top of page

DIASPORA: Baniani Mbaya Kiatu Chake Dawa?

10 minutes ago
5 min read

Na Rev. Godwin Chilewa



Tangazo la Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mhe. Neema Lugangira, linalowaalika Watanzania waishio nje ya nchi kushirikiana na Arumeru kwa mawazo, utaalamu, uwekezaji na misaada, limefungua mjadala muhimu kuhusu nafasi ya diaspora katika maendeleo ya Tanzania. Ujumbe wake kwamba, “Popote ulipo Tanzania na duniani, Arumeru ni nyumbani,” ni kauli inayobeba dhana ya uzalendo, mshikamano na wajibu wa pamoja katika kujenga jamii.


Hata hivyo, katika masuala ya diaspora, nia njema na kauli za ukaribisho pekee hazitoshi. Ushirikiano wa kweli unahitaji mazingira yanayojenga uaminifu, kutambua haki na mchango wa wananchi, na kuondoa vikwazo vinavyowafanya baadhi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi wajihisi kuwa wanahitajika wanapotoa fedha, lakini wanatiliwa shaka wanapotoa maoni.


Kwa hiyo, ushauri kwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru ni kwamba, pamoja na kuendelea kuhamasisha diaspora kuwekeza na kuchangia maendeleo ya wilaya, ni muhimu pia kuelewa mazingira ya kisiasa, kijamii na kitaasisi yanayoathiri uhusiano kati ya diaspora na Serikali. Bila kuyatambua mazingira hayo, wito wa ushirikiano unaweza kuwa na mvuto wa maneno lakini ukakosa mwitikio unaotarajiwa.


1. Kivuli cha Oktoba 29 na changamoto ya kujenga upya imani

Matukio ya kisiasa yaliyohusishwa na uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, na athari zake kwa uhusiano kati ya Serikali, wananchi na makundi mbalimbali ya Watanzania, yameacha maswali na hisia ambazo haziwezi kuondolewa kwa kutangaza fursa za uwekezaji pekee.


Kwa baadhi ya Watanzania waishio nje ya nchi, kipindi hicho kimeongeza wasiwasi kuhusu haki za kiraia, uhuru wa kutoa maoni, usalama wa wananchi na namna ambavyo sauti zinazotofautiana na msimamo wa Serikali zinavyopokelewa. Hizi ni hisia na mitazamo inayopaswa kuchunguzwa kwa mazungumzo ya wazi, badala ya kudhani kuwa kila Mtanzania aliye nje ya nchi ana mtazamo mmoja.


Ni muhimu kutambua kwamba diaspora si kundi lenye msimamo mmoja wa kisiasa. Wapo wanaoiunga mkono Serikali, wanaoikosoa, wanaopendelea vyama tofauti, na wengine ambao hawajishughulishi kabisa na siasa. Kinachowaunganisha ni uraia wao, uhusiano wao na Tanzania, pamoja na maslahi yao katika mustakabali wa nchi. Aidha kuishauri au kuikosoa serikali hakuondoi thamani yake, utaifa au uzalendo wa mtu. Mara nyingine ni wajibu usiokwepeka.


Mkuu wa Wilaya anapaswa kuelewa kuwa mtu anayeombwa kuwekeza katika eneo fulani anahitaji kuamini kuwa mazingira ya uwekezaji ni salama, mikataba itaheshimiwa, mali zake zitalindwa na maswali yake yatapokelewa kwa haki. Vivyo hivyo, mtu anayeombwa kutoa utaalamu au kuunga mkono miradi ya maendeleo anahitaji kuona kuwa ushirikiano huo hauishii kwenye kupokea rasilimali zake, bali unajumuisha pia kuheshimu utu na maoni yake.


Imani haiombwi kwa tangazo; hujengwa kwa matendo yanayothibitisha kuwa anayekualika yuko tayari kukusikiliza hata unaposema jambo asilopenda kulisikia.


Kwa hiyo, kabla ya kutarajia mwitikio mkubwa kutoka diaspora, ni muhimu kuunda mazingira ambayo yanaruhusu mazungumzo ya wazi kuhusu changamoto za nchi, bila kuwafanya washiriki wajisikie kuwa maoni yao yanaweza kutafsiriwa moja kwa moja kama uadui dhidi ya Serikali. Ondoe


2. Kuonekana kama wachochezi au watu wanaotumiwa na mabeberu

Miongoni mwa vikwazo vinavyoweza kuathiri ushirikiano na diaspora ni mtazamo unaowachukulia baadhi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi kama watu wanaochochea machafuko, wanaohujumu maslahi ya taifa au wanaotumiwa na mataifa ya kigeni.


Ni kweli kwamba katika mahusiano ya kimataifa, mataifa na taasisi mbalimbali huendeleza maslahi yao kwa kutumia diplomasia, misaada, ushawishi wa kisiasa na njia nyingine. Hata hivyo, ukweli huo hauwezi kutumika kama msingi wa kuwashuku Watanzania wote wanaoishi nje ya nchi.


Diaspora inajumuisha wataalamu wa afya, wahandisi, wanasheria, walimu, wafanyabiashara, wafanyakazi wa kawaida, wanafunzi, wawekezaji na wajasiriamali. Baadhi yao wana familia na mali Tanzania, wanatuma fedha kwa ndugu zao, wanajenga nyumba, wanaanzisha biashara na wanachangia gharama za elimu na afya. Wengine wana ujuzi ambao unaweza kusaidia kuboresha huduma za umma na uzalishaji.


Pia wapo wanaotumia haki yao ya kutoa maoni kuhusu mwenendo wa nchi. Kukosoa sera, kuhoji maamuzi ya viongozi au kutaka uwajibikaji si ushahidi wa moja kwa moja kwamba mtu huyo anatumiwa na nchi ya nje.

Ni muhimu kutofautisha kati ya ukosoaji wa kisiasa, ambao unaweza kuwa sehemu ya mjadala halali wa kitaifa, na vitendo maalumu vinavyoweza kuthibitishwa kuwa vinakiuka sheria. Tofauti hiyo inapopuuzwa, madhara yake yanaweza kuwa makubwa: watu wenye utaalamu wanaweza kujitenga, wawekezaji wanaweza kusita, na fursa za kubadilishana maarifa zinaweza kupotea.


Kwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, ujumbe unaofaa ni huu: diaspora isichukuliwe kama kundi linalopaswa kwanza kuthibitisha uaminifu wake wa kisiasa kabla ya kusikilizwa. Izingatiwe kama sehemu ya jamii ya Watanzania ambayo ina mitazamo tofauti, lakini inaweza kukutana kwenye masuala ya maendeleo yanayowagusa wananchi.


Ushirikiano unaweza kuanza kwa miradi ya maji, afya, elimu, kilimo, utalii, teknolojia na ajira. Lakini mafanikio yake yatategemea kama watu wanaweza kushiriki bila kubebeshwa tuhuma za jumla kutokana na mahali wanapoishi au maoni wanayotoa. Aidha suala la kudai haki na uwajibikaji si dhambi, bali ni haki ya kikatiba na msingi wa utu na maendeleo.


3. Uraia pacha na hadhi maalumu: pengo kati ya mchango na utambuzi

Moja ya masuala yanayohitaji kuangaliwa katika mjadala wa diaspora ni uraia pacha na uwezekano wa kuweka hadhi maalumu kwa Watanzania waliohamia nchi nyingine na kupata uraia wa nchi hizo. Kwa baadhi ya Watanzania walioishi nje kwa muda mrefu, suala hili si la urahisi wa kusafiri pekee. Linahusu utambulisho, uhusiano wa kisheria na nchi yao ya asili, uwezo wa kupanga maisha ya muda mrefu, urithi wa familia na namna ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Tanzania.


Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanaweza kuwa wamepata elimu, uzoefu, mitandao ya kitaaluma na uwezo wa kifedha ambao unaweza kuwa na manufaa kwa nchi. Hata hivyo, mchango huo haupaswi kutumika kama hoja pekee ya kuamua haki zao. Haki, hadhi ya kisheria na mchango wa kiuchumi ni masuala yanayohusiana, lakini si kitu kimoja.


Uraia pacha ni suala la sera na sheria za kitaifa ambalo linahitaji kujadiliwa kwa kuzingatia Katiba, sheria, maslahi ya taifa, wajibu wa uraia na uzoefu wa nchi nyingine. Vilevile, hadhi maalumu inaweza kuchunguzwa kama njia ya kuweka utaratibu unaoeleweka kwa Watanzania walio nje ya nchi ambao wanataka kuendelea kuwa na uhusiano wa karibu na Tanzania.

Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha mapendekezo ya kisera na hali ya sasa ya sheria.


Tangazo la Mkuu wa Wilaya haliwezi lenyewe kubadili masharti ya uraia, na mamlaka ya Wilaya haiwezi kuchukua nafasi ya Serikali Kuu au Bunge katika masuala yanayohitaji maamuzi ya kitaifa. Lakini hilo halimzuii Mkuu wa Wilaya kufanya jambo muhimu: kukusanya maoni ya diaspora ya Arumeru, kuandaa mapendekezo yenye ushahidi, na kuyawasilisha kwa mamlaka husika.


Kumbe DC ambaye anaijua diaspora, alipaswa kuanza kwa kujiuliza: Ni vikwazo gani vya kisheria na kiutawala vinavyowazuia Watanzania waishio nje kuwekeza? Ni matatizo gani wanayokutana nayo wanaporudi nyumbani? Ni changamoto zipi zinazohusu mali, urithi, vibali, usafiri, utambuzi wa nyaraka na ushiriki wao katika miradi ya maendeleo? Ni mapendekezo gani yanayoweza kutatuliwa ndani ya mamlaka za eneo, na yapi yanahitaji mabadiliko ya sera za kitaifa?


Maswali haya yatabadilisha wito wa ushirikiano kutoka kwenye kauli ya jumla na kuufanya kuwa mchakato wenye matokeo yanayopimika. Jambo muhimu hapa ni kuitazama diaspora kwa ujumla na umuhimu wake, badala ya kuona au kualika kundi la marafiki waishio nje kwa kisingizio au jina la diaspora.


Nihitimishe kwa kumpongeza mheshimiwa Neema Lugangila kwa maono na kutambua umuhimu na mchango wa diaspora. Ni vyema basi aanze kwa kuishauri serikali kuitambua jumuia hii ki vitendo. Profesa Penina Mlama aliwahi kuandika, akisema “LINA UBANI”


Uwe na amani

Rev. Godwin Chilewa

 
 
 

Comments


bottom of page