Heshima Isiruke Mipaka ya Eda

Na Rev. Godwin Chilewa
Viongozi wengi wanapokwenda kumpa pole na kumfariji Rais Samia Suluhu Hassan huvaa kanzu (hata kama si Waislam). Wengine huenda mbali zaidi kwa kumpigia magoti kama ishara ya heshima na unyenyekevu. Kitendo hicho ingawa kinaweza kuonekana cha kawaida, kiuhalisia kinaweza kumtia doa mjane (mheshimiwa Rais) kuharibu Eda yake, na au kumdharililisha mbele ya umma wa kiislam.
Siku mbili zilizopita Mufti wa Tanzania Shekhe Abubakar Bin Zuberi Bin Ali alieleza kwamba ingawa mama Samia ni Rais wa nchi, lakini mbele ya Mwenyezi Mungu na umma wa kiislam yeye ni mja, na muumini tu anayejitahidi kuishi kwa kadri ya imani yake. Kwa kuzingatia maneno hayo (ya Mufti) ni vyema mtu anayekwenda kumpa pole mheshimiwa Rais hususan kama amejinasibisha kama muislam (kwa mavazi) ni muhimu azingatie mila na desturi za uislam. Kwa sheria na taratibu za kiislam mwanaume hapaswi kumpigia magoti mwanamke na au kumshika mkono (kama si maharam wake). Kitendo hiki hakiruhusiwi kwa ukawaida , lakini zaidi sana wakati wa Eda.

Kwa mujibu wa maulamaa wa kiislam, kupiga magoti si sehemu ya adabu za Kiislamu. Si sunna ya mtume, wala utaratibu wa kutoa pole katika Uislamu. Mbaya zaidi ni kuwa kitendo hicho kinaweza kutafsiriwa vibaya hata kama nia ni njema. Kwa wengine kinaweza kuonekana kama ishara ya mapenzi au unyenyekevu wa kipekee, jambo lisilofaa katika kipindi cha eda. Zingatia kuwa Eda hulindwa kwa heshima na mipaka. Uislamu unasisitiza utulivu, heshima, na kuepuka ishara zozote zinazoweza kuleta kuvuka mipaka,ukaribu usiofaa au mashaka bila kujali hadhi ya mtu.
Nifafanue hapa kwamba mtu aliyevaa mavazi mengine (yasiyomnasibisha kama muislam) angeweza kueleweka zaidi akipiga magoti, au kumsalimu Rais kwa namna hiyo kwani yako baadhi ya makabila ambayo kupiga goti au kuinama ni sehemu muhimu katika salamu ya mila na desturi zao, Hata hivyo kwa vile Rais yuko katika maombolezo yanayosimamiwa na sheria za Eda ni muhimu watu wa aina hiyo pia wakaendana na utaratibu huo ili kuepusha mkanganyiko na pia kulinda heshima ya Eda.

Kumbe ni muhimu sana wasaidizi wa Rais kuwapa maelekezo sahihi ya kutoa pole wale wote wanaopewa nafasi ya kuonana na Rais (mjane) katika kipindi hiki cha Eda. Hii ni pamoja na namna ya kujiwasilisha, kutumia maneno ya faraja na dua kwa heshima na kudumisha mipaka ya maadili ikiwa pamoja na kuepuka kumshika au ishara za ukaribu (ikiwa si mahram).
Nisisitize hapa kwamba mama Samia Suluhu Hassan ni Rais wa nchi, lakini pia ni mja wa mola, na muumini wa dini ya kiislam. Kwakuwa suala la maombolezo na Eda linasimamiwa na kuwekewa mipaka kwa mujibu wa taratibu za kiislam kwa maoni yangu naona ni muhimu sana wanasiasa, viongozi na wananchi wote wasilichukulie kama fursa ya kujionyesha kwa kufanya vitendo vinavyoweza kuharibu Eda au kudharilisha uislam.
Uwe na amani.






Comments