata nafasi ya kutembelea kwa magrupu na kujifunza.
(d) Kivutio cha Utalii wa Kilimo na Ufugaji
Sekta ya kilimo na ufugaji nchini Tanzania inayo nafasi kubwa ya kuvutia watalii na kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji wa ndani. Serikali inaweza kuanzisha vituo vya mafunzo na maonesho ya kilimo na ufugaji ambavyo vitakuwa wazi kwa wageni wa ndani na nje. Watalii wangeweza kujifunza kuhusu mimea ya asili ya Tanzania, ufugaji wa wanyama wa kienyeji, na njia za kilimo endelevu. Kivutio hiki kingeweza kutoza kiingilio na kutoa mapato ya ziada, huku kikikuza uelewa kuhusu sekta ya kilimo.
(e) Maonesho ya Sanaa na Utamaduni wa Tanzania
Tanzania inajivunia utamaduni na sanaa tajiri, ikiwa ni pamoja na ngoma, mavazi, na vyombo vya muziki vya asili. Serikali inaweza kuanzisha kituo cha maonesho ya sanaa na utamaduni wa Tanzania, ambapo wageni wangeweza kujionea historia ya vyombo vya muziki, mavazi ya jadi, na vyombo vya mikono. Vituo hivi vya maonesho vingetoza kiingilio kidogo na hivyo kuleta mapato, huku vikichangia utunzaji na uendelezaji wa urithi wa kitamaduni. Hivi sasa vituo kama Nyumba ya Sanaa na Kijiji cha Makumbusho vimepoteza mvuto wake.
(f) Mapumziko ya Asili kwenye Misitu na Milima
Serikali inaweza kuweka utaratibu wa kuendeleza maeneo ya misitu na milima kwa ajili ya watalii wanaotaka kupata mapumziko ya asili. Hii inaweza kufanyika katika maeneo kama Chisuhe au Mlima Kilimanjaro, ambapo wageni wanaweza kutozwa ada ndogo kwa kuingia na kufurahia utulivu wa mazingira. Kupitia utalii wa mapumziko ya asili, Tanzania inaweza kufungua fursa mpya za mapato huku ikilinda urithi wa mazingira.
(f) Uhamasishaji wa Utalii wa Bahari na Mazingira ya Majini
Tanzania ina bahari yenye mandhari nzuri na maisha ya baharini ya kuvutia. Serikali inaweza kuanzisha maonesho ya mandhari ya bahari na mazingira ya majini, kama vile ufugaji wa samaki wa bahari na uvuvi endelevu. Wageni wanaweza kutembelea vituo hivi kwa ada ndogo na kujifunza kuhusu mfumo wa mazingira wa bahari, viumbe vya majini, na utunzaji wa fukwe. Serikali pia inaweza kuhamasisha wawekezaji kufanya biashara za ukodishaji maboti na pikipiki za majini.
3. Kupunguza Kodi na Tozo kwa Biashara Ndogo:
Ni muhimu kuweka viwango vya kodi vinavyolingana na uwezo wa biashara ndogo na za kati, na kutoa motisha kwa wajasiriamali ili waweze kuanzisha na kupanua biashara zao bila kuwa na hofu ya mzigo wa kodi na tozo.
4. Kubana Matumizi ya Serikali:
Serikali inapaswa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuelekeza rasilimali kwa huduma za umma ambazo zitaboresha maisha ya wananchi, kama vile afya, elimu, na maji safi. Uwajibikaji wa fedha za umma unapaswa kupewa kipaumbele.
5. Kujenga Mazingira Bora ya Uwekezaji:
Serikali inapaswa kuunda sera za kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje kwa kuondoa urasimu na kutoza kodi na tozo kwa uwiano unaolingana na faida za kiuchumi. Uwekezaji kutoka nje utasaidia kuleta teknolojia, ujuzi, na kuongeza ajira kwa wananchi.
6. Kukuza Utamaduni wa Uzalishaji na Ubunifu:
Ni muhimu kuwahamasisha Watanzania kuwa wabunifu na wazalishaji. Serikali inaweza kuanzisha programu za mafunzo na usaidizi kwa vijana ili kuwaandaa kuwa na ujuzi wa kiufundi na ubunifu.
Hitimisho:
Umuhimu wa kuzalisha bidhaa na huduma zinazoweza kuuzwa nje ni mkubwa kwa Tanzania. Kutegemea kodi na tozo hakutatosha kuleta maendeleo endelevu wala kuondoa umaskini. Ni wakati wa serikali kuachana na sera za kifedha zinazowalemea wananchi na kuanza kuweka mikakati ya kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kuwanufaisha wananchi wote, si viongozi wachache.
Kwa kuweka mkazo katika uzalishaji wa ndani, kudhibiti matumizi ya serikali, na kuboresha mazingira ya uwekezaji, Tanzania inaweza kufikia uchumi endelevu unaotegemea uzalishaji na kupunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa kodi na tozo kwa wananchi.
Rev. Godwin Chilewa
Comentários