Umuhimu wa Tanzania Kujiandaa kwa Majanga na Dharura za Kitaifa
- Rev. Godwin Chilewa
- Feb 11, 2025
- 4 min read

Katika dunia ya leo yenye changamoto nyingi za kiuchumi, kijamii, na kiusalama, nchi yoyote inayotaka kuendelea ni lazima iwe na mikakati madhubuti ya kujiandaa kwa dharura na majanga. Tanzania, kama ilivyo kwa mataifa mengine yanayoendelea, inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile ukame, magonjwa, mabadiliko ya tabianchi, na hata vitisho vya kiusalama.
Si hivyo tu, hivi karibuni, Tanzania ilijikuta katika kadhia nyingine baada ya serikali ya Marekani kusitisha misaada ya huduma za afya zilizokuwa zikitolewa kupitia shirika lake la USAID. Ingawa serikali imefanya juhudi kubwa za kukabiliana na hali hiyo ni muhimu sana ikafanya tathimini ya kina kuhusu uwezo wa nchi kujitegemea na kukabiliana na nyakati za dharura na majanga.
Yapo mambo mengi ya muhimu ambayo serikali inapaswa kuyaimarisha au kuyaangalia kwa kina ili kuhakikisha usalama wa watanzania nyakati za dharura. Baadhi ya mambo hayo ni ya wazi, na mengine ya faragha ambayo hayatahili kuanikwa hadharani. Katika hali ya kawaida tunaweza kuamini kuwa serikali inayajua mambo haya, na imejiandaa lakini uzoefu umetufundisha kutambua kwamba mara nyingine wakubwa huwa wanasahau au kujisahau.
Jambo la kwanza ni akiba ya mafuta ya petroli. Kimsingi mafuta ni uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yoyote. Sekta za usafirishaji, viwanda, kilimo, na hata huduma za dharura zinategemea mafuta kwa ufanisi wake. Endapo Tanzania itakumbwa na mgogoro wa kimataifa unaosababisha uhaba wa mafuta au hata vita vinavyoweza kusababisha mataifa yanayotupatia mafuta kusitisha usambazaji, taifa litaingia katika hali ngumu sana kiuchumi na kijamii.
Kwa bahati mbaya uzoefu tulio nao umetuonesha serikali hailipi kipaumbele suala la akiba ya mafuta kama inavyotakiwa. Huko nyuma aliyekuwa waziri wa nishati mheshimiwa Yusufu Makamba aliwahi kujigamba kuwa serikali ina akiba ya mafuta ya kutosha mwezi mmoja. Ingawa kwa wananchi wa kawaida taarifa hii ilikuwa ya faraja, kwa wajuzi wa mambo ilikuwa ni fedheha kubwa. Ili kuepuka hali hii, ni muhimu serikali ianzishe na kuhifadhi akiba ya mafuta itakayoweza kutumika angalau kwa miezi sita. Mataifa mengine kama China na Marekani yana hifadhi kubwa za mafuta kwa dharura, ambazo zinasaidia kudhibiti athari za migogoro ya mafuta duniani. Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwao kwa kujenga maghala makubwa ya kuhifadhi mafuta na kuhakikisha hifadhi hiyo inasasishwa mara kwa mara.
Jambo la pili ni akiba ya chakula cha dharula. Hili ni muhimu sana kwani ukame, mafuriko, au milipuko ya magonjwa ya mimea kama vile nzige wanaoweza kushambulia mashamba kwa wingi vinaweza kusababisha baa la njaa. Historia inatufundisha kuwa mataifa yanayojipanga kwa majanga haya hupunguza madhara kwa wananchi wake na hata kuokoa uhai. Biblia inasimulia jinsi Yusufu alivyomshauri Farao wa Misri kuhifadhi chakula cha miaka saba ili kujiandaa kwa njaa iliyokuwa inakuja. Huu ni mfano mzuri wa kupanga kwa ajili ya dharura.
Serikali ya Tanzania inapaswa kuwekeza katika maghala makubwa ya kuhifadhi chakula cha kutosha angalau kwa mwaka mmoja. Hii itahakikisha kuwa hata wakati wa ukame au majanga mengine, wananchi hawataathirika vibaya kwa upungufu wa chakula. Aidha, ni muhimu pia kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kuhifadhi nafaka kwa muda mrefu bila kuharibika. Jambo hili linaweza kutekelezeka endapo serikali itadhibiti uuzaji wa nafaka nje ya nchi kiholela.
Usalama wa maji mijini na vijijini ni jambo lisilopaswa kupuuzwa kwani maji ni uhai. Miji mikubwa kama Dar es Salaam na Dodoma inategemea vyanzo vichache vya maji, hususan Mto Ruvu kwa Dar es Salaam. Endapo adui watashambulia au kuhujumu chanzo hiki cha maji, jiji lote la Dar es Salaam litaingia katika janga kubwa kiasi cha kuweza kusababisha maafa au magonjwa ya mlipuko.
Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa kuna hifadhi kubwa za maji zinazoweza kutumiwa wakati wa dharura. Ujenzi wa matanki makubwa ya maji mijini, na hata vijijini, utasaidia kupunguza athari za ukame au hujuma za kimkakati zinazoweza kutokea. Mataifa kama Israel yamefanikiwa sana katika uhifadhi wa maji kwa kutumia teknolojia za kisasa kama uvunaji wa maji ya mvua na uchenjuaji wa maji ya bahari.
Jambo la nne ni uboreshaji wa vikosi vya uokoaji na dharula. Vikosi hivi ni muhimu kwani janga lolote linapotokea, iwe ni mafuriko, tetemeko la ardhi, au ajali kubwa, na hata vita, vikosi vya uokoaji vina jukumu muhimu la kuokoa maisha. Tanzania inapaswa kuwekeza zaidi katika mafunzo na vifaa vya kisasa kwa vikosi vya zimamoto, polisi, wanajeshi, na mashirika ya misaada ya kibinadamu. Ingawa Tanzania imekumbwa na majanga mengi bado hatujawekeza vya kutosha katika sekta hii.
Mfano mzuri ni jinsi mataifa kama Japan yalivyojifunza kutokana na majanga ya tetemeko la ardhi na tsunami kwa kuwekeza katika vikosi vyao vya uokoaji na mifumo ya tahadhari ya mapema. Tanzania inaweza kutumia teknolojia kama drones na mifumo ya kidijitali ya kufuatilia majanga kwa wakati halisi ili kuimarisha ufanisi wa vikosi vya uokoaji.
Serikali pia inapaswa kufanya uwekezaji mkubwa katika viwanda vya madawa. Hii ni kwa kuwa afya ya wananchi ni kipaumbele cha taifa lolote. Kutegemea dawa kutoka mataifa ya nje ni hatari, hasa katika nyakati za dharura kama vile mlipuko wa magonjwa au vikwazo vya kimataifa vya biashara. Pia hivi sasa lipo tatizo kubwa la uingizaji dawa bandia au zisizofaa kwa matumizi. Tanzania inapaswa kuimarisha viwanda vyake vya dawa ili kuhakikisha kuwa ina uwezo wa kuzalisha dawa za msingi kwa wananchi wake bila kutegemea uagizaji kutoka nje.
Mfano wa mafanikio ni India, ambayo imewekeza kwa kiasi kikubwa katika viwanda vya dawa na sasa ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dawa duniani. Tanzania inaweza kuchukua hatua kama hizo kwa kuweka sera zinazovutia wawekezaji katika sekta ya dawa na kuhamasisha utafiti wa kisayansi katika vyuo vikuu vyake.
Zaidi ya yote, Tanzania inapaswa kupunguza matumizi ya anasa kwa viongozi na kuimarisha usalama wa Taifa. Hatua hii ni muhimu mno ili fedha zaidi ziwekezwe katika maeneo yenye umuhimu wa kimsingi kama vile hifadhi ya chakula, mafuta, na huduma za dharura. Serikali inapaswa kuhakikisha kuwa bajeti inatengwa kwa vipaumbele vya kitaifa badala ya matumizi ya anasa na miradi isiyo ya lazima.
Tanzania inapaswa kuiga mfano mzuri wa nchi za Scandinavia, ambazo zinahakikisha kuwa bajeti ya serikali inatumika kwa maendeleo ya wananchi badala ya matumizi yasiyo ya lazima. Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwao kwa kubuni sera madhubuti za kudhibiti matumizi ya fedha za umma.
Kujiandaa kwa majanga na dharura si jambo la hiari bali ni wajibu wa serikali kwa wananchi wake. Ni wakati mwafaka kwa Tanzania kuweka mikakati madhubuti ya kujitegemea ili kuhakikisha usalama na ustawi wa wananchi wake kwa miaka ijayo.
Rev. Godwin Chilewa






Comments