top of page

Umilikishaji Silaha Kiholela - Tutavuna Tunachopanda


Kumiliki silaha ni jukumu kubwa linalohitaji mafunzo maalum, nidhamu, na uangalifu wa hali ya juu. Madhara ya kuongezeka kwa umiliki wa silaha miongoni mwa wananchi, hasa vijana wasiokuwa na mafunzo ya kijeshi au nidhamu madhubuti, ni makubwa na yanaweza kusababisha athari za kijamii na kiusalama.


Ni ukweli usiopingika kwamba mtu aliyebeba silaha ni rahisi zaidi kufanya jeuri, ukorofi na kuanzisha ugomvi kuliko mtu asiye na silaha. Hili ni suala la kisaikolojia na halijalishi muhusika ni mtu wa wapi au dini gani. Uchunguzi uliofanywa sehemu mbalimbali duniani umethibitisha kuwa askari, polisi mwenye bunduki huweza kutumia nguvu ya ziada zaidi kumdhibiti mhalifu kuliko asiyebeba bunduki au mwenye rungu tu. Kwa ujumla silaha si kitu cha kushangilia kuwa nacho.


Wakati serikali ya Tanzania imerahisisha taratibu za raia na makampuni ya ulinzi kumiliki silaha ni vyema viongozi wajiulize kama nchi iko tayari kwa suala hilo. Hii ni kwa sababu hivi sasa Marekani, pamoja na kuwa na polisi na vyombo vingine vingi vya usalama lakini inahangaika kudhibiti mauaji yanayotokana na silaha zilizomilikishwa kihalali kwa wananchi. Baadhi ya majimbo kama New York yameweka taratibu ngumu zinazowabana wamiliki wa silaha toka majimbo mengine kuingia nazo au kuzibeba mitaani wanapokuwa jijini New York.


Kwa ujumla watanzania hatujafikia kiwango cha kila mtu kumiliki silaha. Lakini kama serikali isipoangalia itafika wakati vijana wote wa mjini watakuwa na bastola. Zingatia kwamba mtu anapobeba silaha anashawishika kufanya ubabe bila kujali kama ameipata kihalali au la! Anaimiliki kibinafsi au ni silaha ya serikali. Ili mradi mtu anayo, anaweza kufanya lolote, kwa sababu yoyote, kwa kukusudia au kwa bahati mbaya.


Baadhi ya madhara ya kumiliki au kutembea na bastola ni kama ifuatavyo:


1. Hatari ya Matukio ya Bahati Mbaya:

Watu wengi ambao hawajapitia mafunzo ya kijeshi au usalama wanaweza kukosa ufahamu wa matumizi salama ya silaha. Kwa mfano, mtu anaweza kusahau kuweka silaha katika hali salama au anaweza kuitumia vibaya katika mazingira ya kawaida kama ofisini au nyumbani, hivyo kuongeza uwezekano wa tukio la bahati mbaya. Tukio hili linaweza kuwa hatari zaidi ikiwa kuna watoto wenye udadisi na nafasi ya kugusa silaha hiyo bila uangalizi.


2. Ongezeko la Mauaji ya Wivu na Migogoro ya Kinyumbani:

Mara nyingi, hisia za hasira, wivu, au kutoridhika zinaweza kutokea katika mazingira ya kawaida. Mtu anayemiliki silaha na ambaye hana nidhamu au uvumilivu anaweza kuishia kutumia silaha kwa kushawishiwa na hasira za muda mfupi. Migogoro ya kindugu, mapenzi au biashara inaweza kugeuka kuwa ya hatari ikiwa silaha zitahusishwa. Kijana anaweza kutumia silaha kutishia watu anaohisi wanamnyemelea mpenzi wake na au kujaribu kumtawala mpenzi wake kwa vitisho.


3. Ujambazi na Uhalifu wa Kupangwa: Umiliki wa silaha pia unaweza kuwashawishi baadhi ya vijana wenye utovu wa nidhamu au wanaopenda starehe kujiingiza kwenye tabia hatari ya uhalifu. Wanaweza kuhisi wamepata nguvu au ujasiri wa kufanya ujambazi, kutumia vitisho kwa jamii, au hata kuunda magenge ya kihalifu. Silaha ikitumiwa vibaya, inaweza kuathiri usalama wa raia na kupunguza hali ya amani katika jamii. Kwa kifupi wingi wa silaha mtaani ni hatari kubwa kwa polisi na watumishi wa vyombo vingine vya dora. Nchini Marekani maafisa wa Polisi hujikuta matatani mara nyingi kwa kuua watu wanaodhani wamebeba silaha kumbe sivyo. Hii ni kwa sababu asilimia kubwa ya raia wanatembea na silaha .


4. Hatari ya Mauaji ya Haraiki (Mass Shootings)

Uwepo wa silaha mikononi mwa watu wengi bila udhibiti madhubuti unaweza kuchochea matukio ya mauaji ya haraiki katika maeneo ya umma, kama vile shule, vyuo, au sehemu za burudani. Katika mazingira ambayo jamii inaweza kuingiwa na wasiwasi au kuhisi kutishiwa, ni rahisi mtu aliyekosa utulivu, mwenye matatizo ya kiakili au anayeingiliwa na msongo wa mawazo kuchukua hatua za kuumiza watu wengi. Miaka michache iliyopita wakazi wa Dar es Salaam walishuhudia tukio la kutisha la mtu mmoja aitwae Hamza, aliyefanikiwa kupora silaha ya risasi na kuanza kushambulia watu, hususan polisi kwa bunduki hiyo. Ongezeko la silaha mitaani linaweza kuzalisha wingi wa matukio ya aina hiyo.


Ushauri kwa Serikali ya Tanzania

Serikali inapaswa kuweka vigezo vya umiliki wa silaha ambavyo vitahakikisha kuwa si kila mtu anayeweza kupata silaha kirahisi. Umri, historia ya mtu (hasa kuhusu uhalifu au matatizo ya kiakili), na kiwango cha nidhamu viwe ni baadhi ya vigezo vya msingi. Utaratibu wa sasa hauna matokeo chanya kwani baadhi ya waombaji wamekua wakitumia hila na udanganyifu kupitisha maombi yao kwenye kamati.


Ni muhimu pia serikali iwe makini na askari wanaopewa silaha, na itengeneze utaratibu wa kufuatilia matumizi ya silaha hizo. Hii ni muhimu sana hasa katika kipindi hiki ambapo kuna tuhuma (ambazo hazijathibitishwa) kwamba askari wanatumia silaha kufanya vitendo vya kihalifu ikiwa pamoja na utekaji nyara. Ni vyema jeshi la polidi lichukue hatua kulinda taswira yake isiharibiwe na askari wachache wasio na nidhamu.


Ni vyema serikali iweke utaratibu wa kuhakikisha mtu anayeomba kibali cha kumili silaha awe amepitia mafunzo maalum. Mafunzo haya yanapaswa kuhusisha usalama wa matumizi ya silaha, hatua za kisheria na kiusalama, namna ya kuzuia matumizi mabaya, na pia yajumuishe sehemu ya kisaikolojia ili kupima utayari wa mtu kimwili na kiakili kubeba jukumu la kumiliki silaha. Hivi sasa Tanzania hazina sehemu za kibiashara ambapo raia wanaweza kwenda kufanya mazoezi ya kulenga shabaha. Hii inafanya wamiliki wengi, wasio maaskari kuwa na silaha wasizoweza kuzitumia ipasavyo. Serikali ilishauri jeshi la polisi kujenga sehemu ya shabaha (shooting range) na kuiendesha kibiashara, au itoe fursa kwa muwekezaji binafsi kufanya hivyo.


Ni vyema pia ianzishe mfumo wa usimamizi wa umiliki wa silaha unaojumuisha ukaguzi wa mara kwa mara kwa watu wote wanaomiliki silaha. Wamiliki wa silaha wawe na wajibu wa kuonyesha kwa mamlaka husika kuwa wanatumia silaha hizo kwa njia salama na kwa madhumuni ya kisheria. Jambo hili liende sambamba na utoaji elimu kwa umma kuhusu madhara ya matumizi mabaya ya silaha, hasa kwa vijana. Serikali na wadau wengine wafanye kampeni zinazowaelimisha wananchi juu ya athari za kimwili, kisheria, na kijamii za matumizi mabaya ya silaha.


Ili kuzuia matumizi mabaya, sheria kali zitungwe kwa yeyote atakayehusishwa na matumizi yasiyo halali ya silaha. Adhabu kali zitawatia watu hofu na kuwafanya waepuke tabia za kujihusisha na uhalifu unaohusisha silaha.


Hitimisho:

Kwa kumiliki silaha, mtu anakuwa na jukumu kubwa la kulinda si tu usalama wake tu bali pia usalama wa jamii nzima. Ni jukumu la serikali kuhakikisha kwamba hatua zinazotakiwa zinachukuliwa ili kuzuia matumizi mabaya ya silaha, na vilevile kuwapa wamiliki wa silaha maarifa na ufahamu wa kutosha. Serikali ya Tanzania inahitaji kufanya kazi kwa pamoja na wananchi, kuwapa elimu, na kutekeleza sera kali za usimamizi wa umiliki wa silaha ili kulinda amani na ustawi wa jamii.

 
 
 

Comentarios


bottom of page