top of page

Matumizi ya Viuatilifu Hatari Nchini - Rais Anadanganywa?


Katika jitihada za kuinua kilimo na kukabiliana na changamoto za uzalishaji, Tanzania imeendelea kuruhusu matumizi ya viuatilifu ambavyo vimepigwa marufuku katika mataifa mengine kama Marekani na Ulaya. Viuatilifu hivi hatarishi vinaweza kusaidia kwa muda mfupi katika kuzalisha mazao mengi lakini vina madhara makubwa ya muda mrefu kwa afya ya binadamu, mazingira, na uchumi wa taifa. Makala hii inaangalia kwa kina uhusiano wa kuendelea kwa matumizi ya viuatilifu hivyo na taarifa anazopewa mheshimiwa Rais na wataalam wake.


Kwa kifupi mjadala wa matumizi ya viuatilifu hatari nchini umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu. Wataalam na wahamasishaji wa kilimo hai wameishauri serikali mara nyingi kuhusu hatari ya kuruhusu matumizi ya viuatilifu hivyo, na kutaka viondolewe. Kwa kifupi kuendelea kuruhusu matumizi ya viuatilifu hivyo ni sawa na kumuacha nyoka mwenye sumu akae chumbani kwako kwa sababu anakula panya wanaokusumbua. Yamkini uwepo wa nyoka huyo ni hatari kuliko panya . Ni kwa sababu hii tumeamua kulitupia macho mawili jambo hili kuona undani wake.


Tarehe 6 Novemba 2024 Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya Muhimbili (MUHAS) kiliendesha kongamano lililojadili suala la viuatilifu na afya katika Afrika mashariki. Kongamano hilo lilimalizika kwa kutoa chapisho lililoainisha viuatilifu hatarishi na madhara yake. Chapisho hilo lililoandikwa na William Nelson Mwakilasya, Baldwina Tita Orlik, Edson Mathias Protas na Aiwerasia Vera Ngowi limeeleza kwa kina hatua zinazopaswa kuchukuliwa kulinda afya ya watu na usalama wa mazingira. (Soma Kiambatisho A chini kabisa)


Naye Dokta Mwatima Juma wa Kilimo Hai aliwahi kueleza wasiwasi wake kuhusu serikali kutochukua hatua za kudhibiti viuatilifu vinavyojulikana kuwa na madhara . Kabla ya hapo Taasisi iitwayo Pestcide Action Network International (PAN International) ilitoa orodha ya viuatilifu hatari, vyenye sumu inayoweza kuleta madhara kwa binadamu, wanyama, wadudu na mazingira. PAN International ilitoa pendekezo kwa serikali za nchi husika kuondoa viuatilifu hivyo kwa manufaa ya watu wake na mazingira (Soma hapa) https://pan-international.org/pan-international-consolidated-list-of-banned-pesticides/


Pamoja na ushauri huo serikali imeonesha kusita kuchukua hatua kwa kisingizio cha kuogopa kutokea mlipuko wa wadudu wa mazao na kushuka kwa uzalishaji unaoweza kuathiri taifa. Wataalam mbalimbali wa wizara ya Kilimo wamepinga hadharani na kutoa matamko kwenye vyombo vya habari wakitetea haja ya kuendelea kutumia viwatilifu hivyo kwa sababu zilizotajwa. Hivi karibuni profesa Joseph Ndunguru wa afya ya Kilimo alitoa maelezo kupitia TBC akipinga kuondolewa haraka kwa viwatilifu hatari kwa sababu mbalimbali.


Mbaya zaidi mamlaka inayosimamia viwatilifu TPHPA imeondoa orodha ya viwatilifu vinavyotajwa kuwa hatari kwenye tovuti yake jambo linaloashiria kutaka kuwaficha ukweli wananchi ili waendelee kuvitumia.. Wakulima na wadau wengine wanajiuliza kwanini mamlaka hiyo yenye wajibu wa kusimamia viwatilifu inafanya uhuni huo? Kwa lengo gani na kwa faida ya nani? Kwa nini inaamua kuwaficha ukweli wananchi?


Jambo hili limeleta ukakasi mkubwa kwa wananchi. Wengi wanafikiri hizo ni njama za baadhi ya wakubwa katika wizara ya Kilimo na serikalini kulinda matumizi ya viuatilifu hatari kwa manufaa yao. Zipo taarifa kwamba baadhi ya wakubwa katika wizara ya kilimo na serikalini ndio wamiliki wa makampuni yanayosambaza viwatilifu vilivyopigwa marufuku. Viwatilifu hivyo huwapatia faida kubwa kwani huingizwa nchini kwa bei rahisi kwa kuwa vimepigwa marufuku sehemu nyingine duniani, lakini huuzwa nchini kwa bei ya juu kwa sababu wakuluma (wasio na elimu) wamesha vizoea


Baadhi ya viuatilifu hatarishi vinavyotumika Tanzania ni pamoja na:Paraquat ambayo madhara yake ni kuvuruga mfumo wa upumuaji na figo kwa binadamu, lakini pia huchafua udongo na maji, na kudhuru viumbe hai muhimu kama wadudu wa asili na minyoo.


Kiuatilifu Chlorpyrifos husababisha matatizo ya mfumo wa neva, hasa kwa watoto, na kuhusishwa na magonjwa sugu kama saratani. Pia huharibu mazingira kwa kuua mifumo ya ikolojia kwa kuathiri wadudu wa manufaa kama nyuki na ndege.


Kiuatilifu DDT (Hata kama matumizi yake yanapungua bado hutumika kinyume cha sheria) Husababisha saratani na matatizo ya homoni. Pia huharibu mazingira kwa kuweka sumu kwenye mnyororo wa chakula, kuanzia viumbe vidogo hadi wanyama wakubwa.


Kiuatilifu Atrazine husababisha matatizo ya mfumo wa uzazi na saratani na pia huharibu mazingira kwa kuua viumbe vya majini kwa kuchafua vyanzo vya maji.

(Kusoma orodha kamilifu angalia jedwali lililoambatishwa).


Kwa ujumla viuatilifu hatari husababisha Kuongezeka kwa magonjwa kama vile sumu kali, uharibifu wa ini na figo, na matatizo ya kupumua kwa wakulima na walaji wa mazao yenye mabaki ya viuatilifu. Kuongezeka kwa mzigo wa magonjwa sugu, na hivyo kuongeza gharama za huduma za afya.


Kiuchumi Viuatilifu hatari hupunguza uwezo wa mazao ya Tanzania kushindana katika masoko ya kimataifa. Nchi zilizoendelea zinazuia uingizwaji wa vyakula vilivyozalishwa kwa viuatilifu hatari na iko hatari ya kuua kabisa soko la nje. Pamoja na hilo viuatilifu hivi huathiri udongo, maji, na hewa, na kuharibu viumbe wa asili kama nyuki na wadudu wanaosaidia uchavushaji.


Hatua Zinazopaswa Kuchukuliwa na Serikali:

Ni muhimu serikali ifuate mfano wa mataifa yaliyoendelea kwa kuharamisha moja kwa moja matumizi ya viuatilifu hatarishi kama Paraquat, Chlorpyrifos na vyote vilivyothibitika kuwa na madhara kwa binadamu na mazingira. Serikali isikubali kuingizwa kwenye mtego wa kusubiri kwani madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi baadae.


Serikali iendelee kutoa elimu kwa wakulima mbinu za kilimo cha asili zisizohitaji viuatilifu au kutumia viuatilifu mbadala salama. Hili liende sambamba na kuimarisha mfumo wa udhibiti wa ubora wa viuatilifu vinavyoingizwa nchini kupitia maabara za kisasa, na kuboresha Taasisi za utafiti kama TARI (Tanzania Agricultural Research Institute) kufanya tafiti za mbadala wa viuatilifu hatarishi.


Serikali pia iweke mkazo kwenye mipango ya muda mrefu hasa Katika Kilimo Hai. Hii ni pamoja na kuwekeza katika mafunzo, teknolojia, na masoko ya kilimo hai ambacho hakitegemei viuatilifu vya kemikali. Sambamba na hili serikali iangalie sera zinazohimiza matumizi ya viuatilifu salama pekee, na kuruhusu teknolojia za kisasa kama vile kilimo cha mseto na matumizi ya bio-pesticides.


Ili kukomesha uingizaji haramu wa viuatilifu hatari ni muhimu serikali iwekeze kwenye ushirikiano wa kikanda na mikataba ya kimataifa kama Stockholm Convention na Rotterdam Convention inayolenga kudhibiti kemikali hatarishi.

Mhe. Rais, ni muhimu aendelee kuona umuhimu kuwa afya ya wananchi na ustawi wa mazingira ni mambo ya msingi kwa maendeleo ya taifa letu. Matumizi ya viuatilifu hatari ni kikwazo kwa malengo haya. Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka na za muda mrefu kuhakikisha kuwa kilimo chetu kinakuwa endelevu, salama, na chenye tija bila kudhuru maisha na mazingira. Ni wakati wa kuchukua hatua thabiti kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.



 
 
 

Comentarios


bottom of page