top of page

Tukubali, Tusikubali Tuna Bunge la Hovyo Sana!


Tukubali tusikubali, tuna Bunge la hovyo. Hii ni kauli inayozidi kuenea miongoni mwa Watanzania wengi waliokerwa na mwenendo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT), hususan jinsi linavyoshughulikia hoja nzito za kitaifa. Tukio la karibuni kabisa linalothibitisha hali hii ni mjadala uliozuka bungeni kufuatia hoja ya Mbunge Josephat Gwajima kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na udhalilishaji wa raia wa Kenya waliokuja nchini kushiriki katika kesi ya Tundu Lissu. Badala ya kuchambua kwa kina hoja zilizotolewa, wabunge wengi walijikita katika kumpinga Gwajima na “kumtetea” Rais kwa jazba zisizo na mantiki wala mshiko wa kisheria au kimaadili.


Kwa masikitiko makubwa, baadhi ya wabunge waliochangia hoja ya waziri wa Mambo ya Ndani walifikia hatua ya kusifia vitendo vya udhalilishaji vilivyowakumba Martha Karia na Boniface Mwangi — raia wa Kenya waliokuja Tanzania kufuatilia haki — huku wengine wakishangazwa kwanini “hawakuuawa.” Hii si tu fedheha kwa taifa, bali ni doa jeusi katika historia ya Bunge kama mhimili unaopaswa kuwa nguzo ya haki, ulinzi wa katiba na utetezi wa watu wote bila kujali uraia wao.


BUNGE LILILOPOTEA MUELEKEO


Tukio hili si la kwanza kuonesha udhaifu wa Bunge letu. Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia:


  1. Upitishaji wa Sheria kwa Pupa.


Bunge linapaswa kuwa chombo makini katika utendaji wake. Lakini bunge letu halifanyi kazi kwa weledi, halizingatii matakwa ya wananchi, na mara nyingi hufanya maamuzi kwa pupa: Mifano ni kama vile Sheria ya Takwimu (2015), Sheria ya Vyama vya Siasa (2019), na marekebisho ya sheria ya vyombo vya habari — zote zikipitishwa kwa pupa bila mashauriano ya kina, na kwa nia ya kudhibiti uhuru wa raia badala ya kuuhifadhi.


  1. Ubwete na Upendeleo wa Kisiasa (Bias)


Bunge ni chombo cha wananchi kinachopaswa kufanya kazi zake kwa kuangalia maslahi mapana ya taifa. Hata hivyo Bunge la Tanzania limejivua utaifa na kujivika uchama. Mara nyingi wabunge wa chama tawala hujikita kulinda maslahi ya chama na viongozi wake kuliko maslahi ya wananchi. Mbunge anapojaribu kutoa hoja inayokosoa mamlaka, hujibiwa kwa kejeli, dharau au hata vitisho. Hili linajidhihirisha katika mjadala unaoendelea kuhusu kauli ya Mhe. Askofu Josephat Gwajima (MB). Badala ya kujadili hoja wabunge wamejikita kutoa kauli za kujipendekeza kwa Rais bila kuchambua chanzo halisi cha kauli ya Gwajima.


  1. Viti Maalum vya Kupitisha Ajenda


Nafasi za viti maalum ziliwekwa kwa lengo la kuongeza makundi maalum Bungeni kwa manufaa ya taifa. Hata hivyo wabunge wa viti hivyo wamegeuka kuwa mwiba kwa wananchi. Wabunge hawa mara nyingi wamekuwa kama kura za mkononi kwa serikali, pasipo msimamo huru au mchango wa kitaaluma. Wanapotosha dhana ya uwakilishi wa wanawake kwa kuwa wengi wao huteuliwa kwa misingi ya uaminifu wa kisiasa, urafiki na kujuana, wala si uwezo au weledi wa mhusika.


  1. Kutokuwa na Elimu au Uwezo wa Kuchambua Sera


Wabunge wengi hawana elimu ya kutosha wala uwezo wa kuchambua miswada ya sheria au hoja za msingi. Hii imesababisha hoja nyingi muhimu kupuuzwa au kufanyiwa maamuzi bila mantiki ya kina. Baadhi ya wabunge hufanya mizaha, na kuropoka mambo mazito yanayoathiri taswira ya nchi kimataifa. Hebu fikiria kauli ya mbunge wa Iringa aliyetamka bungeni kwanini raia majigambi kwamba ni kawaida ya polisi jimboni kwake kuwapiga na kuwatesa wananchi wanaofikishwa katika vituo vya polisi. Au tafakari kauli ya yule mbunge wa Zanzibar aliyeshangaa kwanini raia wa Kenya waliokamatwa na polisi hawakuteswa zaidi au kuuawa kabisa! Hizi ni kauli za watu wasiojua hadhi na maana ya Bunge.


MAPENDEKEZO YA MABADILIKO


Ili kurejesha heshima, mamlaka na tija ya Bunge la Tanzania, yafuatayo yapaswa kufanyiwa kazi: Kwanza kabisa ni mabadiliko ya katiba yatakayolipa Bunge uhuru kamili kama mhimili wa dola unaojitegemea, bila kuingiliwa na serikali au chama tawala. Viongozi wa Bunge hususan Spika na Naibu Spika wachaguliwe kwa uwazi na kwa misingi ya sifa na weledi, si uaminifu kwa chama pekee, kujuana, au kulipa fadhila.


Pili, ni muhimu iundwe Tume Huru ya Kikatiba kwa ajili ya mchakato wa katiba mpya inayoweka msingi imara wa mgawanyo wa madaraka na uhuru wa mihimili. Hivi sasa hakuna muelekeo wowote wa mchakato wa katiba mpya kwani viongozi wamejikita katika kampeni za uchaguzi, na kujihakikishia usalama na ustawi wa baada ya kipindi hiki. Ni vyema mchakato wa Katiba Mpya urejeshwe haraka iwezekanavyo.


Tatu, yafanyike marekebisho ya kikatiba na sheria kufuta nafasi za ubunge wa viti maalum. Wabunge hawa wamekuwa nyenzo ya kisiasa ya kupitisha ajenda, na si chombo cha uwakilishi wa kweli Bungeni. Badala yake, uwepo uwiano wa jinsia kupitia ushindani huru wa nafasi za ubunge wa majimbo. Hivi sasa wanawake wana mwamko mkubwa wa kushiriki katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Ni vyema vyama vya siasa vihamasishwe kuwapa nafasi wanawake kugombea kwenye majimbo yao.


Nne, sheria ibadilishwe kuweka kiwango maalum cha elimu kwa Wagombea Ubunge: Ingefaa sana liwekwe sharti kwamba mgombea wa nafasi ya ubunge awe angalau na shahada ya kwanza (degree) ili kuhakikisha wanaingia bungeni watu wenye ufahamu na uwezo wa kuchambua sera, kuielewa miswada, na kuchangia hoja za kitaalam kwa weledi na takwimu. Bunge si mahali pa mzaha au siasa za matusi na mipasho, bali kiini cha maamuzi ya taifa. Ni lazima liwe na watu wenye uwezo wa kupima matokeo ya kisera na sheria, na kuona athari zake kwa wananchi.


Tano, ziundwe Kamati Huru za Uchunguzi na Uwajibikaji: Kamati za Bunge ziwe na mamlaka ya kweli ya kuchunguza malalamiko ya wananchi na kuchukua hatua bila hofu wala upendeleo. Hoja kama zile zilizotolewa na Mbunge Gwajima kuhusu haki za binadamu zilipaswa kufanyiwa uchunguzi rasmi, na kutolewa majibu si kupuuzwa kwa jazba na kujipendekeza.


Pamoja na hilo ni muhimu pia Kila mbunge ahudhurie mafunzo ya uongozi, maadili ya umma, na usimamizi wa sheria kabla ya kuanza rasmi kazi za kibunge. Wabunge wengi wa sasa hawazingatii maadili ya nafasi yao, hawatimizivwajibu wao kwa weredi, na wamegeuka kuwa chawa wa mama na chama tawala. Hili ni tatizo kubwa linalopaswa kutatuliwa mara moja.


HITIMISHO


Mwenendo wa sasa wa Bunge la Tanzania ni dalili ya mifumo iliyokufa kiuhuru, kifikra, na kimaadili. Kushangilia udhalilishaji wa binadamu, kusifia vitisho vya kifo dhidi ya wageni, na kupuuza hoja nzito za kitaifa si tu aibu, bali ni hatari ya kiusalama wa ndani na wa kimataifa.


Ni wakati wa wananchi, asasi za kiraia, na viongozi wa kweli kusimamia mapambano ya mabadiliko ya katiba, kufuta viti maalum, kuweka viwango vya kielimu, na kurejesha heshima ya mhimili huu muhimu wa nchi.


Bunge la kweli linapaswa kuwa sauti ya watu, si kinga ya mamlaka.


Rev. Godwin Chilewa

 
 
 

Comentarios


bottom of page