top of page

Ukimya ni Dhahabu: Hekima ya Uongozi Katika Kunyamaza


Katika historia ya mataifa mengi duniani, uongozi bora haujapimwa tu kwa uwezo wa kusema, bali pia kwa hekima ya kuchagua wakati wa kunyamaza. Biblia, ambayo ni hazina ya hekima ya milele, inasisitiza kuwa mtu mwenye hekima si yule anayejibu kila jambo, bali yule anayeweza kuzuiya ulimi wake katika misukosuko ya hoja na shinikizo la umaarufu.


Katika siku za hivi karibuni, tunashuhudia mwenendo unaozua maswali kuhusu mtindo wa mawasiliano wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Ni dhahiri kwamba mheshimiwa anacho kipaji cha kuzungumza kwa ufasaha. Hata hivyo kuna jambo moja linalotia shaka. Hivi sasa kila hoja ya kichokozi au ukosoaji unaomwelekea mheshimiwa Rais hutoa majibu yenye ukali, kejeli au hata mashambulizi binafsi kwa mhusika, au taasisi hali inayoweza kuathiri taswira ya urais na mshikamano wa kitaifa.


Mfano halisi ni pale Askofu Josephat Gwajima (MB) alipotoa hoja kuhusu matukio ya utekaji nyara nchini. Mbunge huyo alikumbana na majibu makali kutoka kwa Rais, aliyemkejeli hadharani, tena kwenye mkutano mkuu wa CCM na baadaye kufunga kanisa lake.


Naye mbunge wa Kisesa, Charles Mpina, aliposema kwamba wananchi wa jimbo lake wanamlaumu Rais kwa kutotimiza ahadi, alijibiwa hadharani kwa maneno makali, huku Rais akiwataka wananchi kutomchagua tena kama mbunge wa jimbo hilo akisisitiza mbunge huyo amejifanya mbunge wa taifa na hajasimamia maslahi ya jimbo lake. Rais alifanya hivyo bila kujali kuwa Mpina ametumwa na wana Kisesa.


Pengine unaweza kusema mheshimiwa Rais amekuwa mkali hivyo kwa sababu ya homa ya uchaguzi. Hili si kweli. Huko nyuma Spika wa Bunge wa wakati huo, Job Ndugai, alipotoa hoja ya tahadhari kuhusu mzigo wa mikopo ya taifa, alikumbana na maneno makali na ya ghafhabu kubwa kutoka kwa Rais. Baadae Ndugai alilazimishwa kujiuzuru ili kumpa Rais ahueni.


Tena si mheshimiwa Ndugai peke yake aliyekutana na dhoruba hiyo. Viongozi wa baraza la maaskofu katoliki, na wananchi wengine waliohoji mkataba wa Bandari na DP World wote walijikuta wakipewa vipande vyao na mheshimiwa rais mwenyewe.


Katika matukio haya yote, hoja zilizotolewa zilikuwa za msingi na maslahi ya taifa. Hata hivyo ziligubikwa na majibu ya hasira badala ya mjadala wa kistaarabu. Kama hoja hizo hazikuwa na uzito, ukimya au majibu ya kisera yangekuwa silaha bora zaidi kwa mheshimiwa rais na serikali anayoiongoza.


Labda nionye kwamba si nia yangu kumdharilisha au kumkejeri mheshimiwa rais kwa namna yoyote ile. Nia yangu ni kujenga hoja itakayomtafakarisha na pengine kumsaidia katika kipindi kigumu anachopitia, na naamini hii ni njia muafaka ya kumfikia.


Pamoja na hilo, kwa mtazamo wangu naona kuna tatizo kubwa mno katika ofisi ya Rais, watu wanaomshauri au wataalam wanaomsaidia kuandaa hotuba zake. Jambo linalomdhalilisha mheshimiwa rais.


Biblia inatufundisha kuwa kunyamaza ni hekima, si udhaifu. Neno linasema “Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa kuwa mwenye hekima.” (Mithali 17:28) Naye Mhubiri aliandika akionya “Kuna wakati wa kunyamaza, na wakati wa kusema.” (Mhubiri 3:7). Tena mtume Yakobo anatufundisha “Kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, si mwepesi wa kusema.” (Yakobo 1:19)


Kwa viongozi, hasa wa ngazi ya juu kama Rais wa nchi, majibu yake yana maana nzito kwa dunia nzima. Lakini kutoa majibu ya kila hoja kunaweza kupoteza hadhi yake, na kugeuza mjadala wa kisera kuwa vita vya maneno na mihemko. Kimsingi hakuna sababu ya Rais kujiingiza kwenye malumbano na raia au viongozi wake.


Ieleweke kwamba Rais si mwanasiasa wa mtaani; yeye ni nembo ya umoja wa taifa. Kujibizana hadharani huondoa haiba ya ofisi yake. Wananchi hufuata sauti ya kiongozi. Kauli zenye ukali au kejeli huweza kuongeza chuki, mifarakano, na migawanyiko ya vyama au dini.


Si hivyo tu, kitendo cha Rais kujiingiza kwenye malumbano hudhoofisha demokrasia, kuzuia uhuru wa kujieleza, jambo linalozorotesha utamaduni wa majadiliano ya wazi. Kauli ya Rais ina utisho unaoweza kujenga hofu kwa Viongozi Wengine. Wabunge, mawaziri au viongozi wa dini wakihofia kujibiwa kwa kejeli, huacha kuzungumza mambo ya msingi kwa ajili ya taifa, na hivyo kunyamazisha sauti za tahadhari muhimu.


Zaidi ya yote, kitendo cha Rais kujibu kila hoja huweza kutoa mwanya kwa wakorofi kutafuta nafasi ya kujipatia umaarufu, na watu wa maana wenye hoja za msingi kuonekana wakorofi (kwa kuwekwa kundi moja na wajinga wasiojua wajibu wao)


Ni kwa sababu hii Kwa heshima na moyo wa uzalendo, tunatoa mapendekezo haya kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mhesimiwa Samia Suluhu Hassan:


Jenga Uvumilivu wa Kiongozi Mkubwa Sio lazima kila hoja ijibiwe. Viongozi wakuu duniani hufanyiwa ukosoaji mkubwa, lakini hulazimika kuweka mbele busara na uvumilivu kuliko mihemko. Hekima ya kimya chako inatosha kujibu kwa nguvu.


2. Tumia Wasemaji wa Serikali Si kila hoja ni ya kushughulikiwa na Rais binafsi. Katibu Mkuu, Msemaji Mkuu wa Serikali, au Mawaziri wanaweza kutoa majibu ya kitaalamu na yenye mwelekeo wa sera.


3. Wekeza katika Majibu ya Kisera, Si Kisiasa Badala ya kejeli, toa taarifa za maendeleo au ufanisi wa serikali. Hii huondoa nguvu ya wakosoaji bila malumbano.


4. Kumbatia Mawazo Tofauti kama Mvuto wa Demokrasia. Uongozi imara huvumilia kukosolewa, hujifunza kutoka kwa hoja zenye msingi, na kuimarika kupitia mijadala ya wazi.


5. ⁠Usiruhusu jazba au mihemko kuteka fikra na hadhi yako. Ndiyo, wewe ni binadamu, una roho na hisia. Lakini pia wewe ni Rais, jemedari na amiri jeshi mkuu wa nchi. Hasira yako ni moto ulao. Ukichukulia mambo kwa hasira wengi wataumia. Tuliza roho, vuta subira. InnAllahu maswabirina.


Kama taifa, tunahitaji uongozi unaojua kutofautisha sauti za kujenga na kelele za kuchafua. Taifa halihitaji Rais ambaye hujibu kila mtu, au anayevutwa na jazba, bali kiongozi ambaye kwa kimya chake hutoa ujumbe mkubwa wa utu uzima wa kisiasa. Kiongozi ambaye anaweza kusema, lakini anachagua kunyamaza kwa sababu ya hekima, Kama Methali inavyotufundisha, “Yeye azuiaye maneno yake ana maarifa” (Methali 17:27). Na kwa hakika, “Ukimya ni dhahabu.”

 
 
 

Comments


bottom of page