top of page

NIA NJEMA AU HATARI KUBWA? Uamuzi wa Waziri Unapotikisa Utawala wa Sheria



Kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Katambi, kumshauri Shekhe Said Mwaipopo kusajili kikundi chake cha “Chui” ili kiweze kushiriki katika shughuli za ulinzi, imeibua mjadala mzito unaogusa msingi wa usalama wa taifa. Licha ya kwamba kauli hiyo imeambatana na kukiri kwamba kikundi hicho kilianzishwa nje ya utaratibu wa kisheria, lakini pia, historia ya kikundi hicho imekuwa ikihusishwa na viashiria vya ugaidi wa ndani. Hii inafanya suala hili kuwa nyeti zaidi kuliko linavyoonekana kwa juu.


Katika muktadha wa kiintelijensia, kauli ya mheshimiwa Katambi inaangaliwa kwa mtazamo wa kisiasa au kijamii, na pia kupimwa kwa athari zake za muda mfupi, wa kati, na wa muda mrefu kwa uthabiti wa dola. Kwa msingi huo ni sahihi kusema kuwa ndani ya mfumo wowote imara wa serikali, matumizi ya nguvu na usimamizi wa usalama ni jukumu linalopaswa kubaki mikononi mwa taasisi rasmi pekee. Hii ni kanuni ya kisheria, na msingi wa kuzuia machafuko, migongano ya mamlaka, na kuibuka kwa nguvu mbadala zisizo na uwajibikaji.


Kauli ya kuhalalisha kikundi kilichoanzishwa nje ya mfumo wa sheria inaleta taswira ya uwezekano wa kukuza kwa kile kinachojulikana kitaalamu kama “informal militarization.” Hali hii hutokea pale ambapo vikundi vya kiraia vinaanza kupewa au kujichukulia majukumu ya kiusalama bila kuwa sehemu ya muundo rasmi wa dola. Katika hatua za mwanzo, utaratibu huu huonekana kama suluhisho la haraka kwa changamoto za usalama, lakini kwa muda hujenga mifumo isiyodhibitiwa ambayo inaweza kugeuka kuwa tishio kwa taifa lenyewe.


Historia ya ugaidi wa kimataifa inaonesha kuwa vikundi vingi vilivyoanza kama “ulinzi wa jamii” vilipata uhalali wa kijamii kwa sababu ya mazingira ya hofu au udhaifu wa taasisi rasmi. Hata hivyo, mara nyingi vilibadilika na kuwa vituo vya msimamo mkali, vikianza kujiendesha kwa misingi ya itikadi au maslahi binafsi badala ya sheria za nchi. Katika muktadha huu, hoja ya “nia njema” haiwezi kuwa kigezo cha msingi wa uhalali wa kikundi kinachoshughulika na usalama, kwa sababu usalama wa taifa haujengwi juu ya nia bali juu ya mifumo thabiti ya udhibiti na uwajibikaji.


Zaidi ya hapo, hatua ya kuhalalisha kikundi cha shekhe Mwaipopo inaleta changamoto kubwa kwa mifumo ya kiintelijensia. Vyombo vya usalama hutegemea sana uwezo wa kufuatilia, kudhibiti, na kuchambua taarifa kwa usahihi. Kikundi huru kinapopewa nafasi ya kufanya shughuli za kiusalama, kinakuwa nje ya mnyororo rasmi wa amri na ufuatiliaji. Hali hii inaweza kusababisha mkanganyiko wa taarifa, uwezekano wa matumizi mabaya ya nguvu, na hata kuibuka kwa tishio la ndani kutoka kwa kundi ambalo hapo awali lilionekana kuwa mshirika.


Hatari nyingine kubwa ni kuibuka kwa mfumo sambamba wa usalama. Mfumo huu hutokea pale ambapo wananchi wanaanza kuamini zaidi vikundi visivyo rasmi kuliko taasisi za serikali. Taratibu, uhalali wa dola hupungua, na vikundi hivyo hupata nguvu ya kijamii na hata kisiasa. Katika mazingira ya mvutano wa kisiasa, hali hii inaweza kupelekea vikundi hivyo kutumiwa kama zana za kulinda maslahi fulani au kushinikiza ajenda maalum, jambo ambalo linaweza kuchochea migogoro ya ndani. Kwa kifupi kauli ya waziri inatoa mwanya wa uundwaji wa makundi ya ki-MAFIA nchini.


Inawezekana waziri kwa maono yake anadhani hatua ya kuruhusu kundi la Mwaipopo itasaidia kuimarisha ulinzi shirikishi au “community policing.” Hata hivyo, ulinzi shirikishi una kanuni zake zilizo wazi: hufanyika chini ya usimamizi wa polisi, hufuata sheria zilizowekwa, na hauhusishi matumizi ya nguvu za kijeshi nje ya udhibiti wa dola. Kikundi kilichoanzishwa nje ya mfumo huo hakiwezi kubadilishwa ghafla na kuwa sehemu ya mfumo rasmi bila kupitia tathmini ya kina na marekebisho makubwa ya kimuundo.


Suala hili likichukuliwa kisiasa linaweza kuonekana la kawaida.Hata hivyo athari za kimkakati za uamuzi wa aina hii zinaweza kuwa pana zaidi. Taifa linaweza kushuhudia ongezeko la vikundi vinavyojitangaza kuwa walinzi wa jamii, kila kimoja kikiwa na malengo na misingi yake. Hali hii inaweza kuleta mgawanyiko wa kijamii, migongano ya kimaslahi, kupungua kwa imani ya wananchi kwa vyombo vya dola, na kuibuka kwa ma God father. Aidha, kwa mtazamo wa kimataifa, hatua kama hii inaweza kuibua maswali kuhusu uthabiti wa mfumo wa usalama na utawala wa sheria nchini.


Kinachofanya suala hili kuwa nyeti zaidi ni athari ya kisheria na kisera inayoweza kujitokeza. Kauli ya Waziri inaweza kutafsiriwa kama ujumbe kwamba uvunjaji wa sheria unaweza kuvumiliwa endapo utaonekana kuwa na nia njema au unaunga mkono chama tawala. Hii ni tafsiri hatari inayoweza kuhamasisha makundi mengine kuanzisha vikundi vyao kwa matarajio ya kuhalalishwa baadaye, au kufanya uhalifu kwa kifuniko cha “Nia njema”


Kwa kuzingatia hali hii, hatua za tahadhari zinahitajika kuchukuliwa kwa umakini mkubwa. Ni muhimu kuhakikisha kuwa hakuna kikundi cha kiusalama kinachopewa uhalali nje ya mfumo rasmi wa dola. Aidha, uchunguzi wa kina wa kiintelijensia unahitajika ili kubaini muundo, malengo, na uwezo halisi wa vikundi vyote. Wakati huo huo, serikali inapaswa kuimarisha mifumo ya polisi jamii kwa njia rasmi ili kujenga ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya dola bila kuhatarisha usalama wa taifa.


Mwisho wa yote, jukumu la kulinda uthabiti wa taifa liko juu ya uongozi wa juu wa nchi. Ni muhimu kwa TISS kutathmini kwa kina mwelekeo huu na kuchukua hatua za haraka kurekebisha hali kabla haijazalisha athari zisizoweza kudhibitiwa. Historia inaonesha wazi kuwa mifumo ya usalama inapovurugika, gharama ya kurekebisha huwa kubwa zaidi kuliko kuzuia mapema. Suala la msingi si kama nia ya Mwaipopo ilikuwa njema, bali ni kama uamuzi wa Waziri Katambi unalinda au unahatarisha mustakabali wa usalama wa taifa.


Uwe na amani

 
 
 

Comments


bottom of page