top of page

Hakuna Mungu?



Wakati wa vita kuu ya pili ya dunia, kundi moja la wanajeshi wa Urusi lilijikuta katika wakati mgumu sana. Baada ya mapigano makali, yaliyodumu kwa muda mrefu, wanajeshi hao walizungukwa na majeshi ya adui kila upande, wasiweze kukimbia. Kwa siku kadhaa walilazimika kujificha katika mapango, bila chakula wala maji ya kutosha.


Mbaya zaidi, wakati huo ulikuwa ni wa majira ya baridi kali, hivyo theruji ilikuwa imeanguka kila mahali na kuzidisha mateso. Mamia ya wanajeshi walipoteza maisha yao kwa kukosa matibabu, njaa na baridi kali. Wenye nguvu kidogo, hawakuwa na uwezo wa kufanya jambo lolote kusaidia wenzao isipokuwa kuomba msaada wa Mungu tu


Baada ya siku nyingi za shida na mateso, hatimaye majeshi ya ukombozi yalifanikiwa kuyafukuza majeshi ya Ujerumani na washirika wao na kukifikia kikosi kile kilichokuwa kimezungukwa. Maelfu ya wanajeshi walikuwa wameshakufa, na waliobaki walikuwa katika hali mbaya sana. Hata hivyo baada ya kupewa huduma ya kwanza walipata nafuu, na wengine kupona kabisa.



Jambo la kushangaza ni kuwa wanajeshi walionusulika kifo, baada ya kurudi kwao walimuasi Mungu, na Kukanusha kabisa uwepo wake. “Hakuna Mungu” walisema. “Kwa maana kama Mungu angelikuwepo, bila shaka angetokea na kutusaidia siku zile tulizokuwa tumezungukwa na maadui. Tuliomba mchana kutwa, na usiku kucha, lakini Mungu hakuonekana. Na kama hakuonekana wakati ule, basi hataonekana kamwe (hayupo) kwani hakuna kipindi tulichoomba na kumlilia kama hicho”


Ajabu ni kwamba, waliokuwa wakilalamika na kumkufuru Mungu, ni wale waliokuwa wamesalimika. Waliokombolewa kwa namna ya ajabu, na kuyaepuka mauti. Lakini kwa sababu (kwa mtazamo wao) msaada ulichelewa mno kufika, walifikia hitimisho kuwa msaada huo haukutoka kwa Mungu, bali kwa majeshi rafiki yaliyojitoa kupigana na maadui zao ili kuwakomboa.


Pengine wewe pia umeshawahi kupambana na hali ngumu ya maisha, au kupitia jaribu lililokufanya utafakari mara mbili kuhusu uwepo wa Mungu. Au labda umewahi kushuhudia mambo mabaya yakimpata mmoja wa ndugu au rafiki zako kiasi cha kukufanya ujiulize mara mbili kama kweli Mungu yupo?? Kama ndivyo, usishangae.


Miaka mingi iliyopita mtumishi wa Mungu, nabii Habakuki naye alipita katika kipindi kama hicho. Baada ya kushuhudia mambo mengi magumu alimlilia Mungu akisema ”Ee BWANA, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa. Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea (Habakuk 1:2-4)


Ni kwa sababu hii Unapaswa kusimama hapa, na kujiuliza kwa nini unamwabudu Mungu. Je! Unamwabudu kwa sababu amekupa nyumba nzuri, magari ya thamani, na vitu vingine vya maana? Au unamwabudu kwa sababu amekupa kazi nzuri, biashara za maana, na familia bora kabisa?? Kama hizo ndizo sababu zinazokufanya umwabudu Mungu, jua hakika umechelewa sana!


Hatumwabudu Mungu kwa sababu ya vitu alivyotupa, ambavyo pia anaweza kuvichukua; bali tunamwabudu kwa kuwa yeye ni MUNGU. Ndiye aliyetuumba, ametupa uhai, na sisi tu watu wake na kondoo wa malisho yake. Kwa hiyo tunapaswa kumwabudu Mungu tukiwa matajiri au maskini; tukiwa tumeshiba au tuna njaa, na katika mazingira yoyote yale. Tunapaswa kumwabudu tukiwa katika amani, na hata katika vita pia.



Ndiyo maana mtume Paulo aliwaandikia waraka Warumi kuwakumbusha uzito wa imani yao akisema “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. (Warumi 8:35-37)


Mtume Paulo aliandika barua hii akiwa nyumbani kwa Gayo, mmoja wa waamini aliyekuwa akiishi Korintho. Hii ilikuwa wakati wa safari zake za kitume. Pamoja na shida nyingi alizokuwa akipambana nazo (kupigwa, jua, baridi, dhoruba za safari, na hata kutaka kuuawa) Paulo aliamini kwa dhati nguvu ya upendo wa Mungu iliyo katika kristo Yesu. Na kwa sababu hiyo akahitimisha kuwa “Hakuna chochote kinachoweza kututenga na upendo wa Mungu”



Kumbe tunapopita katika nyakati ngumu, changamoto za maisha, au kukabiliwa na majanga kama hili la COVID19 tunapaswa kukumbuka kuwa Mungu wetu hajatuacha, na kwamba bado tu washindi kama mtume Paulo anavyosisitiza. Tunapaswa kujitia moyo sisi wenyewe, na kuwainua wengine waliovunjika moyo ili wasimame kwa imani, wakiwa na hakika kuwa matatizo yanayotukabiri ni ya muda tu, na katika wakati uliokubalika neema na baraka za Mungu zinazotushukia kila siku zitajidhihirisha katika maisha yetu.


Kamwe tusiwe kama wanajeshi wale, waliokata tamaa, na kumuacha Mungu baada ya kukombolewa, wakisahau kuwa wokovu uliowafikia ulitokana na neema ya Mungu isiyo na upendeleo wowote. Wakati wote jitahidi kukumbuka, na kushukuru kwa matendo makuu Mungu aliyokutendea, hata kama unajiona uko katika dhiki. Mara nyingine jambo unalolichukia, linaweza kuwa ndiyo neema ya kukutoa katika jaribu lingine linalokusumbua, au linalokujia. Kwa sababu hiyo, ni vema kumshukuru Mungu kwa kila jambo kwa maana yote ni mapenzi yake (1 Wathesalonike 5:18).


Uwe na amani.

Rev. Godwin Chilewa









Comments


bottom of page