top of page

Niende Kwa Mungu Nikiwa Uchi? Tena na Janaba?



Miaka mingi iliyopita alikuwepo mfanya biashara mmoja tajiri, na maarufu sana. Mfanyabiashara huyu licha ya kuwa na pesa nyingi, aliheshimika sana kwa sababu ya mambo makuu mawili: Kwanza, alikuwa mcheshi, mkarimu na mwenye kujitoa katika jamii. Pili yeye ndiye aliyekuwa muuzaji maarufu wa sanda (nguo ya kuzikia) katika mji aliokuwa akiishi, bidhaa ambayo kila mtu kwa wakati wake aliihitaji. Mfanya biashara huyu alikuwa tayari kumkopesha sanda mtu yeyote aliyefiwa, na kamwe hskutaka kulipwa haraka au kwa riba. Utaratibu huo ulimfanya aheshimike, na kutawala soko la vifaa vya kuzikia. Pamoja na utajiri wake, mfanyabiashara huyu alikuwa na siri kubwa ambayo hakuna mtu yeyote aliyekuwa akiijua. Ya kwamba sanda zote alizokuwa akiziuza zilikuwa mitumba! Naam, huyu bwana alikuwa na tabia ya kufukua makaburi, na kuwavua sanda maiti waliozikwa, kisha akaenda kuzifua kwa sabuni na madawa na kuziuza tena. Kwa vile yeye ndiye aliyekuwa muuzaji na mshonaji wa sanda, hakuna yeyote aliyeweza kufikiria kuwa sanda anazouza ni mitumba. Ujanja huo ulimpatia faida kubwa kwani sanda moja aliyoinunua, aliweza kuiuza hata mara ishirini, Siku moja majira ya saa tisa usiku mfanya biashara huyo alikwenda makaburini kuchukua sanda aliyokuwa ameiuza mchana wa siku hiyo. Mara tu baada ya kufika eneo hilo la kutisha, akachukua koleo na kuanza kufukua kaburi alilokuwa amelikusudia.. Kaburi lenyewe lilikuwa limechimbwa sehemu yenye mchanga, na mazishi yalifanyika kiasi cha masaa kumi hivi yaliyopita, kwa hiyo haikumuwia vigumu kulifukua. Muda mfupi tu baadae akawa ameshaifikia maiti na kuitoa nje. Akailegeza mishipi iliyokuwa imezinga sanda na kuitoa maiti, akaiweka chini pembeni ya kaburi.. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake mfanyabiashara akapigwa na butwaa! Maiti ilikuwa ya msichana mzuri kupindukia. Alikuwa binti wa miaka 17 hivi. Sura yake ilikuwa nzuri kama malkia wa Sheba, na umbo lake lilivutia kama Bethsheba. Pale chini alipokuwa amelazwa alionekana kama mtoto aliyelala usingizi. Midomo yake mizuri ilionesha tabasamu kama la mtu anayeota ndoto ya kufurahisha.

Uzuri huo ulimvutia sana mfanya biashara, Kwa sekunde kadhaa akamkodolea macho binti yule kwa tamaa, huku moyo wake ukidunda kwa kasi, na miguu ikimtetemeka. Taratibu akanyoosha mkono wake kumpapasa kifuani. Akashangaa kuona mwili wa binti huyo ukiwa ungali moto kana kwamba alikuwa mzima. Bila kufikiri mara mbili akavua nguo zake na kumuingilia kimwili. Akalala naye!

Kwa muda usiojulikana akaendelea kufanya uchafu huo bila kukumbuka kwamba alikuwa akicheza na maiti. Alipoona ameridhika akasimama, na kuchukua nguo zake ili avae kisha airudishe maiti kaburini na kufukia kabla hakujaanza kupambazuka. Lakini kabla hajaanza kuvaa suruali yake, ile maiti ikafumbua macho na kukaa kitako, ikamuuliza “Hivi wewe huna aibu, na hata humuogopi Mungu wako? Yaani unataka mimi niende kwa Mungu wangu nikiwa uchi, tena na janaba?" Baada ya maneno hayo binti yule akafumba macho na kujilaza chini; akarudi kuwa maiti kama alivyotolewa kaburini.

Kitendo hicho kilimshitua sana yule mfanya biashara. Kwa dakika kadhaa alibaki akiwa ameduwaa, asijue la kufanya. Akili ilipomrudia ndipo alipotambua ubaya wa tendo alilolifanya. “Nimezini, tena na maiti? Alijisemesha huku akilia kwa sauti kubwa. Bila kuvaa nguo akatoka mahali pale mbio kuelekea katika nyumba ya ibada iliyokuwa umbali mfupi tu kutoka pale. Alipofika akawakuta watu waliokuwa wamekesha wakimuomba Mungu, na wachache waliokuwa wamejidamka kuwahi sala ya alfajili. “Naombeni mnipige mawe mpaka nife, maana kwa dhambi niliyofanya sistahili kuishi” Aliwaeleza waungwana hao huku akilia kwa sauti ya juu. “Imekuwaje? Walimuuliza kwa mshangao baada ya kumstiri kwa shuka, na kumtuliza wakidhani amerukwa na akili.


Ndipo mfanya biashara huyo alipoeleza madhambi yake yote. Kuanzia siri yake ya kuuza sanda zilizotumika, na mambo yote aliyoyafanya usiku ule. Baada ya maelezo hayo mfanyabiashara akawaongoza watu hao makaburini ambako waliikuta ile maiti ikiwa bado imelazwa nje ya kaburi. Tukio hili liliwaudhi sana watu wote waliolishuhudia. “Tumpige mawe” baadhi yao walisema. “Hapana, kumpiga mawe haitoshi, tumchome moto” wengine walidakia huku kila mmoja akitaja adhabu anayodhani itakuwa kubwa zaidi.


Baada ya malumbano ya muda mfupi, mzee mmoja mwenye hekima akapaza sauti kuomba asikilizwe. “Ndugu zangu, hatuna sababu ya kumuhukumu huyu mwenzetu, kwa sababu Mungu amekwisha msamehe. Kumbukeni mtu huyu alifanya mambo haya akiwa peke yake. Kama angetaka angeweza kufukia hii maiti, na kurudi nyumbani kwake kimyakimya, na wala hakuna mtu yeyote angejua kilichotokea. Lakini yeye mwenyewe kwa hiari yake ameamua kutufuata, tena akiwa amekwisha jihukumu kifo kwa kujua ukubwa wa dhambi alizofanya. Kwa kitendo hicho nina imani mwenyezi Mungu amemsamehe, maana yeye ni mwingi wa huruma. Na kama Mungu amemsamehe, sisi tuna haja gani ya kumuhukumu ?”. Kwa maelezo hayo watu wote waliokuwapo pale wakaridhia kumsamehe, na kuanzia siku hiyo mfanya biashara yule akawa mcha mungu kwelikweli (Hadithi ya kiislam - italiki ni zetu).

Pengine katika maisha yako umewahi kufanya mambo mabaya, ya kutisha na au yakuumiza mioyo ya watu wengi. Huwenda baadhi ya mambo hayo umeyafanya hadharani, na mengine sirini,hivyo hakuna yeyote anayeyajua iwe mkeo, mumeo, au wazazi wako. Lakini kumbuka Mungu alikuona, na shetani alikuwa pamoja nawe. Ndiyo maana (shetani) anaendelea kukutesa, kukukejeli na kukufunga ili usiwe na amani. Nataka kukukumbusha rafiki yangu, kuwa Mungu wetu ni mungu wa msamaha. Ni yeye pekee anayeweza kukusamehe uovu wako wote, kukusafisha, na kukufanya kuwa kiumbe kipya.

Kwa hiyo haijalishi dhambi zako ni chafu kiasi gani, au umezifanya kwa miaka mingapi. Kama ukiamua kutubu na kuziacha, yeye yuko tayari kukusamehe, kwani yeye huwa anatusamehe sisi kwa ajili yake yeye mwenyewe. Ndiyo maana hachoki kutuita akisema "Njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha (Mathayo 11:28). Haishii hapo, anaendelea kutubembeleza akisema “Haya, njoni, tusemezane...Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi (Isaya 1:18-19).

Kwa ujumla Mungu anafahamu kuwa sisi ni viumbe dhaifu, na ndiyo maana huwa anatusamehe dhambi zetu kila tunapomwendea kwa unyenyekevu na toba. Tena yeye huwa hafufungulii akaunti za makosa, bali akishatusamehe huwa hazikumbuki dhambi hizo tena. Kama mashariki ilivyo mbali na maghalibi ndivyo anavyoziweka dhambi zetu mbali nasi (Zaburi 103:12). Sisi tunachopaswa kufanya nikumwendea tu na kuupokea msamaha bure. Yeye anasema “Tazama nasimama mlangoni na kubisha hodi, mtu akiisikia sauti yangu nitaingia kwake (Ufunuo 3:20). Je uko tayari kumwendea Mungu kwa toba?

Inawezekana ungependa kufanya hivyo lakini unaogopa au unaona aibu. Inawezekana unazo sababu za msingi kufanya hivyo. Pengine wewe ni mtu mkubwa, maarufu, tajiri na au mwenye familia bora kabisa ya kuigwa, hivyo unaona kitendo cha kumwendea Mungu kwa toba kitakupunguzia hadhi, au kuwafanya watu wakudharau. Lakini kumbuka yule mfanya biashara alikuwa hivyo, na pengine bora kukushinda wewe. Lakini alichagua kumwendea Mungu kwa toba ili roho yake isalimike. Sasa ni wakati wako. Chagua lililo jema ili nawe usalimike. Chagua toba, chagua rehema.

Ubarikiwe sana

Rev. Godwin Chilewa

댓글


bottom of page