UTEKAJI NA USALAMA NCHINI: Uchambuzi wa Kauli ya Mhe. Gwajima na Mapendekezo ya Kuimarisha Ulinzi wa Raia
- Rev. Godwin Chilewa
- 5 days ago
- 3 min read

Tarehe 24 Mei 2025, Mbunge wa Jimbo la Kawe, Mhe. Askofu Dkt. Josephat Gwajima, alizungumza na waandishi wa habari na kutoa tahadhari juu ya ongezeko la matukio ya utekaji na mauaji akidai kuwa hali hiyo inatishia maisha ya wananchi na kuitia doa taswira ya taifa kimataifa. Kikubwa zaidi ni kwamba mbunge huyu alimtaja (indirectly) mtu au kiongozi aliye nyuma ya matukio ya utekaji nyara na mauaji yanayoendelea nchini (Mwenye ufahamu na afahamu).
Kauli hizi zimeibua hisia tofauti miongoni mwa wananchi. Wakati baadhi wakimuunga mkono kwa kueleza ukweli usiosemwa, wengine wamehoji mantiki ya kauli hizo na mapendekezo aliyotoa. Katika makala hii, tunafanya uchambuzi wa kiintelijensia juu ya maoni ya Mhe. Gwajima, tunapima mapendekezo yake, tunabainisha mapungufu yaliyopo, na kutoa njia mbadala zinazoweza kusaidia kuboresha mfumo wa usalama nchini.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mhe. Gwajima alieleza kushangazwa na kile alichokiita “kimya cha vyombo vya usalama” licha ya matukio ya utekaji kuongezeka. Alitoa wito kwa serikali kutowatumia wakuu wa vyombo vya usalama kama vikaragosi wa kisiasa, na badala yake kuwapa uhuru wa kutekeleza majukumu yao kwa weledi na bila hofu ya kufukuzwa kazi. Aidha, alitaka vyombo hivyo viwe na uwajibikaji wa moja kwa moja kwa taifa na si kwa wanasiasa waliowateua.
Kauli hizi, ingawa zinaakisi hali halisi kwa kiasi fulani, hazitoshi katika kushughulikia tatizo linalozidi kuwa sugu. Hivyo basi, tunahitaji mjadala mpana zaidi wa kitaasisi, kisera na kisheria.
Mapungufu ya Mapendekezo ya Gwajima
1..Mhe. Gwajima alitumia takwimu za matukio ya utekaji, kukazia uzito wa hoja yake, lakini hakueleza kwa kina vyanzo vya takeimu hizo jambo ambalo linaweza kudhoofisha uhalali wa madai yake na kufungua mianya ya upotoshaji. Uzuri ni kwamba matukio ya utekaji yanafanyika hadharani na hakuna mtanzania anayehitaji kuona takwimunili kuthibitisha. Hali inajionesha waziwazi jinsi wananchi walivyo na wasiwasi.
2.: Ingawa mhe. Gwajima alisisitiza umuhimu wa uhuru wa vyombo vya usalama, hakutoa mapendekezo ya wazi kuhusu jinsi mfumo wa uteuzi na uwajibikaji wa viongozi wa vyombo hivyo unavyopaswa kuboreshwa kisheria. Udhaifu wa Bunge la Tanzania unalifanya lisiaminike kupewa jukumu alilopendekeza Gwajima ukizingatia Rais ana nguvu kubwa kiasi cha kuweza kuliburuza Bunge apendavyo.
3. Pamoja na maelezo mazuri, Mhe. Gwajima hakueleza hatua zozote alizochukua kama mbunge kushirikiana na Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama au taasisi nyingine katika kushughulikia tatizo hili. Kinyume chake historia inaonesha Bunge liliwahi kukataa kujadili hoja zote zilizopendekeza kufanyika kwa uchunguzi wa matukio ya utekaji nyara.
Mapendekezo Mbadala: Njia Endelevu za Kuimarisha Usalama
1.Kuanzisha Tume Huru ya Usalama wa Ndani
Ni muhimu ipitishwe sheria ya kuanzishwa kwa Tume Huru ya Usalama wa Ndani. Tume hii ipewe mamlaka na uhuru wa kuchunguza malalamiko ya utendaji wa vyombo vya dola. Tanzania inaweza kuiga mfano wa Uingereza ambayo ina Independent Office for Police Conduct (IOPC) inayochunguza kwa uhuru vitendo vya ukiukwaji wa maadili na kushughulikia malalamiko dhidi ya vyombo vya usalama. Tume huru itakayoanzishwa nchini itapaswa kuwa na mamlaka ya kuchunguza matukio kama ya utekaji, na mateso wanayofanyiwa wananchi wakiwa mikononi mwa Polisi bila kuingiliwa na mamlaka ya kisiasa.
2: Marekebisho ya Mfumo wa Uteuzi wa Wakuu wa Vyombo vya Usalama
Utengenezwe mfumo wa kikatiba unaoweka uwazi katika uteuzi, na vigezo vinavyozingatia taaluma, rekodi ya kazi na nidhamu.ya nchi kama Canada na Ujerumani inaweka mchakato wa uteuzi wa viongozi wa usalama kupitia Bunge au kamati maalum ya usalama, si kwa ridhaa ya mtu mmoja. Hii huongeza uwajibikaji na kupunguza ushawishi wa kisiasa. Hili litawezekana kama uongozi ulioko madarakani utaruhusu mabadiliko ya Katiba.
3: Kuanzisha Mfumo Madhubuti wa Taarifa za Kiintelijensia wa Kiraia (CITIS)
Mataifa kama Israel kupitia shirika lake la Shin Bet, na Australia kupitia Australian Security Intelligence Organisation (ASIO), yamewekeza sana katika mitandao ya kiintelijensia ya kiraia. Tanzania inaweza kuanzisha mfumo wa kiintelijensia unaowashirikisha wananchi kutoa taarifa za uhalifu kwa njia salama na ya siri, kwa kutumia teknolojia rahisi kama namba maalum za dharura au programu za simu.
4: Ushirikiano wa Serikali na Asasi za Kiraia
Hali ya usalama haipaswi kuachiwa serikali pekee. Kwa mfano, nchini Kenya, mashirika yasiyo ya kiserikali kama Haki Africa hushirikiana na polisi kutoa elimu ya usalama kwa jamii na kufuatilia ukiukwaji wa haki. Tanzania inapaswa kuhamasisha mashirika ya kiraia kushiriki katika kudhibiti utekaji kwa kutoa msaada wa kisaikolojia kwa waathirika, kufanya tafiti na kampeni za uhamasishaji.
5.Kuweka Mfumo wa Uwajibikaji wa Umma (Public Oversight)
Tume maalum ya Bunge inayosimamia ufanisi wa vyombo vya usalama iwe na mamlaka ya kuwaita wakuu wa taasisi za usalama na kupokea taarifa kwa uwazi kuhusu mafanikio na changamoto, kama ilivyo kwenye Congress ya Marekani ambako kamati ya House Intelligence Committee hufanya kazi hii kwa karibu.
Hitimisho
Hali ya usalama ni msingi wa maendeleo ya taifa lolote. Kauli za Mhe. Gwajima zimeibua mjadala muhimu, lakini ili taifa lisikie na kuona mabadiliko ya kweli, ni lazima mjadala huo uendelezwe kwa mapana na kwa msingi wa kisera na kitaasisi. Tanzania haiwezi kupambana na uhalifu kwa kauli pekee, bali kwa kujenga mifumo huru, yenye uwazi na inayoheshimu taaluma ya ulinzi na usalama. Viongozi wote, bila kujali itikadi, wanapaswa kushirikiana kulinda maisha ya Watanzania.
Rev. Godwin Chilewa
Comments