Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) - Imeshindwa Kuidhibiti CCM?
- Rev. Godwin Chilewa
- Oct 23, 2024
- 5 min read
Updated: Oct 24, 2024

Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) ni chombo cha kipekee na chenye umuhimu mkubwa katika kulinda usalama wa taifa, kutoa ushauri wa kimkakati kwa viongozi wa serikali, na kuhakikisha kuwa nchi inaelekea kwenye amani, ustawi wa kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Kwa ujumla TISS imekuwa msingi wa ulinzi wa maslahi ya kitaifa ya Tanzania kwa miaka mingi. Hata hivyo, hivi karibuni kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu utendaji wa idara hii, hususan ushirika wake na CCM jambo linaloashiria kwamba kuna mahali haijatimiza majukumu yake kama inavyotarajiwa. Je, tatizo ni nini hasa? Makala hii inaingia ndani ya idara kutafuta mchawi wake.
Idara ya Usalama wa Taifa ilianzishwa rasmi mwaka 1964 baada ya kuvunjwa kwa Shirika la Kijasusi la Uingereza (Special Branch) kufuatia uhuru wa Tanzania. TISS ni idara inayojitegemea iliyoundwa chini ya sheria namba 15 ya Idara ya Usalama wa Taifa iliyopitishwa na bunge na kutiwa saini na Rais Benjamin William Mkapa mwaka 1997. Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho hivi karibuni kuiongezea nguvu idara.
TISS ina wajibu wa kuhakikisha usalama wa taifa kwa kudhibiti vitisho vyovyote, ikiwa ni pamoja na ugaidi wa nje na ndani, ujasusi wa kigeni, uzandiki, migogoro ya kisiasa, na harakati za kijamii zinazolenga kuhujumu nchi. Idara pia inapaswa kutoa ushauri wa kiitelijensia na wa kisera kwa serikali kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu uchumi, siasa, na jamii. Ushauri huu unategemea taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa na kuchambuliwa na watalaam wa ndani wa idara.
Changamoto na Sababu za Kudhoofika kwa Utendaji wa TISS:
Idara imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kulinda usalama wa Tanzania. Ni ukweli usiopingika kwamba nchi hii ni mojawapo ya mataifa machache barani Afrika ambayo hayajakumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Aidha, Tanzania ni mojawapo ya sehemu salama kwa wageni na watalii. Zaidi ya yote Watanzania wamekua wakiheshimika duniani kote kwa utu wema, na kuheshimu ubinadamu. Jambo hili linaweza lisieleweke kwa watu wengi. kwa sababu ya uelewa mdogo wa jinsi idara za usalama na vyombo vya kijasusi vinavyofanya kazi ya kuwatengeneza raia na muelekeo wa nchi kwa ujumla.
Pamoja na mafanikio hayo TISS inakabiliwa na changamoto lukuki ambazo zimekuwa zikidhofisha ufanisi wake na kupelekea malalamiko kutoka kwa wananchi. Baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na:
Kutokuwa Huru Kiutendaji na Kisiasa:
Idara hii, ingawa inapaswa kufanya kazi kwa kujitegemea, mara nyingi imekuwa ikiingiliwa na siasa za chama tawala. Hii inatokana na ukweli kwamba Rais ndiye anayemteua Mkurugenzi mkuu wa TISS (DGIS) na wakurugenzi wengine wote. Kimsingi Rais ndiye anayeitengeneza idara anayoitaka. Mbaya zaidi ni kuwa rais pia ana uwezo wa kumuondoa mkurugenzi huyo muda wowote anaotaka, endapo ataona mkurugenzi huyo hafai, au hakubaliani na ushauri wake hata kama ndio wenye manufaa kwa taifa. Hili limeifanya TISS ionekane kama chombo cha kumlinda rais na watu wake.
Pamoja na hilo mfumo huu umeifanya idara kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa haki, na kwa faida ya taifa hasa inapokuja suala la usimamizi wa harakati za kisiasa za upinzani. Mara nyingi idara imeshinikizwa kutoa taarifa za kukisaidia chama tawala au kulinda uongozi uliopo jambo linalosababisha TISS kuhusishwa na matumizi mabaya ya vyombo vya dola kwa ajili ya kudhoofisha wapinzani wa kisiasa badala ya kulinda maslahi ya taifa kwa ujumla.
Kwa ujumla nguvu kubwa ya Rais dhidi ya TISS na watendaji wake wakuu, imechangia sana kuporomoka kwa heshima ya TISS. Baadhi ya viongozi walio karibu na mheshimiwa rais wamekua wakipuuza ushauri wa idara hasa unapoingilia maslahi yao binafsi, na kupendelea ushauri wa watu wa karibu (wasio maafisa wa idara wala utaalam wa intelijensia). Utaratibu huu unadhofisha nguvu ya idara na kutoa mwanya wa kutengenezeka kwa vitendo vya kiadui ndani ya idara na mifumo ya serikali ikiwa pamoja na uvujishaji wa siri za serikali na viongozi wake.
Ukosefu wa Rasilimali na Vitendea Kazi
Pamoja na kuwa chombo muhimu, TISS inakabiliwa na changamoto za rasilimali, ikiwa ni pamoja na uhaba wa teknolojia ya kisasa ya ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa, upungufu wa wafanyakazi wenye ujuzi wa hali ya juu wa kiintelijensia, na wachambuzi wa fani maalum wenye nguvu ya ushawishi. Hii imepelekea idara kushindwa kukabiliana ipasavyo na vitisho vipya vya usalama kama vile uhalifu wa mtandaoni (cybersecurity), ugaidi wa ndani na kimataifa, na ujasusi wa kiuchumi.
Matumizi ya Mbinu Zilizopitwa na Wakati:
Katika ulimwengu wa sasa wa kiteknolojia, idara nyingi za usalama wa taifa zinahitaji kutumia mbinu za kisasa na za kiteknolojia katika kukusanya na kuchambua taarifa za kiintelijensia. TISS, kwa kiasi kikubwa, bado inategemea mbinu za kizamani, jambo linalowafanya washindwe kufikia viwango vya kimataifa vya uchunguzi na utekelezaji wa operesheni za usalama.
Matatizo ya Uaminifu na Uwajibikaji
Kumekuwa na tuhuma za ndani ya TISS zinazohusisha baadhi ya maafisa wake kushiriki kwenye vitendo vya hujuma na ufisadi ama moja kwa moja au kwa kutumia watu wengine. Hali hii inavuruga mfumo mzima wa utendaji wa idara, kwani inaondoa dhana nzima ya nidhamu na uaminifu kwa taifa. Kwa vyombo vya usalama wa taifa, uaminifu ni nguzo muhimu, na unapokosekana, utekelezaji wa majukumu muhimu unakuwa dhaifu.
Je, TISS Imeshindwa Kutimiza Wajibu Wake?
Licha ya changamoto hizo, haimaanishi kwamba TISS imeshindwa kabisa kutimiza majukumu yake. Kuna mafanikio mengi ambayo yamepatikana kwa usiri mkubwa, hasa katika kudhibiti vitisho vya ugaidi na ujasusi wa kigeni. TISS imefanikiwa kuzuia baadhi ya matukio ya hatari kwa taifa ambayo yasingetambulika bila mchango wake. Hata hivyo, malalamiko mengi yanatokana na kutokuwepo kwa uwazi katika utendaji wake na kushindwa kudhibiti kikamilifu vitendo vya kisiasa vinavyohatarisha amani na maendeleo.
Nini Kifanyike Kuiboresha TISS?
Ili kurejesha ufanisi na kuimarisha imani ya wananchi kwa TISS, mambo yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:
Marekebisho ya Sera na Mfumo:
Jambo la kwanza ni kuundwa kwa sera na mfumo thabiti utakaoiwezesha TISS kufanya kazi zake kwa uhuru, weledi na bila kuingiliwa na wanasiasa. Idara inahitaji kuwa huru kisiasa, na serikali inapaswa kuweka mazingira bora ya kisheria kuhakikisha idara hii inafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kwa kufuata muongozo wa katiba ya nchi, na bila hofu ya kuingiliwa.
Idara inapaswa kulinda jamhuri ya muungano wa Tanzania, kulinda wananchi bila kujali itikadi zao, na kulinda mfumo wa siasa wa vyama vingi kama ulivyoundwa kisheria bila kutoa upendeleo kwa chama tawala, na kuvionea au kuvipiga vita vyama vya upinzani. TISS si sehemu ya chama chochote cha siasa, maafisa wa idara si wanachama wa chama chochote cha siasa, na utendaji wake unapaswa kutoonesha upendekeo kwa chama chochote. Hii itasaidia pia TISS isisambaratike kama ikitokea chama cha upinzani kikashinda uchaguzi na kutwaa madaraka.
Kuwa na Uongozi Thabiti:
Idara inapaswa kuongozwa na mtu
mwenye elimu, uzoefu wa uongozi na weledi wa mambo ya intelijensia. Hivi sasa idara inaongozwa na Sulemani Abubakar Mombo, jasusi nguli mwenye uwezo na kila sifa ya kuwa DGIS. Hata hivyo, uwezo wake mkubwa hauwezi kudhihirika, wala taifa halitofaidika endapo mfumo uliopo utaendelea kumdhibiti, kumpunguzia kasi ya utendaji, au kupuuza ushauri anaoutoa. Ni muhimu sana serikali ithamini ushauri na ikibidi maelekezo ya kitaalam ya idara katika kukabiliana na matatizo ya kiuchumi, kijamii na kiusalama.
Uwekezaji katika Teknolojia:
Uwekezaji mkubwa unahitajika katika teknolojia ya kisasa ya kiintelijensia ili kukabiliana na vitisho vya kisasa kama ugaidi wa ndani na wa kimataifa, uhalifu wa mtandao, na ujasusi wa kiuchumi.
Kujenga Nidhamu na Uwajibikaji
Idara inapaswa kuhakikisha nidhamu ya hali ya juu miongoni mwa maafisa wake na kuwa na mfumo wa uwajibikaji ili kuzuia vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya mamlaka.
Kuongeza Uwazi kwa Umma
Ingawa ni idara ya siri, TISS inaweza kuongeza uwazi kwa kiwango fulani kuhusu jinsi inavyofanya kazi na mafanikio yake, ili kujenga imani ya wananchi kwa chombo hiki muhimu.
Kwa kuchukua hatua hizi, TISS inaweza kurejesha ufanisi wake na kuhakikisha inatimiza wajibu wake kikamilifu katika kulinda usalama na maslahi ya taifa.
Rev. Godwin Chilewa
Comments