Sikio Lisilotahiriwa: Kilio cha Nabii Yeremia na Ukimya wa Vijana wa Kitanzania
- Rev. Godwin Chilewa
- Apr 23, 2025
- 2 min read

Ukisoma Biblia, kitabu cha Yeremia 6:10, utaona nabii huyo akitoa kilio cha uchungu, akisema: “Niseme na nani, na kushuhudia ili wapate kusikia? Tazama, sikio lao halikutahiriwa, hawawezi kusikiliza; tazama, neno la Bwana limekuwa kitu cha dhihaka kwao, hawalipendi.” Maneno haya si tu historia ya kale bali ni picha halisi ya kizazi chetu leo—hasa kwa vijana wa Kitanzania.
Leo, katika taifa letu, vijana wanaonekana kuzidi kupoteza masikio ya kusikia yale yenye manufaa ya kweli: haki, uhuru wa kisiasa, ukombozi wa kiuchumi na wa fikra. Badala yake, nguvu, muda, na akili zao nyingi huwekezwa katika simulizi za mapenzi ya kisanii, udaku wa mastaa, mijadala ya soka, na vichekesho visivyojenga fikra. Utafiti wa kijamii wa hivi karibuni unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya vijana hujishughulisha zaidi na maudhui ya burudani kuliko taarifa za kisiasa au kijamii zinazoweza kuwasaidia kuelewa hali ya nchi yao.
Katika mazingira haya ya ukiziwi wa kiroho na kifikra, bado wapo wachache wenye ujasiri wa kujaribu kuliamsha taifa. Wanasiasa na wanaharakati kama Tundu Lissu, John Heche, Profesa Tibaijuka, Maria Sarungi, na Joram Nkumbi wamekuwa kama sauti za Nabii Yeremia wa sasa—wakihubiri kwa bidii umuhimu wa demokrasia, utawala bora, haki za binadamu, na kujitegemea kiuchumi. Hawa ni watu waliotahiriwa masikio ya mioyo yao, lakini wanaongea mbele ya kizazi kisichotaka kusikia.
Cha kusikitisha, badala ya vijana kuamka na kujiunga na juhudi hizi za kiukombozi, wengi wao wamebobea kuwa “machawa” wa chama tawala. Uchawa huu unajidhihirisha katika namna vijana wanavyotetea kila kosa la mamlaka, kukataa kuhoji, na hata kuwadhihaki wanaojaribu kufikiri tofauti. Wanaingia mitandaoni si kuelimisha au kujenga hoja za mabadiliko, bali kulamba miguu ya wanasiasa kwa kutarajia vyeo, ajira au ‘likizo za chama’.
Kwa ujumla uchawa una madhara makubwa mno katika jamii. Hudumaza akili na kuwafanya vijana kuwa watumwa wa fikra za chama au mtu mmoja, taifa linakosa fikra mbadala ambazo ni msingi wa maendeleo ya kweli: Uchawa hutengeneza woga wa kusema ukweli na kulifanya Taifa kupoteza uwezo wa kujikosoa na kujirekebisha.
Si hivyo tu, uchawa pia hutengeneza Kizazi Kisichojitambua: Badala ya kujenga vijana walio huru kufikiri, Taifa huzalisha kizazi cha wafuasi na waoga—wasio na uthubutu wa kusimama kwa haki. Hili husababisha ufukara wa Kudumu kwani bila fikra huru na mijadala ya maendeleo, changamoto kama ukosefu wa ajira, ufisadi, na ukosefu wa huduma bora huendelea kutafuna taifa kwa vizazi. Ni kwa sababu hii mwalimu Julius Nyerere aliwahi kueleza masikitiko yake kwa kutengeneza taifa la watu waoga, na akasisitiza kwamba hilo halikuwa lengo lake.
Ni kwa sababu hii nasi tunapaswa kuomboleza kama alivyoomboleza. Ni lazima tuyatahiri masikio ya vijana wetu—tuwaamshie kiu ya maarifa na sauti ya mabadiliko. Kizazi kinachopenda simulizi za mapenzi kuliko simulizi za uhuru, haki na uchumi, kinajitayarisha kuzikwa katika kaburi la utumwa mpya: utumwa wa fikra. Kila mtanzania bila kujali kabila, dini au chama chake cha siasa lazima atambue umuhimu wa mabadiliko, na kukubali kubadilika. Mwalimu Nyerere alisema ni mtu mnyonyaji (aliyeshiba) tu anayeogopa mabadiliko.
Kama taifa, tusipoamka sasa, tutalazimika kushuhudia kizazi kizima kikizama gizani—si kwa kukosa nuru, bali kwa kuchagua kuifumbia macho.
Rev. Godwin Chilewa






Comments