top of page

Tumedhamiria Kuua Demokrasia?


Tarehe 10 Juni 2025 Mahakama nchini imetoa zuio la shughuli zote za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nchini. Zuio hilo limeitaka CHADEMA kusitisha shughuli zote za kiutendaji, ikiwa pamoja na mikutano ya hadhara. Mahakama imetoa agizo hilo kufuatia mashitaka yaliyofunguliwa na viongozi wa CHADEMA upande wa Zanzibar kuhusu kubaguliwa, matatizo ya kiutawala na matumizi ya fedha za chama hicho upande wa Zanzibar.


Kimsingi mahakama ni chombo cha kisheria na utoaji haki kisichopaswa kuingiliwa. Hata hivyo, namna hukumu hiyo ilivyotolewa imeibua maswali mengi kuhusu uhalali wa mchakato wa kisheria uliotumika, haki ya upande wa utetezi, na nia halisi ya uamuzi huo uliotolewa kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu, tena huku kukiwa na sintofahamu kubwa kuhusu namna serikali ya Chama cha Mapinduzi ilivyodhamiria kuua upinzani nchini.


Yapo mambo mengi yanayowasukuma watanzania wengi kuamini kwamba hukumu hiyo ni ya kimkakati, na kwamba mahakama imekuwa ikiendelea kutumika kama mkono wa serikali kuwadhibiti wapinzani ukizingatia jinsi mashauri mengi yanavyoshughulikiwa. Kwa mfano, mojawapo ya kanuni za msingi za haki katika utawala wa sheria ni haki ya kusikilizwa kwa pande zote mbili katika shauri husika. Katika kesi hii, CHADEMA hawakupewa haki hiyo baada ya wakili wao kujiondoa kwa sababu zisizofahamika


Kitendo cha wakili kujiondoa katika kesi ni cha kawaida katika mchakato wa kisheria, jambo ambalo lingeweza kutafsiriwa kama pengo la muda tu. Kwa kawaida, jaji alipaswa kuahirisha shauri hilo na kuwapa CHADEMA nafasi ya kupata wakili mwingine atakayewaongoza katika shauri lao kwa mujibu wa sheria Kwa ujumla uamuzi wa kuendelea na kesi bila wakili una madhara makubwa kwa chama, wanachama wake, na mustakabali mzima wa siasa za nchi.


Pamoja na hilo, yamejitokeza malalamiko mengi kuhusu konakona na kutokuwepo kwa uwazi unaotarajiwa katika masuala ya umma, hasa yale yanayohusisha taasisi za kisiasa. Mahakama zimekuwa zikivichukulia vyama vya siasa kama mali za watu (wapinzani) na si taasisi huru zilizoundwa kisheria kwa mujibu wa katiba. Hii imefanya kutokuwepo kwa maelezo ya kina kwa umma kuhusu msingi wa tuhuma, ushahidi uliowasilishwa, au vigezo vilivyotumika kutoa hukumu hiyo kali. Upungufu huu wa uwazi unatoa mianya ya mashaka, na kuibua hisia kwamba mahakama inatumika kama chombo cha kisiasa badala ya kuwa msuluhishi huru wa haki na kimbilio la mwisho kwa watanzania.


Sambamba na hilo, Jaji aliyesikiliza shauri hilo hakuwa na sababu ya msingi ya kuweka zuio la utendaji dhidi ya chama cha siasa katika kipindi cha uchaguzi kwa kuzingatia athari kubwa zinazoweza kujitokeza kwa mfumo wa vyama vingi na haki ya wananchi kushiriki siasa kwa uhuru. Mahakama ilipaswa kuwa makini zaidi na kupima uzito wa hatua hiyo kwa muktadha mpana wa haki za kiraia, ushiriki wa wananchi katika siasa, haki ya kuchagua na athari kwa mustakabali wa demokrasia nchini.


Kwa ujumla zuio dhidi ya CHADEMA ni pigo kubwa kwa mfumo wa vyama vingi ambao Tanzania iliamua kuingia zaidi ya miaka 30 iliyopita. CHADEMA ni chama kikuu cha upinzani, na kimekuwa jukwaa muhimu kwa maoni mbadala, ukosoaji wa serikali, na kushinikiza uwajibikaji. Kupiga marufuku shughuli za chama hiki ni sawa na kunyamazisha sauti muhimu katika ujenzi wa taifa.


Pengine wako wanaofikiri kuwa zuio hili lina faida kwa serikali au litasaidia Chama Cha Mapinduzi kushinda uchaguzi mkuu kwa urahisi. Hawa watakuwa wanajidanganya sana. Madhara ya uamuzi huu ni makubwa kuliko faida zake, ukizingatia mpaka wakati huu hali inaonesha wazi kuwa CCM itajitwalia ushindi wa uchaguzi mkuu ujao kwa nguvu.


Ni dhahiri kwa tukio hili limepooza nguvu ya vyama vingine vya siasa, ambavyo vinaweza kuona kuwa hata migogoro ya ndani inaweza kutumika kama kisingizio cha kuvizuia kushiriki chaguzi, au kuviua kabisa. Hofu ya kufungiwa inaweza kuzima ujasiri wa kisiasa na kuharibu misingi ya ushindani wa haki na uwazi katika siasa na kuishauri serikali.


Si hivyo tu bali pia wananchi wanapoona vyombo vya sheria vikitumika kuwakandamiza wale wanaokosoa serikali, hupoteza imani na taasisi hizo. Hii inaweza kusababisha kushuka kwa hamasa ya kisiasa, kupungua kwa ushiriki wa wananchi katika uchaguzi, na kuongezeka kwa ukosefu wa matumaini katika mabadiliko ya amani.


Baadhi ya wananchi tayari wameanza kulalamika kwamba uamuzi wa mahakama hii haukuzingatia athari za kidiplomasia na kiuchumi zinazoweza kujitokeza. Tanzania imekuwa ikiheshimika kama kisiwa cha amani na ustahimilivu wa kisiasa barani Afrika. Hata hivyo, hatua kama hii inazidi kuchochea sifa mbaya, na kuitangaza nchi kama inayokwenda njia ya udikteta wa chama kimoja, jambo linaloweza kuathiri ushirikiano wake na mashirika ya kimataifa na wafadhili. Zingatia kuwa asilimia kubwa ya bajeti ya Tanzania hutokana na michango ya wafadhili.


Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), SADC, na Umoja wa Afrika (AU), ambazo zote zinahimiza demokrasia na utawala wa sheria. Hatua hii pia inaweza kuibua wasiwasi wa kisiasa katika jumuiya hizi, na hata kushawishi mashinikizo ya kidiplomasia au vikwazo vya kisiasa.


Kwa ujumla mlolongo wa matukio ya kisiasa na kiusalama yanawaweka washirika wetu na hasa wawekezaji katika hali ngumu kwani wanahitaji mazingira tulivu na uhakika wa kisiasa. Pale ambapo kuna ishara ya ukandamizaji wa kisiasa na ukosefu wa haki, wawekezaji hukosa imani na huamua kuwekeza katika nchi nyingine zenye mazingira bora zaidi ya kisheria na kisiasa.


Zaidi ya yote maamuzi haya yanazorotesha dhana ya ukweli, uwazi na utawala bora. Upinzani husaidia kuishinikiza serikali kutimiza majukumubyake kwa misingi ya uwajibikaji. Kupungua kwa nguvu ya upinzani kunaweza kuchochea ongezeko la matumizi mabaya ya rasilimali, miradi isiyo na tija, na ufisadi, yote ambayo huishia kudhoofisha uchumi wa taifa.


Ipo pia hatari ya kudorora kwa mapato ya kigeni yatokanayo na utalii. Wageni hawapendi kutembelea mataifa yenye mivutano ya kisiasa. Hatua za kupiga marufuku vyama vya upinzani hujenga picha ya taifa lisilo salama, hivyo kupunguza mapato ya taifa na ajira zinazotokana na sekta hii.


Kumbe uamuzi wa Mahakama kuzuia shughuli za CHADEMA si tu kwamba umeibua maswali ya kisheria na haki za msingi, bali pia unaonekana kama tishio kwa msingi wa demokrasia ya Tanzania. Makosa ya wazi katika mchakato wa kutoa hukumu, kama vile kutowapa muda wa kujitetea, yanaweka doa kubwa kwenye heshima ya mahakama kama chombo huru. Zaidi ya hapo, hatua hii ina athari za mbali zaidi kwa siasa za ndani, uhusiano wa kimataifa, na ustawi wa uchumi wa taifa. Ni wakati sasa kwa wadau wote wa haki na demokrasia – wa ndani na wa kimataifa – kusimama kidete kutetea uhuru wa kisiasa, utawala wa sheria, na mustakabali wa demokrasia ya Tanzania.


Rev. Godwin Chilewa

 
 
 

Comments


bottom of page