Viaticum - Sakramenti ya Mwisho
- Rev. Godwin Chilewa
- May 2, 2025
- 32 min read
Updated: May 4, 2025

Ilikuwa jioni tulivu kwenye viwanja vya ikulu ya Kipapa ya Vatican. Jua lililokuwa likizama lilitengeneza vivuli virefu vya rangi ya kahawia juu ya barabara za mawe na majengo ya kale. Juu kabisa, mnara wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro ulisimama kama mlinzi asiyetikisika, uso wake wa marumaru ukimulikwa na mwanga wa dhahabu. Ikulu ya Kipapa yenyewe, jengo kubwa lenye vyumba vya kifahari, korido za siri, na vyumba vya chini ya ardhi vilivyofichwa, ilisimama kama ngome ya nguvu ya kiroho na hila.
Ndani ya ikulu, muadhama Kardinali Giovanni Rizzo alikaa ofisini kwake, amezungukwa na rafu ndefu za vitabu vya zamani vilivyojaa maandishi ya kale na vitabu vya ngozi vilivyofungwa kwa uangalifu. Meza yake, kubwa iliyotengenezwa kwa mti wa mwaloni uliopambwa kwa alama za upapa, ilijaa nyaraka, barua, na ramani ya kina ya Afrika. Harufu nzito ya makaratasi ya zamani ilijaza chumbani ikitawala kama tumbaku kavu.
Kardinali Rizzo alirekebisha vazi la rangi nyekundu alilovaa, huku vidole vyake vikigonga kwa wasiwasi juu ya meza. Alikuwa akisubiri ripoti kutoka kwa mpelelezi wa kuaminika wa Vatican, ripoti ambayo ingeweza kufunua njama iliyokuwa ikihusisha ngazi za juu kabisa za Kanisa. Mahali fulani, ndani ya kumbukumbu za Vatican, hati ya siri kuu kwa kanisa ilikuwa imeibiwa—hati iliyokuwa na taarifa za kutisha kuhusu unabii uliofichwa.
Ni ajabu kwamba wahalifu waliweza kufikiria kuifikia hati hii, au hata tu kujua mahali ilipotunzwa. Hati hii ya siri kuu ilifichwa kwenye chumba kinacholindwa vikali, kilichozikwa ndani ya jumba la Kumbukumbu la Mitume. Mlango wa chumba hiki ulikuwa umefungwa kwa karne nyingi kulinda usalama wa nyaraka na hati nyingi zilizobeba siri zenye nguvu na hatari kubwa. Makadinali wachache tu waliojua kuwepo kwake.
Ghafla, milango miwili ya ofisi hiyo ikafunguliwa kwa utulivu, na Monsinyo Marco Bianchi akaingia kwa haraka, joho lake jeusi likiburuza sakafu ya marumaru.
“Muadhama,” Marco aliita huku akiinama kidogo. “Nina habari za kusikitisha. Tumethibitisha.”
Macho ya kadinali Rizzo yakajaa giza, jasho jembamba likamtiririka usoni. Alikuwa mmoja wa watu wachache waliokuwa wameaminiwa kiasi cha kuambiwa mahali hati hiyo ilipokuwa. Sasa uaminifu huo ulikuwa umevunjika.
“Enhee endelea padri.” Aliongea sauti yake ikitetemeka, miguu ikielekea kulegea kwa hofu.
“Tunaamini hati imeshavushwa mpaka, iko nje ya Vatican,” Monsinyo Marco aliongea kwa sauti ya kunong’ona. “Ujumbe wa mwisho tuliounasa ulitaja Tanzania. Hapo ndipo ilipotoweka kabisa. Hatujui imepelekwa wapi.”
“Tanzania?” Kadinali Ruzzo aliuliza kwa mshangao”
“Tunaamini mtandao uliohusika ni mkubwa zaidi kuliko tulivyofikiri. Inawezekana makardinali kadhaa wanahusika na wizi huo.” Monsinyo Marco alifafanua.
Kardinali Rizzo akasimama ghafla, kiti chake kikiburuza sakafuni kwa kishindo. Moyo ulimdunda kwa kasi, pumzi zilimuelemea. Historia ya giza ya Vatican ilikuwa imejaa siri, lakini hii—hii ilikuwa ya kipekee.
“Makardinali? Inawezekanaje?” Aliuliza kwa unyonge.
Monsinyo Marco akatikisa kichwa, uso wake ukiwa umejaa huzuni. “Mambo ni ya kutisha kuliko tulivyofikiri. Askofu mmoja wa Tanzania aliuawa siku mbili zilizopita. Mwingine ametoweka, hajulikani aliko. Wahalifu walioiba hati si wababaishaji, wanajua wanachofanya.”
Kabla Kardinali Rizzo hajajibu, taa zikatetemeka na kisha kuzima, chumba kizima kikaingia kwenye giza la ghafla. Ukimya wa kutisha ukatanda, ukivunjwa tu na vishindo vya miguu inayosikika kwa mbali kwenye korido.
Hisia za Monsinyo Marco zikaamka. “Muadhama, kaa chini tafadhali!” alionya, akaingiza mkono mfukoni na kutoa bastola ndogo aina ya Sig Sauer P365 kutoka kwenye joho lake kisha akasogea karibu na mlango.
Kardinali Rizzo, hakuweza kujizuia kutetemeka, akainama kujificha nyuma ya meza yake. Ofisi yake mara zote ilikuwa na hisia ya usalama, mahali pa kutafakari na kuwa na mamlaka, lakini sasa aliiona kama kaburi. Giza lilitawala, likipunguzwa nguvu na mwanga hafifu wa jua unaopenya kwenye dirisha la vioo vya rangi nyuma yake.
Monsinyo Marco akasogea polepole karibu na mlango, macho yake yakichungulia gizani. Kuna jambo lisilo la kawaida linaendelea—jambo baya sana. Akashika mpini wa mlango wa shaba kwa tahadhari, akausukuma taratibu, na kuchungulia kwenye korido yenye mwanga hafifu.
Korido yenyewe ilipambwa kwa michoro ya mapapa wa zamani, nyuso zao zenye huzuni zikiangalia njia hiyo kama walinzi wa kale. Kwa kawaida, walinzi wa papa wajulikanao kama Swiss guard walikuwa wakilinda sehemu hii ya Ikulu ya Kipapa, lakini sasa ilikuwa na ukimya wa kutisha. Chandeliers zenye taa juu zilikuwa zikining'inia kwa utulivu, zikitoa vivuli vya kutetemeka kwenye kuta.
Ghafla, wakasikia vishindo vya nyayo za watu wakikimbia upande wa mwisho wa korido. Moyo wa Monsinyo Marco ukaongeza spidi ya mapigo yake.
"Kaa hapahapa, Muadhama Kadinali" alisema huku akisogea taratibu, akatoka ofisini na kuingia kwenye korido. Akatembea haraka lakini kwa uangalifu, miguu yake ikinyata bila kutoa sauti kwenye sakafu ya marumaru.
Haraka haraka aliendelea kuzifuata sauti za watu wale kuelekea maneno ya chini hadi kwenye makutano ya korido, akapita ngazi kuu inayoelekea kwenye vyumba vya upapa. Akaingia kwenye njia ndogo ya pembeni. Hapo sauti za mazungumzo zikaongezeka.
Alipopinda kona akaona watu watatu waliovaa majoho ya mapadre wa Vatican, wakiwa wamesimama karibu na mlango mkubwa wa chuma unaoelekea kwenye moja ya hifadhi zilizofichwa za Vatican. Milango ya hifadhi hiyo ilikuwa imepambwa kwa michoro ya watakatifu, na nyuma yake kulikuwa na sehemu zinapohifadhiwa baadhi ya siri za Kanisa zilizolindwa zaidi.
Kwa sekunde chache Monsinyo Marco aliwaangalia mapadri hao, akaona kitu fulani kilikuwa kimepungua. Watu hao hawakuwa mapadre wa kawaida.
Kutoka pale aliposimama aliweza kuona mng'ao wa silaha zilizofichwa chini ya majoho yao. Akahisi pumzi yake ikimkaba kooni. Watu hawa hawakuwa hapa kwa ajili ya sala au ulinzi—walikuwa hapa kwa lengo lingine.
Akaelekeza bastola yake, moyo wake ukidunda kwa kasi. "Simameni! Kwa jina la Mtakatifu See!"
Watu wale wakapigwa na butwaa, kisha bila onyo mmoja wao akageuka ghafla, akatoa bastola kutoka kwenye joho lake na kufyatua risasi. Risasi ikapita karibu na kichwa cha Marco, ikapiga sanamu ya malaika iliyokuwa karibu nao. Vumbi la marumaru likatanda hewani wakati Marco akijificha nyuma ya nguzo
Yule mtu akacheka, kicheko cha ukatili kisicho na furaha. "Umechelewa sana. Magurudumu tayari yameshaanza kuzunguka. Huwezi kuzuia kinachokuja." Aliongea kwa kejeli.
Kabla Marco hajaamua la kufanya, mtu huyo akaingiza mkono ndani ya joho lake na kutoa silinda ndogo ya chuma iliyofichwa kwenye mkanda wake. Monsinyo Marco akakodoa macho kwa hofu alipotambua kitu kile ni nini. Bila kufikiri mara mbili, akageuka na kukimbilia mlangoni, akajitupa nyuma ya nguzo ya mawe muda mfupi kabla bomu la kutupa kwa mkono halijalipuka.
Mlupuko ulikuwa mkubwa kiasi cha kutikisa chumba hicho kwa nguvu. Vitabu na vitu vya kale vikaporomoka chini kwa kishindo na kusambaa kila mahali.
Monsinyo Marco akalala chini, masikio yake yakiwa yanauma, vumbi na mabaki vikijaza hewa. Moyo wake ulikuwa ukidunda kwa kasi alipoinuka kwa shida, akikohoa kwa nguvu kujaribu kusafisha koho na kurudisha fahamu zake. Chumba kilikuwa kimeteketezwa, lakini alikuwa amepona.
Yule mtu—mhalifu na mwenzake walikuwa wametoweka. Hakukuwa na kitu kilichobaki isipokuwa vumbi, vitabu vilivyoharibiwa, na shimo dogo lililojitokeza pale ambapo bomu lilipuka.
Marco akasogea kuelekea kwenye mlango, akiwa ameshikilia kitabu kimoja kwa nguvu kwenye mkono wake wa kuume, akili ikimzunguka. Nje ya kuta hizi, roho zenye nguvu zilikuwa zikitenda kazi, na vita ya kuilinda Kanisa—na ulimwengu—ilikuwa ndiyo kwanza imeanza.
. . .
SIKU ILIYOFUATA, jua la asubuhi lilikuwa limeupamba mji wa Vatican kwa mwanga wa dhahabu laini iliyotolewa motoni. Katika hali isiyo ya kawaida muda huu Monsinyo Marco alikuwa mbele ya lango la Maktaba ya Vatican, akizungusha macho huku na kule.
Jengo hili kubwa la mawe, lenye umri wa miaka mingi na lenye kutisha, lilikuwa limehifadhi maarifa ya milenia ndani ya kuta zake. Lakini asubuhi hii, Monsinyo Marco hakuwa akitafuta maarifa. Alikuwa akifuatilia dalili na chochote kile kitakachomsaidia kufuatilia hati iliyoibiwa kabla ya kutumiwa kwa malengo mabaya.
Matukio ya usiku uliopita yalimzidi nguvu. Mashambulizi ya risasi na bomu la kutupa kwenye chumba maalum ndani ya Ikulu ya Kipapa yalimuacha akiwa ameshangazwa, lakini hakuwa na muda wa kujiuliza maswali. Yeyote aliyepanga wizi huo alikuwa bado yuko huko nje, na tayari alikuwa na mwanzo mzuri wa safari.
Moyo wake bado ulikuwa ukimwenda mbio na mkono wake ulikuwa ukimuuma kidogo mahali alipojigonga wakati akijirusha chini. Akaunyoosha taratibu kurekebisha kola ya joho lake, akijaribu kutuliza msisimko wa adrenalin uliokuwa ukimzunguka.
Ndani ya maktaba, hewa ilikuwa baridi iliyojaa harufu ya maandishi ya kale na vumbi. Juu ya kichwa chake dari kubwa zenye miinuko zilipambwa ipasavyo, na pembeni safu baada ya safu za vitabu vya kale na magombo ya maandishi vilijaza kuta, vikionyesha historia na maarifa ya karne nyingi. Mwanga uliopenya kupitia madirisha membamba ulitupa miale ya jua juu ya sakafu za marumaru kutengeneza mandhari ya kuvutia. Mahali fulani ndani ya kuta hizi, Marco alitumaini kupata dondoo zitakazomwongoza kwenye hati iliyoibiwa.
Alitembea haraka kupitia barabara za maktaba, hatua zake zikisikika ndani ya jengo hili lenye ukimya. Alikuwa akielekea kwenye hifadhi ya siri—vyumba vya siri ambavyo hata wengi ndani ya Vatican hawakuwa wakivifahamu. Hifadhi hizi zilificha si maandiko ya kidini tu, bali pia vitu vya kale na rekodi ambazo zilionekana kuwa hatari sana kwa ulimwengu kufahamu.
Alipokaribia mlango wa hifadhi hizo, Marco akamwona Padre Ignazio, kasisi mzee aliyesimama kama mlinzi wa siri hizo. Padre huyu mwenye macho makali na mwili uliopinda kwa umri, alikuwa mlinzi wa siri za Vatican kwa miongo mingi.
"Monsinyo Marco," Padre Ignazio alimsalimu kwa nodi ya kichwa, sauti yake ikiwa nzito kutokana na umri. "Nimesikia kuhusu tukio la jana usiku. Umefika kwa ajili ya rekodi, siyo?"
Monsinyo Marco alitikisa kichwa, uso wake ukiwa umejawa na huzuni. "Nahitaji kujua kila kitu kuhusu hati iliyoibiwa—historia yake, kusudi lake, na kwa nini mtu angetaka kuua kwa ajili yake."
Padre Ignazio akapepesa macho kidogo kwa uzito wa ombi aliloambiwa. "Unatembea kwenye njia ya hatari mno, mwanangu. Kuna mambo ndani ya hifadhi hizi ambayo ni bora kubaki yamefukiwa."
"Niambie, Padre, ningekuwa na uwezo wa kuacha mambo yakiwa yamefukiwa, ningefanya hivyo. Lakini sina budi, hali niliyofikishwa nalazimika kupeta na kupembua."
Padri Ignazio akatingisha kichwa kwa huzuni, hakutaka maneno mengi. Akamruhusu Monsinyo Marco aingie kupitia kwenye lango la chuma linaloongoza kwenye hifadhi za siri. Mlango mzito ulitoa sauti hafifu wakati ukifunguka, ukifichua ngazi ndefu na nyembamba zinazoshuka chini kabisa ya jengo hilo.
Monsinyo Marco akashuka taratibu, hisia zake zote zikiwa makini. Hifadhi hizi zilikuwa zimejengwa chini ya ardhi kabisa, kwenye vyumba vilivyoundwa kuhimili mikikimikiki yote muda wote. Vatican ilikuwa imehifadhi siri zake kwa karne nyingi, na ilionekana kupitia unene wa kuta za mawe na kufuli za kisasa kwenye milango yake. Kila hatua aliyochukua kwenye ngazi hizo ilikuwa kama hatua ya kuingia zaidi ndani ya historia.
Hewa ilizidi kuwa baridi zaidi alipofika chini. Chumba alichoingia kilikuwa kimeangazwa na taa moja kubwa iliyoning’inizwa, ikitoa vivuli virefu juu ya safu za rafu na makabati yaliyojaa. Magombo ya maandiko ya kale, vifaa vya zamani, na nyaraka ziliwekwa kwa uangalifu kwenye hifadhi hii iliyojificha. Katikati ya chumba hicho kulikuwa na meza kubwa ya mbao, ikiwa laini kutokana na matumizi ya wasomi waliopita.
Monsinyo Marco hakupoteza muda. Akaanza kuchunguza rafu, akitafuta kumbukumbu zozote za hati iliyoibiwa. Haikuchukua muda mrefu kabla hajapata kile alichokuwa anakitafuta—kitabu kikubwa kilichofungwa kwa ngozi, kikiwa kimejaa vumbi. Kichwa chake, kilichoandikwa kwa Kilatini, kilimaanisha "Unabii Uliozuiwa wa Kanisa."
Moyo wake uliyeyuka alipokifungua kitabu hicho, akaanza kuchunguza kurasa za zamani kwa uangalifu. Hati hiyo iliyoibiwa ilitajwa mara kadhaa, kila mara kwa hofu, kana kwamba waandishi wenyewe waliogopa nguvu zake. Ilisemekana kuwa na maelezo ya unabii uliotabiri anguko la Kanisa na kuibuka kwa utawala mpya—utawala usioongozwa na imani, bali na udhibiti na hila.
Pumzi ya Marco ilikata alipoendelea kusoma. Hati hiyo ilikuwa imefichwa Vatican kwa karne nyingi, ikifungiwa na kikundi cha siri cha viongozi wa juu walioamini kuwa yaliyomo yalikuwa hatari sana kwa umma kujua. Ikianguka mikononi mwa watu wabaya, ingeweza kutumika kuvuruga serikali, kuchochea vita, na kuleta vurugu ulimwenguni.
Kelele zilizosikika nyuma yake zilimfanya Monsinyo Marco kushituka kidogo. Mara moja akaingiza mkono kwenye mfuko kushika bastola iliyofichwa chini ya joho lake. Asubuhi hii alibeba Glock 19 yenye risasi 16.
"Nani yuko hapo?" aliuliza kwa sauti thabiti licha ya hofu ya ghafla iliyomwingia.
Kiumbe kikatokea kutoka gizani—mtu mrefu aliyevaa joho jeusi la padri wa Vatican, lakini Marco alihisi mara moja kuwa kuna kitu kibaya. Macho ya mtu huyo yalikuwa baridi, yenye kukokota, na kulikuwa na uvimbe mdogo chini ya joho lake ambako silaha ilikuwa imefichwa.
"Monsinyo Marco," mtu huyo alisema, sauti yake ikiwa laini na ya upole kabisa. "Umeenda mbali sana."
Monsinyo Marco akashika bastola yake kwa nguvu tayari kwa kuichomoa haraka mara tu atakapolazimika kufanya hivyo. "Wewe ni nani? Unataka nini?"
Mtu huyo akatabasamu, lakini hakukuwa na joto katika tabasamu lake. "Jina langu si la muhimu. Kilicho muhimu ni maneno nitakayokwambia. Nipe kitabu hicho na uachane na uchunguzi huo uliouanza"
Monsinyo Marco akajitahidi kutulia kuficha wasiwasi uliomkaba. "Na nikikataa?" Aliuliza kwa sauti kavu.
Tabasamu la mtu huyo likapotea. Kwa haraka, akatoa bastola kutoka chini ya joho lake, akaielekeza kwenye paji la uso wa Monsinyo Marco. "Sikushauri kufanya hivyo."
Kwa muda, hakuna hata mmoja aliyesogea. Chumba kilijawa na mvutano, hewa ikawa nzito. Kila mmoja akipiga hesabu ya jambo la kufanya haraka. Monsinyo Marco alikuwa na muda wa sekunde chache tu kufanya maamuzi, na alijua kuwa hatua atakayochukua ingeweza kuamua kati ya maisha na kifo.
Kwa kasi ya ajabu, Monsinyo Marco akajitupa nyuma ya rafu ya karibu na wakati huohuo yule mtu akafyatua risasi. Risasi ikapiga ukuta wa mawe nyuma yake, vumbi la marumaru likasambaa hewani. Marco akajigeuza haraka, akatoa bastola yake na kufyatua risasi mbili kwa haraka kumuelekea yule mhalifu.
Yule mtu akajirusha nyuma ya nguzo, akaendelea kurusha risasi. Sauti za risasi zikavuma kwenye chumba hicho kidogo. Marco akaendelea kusogea, akitumia rafu na nguzo kama kifuniko, moyo wake ukidunda kwa kasi.
Alijua kuwa alihitaji kumaliza pambano hili haraka. Kadri vita vitavyochukua muda mrefu, ndivyo hatari itavyokuwa kubwa hasa kama washirika wa yule mtu wakisikia milio ya risasi na kuja kumsaidia—ukizingatia hakuwa na uhakika ni watu wangapi na au kina nani walihusika katika njama hii.
Wakati yule mtu akihama kutafuta nafasi nzuri, Marco akaiona nafasi yake. Kufumba na kufumbua, akajitupa kutoka nyuma ya nguzo na kufyatua risasi mbili Risasi moja ikampiga yule mtu tumboni, nyingine ikamuingia mguuni, akapiga kelele huku akianguka chini.
Marco akamsogelea kwa tahadhari, bastola yake akiwa amemuelekezea kichwani. "Nani amekutuma?" alimuuliza kwa sauti kali isiyo na chembe ya mzaha.
Mtu yule akacheka, kicheko cha maumivu kisicho na furaha. "Hutopata chochote toka kwangu" Alijibu kwa sauti iliyojaa ufedhuli, halafu akacheka tena.
Kabla Monsinyo Marco hajachukua hatua yoyote, mtu huyo akaingiza mkono kwenye joho lake haraka, akatoa kisu kidogo kilichokuwa kimefichwa kwenye ala iliyofungwa kwenye mkanda wake. Macho ya Marco yakapanuka kwa mshangao kuona jinsi mtu huyo alivyoshika kisu hicho kilichojikunja kama ndoano.
“Achaaa” Monsinyo Marco akapiga kelele kumzuia
Ghafla kama umeme yule mtu akapeleka kile kisu shingoni kwake, akajikata koho. Damu ikaruka toka kwenye jeraha lake kama bomba la maji lililopasuka.
Monsinyo Marco akaruka, akakimbia kuelekea mlangoni, mkono wa kuume akiwa ameshikilia bastola yake, na mkono wa kushoto amebeba kile kitabu cha ‘Unabii Uliozuiwa kwa Kanisa’. Kwa mara nyingine alishuhudia damu ikimwagika mbele ya macho yake. Mbaya zaidi hakuwa na hakika ni kwa kiasi gani damu hiyo ingeendelea kumwagika zaidi.
____________
SURA YA KWANZA
Ilikuwa imeshatimia saa tatu na nusu asubuhi, muda ambao kwa kawaida humkuta kepteni Eddy Kashe akiwa kwenye pilikapilika nyingi; lakini siku hii ilikuwa ya tofauti sana. Pamoja na kusoma barua pepe za siku mbili, na kupitia kitabu chake cha kumbukumbu za kila siku, hakuona jambo lolote la kusisimua.
Akanyanyua simu yake ya mkononi, akaangalia kwa makini kuona kama kuna ujumbe wowote unaohitaji kupewa kipaumbele. Bado, hakuona lolote la maana. Siku hii ilianza kwa utulivu, bila makeke hata kidogo.
Kama ungemuona asubuhi hii bila shaka ungempenda kwa jinsi alivyoumbika kiume hasa. Mrefu kiasi cha futi sita inchi moja, si mnene wala si mwembamba. Mwili wake ulijengeka vyema kutokana na mazoezi ya nguvu aliyofanya tangu alipokuwa mdogo. Uso wake wa duara na macho ya ujanjaujanja ulificha umri wake wa miaka therathini na miwili. Ngozi yake ya maji ya kunde, nywele zinazotunzwa vizuri na sharubu nyeusi zilizochongwa vyema vilikuwa vivutio kikubwa kwa mabinti wa mjini wanaowinda vijana wenye pesa. Asubuhi hii Eddy alivalia shati jeupe, suruali ya kijivu na viatu vya ngozi nyeusi vilivyotengenezwa na Salvatore Ferragamo.
Kwa muda aliendelea kuichokonoa simu yake kuperuzi mitandao ya kijamii hadi alipokinai. Akaweka simu mezani, akavuta faili moja kati ya manne yaliyopangwa upande wa kushoto wa meza yake. Akalifungua, na kulikodolea macho kwa sekunde chache. Halafu ghafla, kama mtu aliyekumbuka kitu fulani akalifunga. Akanyoosha mkono wake wa kulia kuvuta gazeti la Mizani lililokuwa kwenye mtoto wa meza. Akalifungua, akalitandaza mezani, akaanza kusoma habari iliyoandikwa kwenye ukurasa wa mbele.
Jana majira ya saa tano na dakika ishirini asubuhi, majambazi wenye silaha walimuua kwa kumpiga risasi mwenyekiti wa bodi ya mafuta ya petroli nchini (TPDC) Brigedia Jenerali mstaafu Shabani Nyoni na walinzi wake wawili, Sajenti Abdallah Kombo na Koplo John Didi wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ). Watu wengine wanne walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitali ya Muhimbili. Taarifa kutoka makao makuu ya jeshi la Polisi zimeeleza kuwa, majambazi hao walivamia benki ya Taifa ya Biashara (NBC) City Branch na kupora shilingi milioni 300 za kitanzania, dola 25,000 za kimarekani na hazina mbalimbali za wateja zilizohifadhiwa kwenye visanduku binafsi. Jeshi la polisi linaendesha msako mkali kuwatafuta wahalifu hao. Shirika la mafuta ya petroli Tanzania limetangaza zawadi ya shilingi milioni 50 kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa majambazi hao. Eddy alimalizia kusoma sentesi ya mwisho huku akitingisha kichwa kwa masikitiko.
Hii ilikuwa mara yake ya tano kusoma habari hii, lakini kila alipoisoma ilimchoma moyo kana kwamba ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza. Tukio lenyewe lilitokea siku tatu zilizopita na kuandikwa kwenye gazeti la siku iliyofuata. Kwa Eddy ilikuwa Habari nzito kwa sababu ilimhusu Brigedia Nyoni na wanajeshi wengine wa Jeshi la wananchi wa Tanzania. Watu aliowajua vyema.
Katika maisha yake Brigedia Nyoni alishika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwa pamoja na katibu mkuu kiongozi, Waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga Taifa (JKT) na mshauri wa rais wa mambo ya usalama. Kabla ya kuteuliwa kushika nyadhifa hizo za kisiasa jenerali huyo alikuwa mkuu wa brigedi ya Faru ya JWTZ.
Eddy alikuwa na uhusiano wa kipekee sana na brigedia huyu aliyezoea kumuita kwa jina la utani ‘Golong’ondo.’ Kwa mara ya kwanza walikutana 92KJ Ngerengere alipokwenda kwenye mafunzo ya awali ya ukomando. Wakati huo Shabani Nyoni akiwa na cheo cha Luteni kanali ndiye aliyekuwa mkuu wa kikosi. Makomando wote walimpenda na kumheshimu kwa mtindo wa uongozi wake, na hasa kwa jinsi alivyowathamini wapiganaji wake.
Alipomaliza mafunzo ya ukomando, Eddy alichaguliwa kujiunga na chuo cha uongozi Monduli, na baadae akahamishwa kikosi. Hata hivyo aliendelea kuwa na mawasiliano ya karibu na kamanda Nyoni akimchukulia kama mshauri wake mkuu.
Mawasiliano yao yalipungua kidogo baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Brigedia Nyoni kushika nyadhifa za kisiasa na hivyo kuachana na operesheni za kijeshi. Kwa muda mfupi Brigedia huyo alipanda na kuwa mtu mwenye ukaribu zaidi na Rais, na mshauri mwenye nguvu kuliko mtu yeyote nchini.
Jambo lililomshitua na kumkera Eddy ni kule kuongezeka ghafla kwa matukio ya uhalifu mkubwa nchini. Hili lilikuwa tukio la tatu katika kipindi cha mwezi mmoja. Wiki tatu kabla ya tukio hili majambazi wenye silaha za kivita walimvamia Waziri wa sheria na Katiba, wakamuua kwa kumpiga risasi na kupora gari lake aina ya Toyota Landcruiser alilokuwa amepanda. Polisi walijaribu kuwatafuta majambazi hao lakini hawakuweza kuwapata.
Siku kumi baada ya tukio hilo majambazi walimuua kwa kumpiga risasi afisa mwandamizi wa idara ya Usalama wa Taifa anayesimamia operesheni za kificho bwana Magnusi Lime na kumpora gari lake aina ya BMW X1 xDrive 28i.
Tukio hili lilisababisha mshituko mkubwa zaidi kwa sababu majambazi hao walimvamia afisa huyo mchana kweupe, akiwa kwenye maegesho ya ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, sehemu yenye ulinzi wa kuaminika kabisa. Hata hivyo polisi hawakuweza kuwatambua wala kuwakamata.
Matukio haya yalimsumbua sana Eddy kwa sababu uzoefu wake ulimuonesha wahalifu hawa hawakuwa wa kawaida. Majambazi wa kweli hufanya uhalifu wa haraka, na kutoweka kimyakimya bila kuua ili kupunguza uwezekano wa askari kuwafuatilia kwa muda mrefu. Kinyume chake majambazi hawa walikuwa wakifanya mauaji yasiyo ya lazima jambo lililomfanya ahisi walikuwa na sababu nyingine isiyojulikana.
Wakati akiendelea kutafakari habari hiyo mlango wa ofisi yake ukafunguliwa. Stella, katibu muhtasi wake akaingia huku akitabasamu.
Stella ni msichana wa kupendeza sana. Mrefu kiasi cha futi tano inchi sita, mwembamba, mwenye umbo la kuvutia. Ngozi yake laini ya maji ya kunde ilimfanya aonekane kama mwana mitindo. Nywele zake ndefu, nyeusi tii aliweza kuzichana kwa mtindo wowote autakao. Leo hii alizibana kama mkia wa farasi.
Macho yake makubwa yaliyolegea kama binti aliyekula kungumanga yalivutia kiasi cha kuweza kumfanya bosi yeyote mwenye uhanga kumpa talaka mkewe ili aweze kuishi na binti huyu. Lakini si Eddy, mtu mwenye kujiheshimu na kufuata maadili ya kazi.
Asubuhi hii Stella alivalia sketi fupi ya rangi nyeusi, blauzi ya mikono mifupi yenye rangi ya poda na viatu vyeusi vyenye kisigino kirefu.
“Samahani bosi” Stella aliomba radhi huku akitembea taratibu kuelekea mezani kwa Eddy.
“Bila samahani Stella. Vipi, kwema?
“Kuna barua hii nimeipokea sasa hivi toka kwa mfanyakazi wa posta, inaonekana ni ya haraka” Alisema huku akimpa bahasha kubwa ya rangi nyeupe iliyotengenezwa kwa karatasi ngumu.
Eddy akaipokea na kuiangalia kwa makini. Upande wa mbele yalichapwa maandishi makubwa ya rangi ya bluu yaliyosomeka Expedited Mail Service. Pembeni uligongwa muhuri wa rangi nyekundu ulioonesha barua hiyo ilitumwa toka Mwanza.
“Ahsante Stella. Tafadhali keti nikupe maagizo kabla sijatoka humu ofisini” Eddy alisema huku akijiweka vizuri kwenye kiti alichokalia nyuma ya meza kubwa iliyotengenezwa kwa mbao za mninga.
Stella akatupa jicho lake kwa chati kuangalia mezani. Hakukuwa na kitu chochote kipya. Katikati ya meza kulikuwa na skrini mbili za kompyuta ya mezani aina ya Dell zilizounganishwa katika mtandao mmoja. Pembeni ililala kompyuta mpakato aina ya Apple MacBook Air. Upande wa kushoto yalipangwa mafaili kadhaa yanayosubiri kushughulikiwa. Kulia yaliwekwa magazeti ya siku hiyo, na mafaili machache yaliyo katika hatua ya mwisho ya uchunguzi. Nyuma ya kiti alichokalia Eddy kulikuwa na rafu kubwa iliyopangwa vitabu vya aina na lugha mbalimbali
Kwa muda wa miaka mitatu na nusu Stella amekuwa akifanya kazi ofisini kwa Eddy akiwa katibu muhtasi wake. Kampuni yao hushughulika na uandishi wa habari za kipelelezi na uchapishaji wa gazeti la wiki liitwalo Mizani. Ofisi yao iko katikati ya jiji la Dar es Salaam kwenye jengo la IPS lililo mkabala na sanamu ya askari
Gazeti hili hutoka kila siku ya Jumapili likiwa limesheheni habari za kipelelezi zinazohusu matukio ya kushitua moyo, kashfa za viongozi wa serikali na wafanyabiashara wakubwa, taarifa za uchunguzi wa kesi za jinai zilizotelekezwa au kushindikana, na makala mbalimbali za kuelimisha jamii kuhusu haki na wajibu wao kisheria. Jina ‘Mizani’ lilitokana na kauli mbiu ‘Mizani ya haki’ iliyojipatia umaarufu kwa wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu.
Mwanzilishi wa gazeti hili alikuwa marehemu inspekta Godfrey Hatibu, afisa mstaafu wa jeshi la polisi. Huyu aliliendesha kwa miaka miwili tu kabla ya kuuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Kifo chake kilileta taharuki kubwa kwa wananchi. Wengi waliamini kifo hicho kilitokana na njama zilizopangwa na viongozi wa juu serikalini waliochukizwa na jitihada za inspekta Hatibu katika kupinga maovu. Viongozi hao walikanusha uvumi huo kwa nguvu na kusisitiza kwamba marehemu inspekta Hatibu aliuawa kwa njama zilizopangwa na wafanyabiashara wa madawa ya kulevya aliokuwa akiwaandika mara kwa mara magazetini kiasi cha wananchi kushinikiza watu hao kukamatwa na kufunguliwa mashitaka.
Viongozi wa chama tawala wao walimlaumu mkuu wa jeshi la polisi kwa kutompa ulinzi inspekta Hatibu, hasa baada ya gazeti lake kuandika habari zilizosaidia kusambaratishwa kwa mtandao mkubwa wa madawa ya kulevya nchini. Kauli hiyo ilileta mkanganyiko mkubwa kwa sababu ilipingana na taarifa iliyotolewa na jeshi la polisi ambayo ilidai marehemu inspekta Hatibu aliuawa na majambazi waliovamia nyumbani kwake kwa lengo la kupora fedha na vitu vingine vya thamani.
Baada ya kifo cha inspekta Hatibu ndipo Eddy aliponunua hisa zote za kampuni ya Mizani. Uamuzi huo ulisukumwa kwa kiasi kikubwa na mtafaruku uliojitokeza kwenye familia kuhusu mrithi halali wa mali za marehemu. Kwa bahati mbaya inspekta Hatibu hakuwa na mke wala mtoto anayetambulika kisheria, jambo lililoongeza ugumu wa mambo. Ili kuepusha mgogoro mahakama iliteua msimamizi wa mirathi na kuamuru mali zote ziuzwe ili kila anayestahili apewe haki yake.
Kwa kuwa wakati huo Eddy ndiye aliyekuwa mhariri mkuu, mkurugenzi wa fedha na mmiliki wa asilimia 25 ya hisa za kampuni, akaona bora anunue hisa zilizobaki kuliko kuacha zinunuliwe na mtu asiyejua malengo ya msingi ya gazeti hilo. Ndipo akachukua mkopo benki na kulipia asilimia 75 ya hisa zilizokuwa mikononi mwa marehemu inspekta Hatibu.
Kwa bahati mbaya kifo cha inspekata Hatibu kilirudisha nyuma sana umaarufu wa Mizani. Baadhi ya waandishi nguli, wapelelezi maarufu, na wataalam wengine walikimbia kwa kudhani bila inspekta Hatibu hakuna lolote la maana litakaloweza kufanyika. Hili halikumshangaza Eddy, kwani wafanyakazi wengi walimuona inspekta Hatibu kama Fidel Castro wa Cuba, pasipo yeye hakuna mwingine.
Ni katika kipindi hiki Eddy alipouona umuhimu wa Stella. Binti wa watu alimsaidia kwa kila hali kuhakikisha Mizani halipotezi umaarufu wake. Alifanya kazi kwa bidii, mara nyingine mpaka usiku wa manane, tena bila kudai malipo ya muda wa ziada. Baada ya miezi sita ya ubunifu na jitihada kubwa umaarufu wa Mizani ukarudi na kuongezeka mara dufu. Ndipo sasa waandishi wengine wakaanza kukimbizana kutaka kujiunga na Mizani.
Ni kwa sababu hii Eddy huwiwa kumheshimu binti huyu kipekee na kumchukulia kama dada yake wa tumbo moja, japokuwa mara nyingine binti wa watu huonesha dalili za kutaka kuvuka mipaka. Pamoja na kukubaliana na ile nahau ya kiswahili isemayo ‘paka huwa hakatai maziwa’ kwa binti huyu Eddy alilazimika kujifunga kidhibiti mwendo, ili asiharibu kazi.
“Kuna ile kesi ya Makhan, yule mfanya biashara mwenye asili ya kihindi anayetuhumiwa kuua familia yake yote, na kujaribu kujiua kwa kujipiga risasi. Je! umepata lolote kutoka kwa kile chanzo chetu? Eddy alimuuliza Stella huku akimkazia macho.
“Ndiyo. Amesema ataleta taarifa kamili leo kabla ya muda wa chakula cha mchana. Kama ujuavyo yule bwana huwa hamwamini mtu yeyote isipokuwa wewe tu. Hata hivyo, nilipoongea naye alikuwa na furaha mno kiasi cha kunidokeza kwamba anao ushahidi wa kutosha kuthibitisha kuwa Makhani hakufanya yale mauaji. Amebambikizwa ile kesi kwa sababu anazozijua.”
“Mh! Ana ushahidi wa kutosha? Maana hii kesi ni ngumu mno, kila mtu anaitegea sikio”
“Amesema amepata mkanda wa video wenye ushahidi wa kutosha kumaliza kesi”
“Huo mkanda wa video ulirekodiwa na mtu au kamera ya usalama? Isije ikawa mambo ya AI?”
“Sina hakika, lakini kwa jinsi maelezo yake yalivyokuwa inaelekea kuna mtu aliyerekodi tukio hilo kwa simu ya mkononi. Sijui huyo mtu ni nani, alikuwa wapi, na ilikuwaje hata akaweza kurekodi tukio la kutisha vile. Maana anadai tukio lote, toka mwanzo hadi mwisho limo kwenye klipu ya video hiyo”
“Safi sana. Vipi John nae, amefikia wapi? Sikutaka kuuliza habari zake kwenye postmortem maana hakuwepo”
“Amekwenda kufuatilia taarifa ya yule kanali wa jeshi anayetuhumiwa kushirikiana na mabwana wa vita kuuza silaha kwa wapinzani wa serikali ya Kongo”
“Vizuri sana” Eddy alijibu akiwa ameridhishwa na maelezo ya Stella. Basi akachukua kisu cha mpingo, akafungua bahasha aliyopewa. Wakati akifanya hivyo ghafla ukasikika mlipuko mkubwa uliotingisha jengo zima huku ukienda sambamba na kukatika kwa umeme.
“Vipi tena?” Eddy aliuliza kwa mshituko kidogo.
“Usishituke bosi, ni hilo transfoma la umeme hapo nje, naona limelipuka tena. Sisi tumeshalizoea! Leo ni mara ya nne katika kipindi cha wiki mbili linalipuka kwa kishindo na kukata umeme”
“Wenyewe wana habari?
“Wanajua kwamba halifai. Kila likilipuka huwa wanakuja kulichokonoa mpaka linatengemaa, lakini baada ya siku mbili au tatu linalipuka tena. Cha ajabu transfoma lenyewe inadaiwa ni jipya, lilifungwa miezi michache tu iliyopita, kipindi ulipokuwa safarini Singapore.”
“Ukiona hivyo afisa maduhuli aliyelinunua amejenga Mbezi Beach kama siyo Oystebay”
“Ndiyo Tanzania yetu” Stella lisema huku akitingisha kichwa kwa masikitiko.
Maneno hayo yalimuingia Eddy moyoni kama mwiba maana yalijaa ukweli usiopingika. “Inasikitisha kuona hata baada ya nusu karne ya kujitawala bado watu wetu hawatambui na kuthamini maana ya uhuru kamili. Wengi wanajali kujaza matumbo yao na familia zao bila kufikiria uhai na maslahi ya taifa zima” alifikiria.
Mawazo hayo yalimfanya aende mbali zaidi, miaka ya 1970 wakati marehemu Edward Mondrane alipouawa kwa bomu la barua lililotumwa na majasusi wa Kireno. Akajiuliza Msumbiji ingekuwaje leo hii kama Mondrane na Samora Machel wangekuwa bado wakiishi? Hakika Afrika imepoteza mashujaa wengi sana! Alijiambia.
Wakati Stella akinyanyuka kufungua madirisha ya vioo kuruhusu hewa iingie ndani, taa na viyoyozi vikawaka. Mafundi wa Mizani walikuwa wamewasha jenereta ya umeme. Eddy akatabasamu kwa furaha. Watu wake walikuwa hodari, waaminifu, wazalendo na wenye moyo wa kujituma hasa.
Ndani ya bahasha kulikuwa na tiketi moja ya shirika la ndege la Tanzania (ATC) inayofaa kusafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na kurudi. Iliandikwa jina Eddy Kashe. Kwa jinsi tiketi yenyewe ilivyokuwa ilionesha wazi kwamba ilinunuliwa mtandaoni, kwenye website ya Air Tanzania na kuchapwa kwenye karatasi ya kawaida. Jambo hili lilimshangaza kidogo, kwani hakuwa amepanga kwenda Mwanza.
Pamoja na tiketi hiyo, ndani ya bahasha kulikuwa na karatasi nyingine nzito, ya rangi ya maziwa iliyokunjwa vizuri kuhifadhi nyaraka nyingine ndani yake. Eddy akaifungua taratibu kuona kilichomo. Akashituka kuona ni fedha za kigeni, dola mia mia za Marekani.
Akainua macho kumtazama Stella aliyekuwa ameketi mbele yake. Macho yao yakagongana maana naye alikuwa akimuangalia kwa mshangao. Kuona hivyo hakusema neno, akazitoa zile fedha, akaziweka juu ya meza, pembeni ya bahasha, akaelekeza macho yake kwenye ujumbe ulioandikwa kwenye karatasi iliyotumika kufungia fedha. Ulikuwa ujumbe mfupi ulioandikwa kwa kalamu ya wino mwekundu:
“Eddy, hudhuria misa ya watakatifu wote itakayofanyika siku ya Ijumaa tarehe moja, Novemba saa moja kamili asubuhi, kwenye kanisa kuu la Epifania Bugando Mwanza. Usikose”
Viaticum
Kwa sekunde kadhaa Eddy alibaki ameduwaa, akiukodolea macho ujumbe ule kana kwamba ulikuwa haueleweki.
“Vipi bosi, mbona umepigwa na butwaa?” Stella aliuliza baada ya kumuona akiendelea kuikodolea macho karatasi ile bila kusema lolote. Eddy hakumjibu, akanyoosha mkono kumpa ile karatasi ili ajisomee mwenyewe. Stella akaipokea na kuiangalia kwa makini.
“Bosi, mbona huu ujumbe unaeleweka? Aliuliza kwa mshangao huku akimrudishia karatasi hiyo.
“Unaeleweka vipi wakati hauna jina kamili, anuani ya mwandishi, wala sababu za kunifanya niache shughuli zangu kwenda Mwanza?
“Uko sahihi bosi, hata hivyo hilo haliondoi ukweli kwamba yaliyomo humo yanajitosheleza.”
“Una maana gani?”
“Ujumbe huu unakutaka uhudhurie misa ya watakatifu wote inayofanyika mjini Mwanza tarehe moja Novemba ambayo ni kesho kutwa. Hili halina mjadala kwani kila tarehe moja ya mwezi Novemba kanisa katoliki huadhimisha siku ya watakatifu wote duniani. Kwahiyo uwepo wa misa hiyo ni jambo lisilo na shaka”
“Hilo nafahamu Stella”
“Sasa kwa nini unashituka? Kuna ajabu gani mtu kukualika kuhudhuria misa ya watakatifu wakati wewe ni mkristo? Isitoshe mtu aliyekutumia mwaliko huu pia amekutumia tiketi ya ndege, itakayokuwezesha kwenda Mwanza kesho jioni, ambayo ni siku moja kabla ya misa yenyewe, na kurudi Dar es salaam siku inayofuata baada ya misa. Sasa tatizo liko wapi hapo? Zaidi ya yote mtu huyo amekutumia pesa za kutosha kwa matumizi ya safari. Tena katika dola! Huoni kama huyu ni mtu wa maana sana kwako?” Stella alieleza kwa upole na ufasaha mkubwa kama vile mama anayembembeleza mwanawe anayeugua maralia akubali kuchomwa sindano.
“Dada yangu, hayo uliyosema yote niliyafikiria mara tu baada ya kusoma huu ujumbe. Tatizo leo ni Jumatano na misa yenyewe ni Ijumaa asubuhi. Ina maana kwa ratiba aliyonipangia huyu mtu asiyejulikana itanilazimu nipoteze masaa zaidi ya 72 ya kazi kwa ajili ya kuhudhuria misa hiyo tu. Usisahau kwamba muda wetu ni wa muhimu sana, hasa katika kipindi hiki ambacho matukio ya uhalifu yanajitokeza mfurulizo.” Eddy aliongea kama anajitetea.
“Bosi, mimi naamini mtu aliyekutumia mualiko huu analijua hilo. Ndiyo maana akakutumia fedha za kutosha kufidia muda wako na pia kulipia gharama nyingine zinazoweza kujitokeza kwa sababu ya safari hiyo” Stella alisisitiza ingawa kwa sauti ya upole.
Maneno hayo yakamkumbusha Eddy zile dola zilizokuwa pale mezani. Akaziinua na kuziangalia tena kwa makini, kuhakikisha si fedha bandia. Alipojiridhisha akaanza kuzihesabu kwa kutupia noti moja moja mezani. Zilikuwa jumla ya noti 55 sawa na dola 5,500 za kimarekani. Akaziweka mezani, akamgeukia Stella.
“Najaribu kujiuliza huyu mtu ni nani? Ana jambo gani? Na kwa nini amenitumia fedha zote hizi?” Eddy aliuliza huku akimwangalia Stella machoni.
“Inawezekana ni rafiki yako wa zamani, ndugu, classmate, au mtu uliyewahi kumsaidia jambo fulani huko nyuma lakini kwa sababu za kimaisha mkapotezana. Au pengine ni mpenzi wako wa zamani ndiyo maana hataki kujitambulisha ili mtakapoonana iwe furaha zaidi. Mambo ya suprize hayo!” Stella alijibu huku akimuangalia Eddy kwa macho ya wivu kidogo.
Eddy akaangua kicheko.
“Hilo linawezekana, na wala haitakuwa ajabu.” Eddy alisema huku akiendelea kucheka. “Upo pia uwezekano kwamba mtu huyu ana taarifa nzito anayotaka kutupa au kututaka tuichunguze; maana hiyo ndiyo kazi yetu hasa. Lakini swali ninalojiuliza ni lilelile, kwa nini atangulize kutoa pesa nyingi namna hii? Anataka kuninunua au kuninyamazisha?
“Kwanini unafikiria hivyo bosi?”
“Kwa sababu Mizani ina marafiki wengi, na maadui wengi pia. Kwa bahati mbaya marafiki zetu wengi ni watu wanyonge, wasiokuwa na uwezo mkubwa wa kifedha; lakini asilimia kubwa ya maadui zetu ni watu wakubwa serikalini na matajiri. Watu ambao kiu yao ni kuhujumu uchumi wa nchi na kuivuruga serikali yetu tukufu ili mradi wapate maslahi binafsi.”
“Hilo nalijua bosi”
“Ndiyo maana najiuliza mara mbili mbili, isije kuwa ni mtego wa kuniingiza kwenye kundi la wahalifu, au kujaribu kunibambikizia kesi ya rushwa. Hebu fikiria watu wa taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa wakituvamia ghafla muda huu, wakadai pesa hizi tumelipwa baada ya kumtishia kigogo fulani kwamba tuna stori yake tutamlipua gazetini! Si tutakuwa kwenye shida?”
“Mh! Bosi usemayo ni kweli, tumezungukwa na maadui kila upande. Tena nikikumbuka kifo cha inspekta Hatibu ndiyo huwa naishiwa nguvu kabisa. Lakini pamoja na hilo najaribu kufikiria kwa upande mwingine, upendo wa huyo mtu. Kwa maana kama ni rafiki au mtu mliyepotezana kitambo kaamua kuku-suprize kwa kukutumia tiketi ya ndege na hizo dola ili uhudhurie hiyo misa muweze kuonana, halafu usiende, itakuwa mbaya sana. Utakuwa umemdhulumu furaha yake.”
“Uko sahihi Stella, maana hatuna namna ya kumrudishia fedha zake. Kama unavyoona hii bahasha haikuandikwa jina la mtu aliyetuma. Sehemu ilipotakiwa kujazwa jina la mtumaji ameandika jina langu kinyume. Hii ina maana mtu huyo hakutaka ajulikane abadan, na pia ana hakika lazima nitaitikia wito wake”
“Sawa kabisa bosi. Tangu mwanzo hisia zangu zinanisukuma kuamini huyu ni mtu anayekujua vyema. Anajua wewe ni mtu unayeishi kwa kufuata kanuni na maadili; hivyo si rahisi uchukue dola 5,500 kisha utokomee gizani. Ana uhakika wa asilimia tisini na tisa kuwa utaitikia mwito wake. Na hata kama usipoenda, basi mtu huyo yuko tayari kupoteza fedha zake kwa ajili yako. Kwa kifupi huyu si mtu wa kawaida”
“Kweli kabisa. Hicho ndicho kitu kinachonifanya niamini kuwa huyu si rafiki wa kwenda naye club au casino kucheza kamali. Huyu ni muungwana mwenye taarifa nzito anayotaka tuifanyie kazi, au adui mwerevu anayetaka kuniingiza mtegoni. Yote mawili yanawezekana, ingawa sasa naanza kulipa uzito zaidi jambo la kwanza” Eddy alihitimisha.
“Kwa hiyo utakwenda?
“Hebu subiri kidogo” Eddy alijibu huku akinyanyua simu yake ya mkononi toka juu ya meza. Akabonyeza namba kadhaa, kisha akaiweka sikioni kusikiliza wimbo uliokuwa ukichezwa upande wa pili wakati simu ikiita.
“Niambie bosi wangu” Sauti nyororo ya msichana iliita. Binti huyu alikuwa mfanyakazi wa shirika la ndege la Tanzania upande wa tiketi. Ofisi yake ilikuwa kwenye uwanja wa ndege wa Julius Nyerere. Alikuwa mmoja wa watu muhimu na wa karibu sana na Mizani. Licha ya kusaidia kufanya booking za ndege pale zinapojitokeza safari za haraka, pia alikuwa mtoa habari muhimu.
“Habari za leo, Prisca?
“Poa tu mtu wangu, kwema?
“Kwema kabisa, mzee hajambo?
“Hajambo, niambie?
“Nataka kuthibitisha kama kesho mna safari ya kwenda Mwanza”
“Tutakuwa na safari mbili, moja asubuhi na nyingine jioni, lakini ndege zote zimeshajaa?
“Nimekatiwa tiketi na mpenzi wangu mpya, unaweza kuangalia kama jina langu lipo kwenye orodha ya wasafiri?
“Nimeshaangalia, upo ndege ya jioni”
“Hapo ndipo unaponikosha. Uko sharp sana. Ahsante kwa msaada wako”
“Usijali mpenzi wangu, ila usisahau kuja kuniaga na ukirudi toka Mwanza usisahau kuniletea sato wabichi na dagaa waliokaangwa” Prisca alitania.
“Mbona unaagiza kabisa wakati umesema nije kukuaga? Au hutaki jirani zako wasikie?
“Naogopa kuwahiwa”
“Tuliza moyo, mimi ni wako” Eddy alimtania
“Poa baadae basi”
“Baadae” Akakata simu
Eddy akaweka simu mezani, akamgeukia Stella.
“Tiketi iko sawa, huyu mtu hatanii”
“Kwa hiyo utakwenda?
“Ndiyo, nitakwenda. Nilitaka nithibitishe uhalali wa tiketi kabla ya kukupa jibu”
“Kama unaogopa kwenda peke yako naweza kukusindikiza bosi wangu” Stella alisema huku akirembua macho yake makubwa sambamba na tabasamu la kumtoa nyoka pangoni.
“Hapana mama, utanitia wazimu wa mapenzi. Wewe inabidi ubaki hapa kuhakikisha Mizani linapendeza kama kawaida yake”
“Yaani bosi kila nikikwambia tusafiri wote unanikatalia, kwa nini lakini?” Alilalamika
“We mtoto unaweza kunifanya niuze nyumba yangu kwa hasara kwa ajili yako. Ndiyo maana nakuogopa”. Eddy alijibu kwa utani huku akicheka. Akanyanyua zile fedha toka mezani, akazifunga kwenye karatasi kama zilivyokuwa alipozipokea, akazirudisha kwenye bahasha “Chukua hizi fedha pamoja na ujumbe tulioupokea, kafungie kwenye sanduku lako la chuma. Acha zikae humo mpaka nitakaporudi kutoka Mwanza”
“Bosi, mbona unanitisha tena?”
“Ni tahadhari tu. Sitaki tuzitumie hizi fedha mpaka tutakapojua zimetoka wapi, na sababu iliyomfanya huyu mtu aniite huko Mwanza. Kama mambo yakienda sawa itakuwa kheri, vinginevyo itabidi tumrudishie pesa zake. Tena kama alikuwa akijaribu kunipa rushwa kwa sababu yoyote ile nitamfikisha kwenye vyombo vya dola”
“Sawa bosi, hilo hata mimi naunga mkono” Stella alijibu kwa furaha. Akainuka toka kwenye kiti alichokalia, akajitengeneza vizuri sketi yake kwa kuivuta chini na kuinyoosha sehemu ya nyuma kwa viganja vya mikono yake, kisha akainyanyua ile bahasha.
“Sijui kwa nini kila nikiukumbuka ujumbe tuliousoma nywele zangu zinanisisimka! Nahisi safari yako itakuwa na mambo mazito yatakayofanya Mizani liwe na thamani kubwa kiasi cha kuuzwa kwa dola kama sio paundi za kiingereza” Stella aliongea kwa hisia.
“Hata mimi naamini hivyo, tuombe uzima tu”
“Mungu ni mwema atakulinda bosi, maana sisi tunafanya kazi ya kitume japo kwa namna tofauti sana”
“Amen, uko sahihi lakini bado tunapaswa kuchukua tahadhari zote. Mungu ametupa akili na utashi”
“Hilo nakubali asilimia mia moja”
“Ndiyo maana nakwepa kusafiri nawe Stella”
Stella hakujibu, akabinua midomo yake kwa kejeli, akageuka na kuondoka taratibu huku akitingisha sehemu ya chini ya kiuno chake.
____________
SURA YA PILI
Kengele ya saa iliyokuwa ikiendelea kugonga mfululizo ndiyo iliyomzindua Eddy toka kwenye lepe zito la usingizi. Akafumbua macho na kuyatupa moja kwa moja mahali alipoiweka saa hiyo. Japokuwa chumba kilikuwa na mwanga hafifu aliweza kusoma majira bila tatizo. Ilikuwa imeshatimia saa kumi na moja na robo alfajiri. Akanyoosha mkono wake wa kulia, akazima kengele kisha akarudisha saa mahali ilipokuwa.
Saa hii aina ya Omega alipewa na rafiki yake aitwae Mutebi, raia wa Uganda, alipokwenda huko kwa shughuli maalum. Kwa bahati mbaya rafiki yake huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana mwezi mmoja tu baadae. Tangu wakati huo akawa akiitunza saa hii kwa heshima na ukumbusho wa Mutebi, na kuivaa mara chache tu anapokwenda kwenye shughuli maalum.
Baada ya kuweka saa pembeni akanyanyua simu yake ya mkononi, akaangalia kama kuna ujumbe wowote ulioingia. Jumbe zaidi ya ishirini zilikuwa zimeingia. Hata hivyo hakukuwa na ujumbe wowote uliohitaji kushughulikiwa haraka.
Akaweka simu pembeni. Akateremka toka kitandani, akatembea hadi pembeni ya chumba mahali lilipo kabati dogo lililojengewa ukutani. Akafungua milango na kutoa sanduku lake. Akalifungua, akatoa mfuko mdogo wa plastiki aliotumia kuhifadhi nguo zake za kufanyia mazoezi ya karate, wenyewe huziita Gi. Akazivaa, na kujifunga mkanda kiunoni mwake.
Ilikuwa kawaida yake kufanya mazoezi ya karate kila siku alfajiri, kabla ya kuoga na kuanza pilikapilika za siku. Tabia hiyo ilimsaidia sana kulinda heshima ya mkanda mweusi wa Goju-ryu alioupata miaka mingi iliyopita. Eddy alizingatia sana utaratibu huu aliofundishwa na sensei wake alipokuwa na mkanda mweupe. Sensei huyo alimwambia “Mafunzo hayana mwisho. Siku utakayoacha mazoezi na ujuzi ulioupata nao utakuacha taratibu” Maneno hayo yalimkaa vyema kichwani kwake, na ndiyo hasa yaliyomtia moyo kuendelea na mafunzo hadi kupata mkanda mweuzi dani (degree) ya nne.
Baada ya kuweka kila kitu sawa ndipo alipogundua tatizo lililomkabili. Chumba kilikuwa kidogo kuliko kilivyokuwa kikionekana. Hii lilisababishwa na jinsi samani zilivyokuwa zimepangwa ndani humo. Likamjia wazo la kwenda kufanyia mazoezi nje, lakini akaona haitakuwa busara kwani hakuwa nyumbani kwake; bali kwenye moja ya hoteli maarufu mjini Mwanza.
Aliwasili mjini hapa saa kumi na moja jioni ya siku iliyotangulia, kwa ndege ya shirika la ndege la Tanzania. Ndege hiyo iliondoka Dar es Salaam saa kumi jioni na kutua Mwanza saa kumi na moja. Kwa vile hakuwa na mwenyeji wa kumpokea uwanja wa ndege, akachukua taksi na kumuagiza dreva ampeleke Omni Hoteli iliyoko eneo la Kapripointi. Walipofika, dereva huyo aliyejitambulisha kwa jina la Frank akampa namba yake ya simu na kumtafadharisha amtafute muda wowote atakapohitaji usafiri. Kwa vile Eddy hakuwa na safari yoyote jioni hiyo, akamwambia amfuate saa kumi na mbili na nusu asubuhi ya siku ya pili, kumpeleka kanisani.
Baada ya kufikiri kwa sekunde chache Eddy akaona hana sababu ya kwenda nje, au kuahirisha ratiba ya mazoezi kwa sababu ya udogo wa chumba. Akaamua kufanya mazoezi ya viungo kwa wa nusu saa, akakaa kwenye tafakari (meditation) kwa robo saa, kisha akainuka kucheza kata iitwayo sanchin. Alipomaliza kata hiyo akajinyoosha viungo tena kisha akaingia bafuni kuoga.
Alitumia muda mrefu kujimwagia maji ya moto kuondoa uchovu. alipomaliza akatoa nguo alizoziandaa kwa ajili ya siku hiyo: suti nyeusi, shati jeupe, tai nyekundu na viatu vya ngozi nyeusi. Alichagua nguo hizi makusudi kumuonesha mtu aliyemualika jinsi alivyoithamini siku hii.
Kwa wakatoliki rangi nyeusi huwakilisha msiba na maombolezo. Rangi nyekundu huwakilisha damu ya watakatifu iliyomwagika katika kumtangaza Kristo, na rangi nyeupe ni ishara ya utakatifu wanaopokea waaminio kwa neema na msamaha wa dhambi katika Kristo Yesu.
Alipomaliza kuvaa akajipulizia marashi, akaweka vitu sawa, akafunga sanduku na kulirudisha kabatini. Ndipo akatoka chumbani na kufunga mlango.
Mapokezi alimkuta mhudumu aliyempokea na kumuonesha chumba alicholala. Alikuwa msichana mrembo mwenye umri usiozidi miaka ishirini na tano.
“Ng’wangaluka sanchi? Eddy alimsalimu kwa lugha ya kisukuma huku akitabasamu.
Binti wa watu akaangua kicheko cha furaha. Hakutegemea kama mgeni wake angemsalimu kwa lugha ya kwao. Uzoefu alioupata akiwa kazini ulimuwezesha kuwatambua wateja wenyeji, na wale wanaotoka nje ya kanda ya ziwa kwa lafudhi zao tu. Ingawa Eddy alichagua maneno sahihi rafidhi yake ilimsaliti.
“Nilipokuona tu nilijua wewe si mwenyeji wa kanda ya ziwa” Mhudumu huyo alisema huku akiendelea kucheka.
“Ni kweli mimi si mwenyeji wa hapa lakini nimeazimia kuoa Msukuma; kwa hiyo lazima nijifunze lugha ya wakwe” Eddy alijibu huku akicheka.
Basi wakatupiana maneno mawili matatu ya utani kisha Eddy akamuaga na kuondoka.
Alipotoka nje tu akaiona gari aina ya Nissan Altima nyeupe imeegeshwa umbali wa mita ishirini hivi kutoka lango la mbele. Pembeni yake alisimama Frank, akisafisha vioo kwa kitambaa.
“Habari za asubuhi Frank?”
“Njema sana bosi wangu, pole kwa uchovu wa safari”
“Ahsante sana, najisikia vyema”
“Ulipata mwenyeji? Frank aliuliza huku akitabasamu.
“Bado sijapata, mimi ni mtu wa subira sana!” Eddy alijibu akicheka kuashiria ameelewa maana ya swali hilo.
“Ni kweli nyie wakubwa huwa hamna haraka ya maisha, mambo yanawanyookea bila kukunja ngumi” Frank alijibu huku akicheka.
Eddy hakuongeza neno. Ubongo wake ulishaanza kufungua mafaili ya kumbukumbu za shida, vurugu na vitisho anavyopambana navyo mara kwa mara bila wengine kujua yanayomsibu. Akaingia kwenye gari na kufunga mkanda. Frank naye akaingia na kuwasha gari, wakaondoka kuelekea Bugando.
Muda huu msongamano wa magari ulikuwa bado haujaanza. Frank akaendesha kwa kasi kufuata barabara ya Kapripointi inayopita mbele ya jengo la chuo cha benki. Mbele kidogo akakata kona kushoto kuingia barabara ya stesheni, akaendesha moja kwa moja mpaka kwenye makutano ya barabara ya Mkuyuni. Hapo akanyoosha mpaka walipokutana na barabara ya Nyerere. Akapunguza mwendo, akakata kulia kufuata barabara hiyo.
Barabara ya Nyerere huwa na msongamano muda wote kwani ndiyo inayotumiwa na magari yaendayo Nairobi kupitia Magu, Bunda, Tarime hadi Sirari. Kwa hiyo Frank akalazimika kupunguza mwendo. Walipofika njia panda akaingia barabara ya Pamba halafu mbele kidogo akakata tena kushoto kufuata barabara inayokwenda kanisa kuu la Epifania Bugando. Wakati akiegesha gari kwenye maegesho ya kanisa, mishale ya saa iliyo kwenye dashibodi ya gari ilionesha imeshatimia saa moja kasoro dakika ishirini na nne asubuhi. Eddy akampa ujira wake, wakaagana.
Kanisa kuu la Epifania limejengwa karibu na hospitali kuu ya rufaa Bugando ambayo pia ni ya kanisa Katoliki. Kanisa hili ndilo lililokuwa makao makuu ya jimbo kuu la Mwanza kwa miaka mingi kabla ya kuhamishiwa Kawekamo. Waliolijenga waliamua kulipa jina la Epifania kwa heshima ya kumbukumbu ya Epifania ya Bwana, nyota iliyowaongoza wataalam wa nyota (Mamajusi) kutoka mashariki, kwenda kumtembelea mtoto Yesu (Mathayo 2:2). Wanatheolojia hufafanua kwa kusema nyota hiyo ilikuwa ni ishara ya kipekee kwamba Mungu huwaelekeza kwenye wokovu watu wa nyakati zote, wakati wote na mahali pote.
Katika kanda ya ziwa dini ya Kikristo hususan ukatoliki uliletwa na kikundi cha wazungu (White Fathers) zaidi ya miaka mia moja iliyopita. Jitihada kubwa walizozifanya ndizo zilizochangia kuenea kwa ukatoliki kwa kasi katika kanda ya ziwa. Leo hii ukatoliki umeota mizizi kila mahali kiasi cha kuzaliwa majimbo mengi, yenye nguvu kubwa kiimani, kiuchumi na kisiasa chini ya maaskofu wake. Majimbo hayo ni pamoja na Bukoba, Geita, Musoma, Rulenge na Shinyanga; haya yote yakiwa chini ya jimbo kuu la Mwanza ambalo makao makuu yake yalikuwa Bugando, kabla ya kuhamishiwa Kawekamo.
Wakati Eddy akiingia ndani kanisa lilikuwa limeshaanza kujaa. Hiyo ilimpa dalili kwamba watu wa Mwanza ni wacha Mungu, wanaojali ibada. Baada ya kuangalia huku na kule akaona nafasi wazi kwenye benchi la pili kutoka nyuma, karibu kabisa na mahali wanapopita mapadre kutoka altareni. Akaiendea nafasi hiyo, akapiga magoti mbele ya benchi, akasali sara fupi, kisha akaketi kwenye benchi kusubiri.
Kanisa lilikuwa limepambwa vizuri, maalum kwa siku ya watakatifu. Sehemu ya mbele pamoja na altare ilipambwa kwa vitambaa vya rangi nyeupe vilivyotalizwa kwa nyuzi za rangi ya dhahabu. Pembeni, upande wa pili wa kanisa waliketi watawa wa kike (masista) wapatao ishirini na nne waliovaaa mavazi meupe yaliyowafanya waonekane kama Malaika.
Mpaka wakati huo kwaya ilikuwa bado haijaanza kuimba. Mpiga kinanda ndiye aliyekuwa akitoa burudani kwa kupiga kwa ufundi nyimbo nzuri za kumsifu Mungu. Mbele madhabahuni alikuwepo shemasi mmoja, na wahudumu wengine wawili wakikamilisha maandalizi ya misa kwa kuwasha mishumaa na kupanga vyombo vya sakramenti mezani.
Eddy akazungusha macho yake haraka kila upande kuona kama kuna mtu anayemfahamu, au anayeonesha dalili ya kuvutiwa naye. Kwa mafunzo aliyopata na uzoefu aliokuwanao alikuwa na uwezo wa kumtambua mtu anayemtafuta hata akijificha katikati ya watu mia. Hata hivyo hakuona mtu yeyote mwenye sifa alizoziainisha. Watu wote walielekea kuwa waumini wa kawaida, waliiokuja kanisani kwa kusudi la kumuomba Mungu na si vinginevyo.
Ilipotimia saa moja kamili mhudumu akagonga kengele kuashiria muda wa kuanza misa umefika. Waumini wote wakasimama. Kwaya ikaanzisha kuimba wimbo maalum wa siku ya watakatifu, na waumini wakawa wakiitikia kwa kufuata mpangilio wa sauti na vyombo kama ilivyo kawaida.
Pamoja na uzuri wa wimbo huo akili ya Eddy ilikuwa imeanza kwenda mbali. Mpaka wakati huo alikuwa bado hajaona dalili ya mtu aliyemualika. Hata hivyo hakuwa na wasiwasi. Akajitia moyo kuwa misa itakapokwisha mtu huyo atajitokeza mwenyewe. Haiwezekani mtu ajitolee kununua tiketi ya ndege, na kutoa dola 5,500 ili mtu mmoja tu ahudhurie misa ya watakatifu bila sababu yoyote ya muhimu. “Lazima kuna jambo” Alijiambia.
Dakika kumi zikapita bila mapadre kuingia kanisani. Hata hivyo kwaya ikaendelea kuimba kwa shangwe kana kwamba hakuna la ajabu. Zilipopita dakika tano nyingine waumini wenye haraka ya kwenda makazini wakaanza kunong’ona. Mtu mmoja aliyekuwa amekaa benchi la mbele ya Eddy hakuvumilia, akajisogeza pembeni kidogo kumnong’oneza neno muumini aliyesimama kulia kwake.
“Ajabu hii, leo askofu amechelewa kuja kuendesha misa!? Haijawahi kutokea! Mwenziye hakumjibu, akaendelea kumumunya midomo yake kimya kimya. Eddy alipomuangalia akaona alikuwa akisali rozali.
Dakika tano nyingine zikapita bila mapadre kuingia. Hapo minong’ono ikaongezeka zaidi. Waumini wakaanza kupoteza uvumilivu ingawa hakuna aliyethubutu kuondoka. Mara watu wawili wakaingia sakristia, chumba cha maandalizi ya misa, na baada ya sekunde chache padre mmoja aliyevaa kazula nyeupe, akifuatana na shemasi na vijana watumikiaji sita wakaingia kanisani kuanza misa.
Taratibu walitembea kwa unyenyekevu hadi mbele ya kanisa. Wakapiga magoti, kisha padre akapanda madhabahuni, akabusu altare. Hapo vijana wawili watumikiaji waliobeba chetezo na ubani wakamfuata. Yule aliyebeba kibweta chenye ubani akampa padre kijiko. Akakipokea, akachota ubani, akaumwaga kwenye chetezo kilichojazwa makaa ya moto. Mtumikiaji aliyekishika akakifunga kwa kuvuta minyororo yake, kisha akampa. Padre akakipokea na kuanza kufukiza ubani huku akitembea kuzunguka altare. Moshi wenye harufu ya kupendeza ukasambaa kanisa lote.
Alipomaliza kufukiza ubani akasimama, akamrudishia chetezo mtumikiaji, akaenda kusimama katikati ya altare. Hapo wanakwaya wakakatiza wimbo waliokuwa wakiimba kuruhusu misa iendelee. Padre akaanza kwa kutoa salaam.
“Bwana awe nanyi”
“Awe pia nawe” Waumini waliitikia.
“Ndugu zangu leo hii tunaadhimisha misa hii kuwakumbuka watakatifu wote. Watu waliojitoa kwa namna ya pekee kumtumikia Mungu, na wengine hata kupoteza maisha yao kwa ajili ya Kristo” Padre huyo aliendelea. “Katika misa ya leo kwa namna ya pekee na kwa heshima kubwa tunawakumbuka kasisi Michael Mkwama na Daudi Muhando waliofariki dunia miaka zaidi ya hamsini iliyopita. Hawa ni miongoni mwa watanzania wa kwanza kabisa kupewa daraja takatifu nchini Tanzania. Pamoja nao tunawakumbuka mitume, manabii, maaskofu, mapadre, watawa, na watu wote wenye mapenzi mema waliofariki katika Kristo. Tunamuomba Mungu mwenyezi mwenye rehema awajalie raha ya milele na pumziko la amani.”
“Amen” waumini waliitikia kwa pamoja.
“Kabla ya kuendelea na misa napenda kuwaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza. Najua wengi wenu mlijua misa ya leo itaongozwa na mhashamu baba askofu Lucas Simba, lakini kwa mshangao mnaona sura ngeni.” Akanyamaza kidogo kumeza mate, kisha akaendelea.
“Mimi ni padre Nicas Sinda kutoka parokia ya Mwanangi jimbo la Shinyanga. Nimefika mjini hapa jana jioni nikitokea masomoni Nairobi nchini Kenya. Namshukuru Mungu kwa kunipa neema na kibali cha kuongoza misa ya leo. Hii ni baada ya kutokea dharula iliyomfanya baba askofu Lucas Simba kushindwa kuja kushirikiana nasi. Hata hivyo ni tatizo dogo na kwa uwezo wa mwenyezi Mungu tutakuwa naye katika misa ya jioni. Na sasa tujute dhambi zetu kujiweka tayari kutoa sadaka takatifu” Alieleza padre huyo kwa unyenyekevu.
Baada ya maelezo hayo zikafuatia sauti za watu zaidi ya miatano wakisema kwa sauti kubwa sara ya ungamo. Katika hao, Eddy ni miongoni mwa wale wachache ambao hawakuwepo kanisani humo kimawazo. Akili yake ilizama kutafakari uzito wa jambo lililomfanya askofu ashindwe kuongoza misa ya siku hiyo muhimu.
Eddy ni mtoto wa mjini anayependa kazi na bata, lakini huwa hana mzaha na mambo ya Mungu. Wazazi wake walimlea vyema kiasi cha kujenga hofu ya Mungu kwa kiasi fulani ndani yake. Hata hivyo aliona hii ni habari ya kufaa kujaza nafasi katika kurasa za ndani ya Mizani. Inawezekanaje askofu ashindwe kufika kwenye misa aliyopanga kuiongoza? Lazima kuna jambo.
Baada ya ungamo waumini wakaimba “utukufu kwa Mungu” halafu yakafuata masomo ya siku hiyo likianza somo la agano la kale, likifuatiwa na somo la waraka, kisha padre akasoma injili ya siku hiyo. Ndipo yakafuata mahubiri ya siku.
Katika mahubiri yake padre Nicas alisisitiza umuhimu wa kuishi maisha ya utakatifu, kusaidia watu wenye matatizo ya kimwili na kiroho, na kutii mamlaka zilizosimamishwa na Mungu. Aliwakumbusha waumini kuacha kujiingiza katika uuaji wa makusudi kwa kutoa mimba na kudumisha usafi wa maisha ya ndoa kwa kuachana na ngono nzembe ambazo ni chanzo kikubwa cha magonjwa ya zinaa na UKIMWI. Baada ya mahubiri hayo ikafuatia ibada ya ekaristi takatifu.
Wakati misa ikikaribia kwisha, mtu mwingine akaingia kanisani, akatembea kwa heshima kuelekea altareni. Eddy hakuwa na hakika kama mtu huyo alikuwa padre au frateli maana alivaa kanzu nyeupe na sashi nyeusi kiunoni. Alipofika madhabahuni akaenda mahali alipoketi padre Nicas Sinda. Akamuinamia kumnong’oneza jambo fulani. Alipomaliza akageuka, akainama kutoa heshima kwenye altare, kisha akaondoka kupitia mlango ule ule alioingilia.
Wakati huo kwaya ilikuwa ikiimba wimbo wa shukrani. Wimbo huo ulipomalizika Padre Sinda akasimama tayari kwa kumaliza misa. Lakini kabla ya kutoa baraka akaanza kutoa maelezo mafupi akisema:
“Ndugu zangu katika Kristo, nawashukuru sana kwa upendo wenu mkuu na imani kubwa mliyoionesha kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Najua leo ni siku ya kazi na wengi wenu mko mbioni kuelekea vibaruani; lakini bado mmeweza kuja kuadhimisha misa hii takatifu. Mungu awalipe sawasawa na wingi wa rehema na fadhili zake” Akanyamaza kidogo kumeza mate na kuvuta usikivu wa waumini, kisha akaendelea.
“Pamoja nashukrani hizo kuna habari nyingine nzito, na ya kusikitisha sana. Mhashamu askofu mkuu wa jimbo kuu la Mwanza, baba askofu Lucas Simba amefariki dunia akiwa usingizini usiku wa kuamkia leo. Bwana alitoa naye ametwaa, jina lake lihimidiwe.”
___________
Itaendelea Kesho...






Comments