ATCL na Ndoto ya Ndege Nane Mpya: Uwekezaji wa Kimkakati au Kuendelea Kufadhili Hasara?
Na. Rev. Godwin Chilewa

Nianze kwa kuweka angalizo kwamba makala hii haijadili kama Tanzania inahitaji shirika la Ndege, bali kama njia inayotumika kuliendesha ina mantiki kiuchumi? Kwa maana uhitaji wa shirika la ndege ni suala moja na mchakato wa kuliendesha ni suala lingine.
Uamuzi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuongeza ndege nane ifikapo mwaka 2030 umeibua mjadala mpana kuhusu uhalali wa kuendelea kuwekeza fedha nyingi za umma katika sekta ya anga wakati shirika hilo bado halijajijenga kuwa biashara yenye ushindani, yenye faida na inayojitegemea kifedha.
Kwa upande mmoja, ndege ni alama ya maendeleo, hufungua milango ya biashara, utalii na diplomasia. Ndiyo maana nchi nyingi zimewekeza katika mashirika yao ya ndege kama sehemu ya mkakati wa kitaifa. Lakini kwa upande mwingine ni kwamba ndege ni mali yenye gharama kubwa sana, inayohitaji masoko ya kutosha, usimamizi bora, ufanisi wa biashara na uwezo wa kushindana kimataifa.
Kwahiyo hoja kuu si kupinga uwepo wa ATCL. Hoja ni kama Tanzania inaweka fedha zake katika eneo lenye faida kubwa zaidi kwa wananchi wake, au inaendelea kuingiza mtaji mkubwa katika mradi ambao bado haujathibitisha uwezo wa kujisimamia.
1. Historia ya Uwekezaji Mkubwa wa Serikali katika ATCL
Baada ya kufungwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (South African Airways) mwaka 2006, ATCL ilibaki katika hali dhaifu kifedha na kiutendaji. Kwahiyo ufupi shirika hili lilishindwa hata kuendesha safari za ndani. Serikali iliamua kuifufua kama shirika la kimkakati la taifa.
Kuanzia mwaka 2016, Serikali ilifanya mpango mkubwa wa kulifufua shirika hilo kwa kununua ndege mpya kupitia fedha za umma. Ndani ya kipindi kifupi, Tanzania ilinunua ndege za aina mbalimbali, zikiwemo Bombardier Q400 kwa safari za ndani na kikanda, Airbus A220-300 kwa safari za kimataifa, Boeing 787 Dreamliner kwa safari ndefu za kimataifa.
Uwekezaji huu uligharimu mamia ya mabilioni ya shilingi za Watanzania. Lengo lilikuwa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa anga Afrika Mashariki, kuvutia watalii wengi zaidi, kuwezesha wafanyabiashara kusafiri kwa urahisi, na kupunguza utegemezi wa mashirika ya ndege ya nje. Hata hivyo, baada ya miaka kadhaa ya uwekezaji huo, tunapaswa kujiuliza: Je, ATCL imeweza kubadilika kutoka kuwa mzigo wa bajeti ya serikali kwenda kuwa kampuni inayozalisha faida?
2. Tatizo Kuu: Uwekezaji wa Mali Kabla ya Kujenga Soko
Katika biashara ya ndege, kununua ndege siyo sehemu ngumu zaidi. Changamoto kubwa ni kujaza viti kwa kupata abiria wa kutosha kila msimu, kudhibiti gharama za uendeshaji, kumudu ushindani na mashirika yenye uzoefu mkubwa, na kujenga mtandao wa safari wenye faida. Kwa kifupi Ndege ni kama hoteli ya kifahari yenye gharama kubwa: haijalishi umeijenga vizuri kiasi gani, kama vyumba havina wageni, itaendelea kupoteza fedha na kuwa mzigo.
Ni ukweli usiopingika kwamba kwa muda mrefu ATCL imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa. Kwanza ni uhaba wa masoko ya Safari. Ingawa Tanzania ina idadi kubwa ya watalii, lakini soko lake la anga bado ni dogo ukilinganisha na nchi kama Ethiopia, Kenya, Afrika ya Kusini, Misri na Rwanda. Mashirika kama Ethiopian Airlines yamejenga mtandao mkubwa kwa sababu yanaunganisha mabara kupitia Addis Ababa.
Kimsingi hapa tatizo la ATCL ni kwamba bado haijawa na kituo kikubwa cha kimataifa (hub) kinachoweza kuvutia abiria wanaobadilisha ndege. Kwa mfano, Mtanzania anayesafiri kwenda Marekani mara nyingi anaweza kutumia Addis Ababa, Doha, Istanbul au Dubai kwa sababu kuna mtandao mpana wa kuunganisha safari. Zingatia kwamba Ndege moja kubwa haiwezi kutengeneza soko. Soko linatengenezwa na mtandao.
Pili ni gharama kubwa za uendeshaji. Sekta ya ndege ni moja ya biashara zenye gharama kubwa zaidi duniani. Gharama hizo ni pamoja na Mafuta ya ndege ambayo huweza kuchukua sehemu kubwa sana ya gharama za uendeshaji.
Bei ya mafuta inapopanda kimataifa, shirika linaathirika moja kwa moja.
Gharama za Matengenezo pia ni mzigo mwingine mkubwa. Ndege zinahitaji vipuri maalum, mafundi waliobobea, na ukaguzi wa mara kwa mara. Matengenezo ya ndege kubwa kama Boeing 787 ni ghali sana.
Lipo pia suala la mishahara na utaalamu. Marubani, wahandisi na wataalamu wa anga hulipwa mishahara mikubwa kwa sababu ya kiwango cha utaalamu kinachohitajika. Zingatia hapa kwamba ATCL inashindana na mashirika ambayo yana uzoefu wa miongo kadhaa na mitaji mikubwa.
Tatu ATCL imekuwa ikikabiliwa na hasara na Changamoto za Kifedha . Pamoja na uwekezaji mkubwa, Ripoti mbalimbali za ukaguzi wa serikali zimewahi kuonyesha kwamba shirika limekuwa likipata hasara mfululizo kiasi cha kutegemea msaada wa serikali. Hii ina maana kwamba mwananchi anayelipa kodi anabeba sehemu ya gharama. Fedha zinazoweza kwenda kwenye huduma nyingine zinaelekezwa kwenye uendeshaji wa shirika lisilo na faida, na uwajibikaji wa kibiashara unakuwa dhaifu kwa sababu hasara inaweza kufunikwa na serikali.
Zingatia kwamba tatizo kubwa si hasara ya muda mfupi. Mashirika mengi ya ndege duniani hupata hasara katika miaka ya mwanzo, lakini huendelea kukua, kukomaa na hatimaye kutengeneza faida. ATCL imekuwa ikidumaa badala ya kukua, na hakuna mpango maalum unaoonyesha lini ATCL itaweza kusimama yenyewe bila ruzuku ya serikali.
Swali ambalo kila mtanzania anaweza kujiuliza ni: Je, Kununua Ndege nane mpya: gharama Inaweza kuwa kubwa kiasi gani? Jibu ni kwamba bei ya ndege inategemea aina yake. Kwa makadirio Ndege ndogo za kikanda zinaweza kugharimu kati ya dola milioni 30–70, Ndege za ukubwa wa kati zinaweza kuwa dola milioni 80–120, na Ndege kubwa za masafa marefu zinaweza kuzidi dola milioni 200. Kwa hiyo ndege nane zinaweza kuhitaji uwekezaji wa:
Dola milioni 500 hadi zaidi ya dola bilioni 1.5
ambayo ni sawa na mamia ya mabilioni hadi zaidi ya trilioni kadhaa za shilingi za Tanzania.
Hapa ndipo swali la msingi linapoibuka Je, kuna maeneo mengine ambayo fedha hizo zingezalisha ajira na mapato makubwa zaidi? Ukweli ni kwamba fedha za kununulia Ndege nane zinaweza kubadilisha kilimo nchini. Asilimia kubwa ya wananchi wanategemea kilimo moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Kwa sasa kilimo kina changamoto kubwa ikiwa pamoja na ukosefu wa miundombinu ya umwagiliaji, teknolojia duni isiyoendana nacwakati, uhaba wa masoko ya uhakika, utaalam mdogo wa hifadhi ya mavuno na chakula, upotevu mkubwa wa mazao baada ya mavuno. Fedha zinazoweza kununua ndege nane zingeelekezwa kwenye kilimo zinaweza kufanya mapinduzi makubwa.
Badala ya kuwekeza kwenye Ndege, serikali ingeweza kuanzisha maelfu ya hekta za mashamba ya umwagiliaji, kuongeza uzalishaji wa mpunga, mahindi, ngano na mboga. Na kujenga viwanda vya kuongeza thamani kwa kuchambua na kusindika mazao kama kahawa, korosho, pamba, mbogamboga, matunda na nyama. Hii ingeongeza ajira kwa vijana wengi na mapato ya kuuza nje.
Si hivyo tu, bali pia fedha hizo zingeweza kuboresha Teknolojia kwa wakulima hususan katika upatikanaji wa mbegu bora, matrekta, masoko ya kidijitali, na maghala ya kisasa. Mpango huu ungesaidia kupungua kwa umaskini, kuongezeka kwa mapato ya wakulima, na ongezeko la kodi kwa serikali.
Ieleweke hapa kwamba ATCL ni chombo muhimu, na cha manufaa. Ni kweli kwamba Taifa linahitaji miundombinu ya anga, na Ndege ni sehemu ya uchumi wa kisasa. Bila shirika la taifa Tanzania inaweza kutegemea wageni, biashara inaweza kuathirika na usafiri wa dharura unaweza kuwa changamoto.
Ni kweli pia kwamba Tanzania ina vivutio vikubwa kama Serengeti, Kilimanjaro, Zanzibar, na Ngorongoro na hivyo linahitajika .Shirika la ndege imara linaweza kusaidia kuleta watalii wengi. Na hapa inakuja hoja kwamba wakati mwingine serikali huwekeza katika maeneo ambayo si lazima yapate faida kubwa mara moja kama reli, bandari, meli na kadharika, na kwa mtazamo huu, ATCL inaweza kuonekana kama uwekezaji wa kimkakati.
Hoja inayosisitizwa hapa ni kwamba Ndege mpya hazitatatua matatizo ya msingi kama uongozi usio na ushindani, ukosefu wa mkakati wa kibiashara, utegemezi wa serikali;, na mtandao mdogo wa safari. Kununua ndege bila kurekebisha mfumo ni sawa na kumpa mtu gari jipya bila kuhakikisha ana barabara, mafuta na leseni.
Kumbe watanzania wanaihitaji ATCL, lakini si ATCL isiyowajibika, inayowatwisha mzigo mzito, na yenye mwelekeo usioeleweka. Tanzania inaweza kuwa na shirika la ndege lenye mafanikio. Lakini mafanikio hayo hayatapatikana kwa kuongeza idadi ya ndege pekee, ni lazima kwanza matatizo ya msingi yashighulikiwe.
Kabla ya kununua ndege nane zaidi, serikali inapaswa kuuliza maswali magumu:
ATCL imefikia kiwango gani cha kujitegemea kifedha?
Ni masoko gani mapya yatahakikisha ndege hizo zinajaa?
Je, kuna mpango wa wazi wa kupata faida?
Je, fedha hizo zingekuwa na athari kubwa zaidi zikipelekwa kilimo, afya, elimu au viwanda?
Ni muhimu sana viongozi wazingatie kwamba uwekezaji wa ndege unaweza kuwa kichocheo cha maendeleo ikiwa unasimamiwa kitaalamu. Lakini unaweza pia kuwa shimo la fedha za umma ikiwa unafanywa kwa misingi ya fahari ya kitaifa badala ya hesabu za kiuchumi.
Kwa taifa linalokabili changamoto za ajira, umaskini na uzalishaji mdogo mjadala mkubwa unapaswa kuwa “Ni uwekezaji upi utabadilisha maisha ya Watanzania wengi zaidi kwa gharama ndogo na faida kubwa zaidi?”
Uwe na amani.






Comments