top of page

Serikali Inauza Ng’ombe kwa Kesi ya Kuku?

Sep 11
3 min read



Ni ukweli usiopingika kuwa shtaka la uhaini linalomkabili Lissu ni miongoni mwa makosa mazito zaidi katika mfumo wa sheria za jinai, lenye adhabu kali ikiwemo kifo . Aidha, mazingira ya kukamatwa kwake na kufunguliwa mashtaka yalihusishwa na hotuba za kisiasa zilizodaiwa kuchochea kuvurugwa kwa uchaguzi. Hali hii imeifanya kesi hii, kwa mtazamo wa wachambuzi wengi wa ndani na nje ya nchi, kuonekana kuwa na sura ya kisiasa zaidi kuliko ya jinai ya kawaida.


Katika hatua ya hivi karibuni, Mahakama imeagiza kuitwa kwa viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kutoa ushahidi. Kwa lugha ya kiintelijensia, hatua hii inaingia katika eneo la “high-risk institutional exposure.” Kuletwa kwa viongozi hawa katika jukwaa la wazi la mahakama kuna uwezekano mkubwa wa kufichua taarifa nyeti za kiusalama, ikiwa ni pamoja na mbinu za kioperesheni, mifumo ya ukusanyaji taarifa na mienendo ya maamuzi ya ndani ya dola. Hali hii inaweza kudhoofisha uwezo wa muda mrefu wa vyombo vya usalama kulinda taifa dhidi ya vitisho vya ndani na nje.


Zaidi ya hapo, mwenendo wa kesi hii tayari umeingia katika kile kinachojulikana kitaalamu kama “strategic narrative contestation,” ambapo mchakato wa kisheria unabadilika kuwa jukwaa la ushindani wa simulizi za kisiasa. Kwa kuwa mshtakiwa ana uzoefu mkubwa wa sheria na siasa, uwepo wa viongozi wa juu wa dola mahakamani unampa fursa ya kujenga hoja zinazoweza kuibua taswira ya ukandamizaji wa kisiasa. Hali hii ina uwezo wa kugeuza Mahakama kutoka kuwa chombo cha haki na kuwa uwanja wa mvutano wa kisiasa mbele ya umma wa ndani na jumuiya ya kimataifa.


Katika uwanja mpana wa usalama wa taifa, hatua hii inaleta kile kinachoitwa “institutional strain.” Inavunja ule utenganisho muhimu kati ya mifumo ya kiusalama na mchakato wa kisiasa, na hivyo kuhatarisha hadhi, uaminifu na morali ya vyombo vya dola. Aidha, inaweza kuweka mfano hatari wa kisheria (precedent) ambapo viongozi wa juu wa usalama wanaanza kuhusishwa moja kwa moja na migogoro ya kisiasa, jambo linaloweza kudhoofisha mfumo wa amri na udhibiti ndani ya taasisi hizo.


Ni muhimu pia kuzingatia kuwa kesi hii imejengwa katika mazingira ya mvutano wa kisiasa uliofuatia uchaguzi wa mwaka 2025, ambao uliambatana na maandamano, ukamataji wa watu wengi na mijadala mikali kuhusu haki za kisiasa . Katika mazingira kama haya, mwenendo wa kesi unaweza kuwa kichocheo cha kuongeza mgawanyiko wa kijamii na kisiasa, badala ya kuleta utulivu. Kwa kifupi serikali ni kama inauza ng’ombe kugharimia kesi ya kuku.


Kisheria, mamlaka ya kuendesha au kusitisha mashitaka ya jinai yako chini ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa mujibu wa kanuni ya prosecutorial discretion. Ndani ya mfumo wa sheria, mamlaka haya yanajumuisha uwezo wa kuanzisha, kuendesha au kusitisha mashitaka wakati wowote, ikiwa ni pamoja na kutumia utaratibu wa nolle prosequi kusitisha kesi pale maslahi ya umma yanapohitaji hivyo .

Kwa mantiki hii, ipo njia halali kabisa ya kisheria ya kusitisha kesi hii bila kuvunja misingi ya utawala wa sheria, bali kwa kuilinda kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa.


Kwa kuzingatia tathmini ya kiintelijensia, mwenendo wa sasa wa kesi hii unaashiria hatari ya mkusanyiko wa migogoro (multi-domain risk convergence), ambapo changamoto za kisheria, kisiasa na kiusalama zinakutana kwa wakati mmoja. Hatari hizi ni pamoja na kudhoofika kwa taswira ya dola, kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa, uwezekano wa kufichuka kwa siri za kiusalama, na kuimarika kwa simulizi hasi dhidi ya serikali. Katika hali hii, busara ya kimkakati inahitaji kuchukua hatua za kuzuia madhara kabla hayajakomaa. Historia ya mataifa mbalimbali inaonyesha kuwa migogoro ya kisiasa inapopelekwa katika mifumo ya jinai bila utatuzi wa kisiasa, mara nyingi huishia kuongeza migawanyiko badala ya kuutatua.


Kwa msingi huu ni muhimu kwa Rais kutumia nafasi yake kama Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu, kutoa mwelekeo wa kisera na kimkakati kwa vyombo vinavyohusika, hususan Mkurugenzi wa Mashtaka, ili kutumia mamlaka yake ya kisheria kusitisha kesi hii kwa manufaa mapana ya taifa. Hatua hii haitakuwa udhaifu wa dola, bali itakuwa ishara ya uongozi wenye hekima, unaotanguliza umoja wa taifa, uthabiti wa taasisi na mustakabali wa amani ya nchi.

Hatua hiyo inaweza kwenda sambamba na kuanzishwa kwa mchakato mpana wa mazungumzo ya kitaifa (national dialogue) utakaoshughulikia mizizi ya migogoro ya kisiasa, ikiwemo masuala ya katiba, mfumo wa uchaguzi na ushiriki wa kisiasa.


Sio siri kwamba Taifa lipo katika wakati nyeti unaohitaji maamuzi yenye ujasiri, hekima na mtazamo mpana wa historia. Kesi hii imefika hatua ambayo inaweza kuamua mwelekeo wa nchi kama ni kuelekea kuimarika kwa umoja na utulivu, au kuingia katika mzunguko wa mvutano usio wa lazima.


Uwe na amani

Rev. Godwin Chilewa

 
 
 

Comments


bottom of page