KESI YA TUNDU LISSU: Siasa, Usalama, na Mustakabali wa Tanzania
- Rev. Godwin Chilewa
- 2 days ago
- 4 min read
Na Rev. Godwin Chilewa

Katika historia ya siasa za Tanzania, kumekuwa na nyakati chache sana ambazo kesi ya mtu mmoja imebeba uzito mkubwa kiasi cha kuathiri mwelekeo mzima wa taifa. Kesi ya Tundu Lissu ni mojawapo ya nyakati hizo. Kesi hii ni ya kipekee kisheria, na ni kioo kinachoakisi mvutano wa ndani wa mfumo wa kisiasa wa Tanzania kati ya udhibiti wa dola na wito wa mageuzi ya kidemokrasia.
Tundu Lissu ni mwanasiasa wa aina yake katika uwanja wa siasa za Tanzania. Kwa zaidi ya muongo mmoja, amejijengea jina zuri akiwa mwanasheria mahiri, mbunge jasiri, na sauti yenye nguvu ya upinzani. Umaarufu wake uliongezeka zaidi baada ya kunusurika jaribio la kuuawa mwaka 2017, tukio ambalo halikuwahi kuleta uwajibikaji wa wazi kwa waliohusika. Kuanzia hapo, Lissu aligeuka kuwa kiongozi shujaa na alama ya mapambano dhidi ya mfumo unaotuhumiwa kukosa uwazi na uwajibikaji.
Katika muktadha wa kiintelijensia, nguvu ya Lissu haiishii katika nafasi yake ya uongozi, bali katika uwezo wake wa kuunganisha vipengele vitatu muhimu: uhalali wa kisheria, uwezo wa kuhamasisha umma, na kukubalika katika jukwaa la kimataifa. Mchanganyiko huu humfanya kuwa kiongozi ambaye hawezi kupuuzwa kwa urahisi ndani ya hesabu za kisiasa za dola.
Kukamatwa kwake mwaka 2025 na kushtakiwa kwa kosa la uhaini kulifungua ukurasa mpya wenye utata mkubwa. Kisheria, kosa la uhaini ni miongoni mwa makosa mazito zaidi, lenye adhabu ya kifo, lisilo na dhamana na lenye athari kubwa kwa usalama wa taifa. Hata hivyo, tafsiri ya kisiasa ya kesi hii imeibua mjadala mpana ndani na nje ya nchi. Wengi wanaona kuwa hatua hiyo haikulenga kulinda sheria, bali kudhibiti nguvu ya kisiasa iliyokuwa ikikua kwa kasi kupitia wito wa mageuzi ya uchaguzi.
Kwa mtazamo wa kiserikali, sababu za kushikiliwa kwa Lissu zinaweza kueleweka zaidi kupitia mantiki ya usimamizi wa hatari za kisiasa. Kauli mbiu yake ya kudai mageuzi kabla ya uchaguzi ilitafsiriwa kama tishio kwa uhalali wa mchakato wa kisiasa uliopo. Katika mazingira hayo, kumweka kizuizini kulionekana kama mkakati wa kuondoa uwezekano wa uhamasishaji wa umma ambao ungeweza kuathiri utulivu wa uchaguzi.
Zaidi ya hapo, kuna kipengele cha kuzuia uhamasishaji wa wananchi. Lissu ana historia ya kuhamasisha mikusanyiko mikubwa ya kisiasa, na katika mazingira yenye hasira ya vijana, uwepo wake huchochea ari ya mabadiliko. Kumshikilia kunatazamwa kama hatua ya kuzuia uwezekano wa maandamano makubwa au harakati zinazoweza kuvuka mipaka ya udhibiti wa kawaida wa dola.
Kwa jicho la kiitelijensia , kesi ya uhaini hapa imetumika kama chombo cha kisaikolojia katika siasa. Uzito wa kosa hilo umetumika kutuma ujumbe kwa wanasiasa wengine na wanaharakati kwamba mipaka ya kuvumiliwa na dola ina kikomo. Hii ni aina ya mkakati wa kuzuia (deterrence) unaolenga kudhibiti siasa kupitia hofu badala ya majadiliano ya wazi.
Hata hivyo, tathmini ya kina inaonyesha kuwa mgogoro huu si wa mtu binafsi bali ni mgongano wa mifumo miwili: mfumo unaosisitiza udhibiti na utulivu wa haraka dhidi ya mfumo unaodai uwazi, uwajibikaji na mageuzi ya kidemokrasia. Katika hali kama hii, hatua yoyote inayochukuliwa dhidi ya mhusika mmoja huathiri moja kwa moja mizani ya nguvu ndani ya mfumo mzima.
Athari za kuendelea kumshikilia Lissu zinaonekana wazi katika nyanja tatu kuu. Kwanza ni ndani ya nchi, ambapo hali ya kisiasa inaendelea kuwa na mvutano unaochochewa na vijana wanaotafuta mabadiliko. Badala ya kupunguza nguvu ya upinzani, hatua hiyo imeongeza hadhi ya Lissu kama alama ya mapambano, hali inayoweza kugeuka kuwa hatari iwapo itachochea maandamano makubwa au vurugu.
Pili ni katika nyanja ya kidiplomasia. Tanzania kwa muda mrefu imejijengea sifa ya kuwa taifa la amani na utulivu. Hata hivyo, kesi hii imeanza kubadilisha taswira hiyo katika macho ya jumuiya ya kimataifa. Mashirika ya haki za binadamu na taasisi za kimataifa zimeonyesha wasiwasi kuhusu mwenendo wa kesi na hali ya haki. Matokeo yake yanaweza kujumuisha kupungua kwa imani ya wawekezaji na kuongezeka kwa shinikizo la kidiplomasia.
Tatu ni katika usalama wa muda mrefu. Historia inaonyesha kuwa ukandamizaji wa kisiasa usio na njia mbadala ya kujieleza huweza kusababisha kuibuka kwa mitandao ya siri au harakati zisizo rasmi. Hali hii huongeza hatari ya mivutano isiyotabirika na inaweza kuathiri uthabiti wa taifa kwa muda mrefu.
Kwa kuzingatia hali hii, uchambuzi wa kiintelijensia unaonesha uwepo wa njia tatu zinazowezekana. Njia ya kwanza ni kuendelea kumshikilia, ambayo inaweza kutoa utulivu wa muda mfupi lakini ikazalisha mlipuko wa kisiasa kwa muda mrefu, na machafuko makubwa. Njia ya pili ni kumwachia bila masharti, jambo ambalo linaweza kusababisha mshtuko wa kisiasa lakini pia kufungua fursa ya mageuzi. Njia ya tatu, ambayo inaonekana kuwa na faida zaidi, ni kurejesha ushiriki wake katika mfumo wa kisiasa kwa njia iliyodhibitiwa kupitia mazungumzo, hatua za kisheria zilizo wazi, na mageuzi ya taratibu.
Kwa mtazamo huu, ushauri muhimu kwa serikali ni kuepuka makosa ya kimkakati yanayotokana na kudhani kuwa udhibiti wa muda mfupi ni suluhisho la kudumu. Historia ya kisiasa duniani inaonyesha kuwa migogoro ya aina hii haiwezi kutatuliwa kwa nguvu pekee. Badala yake, inahitaji mchanganyiko wa busara, mazungumzo, na hatua zinazoonyesha uhalali wa utawala.
Hii ina maana kwamba, kubadili mkakati kutoka ukandamizaji kwenda usimamizi wa kisiasa ni hatua muhimu. Hii inahusisha kufungua nafasi za mazungumzo, kuruhusu upinzani kufanya kazi zake kwa uhuru ndani ya mipaka ya sheria, na kuonyesha utayari wa kufanya mageuzi ya taratibu yanayojenga imani ya umma. Aidha, matumizi ya nguvu laini (soft power) kupitia uhalali wa kisiasa na uwazi yanaweza kusaidia kupunguza mvutano bila kuhatarisha uthabiti wa taifa.
Hatimaye, kulinda taswira ya Tanzania kama taifa la amani ni jambo la kimkakati. Sifa hiyo imejengwa kwa miongo mingi na imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuvutia uwekezaji na kuimarisha nafasi ya nchi katika diplomasia ya kimataifa. Kesi ya Lissu ina hatari ya kuathiri urithi huo iwapo haitashughulikiwa kwa busara na uangalifu wa hali ya juu.
Kwa ujumla, kesi ya Tundu Lissu ni zaidi ya suala la kisheria. Ni kipimo cha uwezo wa Tanzania kusawazisha na kuweka uwiano kati ya utulivu na mageuzi, kati ya nguvu na uhalali, na kati ya sasa na mustakabali wake wa baadae. Maamuzi yoyote yatakayochukuliwa katika kipindi hiki yataacha alama ya kudumu katika historia ya taifa. Tusipoziba ufa, tutajenga ukuta.
Uwe na amani.






Comments