Kusimama na Kuanguka kwa 4R na Mustakabali wa Siasa za Tanzania
- Rev. Godwin Chilewa
- Oct 3, 2024
- 5 min read

Tanzania ni nchi yenye historia ya kipekee ya kisiasa barani Afrika, hasa kutokana na juhudi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuanzisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi baada ya miaka mingi ya chama kimoja. Kuanzishwa kwa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992 kulifungua ukurasa mpya katika siasa za Tanzania, hatua iliyokuwa na nia ya kuifanya nchi kuwa na mazingira bora ya kisiasa ambapo vyama na viongozi wangeweza kubadilishana madaraka kwa amani, kama ilivyo Marekani.
Katika awamu ya pili ya urais, Rais Benjamin Mkapa (1995-2005) alifanya juhudi kubwa kuimarisha demokrasia, hasa kwa kusimamia uchumi wa soko huria na kuweka misingi thabiti ya uwajibikaji serikalini. Kipindi chake kiliweka mazingira ya maendeleo ya kisiasa na kiuchumi. Alipofuata Rais Jakaya Kikwete (2005-2015), mchakato wa kidemokrasia uliimarika zaidi. Kikwete alifungua nafasi kwa vyama vya upinzani na kutoa uhuru zaidi kwa vyombo vya habari. Chaguzi chini ya Kikwete zilionekana kuwa huru zaidi, ingawa changamoto bado zilikuwapo, kama vile matumizi ya rasilimali za serikali na chama tawala (CCM) kwenye kampeni.
Hata hivyo, muelekeo wa kisiasa ulianza kubadilika wakati wa utawala wa Rais John Magufuli (2015-2020). Magufuli alichukua hatua kali za kudhibiti upinzani, kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari, na kuweka vizuizi kwa asasi za kiraia. Licha ya kuwa na rekodi nzuri katika sekta ya maendeleo ya miundombinu, utawala wa Magufuli ulikuwa wa mabavu, na ulivuruga mchakato wa kidemokrasia, kujenga msingi wa siasa za udhibiti mkali. Hatua hizi zilisababisha uhuru wa kisiasa nchini kudidimia, ambapo uchaguzi mkuu wa 2020 ulikumbwa na ukiukwaji wa haki na kuminya nafasi ya upinzani kushiriki kikamilifu.
Baada ya kifo cha Magufuli, Rais Samia Suluhu Hassan alichukua hatamu za uongozi mwaka na kuja na filosofia ya “4R” – Reconciliation, Resilience, Reforms, na Rebuilding. Lengo lilikuwa kurekebisha makosa ya utawala wa Magufuli. Samia alijaribu kurudisha hali ya upatanishi wa kisiasa kwa kuanzisha mazungumzo na upinzani. Hata hivyo, ingawa alitoa ahadi nyingi za kuleta mageuzi, na kuanza kuzifanyia kazi inaonekana kasi yake ya kuleta mageuzi imepungua.
Zipo sababu nyingi zilizosababisha kasi ya Rais Samia kupungua hususan katika kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa, na baadae (mwakani) uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani.
1. Mabaki ya Mfumo wa Udhibiti Wapinzani
Marehemu Rais Magufuli aliimarisha kwa kiwango cha juu mfumo wa kiutawala uliojengwa kwa misingi ya udhibiti mkali, na matumizi ya nguvu za ziada (mabavu) dhidi ya upinzani. Kuubadilisha mfumo huu imekuwa ngumu, hasa kwa kuwa sehemu ya biongozi wa CCM bado wanaendelea kufurahia faida za kuwa na mfumo wa utawala usioheshimu kikamilifu misingi ya demokrasia. Upo uwezekano mkubwa kwamba Rais Samia anashinikizwa kutupilia mbali filosofia yake ya 4R ili kukisaidia Chama Cha Mapinduzi kupata ushindi katika chaguzi zijazo.
2. Mwenendo wa Kisiasa wa CCM
CCM, kama chama tawala, kimekuwa na ushawishi mkubwa katika mifumo ya kisiasa, kiuchumi, na kijamii. Kuna changamoto kubwa ndani ya chama katika kujitenga na urithi wa udhibiti wa Magufuli, huku baadhi ya wanachama wakipendelea hali hiyo kuendelea ili kulinda maslahi yao. Japokuwa watendaji wa serikali hususan wakuu wa wilaya, wakurugenzi (DED) na watendaji wengine hawatakiwi kubagua au kufanya upendeleo kwa CCM unaopelekea ukiukaji wa haki na uvunjaji wa sheria, viongozi wengi wamekuwa wakifanya hivyo kwa lengo la kulinda maslahi yao na au kuitwa “Si mwenzetu.”
3. Ukosefu wa Kasi ya Mageuzi.
Ingawa mheshimiwa Rais Samia Suluhu ameonesha nia njema ya kuleta mageuzi, utekelezaji wa falsafa yake umekuwa wa taratibu. Hii imefanya wananchi na wapinzani kuona kuwa mabadiliko yanayotakiwa hayafiki haraka, na baadhi yao wanaanza kupoteza matumaini. Kusuasua kwa mageuzi ya falsafa ya 4R kunachangiwa zaidi na hofu ya viongozi wa juu wa CCM kuhusu hatima ya chama chao katika uchaguzi mkuu ujao kama ilivyoelezwa. Kwa bahati mbaya baadhi ya viongozi hao ji watu wenye ushawishi mkubwa.
4. Matatizo ya Kikatiba na Kisheria:
Mfumo wa uchaguzi na taasisi za kikatiba bado zina upungufu katika kuwalinda wapinzani dhidi ya mbinu za matumizi mabaya ya rasilimali za umma na nguvu za dola. Uhitaji wa marekebisho ya katiba, ambayo yatawezesha uhuru wa tume ya uchaguzi na vyombo vya habari, ni jambo lililoahirishwa kwa muda mrefu kwa faida ya chama tawala. Uahirishaji huo ingawa unaonekana kukisaidia chama tawala kwa sasa upo uwezekano wa kuleta madhara makubwa baadae, na hata kwa CCM yenyewe.
Nini Kifanyike?
Ili kurekebisha hali ya kisiasa na kuimarisha demokrasia nchini Tanzania, yafuatayo yanapaswa kuzingatiwa:
1. Marekebisho ya Katiba:
Kuna haja kubwa ya kuundwa kwa katiba mpya, au kufanywa mabadiliko ya kikatiba yanayolenga kuimarisha uhuru wa tume ya uchaguzi, kulinda haki za vyama vya upinzani na vyombo vya habari, na kuhakikisha kuwa wagombea wa urais wanakuwa na uwanja sawa wa kushindana kisiasa. Tanzania inapaswa kuiga kielelezo cha nchi zilizofanikiwa kidemokrasis ambapo ushindani wa kisiasa (upinzani) au kuwa na mawazo tofauti si uadui.
2. Uundaji wa Tume Huru ya Uchaguzi:
Ili kuleta uchaguzi wenye uaminifu zaidi, ni muhimu kuwa na tume huru isiyozingatia maslahi ya chama chochote. Hii itapunguza malalamiko yanayohusiana na udanganyifu wa kura na ukosefu wa haki kwa vyama vya upinzani. Mfumo wa sasa unatoa upendeleo wa wazi kwa chama tawala kwa sababu wateule wa rais ndio walio na dhamana ya kusimamia chaguzi zote.
3. Uhuru wa Vyombo vya Habari:
Vyombo vya habari vinapaswa kuwa huru kabisa kuripoti masuala ya kisiasa bila kuingiliwa. Hii itasaidia kuwapa wananchi taarifa sahihi kuhusu mchakato wa uchaguzi na utendaji wa serikali. Hivi sasa kuna ombwe kubwa katika uhuru wa habari na kujieleza ambapo chama tawala kinapewa nafasi na upendeleo wa kipekee kwenye vyombo vya habari.
4. Usawa katika Matumizi ya Rasilimali za Serikali:
Ni muhimu kuwe na udhibiti wa matumizi ya rasilimali za umma na serikali wakati wa kampeni za uchaguzi ili kuondoa tofauti kubwa kati ya chama tawala na vyama vya upinzani. Hivi sasa chama tawala kinatumia rasilimali nyingi za taifa kubaki madarakani na au kupambana na wapinzani. Ni vyema iundee sheria wazi inayoainisha mipaka ya matumizi ya rasilimali za serikali kwa shughuli za chama.
5. Mazungumzo ya Kisiasa na Upinzani:
Kuendeleza majadiliano ya kitaifa na vyama vya upinzani kuhusu mustakabali wa kisiasa nchini ni njia moja muhimu ya kurudisha hali ya upatanishi wa kisiasa. Hata hivyo jambo hili linapaswa kufanywa kwa moyo safi bila hila na udanganyifu wowote.
Matokeo ya Uchaguzi wa 2025
Uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 unaweza kuakisi changamoto za kisiasa zilizopo sasa. Ikiwa mageuzi ya kisiasa hayatatekelezwa kwa kasi na umakini, kuna uwezekano mkubwa CCM itaendelea kushinda uchaguzi. Hata hivyo, upinzani unaweza kushika kasi ikiwa changamoto hizi zitashughulikiwa. Mgawanyiko ndani ya CCM pia unaweza kuathiri mwelekeo wa uchaguzi, huku wananchi wakiwa na matarajio makubwa ya mabadiliko baada ya awamu mbili zilizopita za urais ambazo zilileta hisia tofauti kuhusu demokrasia ya Tanzania.
Kwa sasa, matumaini ya demokrasia yenye nguvu Tanzania yako mikononi mwa mageuzi ya kisiasa na ahadi za Rais Samia kufanikisha filosofi yake ya “4R”. Ikiwa haitafanikiwa kufanya mabadiliko haya, demokrasia ya Tanzania itaendelea kukwama, na mchakato wa chaguzi huru na haki utakuwa ndoto isiyotimia. Ni muhimu sana viongozi wote watambue umuhimu wa kurekebisha mfumo wa siasa nchini kwa kuanzia na utekelezaji wa falsafa ya 4 R kama alivyoahifi mheshimiwa Rais SSH.
Rev. Godwin Chilewa
Comments