top of page

Athari za Sheria ya Bima ya Lazima kwa Watalii Tanzania na Mustakabali Wa Uchumi wa Utalii

21 hours ago
4 min read

Na Rev. Godwin Chilewa



Katika ushindani mkali wa kimataifa kwenye sekta ya utalii, sera yoyote inayogusa gharama, urahisi wa kuingia nchini, au uzoefu wa mtalii huwa na athari za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa uchumi wa taifa. Hivyo basi uamuzi wa Serikali ya Tanzania kuwataka watalii wote kununua bima ya ndani bila kujali kama tayari wana bima ya kimataifa unapaswa kuchambuliwa kwa jicho la “intelijensia ya kiuchumi,” siyo kwa mtazamo wa mapato ya haraka pekee tu, bali pia kwa athari zake za kimkakati kwa muda mfupi na mrefu.


Uzito wa Sekta ya Utalii katika Uchumi wa Tanzania

Takwimu zinaonesha kuwa sekta ya utalii ni mojawapo ya mihimili mikuu yauchumi wa taifa. Mwaka 2024, Tanzania ilipokea kati ya watalii milioni 1.7 hadi zaidi ya milioni 2, huku mapato yakifikia kati ya dola za Marekani bilioni 3.2 hadi karibu bilioni 3.9 . Aidha, sekta hii inachangia zaidi ya asilimia 17 ya Pato la Taifa (GDP) na karibu robo ya mapato yote ya fedha za kigeni. Kwa upande wa ajira, utalii unasaidia moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja zaidi ya watu milioni 1.4, na hivyo kuwa miongoni mwa waajiri wakubwa nchini . Hii ina maana kwamba mabadiliko yoyote katika mazingira ya utalii yanaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya serikali, ajira, uwekezaji, na ustawi wa jamii kwa ujumla.


Mantiki ya Sera ya Bima ya Lazima

Kwa mtazamo wa sera za mapato (revenue extraction policy), hatua ya kuanzisha bima ya lazima inaweza kuonekana kuwa na mantiki ya haraka. Kwa mfano, iwapo kila mtalii atalazimika kulipa kati ya dola 20 hadi 50 kwa bima, na idadi ya watalii wanaotarajiwa kuingia ni takriban milioni 2 kwa mwaka, serikali inaweza kukusanya kati ya dola milioni 40 hadi 100 kila mwaka.


Zaidi ya hilo, kwa mtazamo wa juujuu inaonekana sera hii inaweza kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa hospitali za ndani, hasa pale watalii wanapopata ajali au kuugua bila kuwa na mfumo wa malipo unaoaminika. Hii inaendana na changamoto ya mifumo ya afya katika nchi zinazoendelea, ambapo baadhi ya gharama hubebwa na taasisi za umma. Kimsingi, sera hii inaleta ulinzi wa soko kwa sekta ya bima ya ndani kwa kuunda mahitaji ya lazima (captive market), jambo linaloweza kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha na ajira zake, na kuboresha huduma za afya.


Hatari za Kiuchumi: Gharama Zisizoonekana (Hidden Strategic Costs)

Ukiangalia sheria hii kiintelijensia hutaishia kwenye mapato ya moja kwa moja na haraka bali utachunguza athari za sera hii katika ushindani wa kimataifa wa Tanzania kama kivutio cha utalii. Sekta ya utalii ni mojawapo ya sekta nyeti zaidi kwa mabadiliko ya bei (price-sensitive industry). Tafiti za kimataifa zinaonesha kuwa ongezeko hata dogo la gharama linaweza kupunguza mahitaji ya safari.


Aidha kwa sasa Tanzania tayari ina gharama za juu kwenye vivutio muhimu ukilinganisha na washindani wake, na pia ina gharama kadhaa za lazima kwa mtalii, ikiwa ni pamoja na visa inayoweza kufikia dola 50 hadi 100 kwa baadhi ya mataifa . Kwahiyo kuongeza gharama ya ziada ya bima ya lazima kunaleta kile kinachoitwa “cost stacking effect,” ambapo mtalii anaona gharama ndogo ndogo ambazo zikijumlishwa huwa kubwa. Katika mazingira ya ushindani na nchi jirani kama Kenya au Rwanda, ambazo hazilazimishi bima ya ndani, Tanzania inaweza kuonekana kama ghali zaidi bila kuongeza thamani ya ziada kwa mtalii.


Athari ya Taswira (Perception Risk)

Katika uchumi wa kisasa wa huduma, perception ni sawa na reality. Mtalii anayelazimishwa kulipia bima ambayo tayari anayo kupitia kampuni za kimataifa anaweza kuona hatua hii kama “double taxation” au sera isiyo rafiki. Historia inaonesha kuwa sera zinazoongeza gharama kwa watalii bila uwazi wa faida hukumbana na upinzani mkubwa. Mfano halisi ni Thailand, ambayo ililazimika kuchelewesha utekelezaji wa ada mpya ya utalii kutokana na malalamiko ya wadau. Hii inaonesha wazi kuwa mtazamo hasi unaweza kuathiri sera hata kabla ya kuanza kufanya kazi kikamilifu.


Athari ya Ushindani wa Kikanda na Kimataifa

Kwa mtazamo wa kiintelijensia ya ushindani (competitive intelligence), Tanzania haiko peke yake katika soko la utalii wa safari. Inashindana moja kwa moja na Kenya (Maasai Mara), Afrika Kusini (Kruger National Park), na Namibia au Botswana. Katika mazingira haya, mtalii anafanya maamuzi kwa kulinganisha gharama, urahisi wa kuingia, na uzoefu. Ikiwa Tanzania itaonekana kuwa na taratibu nyingi zaidi au gharama zisizoeleweka, kuna uwezekano wa kile kinachoitwa “substitution effect,” ambapo mtalii anachagua nchi mbadala.


Hasara ya Multipliers: Pigo Kubwa Kuliko Mapato

Athari kubwa zaidi ya sera hii ni kwenye kupungua kwa watalii, jambo ambalo halipaswi kupuuzwa. Kwa mfano, kama sera hii itasababisha kupungua kwa watalii kwa asilimia 5 tu, kutoka watalii milioni 2 hadi milioni 1.9, na kila mtalii hutumia wastani wa dola 1,500, basi uchumi utapoteza takriban dola milioni 150.

Hii ni zaidi ya mapato yanayotarajiwa kutoka bima ya lazima. Huu ni ukweli ambao wataalam wa serikali hawakutaka kuuzungumzia. Sera ya bima inaweza kuongeza mapato kiasi kwa upande mmoja lakini ikapunguza mapato makubwa zaidi upande mwingine.


Kwa kuzingatia ushahidi wa takwimu na mifano ya kimataifa, sera ya bima ya lazima ina sifa za sera ya “short-term revenue maximization” badala ya “long-term growth optimization.”

Ingawa inaweza kuongeza mapato ya haraka na kulinda sekta ya bima ya ndani, ina hatari kubwa ya kudhoofisha ushindani wa Tanzania katika soko la utalii, kupunguza idadi ya watalii, na hivyo kuathiri mapato makubwa zaidi ya taifa.


Njia Mbadala za Kimkakati (Strategic Alternatives)

Katika mazingira haya, njia bora zaidi si kuongeza mzigo wa moja kwa moja kwa mtalii, bali kubuni mifumo ya mapato yenye “low friction, high yield.” Seriksli inaweza kuongeza mapato kupitia ada zilizofichwa ndani ya huduma tayari zilizopo kama hoteli au hifadhi za taifa, ambapo mtalii halazimiki kufanya malipo mapya yanayoonekana. Aidha, badala ya kulazimisha bima, inaweza kuhamasisha kwa motisha maalum kama huduma za haraka uwanjani au upatikanaji wa matibabu ya kipaumbele.


Njia nyingine ni kutambua bima za kimataifa na kutoza ada ndogo ya uthibitisho, badala ya kuanzisha mfumo wa lazima. Hii inalinda mapato bila kuathiri taswira ya nchi.

Zaidi ya yote, mkakati wa muda mrefu unapaswa kuelekezwa katika kuongeza thamani ya kila mtalii kupitia utalii wa hadhi ya juu (high-value tourism), badala ya kuongeza gharama kwa kila mtalii.


Serikali inapaswa kujifunza kwamba katika ulimwengu wa ushindani wa kimataifa, mafanikio ya utalii hayategemei tu vivutio vya asili, bali pia urahisi wa sera na uzoefu wa mtalii. Tanzania ina rasilimali za kipekee duniani, lakini sera zisizo na mizani zinaweza kupunguza faida ya ushindani huo. Kwa mtazamo wa kiintelijensia ya kiuchumi, sera bora ni ile inayohakikisha mtiririko endelevu wa watalii, uwekezaji, na mapato kwa muda mrefu.


Uwe na amani

Rev. Godwin Chilewa

 
 
 

Comments


bottom of page