SIASA, HEKIMA NA HILA: Sakata la Mhe Nchimbi na Wakili Dhalimu
- Rev. Godwin Chilewa
- 2 days ago
- 2 min read
Na Rev. Godwin Chilewa

Katika Injili ya Luka 16:1–13, Yesu Kristo anatoa mojawapo ya mifano yenye utata mkubwa katika mafundisho yake. Mfano huu unamhusu wakili aliyekuwa msimamizi wa mali za bwana wake, lakini akawa katika hatari ya kufukuzwa kutokana na ubadhirifu alioufanya. Akiwa katika hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wake, wakili huyu alichukua hatua ya haraka na ya kimkakati: aliwaita wadaiwa wa bwana wake na kupunguza madeni yao ili kujijengea mtandao wa watu watakaomkaribisha pindi atakapopoteza nafasi yake.
Kinachoshangaza ni kwamba bwana wake alipogundua alipogundua jambo hilo alimsifu kwa ujanja wake, (sikwa uadilifu wake). Hapa ndipo msingi wa fundisho la Yesu ulipo, kuonyesha umuhimu wa utambuzi wa wakati na kuchukua hatua kwa ufanisi na si kuhalalisha udhalimu kama baadhi ya watu wanavyotafsiri.
Tukilitazama tukio hili kwa jicho la uchambuzi wa kisiasa, linaweza kulinganishwa kwa tahadhari na mabadiliko ya kimkakati yanayoweza kufanywa na viongozi wanapokabiliwa na shinikizo la kisiasa. Katika muktadha wa Tanzania, hususan katika kipindi hiki tunaweza kulinganisha na hatua ya aliyekuwa Makamu wa Rais Mhe Emmanuel kujitenga na muelekeo wa CCM na kujiweka karibu na wananchi wanaodai katiba mpya.
Kwanza, kuna dhana ya utambuzi wa nyakati (crisis awareness). Wakili dhalimu alitambua mapema kwamba muda wake ulikuwa unaisha. Vivyo hivyo, katika siasa, kiongozi anaweza kugundua mabadiliko ya upepo wa kisiasa, kupungua kwa uhalali wa kisiasa (political legitimacy), kuongezeka kwa shinikizo la umma, au mabadiliko ya matarajio ya wananchi. Hatua ya kubadili msimamo inaweza kuwa ishara ya kusoma mazingira kwa umakini na kuona hatari inayokuja.
Pili, kuna kipengele cha hatua ya haraka ya kimkakati (strategic repositioning). Wakili hakusubiri kufukuzwa; alichukua hatua ya haraka ili kujihakikishia mustakabali. Katika siasa, hii inaweza kuonekana kama uamuzi wa kujipanga upya, kuhama kutoka mfumo uliopo kwenda upande unaoonekana kuwa na nguvu ya kijamii au kisiasa. Hapa ndipo tunapoona siasa kama mchezo wa hesabu na muda, ambapo kuchelewa kunaweza kumaanisha kupoteza kila kitu.
Tatu, ni suala la kujenga mahusiano mapya (network realignment). Wakili alitumia fursa alizokuwa nazo kujenga uhusiano na wadaiwa. Katika ulinganisho wa kisiasa, kujiunga na wananchi au harakati za mabadiliko kunaweza kutafsiriwa kama jitihada za kujenga uhalali mpya nje ya mfumo wa zamani. Ni mchakato wa kuhamisha uaminifu kutoka taasisi kwenda kwa umma.
Hata hivyo, tofauti ya msingi kati ya mfano wa Yesu na uhalisia wa kisiasa haiwezi kupuuzwa. Wakili dhalimu alifanya kwa lengo la kujilinda binafsi. Hakukuwa na hoja ya haki au maadili katika hatua yake; ilikuwa ni mbinu ya kuishi. Hivyo basi, katika uchambuzi wa kisiasa, hoja kuu haipaswi kuwa hatua iliyochukuliwa pekee bali pia nia iliyoko nyuma yake. Ni muhimu kuangalia kama hatua iliyochukuliwa ni ya kimaono kwa manufaa ya taifa, au ni mkakati wa kuendelea kubaki katika ushawishi wa kisiasa?
INAENDELEA (Soma sehemu ya pili katika toleo lijalo)






Comments