Viongozi Wetu - Rejeeni Kwenye Dhana ya Dhahabu.
- Rev. Godwin Chilewa
- Oct 4, 2024
- 3 min read

Katika Injili ya Mathayo 7:12, Yesu anasema, "Basi, yote myatakayo watu wawatendee ninyi, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hii ndiyo torati na manabii." Andiko hili linafafanua dhana ya dhahabu ambayo inasisitiza matendo ya huruma, haki, na usawa katika mahusiano ya kibinadamu. Yesu alitoa hotuba hii wakati wa Mahubiri ya Mlimani, ambamo alizungumzia kanuni muhimu za maadili na imani, akiwaelimisha wanafunzi wake pamoja na umati wa watu kuhusu jinsi ya kuishi kwa uadilifu mbele ya Mungu na binadamu.
Historia ya andiko hili inatokana na hitaji la kuweka msingi wa maadili wa kujenga jamii yenye haki. Yesu alikuwa akiishi katika mazingira ambapo kulikuwa na uonevu, ukandamizaji, na ubaguzi, hasa katika utawala wa Kirumi na hata kwa viongozi wa kidini wa Kiyahudi. Kwa kutoa hotuba hii, Yesu alitaka watu wawe na mtazamo wa haki na huruma kwa wenzao, badala ya kuzingatia tu sheria, kujilimbikizia mali, na madaraka bila roho ya upendo.
Sababu za Yesu kutoa hotuba hii
Yesu alitoa hotuba hili ili kuleta mabadiliko ya fikra na mtazamo kuhusu haki na uadilifu. Aliwafundisha wafuasi wake na jamii nzima kuwa, haki inapaswa kuonekana si tu kama kitu kinachotokana na sheria, bali kama jukumu la kila mmoja kumtendea mwenzake kwa upendo na heshima sawa na jinsi ambavyo kila mtu angependa kutendewa. Andiko hili linahusu kuweka mbele huruma, utu, na kutafuta maslahi ya pamoja, badala ya ubinafsi au kutanguliza mamlaka.
Kwa kuzingatia andiko hili, viongozi wa Taifa la Tanzania na wote wenye mamlaka wanapaswa kujifunza kuongozwa na kanuni ya kutenda haki kwa kila raia. Viongozi wanapaswa kuwa na mtazamo wa kutumikia wananchi badala ya kujinufaisha wao wenyewe au makundi maalumu. Kanuni ya Yesu inataka kila kiongozi ajiulize, “Je, ningetaka kutendewa hivi kama mimi ningekuwa mnyonge?” Matendo ya haki, uwajibikaji, na uadilifu yanapaswa kuwa msingi wa maamuzi yote wanayofanya, kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuleta usawa na maendeleo katika jamii.
Binafsi nimesukumwa kuwakumbusha viongozi wetu andiko hili. Ni ukweli usiopingika kwamba asilimia kubwa ya walioshika madaraka serikalini hawasukumwi na kiu ya kutenda haki, bali tamaa ya kujinufaisha binafsi. Hawa ndio wanaowakwamisha wale wachache wenye kiu ya kutenda haki na kuboresha maisha ya watanzania wanyonge. Ni ajabu kwamba waovu huwa na nguvu na umoja kuliko wenye haki. Ni kwa sababu hii kwa mara nyingine nasisitiza mambo yafuatayo:
1. Uadilifu na Uwajibikaji:
Viongozi wa taifa wanapaswa kuwa na uwajibikaji wa kibinafsi na wa kitaasisi kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi na kuhakikisha wanafanya maamuzi yanayoleta faida kwa wote. Haki itekelezwe bila ubaguzi wa aina yoyote – kisiasa, kikabila, au kiuchumi. Tukumbuke hapa duniani tunapita tu, iko siku tutatoa hesabu ya matendo yetu kwa Mungu.
2. Huruma na Utu:
Viongozi wanapaswa kuwa na huruma kwa hali ya watu wao. Wanapofanya maamuzi kuhusu sera za kiuchumi, kijamii, au kisheria, wanatakiwa kuelewa athari kwa walio wanyonge na kuhakikisha kuwa wanasaidia kuinua maisha ya walio na hali ngumu. Ni vizuri kila mtu ajue kwamba maisha yanaweza kubadilika wakati wowote. Misingi mibovu utakayoijenga ukiwa juu inaweza kukuathiri mwenyewe utakaposhuka chini.
3. Usikivu kwa Wananchi:
Viongozi wanapaswa kuwa wasikivu kwa sauti za wananchi. Kama wanavyojua mahitaji yao binafsi, wanapaswa kuelewa kuwa wananchi nao wanahitaji huduma bora, usalama, na maendeleo endelevu. Kuwasikiliza kwa uangalifu na kutatua matatizo yao kwa haki kutaleta umoja na amani. Isitoshe, hakuna furaha wala amani kwa tajiri aliyezungukwa na maskini.
4. Kushirikisha Wananchi Kwenye Maamuzi:
Viongozi wanapaswa kushirikiana na vyama vyote vya siasa na makundi ya kijamii ili kuunda mazingira ya utawala wa haki na demokrasia shirikishi. Hili litasaidia kuleta mshikamano wa kitaifa na kutatua changamoto kwa pamoja. Historia imetufundisha kwamba maamuzi ya pamoja hupunguza uchungu kwa wanaopita kwenye hali ngumu.
5. Kuimarisha Misingi ya Haki na Sheria:
Utawala wa sheria lazima uheshimiwe na kuimarishwa ili kila mtu aweze kupata haki sawa bila upendeleo. Uongozi bora unalenga kuondoa ufisadi, kujenga taasisi imara, na kuhakikisha kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria. Ni muhimu sana mheshimiwa Rais SSH atekeleze falsafa yake kwa vitendo, umakini na haraka ili kuwasukuma viongozi wa chini yake kuondoa ubaguzi wa kivyama na kiitikadi. Inawezekana kujenga taifa la watu wansopendana na kushirikiana bila kujali itikadi zao.
Kwa kumalizia, viongozi wa Tanzania wanapaswa kuongozwa na maadili yaliyofundishwa na Yesu, yaani kuwatendea haki wanaowaongoza kama ambavyo wao wangetaka kutendewa. Hii italeta uadilifu, haki, na maendeleo kwa kila mwananchi, na kuhakikisha kuwa taifa linaendelea kwa umoja na amani.
Rev. Godwin Chilewa.
Comentarios