top of page

Maandalizi ya Uchaguzi Kweli, au Hekaheka za Kutafuta Uhalali wa Kutawala?

Updated: May 18


Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025 yanaendelea kwa kasi, lakini hali ya kisiasa inayoambatana na maandalizi hayo inatia shaka kama kweli taifa linaelekea kwenye uchaguzi huru, wa haki na wa kidemokrasia. Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiendelea na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, taswira kubwa ya kisiasa nchini imegubikwa na ukandamizaji wa wapinzani, vitisho kwa wakosoaji wa serikali, na matumizi ya vyombo vya dola kwa maslahi ya kisiasa.


Kazi ya kuhuisha daftari la wapiga kura ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi wowote. Lakini swali kuu linabaki—je, uboreshaji huo unatekelezwa kwa misingi ya usawa, uwazi na ushirikishwaji wa wadau wote wa kisiasa? Ni maboresho kwa ajili ya Taifa au Chama Tawala? Taarifa zinaonyesha kuwa baadhi ya maeneo ya vijijini na mijini yamekumbwa na changamoto za upatikanaji wa taarifa, pamoja na hofu ya udanganyifu wa taarifa za wapiga kura. Je Tume husika inachukua hatua?


Jambo lingine linalosikitisha ni kuona vyama vya upinzani vinefungwa kabla hata ya pambano. Chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, kimejikuta kikiwa kimenyimwa fursa ya kushiriki uchaguzi ujao kufuatia kukataa kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi. Hatua hiyo imezua maswali mengi kuhusu uhuru wa kisiasa nchini. Tundu Lissu, mmoja wa viongozi mashuhuri wa chama hicho, yuko mahabusu akikabiliwa na kesi ya kile kinachotajwa kama “uhaini,” ikiwa ni mwendelezo wa hali ya kutoaminiana kati ya serikali na wapinzani wake.


Si hivyo tu, uchaguzi unakuja wakati WATU WASIOJULIKANA wakiwa wameshika hatamu. Hali ya usalama wa watu wanaoikosoa serikali imeendelea kuwa mbaya kiasi cha kutisha . Hivi karibuni, Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) alipigwa na watu wasiojulikana, huku Askofu wa Karagwe, Dkt. Benson Bagonza, akitishiwa maisha. Na juzi tu mchungaji mwingine ametekwa hadharani na kushughulikiwa vilivyo kwa kutoa unabii usiowapendeza wakubwa. Wote hawa ni watu wa heshima, wenye mchango mkubwa katika jamii. Ikiwa hata viongozi wa kidini wanakumbwa na vitisho, tunajiuliza: je, wananchi wa kawaida wako salama?


Kinachofanya uchaguzi huu kuwa wa mzaha ni ile ruhusa ya kuchagua bila kujieleza kwa uhuru. Ingawa vyama vingi vimeanza kufanya kampeni zisizo rasmi, lakini mazingira ya kisiasa hayatoi nafasi ya wazi kwa mijadala ya kisera. Uhuru wa kujieleza, ambao ni kiini cha uchaguzi huru, Vyama vimebanwa kupitia sheria, vitisho na matukio ya uvamizi. Hii inatufanya tuhoji: Je, uchaguzi huu ni wa kumpa mwananchi nafasi ya kuchagua, au ni mchakato wa kisheria tu unaolenga kuhalalisha utawala uliopo?


Baya kuliko yote ni ile hali ya dola kuteka uhuru na haki ya raia kuamua. Imani aubushabiki kwa chama fulani inaweza kuwa tiketi ya maisha bora au mateso, manyanyaso na kupoteza uhai. Utu wa mtu unapimwa kwacrangi za nguo aliyovaa au bendera anayopeperusha. Katika mazingira haya, si sahihi kuzungumzia uchaguzi kama tukio la kidemokrasia, bali ni kama zoezi la kuthibitisha mamlaka ya chama tawala. Wakati dunia ikiangalia kama Tanzania itaendelea kuwa mfano wa demokrasia ya Kiafrika, ndani ya nchi hali ni tofauti. Upinzani umebanwa, uhuru wa maoni unadhoofishwa, na wananchi wanabaki na maswali mengi bila majibu.


USHAURI:

Kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan:

Ni muda wa kuandika historia mpya. Acha hofu, ruhusu mashindano ya haki. Fungua milango ya kisiasa kwa kila chama, achilia wanasiasa wa upinzani waliokamatwa, na linda uhuru wa mawazo kwa wote. Jina lako litatajwa kwa wema na heshima yako itadumu vizazi na vizazi.


Kwa Chama Tawala (CCM):

Demokrasia ya kweli hujengwa kwa ushindani wa hoja, si nguvu ya dola. Jipambanueni kwa sera, si kwa kuwadhibiti wapinzani.


Kwa Wananchi:

Jukumu la kulinda demokrasia ni la kila mmoja. Simameni, ombeni, pigieni kura kwa uhuru, na dai haki kwa njia za amani. Uchaguzi si tu zoezi la kupiga kura. Ni sauti ya wananchi. Ni mahali pa kuamua mustakabali wa taifa. Kama sauti hiyo itanyamazishwa, basi Tanzania haitakuwa tena taifa la watu huru, bali taifa linaloongozwa kwa woga na ukimya wa mabavu.


Rev. Godwin Chilewa

 
 
 

Comentarios


bottom of page