UGAIDI AU SIASA ZA HOFU? Uchambuzi wa Kiitelijensia Kuhusu Mkakati wa Serikali Katika Kudhibiti Maandamano Nchini
- Rev. Godwin Chilewa
- 20 hours ago
- 5 min read
Updated: 4 hours ago
Rev. Godwin Chilewa

Hivi sasa kuna mwelekeo unaotia mashaka kwa jinsi serikali inavyoshughulikia maandamano ya raia na upinzani wa kisiasa. Hatua iliyochukuliwa hivi karibuni ya kuwakamata watu zaidi ya 130, wakiwemo wasomi kama muhadhiri wa chuo kikuu cha Dodoma, na kuwafungulia mashtaka ya ugaidi, imezua taharuki na mjadala mpana kuhusu usalama wa taifa na uhuru wa kiraia. Watu wengi ikiwa pamoja na wanasheria na wanasiasa wakongwe wanajiuliza kama mkakati huu unasaidia kuleta utulivu wa kweli au unazalisha mazingira ya hofu yanayoweza kulipua balaa kubwa zaidi?
Msingi wa Kiitelijensia
Kwa kawaida kuna dhana kuu mbili zinazotumiwa zaidi katika uchambuzi wa kiitelijensia hususan katika mazingira na aina ya tatizo kama la Tanzania. Dhana ya kwanza ni kutumia Uwezo wa Nguvu (Coercive Capacity). Huu ni uwezo wa dola kutumia vyombo vyake vya nguvu kama vile polisi, jeshi, sheria kali, na vyombo vya upelelezi katika kulazimisha utiifu wa wananchi au kudhibiti hali ya hatari. Hii inajumuisha kukamata na kushitaki, matumizi ya mabavu au nguvu za kimwili kudhibiti maandamano, kuweka sheria kali au hali ya hatari na kudhibiti taarifa (information control).
Serikali imekuwa ikitumia sana utaratibu huu pengine kwasababu huleta utulivu wa haraka (short-term stability). Hata hivyo njia hii ina hatari kubwa kwani ikitumika kupita kiasi, hujenga hofu, chuki, na upinzani wa ndani kwa ndani hali inayoweza kuchochea vurugu na hata uasi.
Dhana ya pili ni Uhalali wa Kisiasa (Political Legitimacy). Hii hufanya kazi kutegemea kiwango ambacho wananchi wanakubali na kuamini kuwa serikali yao ina haki ya kutawala. Uhalali wa kisiasa hujengwa kupitia uchaguzi huru na haki, haki na usawa mbele ya sheria, uwazi na uwajibikaji, na uwepo wa taratibu za thati katika kusikiliza na kujibu mahitaji ya wananchi
Uhalali wa kisiasa ni muhimu mno kwa serikali. Huleta utulivu wa kudumu (long-term stability) kwa kuwafanya wananchi wawe watulivu hata katika nyakati ngumu. Serikali inapopoteza uhalali wa kisiasa wananchi huacha kushirikiana nayo, na hata hatua ndogo za kiusalama zinakuwa ngumu kutekelezeka. Kwa hiyo dola imara ni ile inayosawazisha nguvu (coercion) na uaminifu (legitimacy).
Matumizi ya mashtaka ya ugaidi dhidi ya raia wanaoshiriki au kuhusishwa na maandamano yanaweza kuingia kwenye kipengele cha kwanza, kuleta utulivu na udhibiti wa haraka na kwa muda lakini unaathiri vibaya kipengele cha pili, uaminifu wa wananchi kwa serikali yao.
Uchambuzi unaonyesha kuwa pale ambapo dola inapoteza uhalali wake, hata kama ina nguvu kubwa ya kiusalama, huweza kuingia kwenye mzunguko hatari kwa kuongezeka kwa upinzani wa chini kwa chini, kupungua kwa ushirikiano wa raia na hatimaye kuibuka kwa migogoro mikubwa zaidi.
2. Je, Kuhusisha Ugaidi ni Mkakati Sahihi?
Kisheria na kiusalama, ugaidi una tafsiri nzito: ni vitendo vinavyolenga kuleta hofu ya kitaifa au kimataifa kwa kutumia vurugu na vitisho dhidi ya raia au miundombinu kwa lengo la kulazimisha jambo fulani. Kuupanua ufafanuzi huu na kuujumuisha katika shughuli za kisiasa au maandamano kuna athari kadhaa:
Kwanza ni Kupunguza uzito wa neno “ugaidi” au kulifanya lipoteze maana yake halisi. Hii inaweza kufanya vita dhidi ya ugaidi halisi kuwa dhaifu. Pili inachochea chuki na mgawanyiko. Wananchi wanapoona sheria ya ugaidi inatumika kisiasa, wanaanza kuichukulia serikali kama mpinzani badala ya mlezi. Hii inaweza kuzalisha “radicalization” ya kimyakimya. Watu waliokuwa na madai ya kawaida wanaweza kuhamia kwenye misimamo mikali zaidi. Kwa lugha ya kiintelijensia, hii huitwa threat amplification through misclassification yaani, serikali inajitengenezea tishio kubwa zaidi kwa kulipa jina lisilo sahihi tatizo lililopo.
3. Athari za Siasa za Hofu (Politics of Fear)
Uzoefu unaonesha kuwa siasa za hofu hutumia nguvu, vitisho, na sheria kali kudhibiti jamii Kwa muda mfupi, zinaweza kuonekana zinafanya kazi. Lakini kwa muda mrefu, zina madhara makubwa. Huweza kuvunja mshikamano wa kitaifa hasa wananchi wanapohisi hawako salama kutoa maoni yao, wanajitenga na dola. Taifa linagawanyika kimtazamo, wanakuwa rahisi kutumika na maadui wa nje.
Mbaya zaidi ni kuwa hali hii inaweza kusababisha kudhofika kwa taasisi za dola. Mahakama, polisi, na vyombo vya usalama vinapoonekana kutumika kisiasa, vinapoteza heshima na uaminifu. Wananchi huwachukia watendaji wake na kuwaweka kwenye kundi la vibaraka au wasaliti. Hali hii pia huchangia kutengeneza intelligence blind sport. Wananchi wanapokosa imani na serikali, hawatoi taarifa muhimu za kiusalama. Hii ni hatari kubwa kwa usalama wa taifa kuliko maandamano yenyewe.
Pamoja na hayo yote, upo uwezekano mkubwa wa kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa. Mashirika ya haki za binadamu na washirika wa maendeleo huanza kuhoji mwenendo wa nchi, jambo linaloweza kuathiri uwekezaji na diplomasia. Aidha
4. Uchambuzi Linganishi
Ili kuelewa vizuri athari za mkakati huu, ni muhimu kuangalia mifano ya nchi nyingine zilizowahi kukumbwa na migogoro.
(a) Egypt
Baada ya maandamano ya 2011, serikali ilitumia nguvu kubwa za kiusalama na kuwahusisha wapinzani na ugaidi. Matokeo yake utulivu wa muda mfupi ulipatikana. Lakini upinzani ulijificha chini kwa chini, nchi ikaingia katika hali ya udhibiti mkali wa muda mrefu na kupungua kwa uhuru wa kiraia
(b) Kenya
Nchi hii nayo ilikabiliwa na msukumo mkubwa wa maandamano ya Gen Z. Katika baadhi ya vipindi vya maandamano, serikali ilijaribu kuchanganya nguvu na mazungumzo. Matokeo yake pale nguvu ilipotumika kupita kiasi, maandamano yaliongezeka. Pale mazungumzo yalipopewa nafasi, mvutano ulipungua na suluhu iliweza kuonekana.
(c) Afrika ya Kusini
Kwa muda mrefu serikali imekumbana na maandamano ya kijamii lakini imewekeza zaidi katika taasisi na mazungumzo. Matokeo yake ni kuwa changamoto bado zipo, lakini uhalali wa kisiasa umeendelea kuwepo, na mfumo haujavunjika
(d) China
Inatumia sana coercive capacity kudhibiti maandamano. China imewekeza katika ufuatiliaji wa kidijitali ikiwa pamoja na utambuzi wa sura (facial identification) na social credit. Matokeo yake kuna utulivu mkubwa wa nje unaonekana, lakini taarifa nyingi hudhibitiwa, na kuna hatari ya migogoro ya ghafla bila onyo (sudden instability risk)
Kwa wana intelijensia hili ni funzo kwamba hakuna nchi inayoweza kudumisha utulivu wa muda mrefu kwa nguvu pekee bila uhalali wa kisiasa.
5. Kitendawili cha Maridhiano
Tatizo lingine ni kuwa serikali inapojitangaza kutaka maridhiano huku ikiendelea kutumia mbinu za ukandamizaji, inajenga kile kinachoitwa katika uchambuzi wa kiintelijensia kama “strategic contradiction.” Hali hii husababisha kupotea kwa uaminifu wa mazungumzo, wapinzani kuona mazungumzo kama mtego, na jamii kushindwa kutofautisha kati ya dhamira halisi na propaganda. Kwa maneno mengine, huwezi kujenga amani kwa kutumia lugha ya maridhiano huku vitendo vyako vikizungumza hofu.
6. Kwa Nini Serikali Inaendelea na Mkakati Huu?
Sababu kadhaa za kiintelijensia zinaweza kueleza mwenendo huu: Sababu ya kwanza ni hofu ya kupoteza udhibiti wa kisiasa. Maandamano huonekana kama dalili ya kuporomoka kwa mamlaka, na kukua kwa nguvu ya upinzani nchini. Kiongozi asiyejiamini huhisi maandamano ni dharau kwake (personal) badala ya nguvu ya msukumo wa kiu ya mabadiliko duniani.
Sababu ya pili ni tafsiri finyu ya usalama wa taifa. Usalama unaangaliwa zaidi kama utulivu wa kisiasa kuliko ustawi wa kijamii. Hili ni kosa kubwa hususan katika siasa za dunia ya leo. Katika nchi zetu hili limechangiwa sana na urithi wa mifumo ya kiusalama ya zamani. Mifumo hiyo ilijengwa katika enzi za udhibiti mkali wa kikoloni, na haijafanyiwa marekebisho hivyo inaendelea kutumika kama ilivyo.
Tatu ni upungufu wa taarifa sahihi (intelligence failure) au makosa ya kiuchambuzi na ushauri. Hii huweza kufanya maamuzi mengine kufanywa kwa hofu, taarifa zisizo kamili, au taarifa zilizoharibiwa kwa ushabiki, uchawa na ubinafsi. Tatizo hili huweza kuanzia kwenye vyanzo vya taarifa, au kwa watumiaji wa taarifa (viongozi wa kisiasa).
7. Ushauri wa Kiintelijensia kwa Serikali
Ili kujenga utulivu wa kudumu, serikali inapaswa kuzingatia yafuatayo:
(a) Kutenganisha wazi kati ya ugaidi na maandamano ya kiraia. Hii itarejesha uhalali wa sheria na kuimarisha vita dhidi ya ugaidi halisi.
(b) Kujenga mifumo ya kusikiliza malalamiko ya wananchi (early warning systems) Badala ya kusubiri maandamano, serikali ichambue viashiria vya hasira ya jamii mapema.
(c) Kuwekeza katika “soft power” ya utawala. Ni muhimu yawepo mazungumzo ya kweli, ushirikishwaji, na uwazi. Vitu hivi vina nguvu kuliko mabavu.
(d) Serikali idhamirie kulinda uhuru wa taasisi. Ni muhimu sana Mahakama na vyombo vya usalama viwe huru ili kurejesha imani ya wananchi.
(e) Yafanyike marekebisho ya mkakati wa mawasiliano ya serikali. Badala ya propaganda, kuwe na mawasiliano ya ukweli yanayojibu hoja za wananchi.
Serikali itambue kwamba kutumia mashtaka ya ugaidi kama chombo cha kisiasa ni mkakati hatari unaoweza kutoa utulivu wa muda mfupi lakini ukazalisha mgogoro wa muda mrefu. Historia inaonyesha kuwa amani ya kweli haijengwi kwa hofu bali kwa haki, usawa, na uaminifu. Kama kweli serikali ya Tanzania inataka maridhiano ya dhati, basi ni lazima ibadili mkakati kutoka “kudhibiti wananchi” kwenda “kuwashirikisha wananchi.” Vinginevyo, kila hatua ya kuwakandamiza leo inaweza kuwa mbegu ya mgogoro wa kesho.
Uwe na amani.






Comments