top of page

WASALITI NDANI YA VYAMA: Je, CHADEMA Ni Dhaifu Kuliko CCM au Tunashindwa Kutambua Chanzo Halisi cha Usaliti?

2 hours ago
7 min read

Na Rev. Godwin Chilewa



Kuna dhana inayozidi kujengwa katika mijadala ya kisiasa Tanzania kwamba CHADEMA ni chama dhaifu kwa sababu kina wasaliti wengi, watu wanaokisaliti chama, kukihujumu kutoka ndani au kuondoka na kujiunga na vyama vingine wakati chama kinapokabiliwa na changamoto, na kwa hiyo hiki ni chama kisichopaswa kuaminiwa.


Kimsingi dhana hii haipaswi kukubalika au kuendelea kusambazwa bila kufanyiwa uchunguzi wa kina japokuwa imeanzishwa na wachambuzi maarufu. Ieleweke kwamba hata wachambuzi maarufu pia hufanya makosa, husongwa na fikra za upendeleo (bias) na mara nyingine hutumiwa kufanya propaganda. Kwa kifupi kauli kama “CHADEMA ni dhaifu kwa sababu ina wasaliti wengi hivyo haiwezi kuaminika” ni kauli ya ki propaganda zaidi kuliko uchambuzi wa kitaalam.


Ni kweli kwamba Godbless Lema amezua taharuki. Lakini kupata ukweli wa kinachoendelea CHADEMA tunapaswa kujiuliza, Je, watu wenye mtazamo tofauti wa kiutendaji, kupingana na viongozi au kutoa taarifa zinazokinzana na msimamo wa chama ni ushahidi wa udhaifu wa taasisi? Je, chama tawala CCM hakina migogoro ya ndani, makundi yanayopingana, viongozi wanaokisaliti chama au watu wanaohama kwa sababu ya kutoridhishwa na uongozi? Tena tunapaswa kujiuliza kama usaliti ni chanzo cha udhaifu wa chama, au wakati mwingine kuhujumiwa kwa taasisi ndio kunazalisha mazingira ya usaliti?


Haya ni maswali muhimu kwa sababu kuna hatari ya kuchanganya matatizo ya uongozi, ushindani wa madaraka, kutokubaliana kisera na usaliti halisi.


1. JE, KUWA NA WASALITI WENGI NI ISHARA YA CHADEMA KUWA CHAMA DHAIFU?

Hapa tunapaswa kutofautisha kati ya udhaifu wa watu na udhaifu wa taasisi. Kwanza, hakuna chama cha kisiasa kinachoweza kuhakikisha kwamba wanachama na viongozi wake wote wana maslahi, matarajio na misimamo inayofanana wakati wote. Vyama vya kisiasa ni taasisi zinazoundwa na watu wenye maslahi tofauti ya kisiasa na kiuchumi, matamanio ya uongozi na madaraka, mitazamo tofauti kuhusu mikakati ya chama, viwango tofauti vya uvumilivu wa changamoto, uwezo tofauti wa kuvumilia gharama za kisiasa. na mitazamo tofauti kuhusu namna ya kushirikiana na serikali.


Kwa hiyo, kuwepo kwa watu wenye mawazo tofauti ya uendeshaji, wanaohama chama au kupingana na viongozi wake si ushahidi wa kutosha kwamba chama ni dhaifu. Udhaifu wa taasisi unapimwa kwa mambo mengine hususan uwezo wake wa kusimamia migogoro, kutekeleza katiba yake, kujenga viongozi wapya, kulinda maadili yake, kuendesha maamuzi ya pamoja na kuendelea kufanya kazi hata viongozi fulani wanapoondoka.


Katika muktadha huo, kuna tofauti kati ya chama chenye wanachama wenye mikikimikiki, chenye wanachama wanaohama, na chama kisicho na uwezo wa kuhimili wanachama wenye mikikimikiki au wanaohama. Chama chenye taasisi imara kinaweza kupoteza viongozi maarufu lakini kikaendelea kufanya kazi kwa sababu kina mifumo, misingi, wanachama na ajenda zinazojitegemea.


Kwa upande mwingine, chama kinachotegemea sana umaarufu wa watu wachache kinaweza kuyumba sana watu hao wanapokuwa na misimamo tofauti au wanapohama kabisa. Kwa hiyo, kipimo cha udhaifu wa CHAMA hakipaswi kuwa idadi ya watu wanaoitwa wasaliti, bali uwezo wake wa kuendelea kuwa taasisi yenye nguvu hata katika mazingira ya migogoro na mabadiliko ya viongozi.


2. JE, CCM HAINA WASALITI, MIGOGORO NA MAKUNDI YA NDANI?

Hapa kuna ndipo tunapoona upendeleo wa kiuchambuzi unaopaswa kuepukwa. Kama kuwa na wasaliti ni udhaifu basi tungesema CCM ni dhaifu zaidi. Historia ya chama tawala imekuwa na ushindani mkubwa wa madaraka, makundi ya kisiasa, kutokubaliana kuhusu uteuzi wa viongozi na uhamaji wa baadhi ya viongozi wake kwenda vyama vingine.


Mwaka 1983 CCM ilikuwa na mgogoro mkubwa uliosababisha kulazimishwa kujiuzuru kwa Rais wa Zanzibar marehemu Abdu Jumbe. Baadae ulifuatia mgogoro mwingine uliomhusu Katibu mkuu wa CCM wakati huo Horace Kolimba ambaye alifariki katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuhojiwa na Kamati Kuu ya CCM.


Ulikuwepo pia mgogoro mwingine uliomhusu Rais Ali Hassan Mwinyi, mzee John Malecela na baadhi ya viongozi wengine wa juu katika chama. Mgogoro huu ndiyo uliomsukuma mwalimu Nyerere kuandika kitabu alichokiita UONGOZI WETU NA HATIMA YA TANZANIA.


Katika miaka ya 1990 CCM ilikumbwa na mgogoro mwingine mzito uliomhusisha Naibu waziri mkuu marehemu Augustino Mrema. Mgogoro huo ilikuwa mkubwa kiasi cha Marehemu Augustino Mrema kukitosa Chama Cha Mapinduzi na kujiunga na NCCR MAGEUZI.


Tena mwaka 2015 uliibuka mgogoro mwingine. Huu ulihusisha makundi yaliyokuwa yanaunga mkono wagombea tofauti. Baada ya Lowassa kutopata uteuzi ndani ya CCM, alihama na kujiunga na CHADEMA kupitia UKAWA, akiwa mgombea urais. Katika migogoro hii yote viongozi waliotajwa walivishwa Lebo ya usaliti na kushambuliwa vibaya kwa maneno ya propaganda.


Pengine tukio kubwa kuliko yote ni hili lililotokea hivi karibuni ambapo aliyekuwa Makamu wa Rais, Mhe Emmanuel Nchimbi alifukuzwa uanachama wa CCM baada ya kujiuzuru nafasi ya umakamu wa rais. Kabla ya kufukuzwa uanachama viongozi kadhaa wa CCM walisikika wakimshambulia mhe. Nchimbi kwa madai ya usaliti.


Matukio haya yanaonyesha jambo moja muhimu, kwamba kuwa na msimamo tofauti au kuhama chama si tatizo linalohusu CHADEMA pekee. CCM ina migogoro yake, CHADEMA ina migogoro yake, na tofauti kubwa mara nyingi ipo katika namna taasisi hizo zinavyoweza kuisimamia, kuizuia isisambae na kuendelea kufanya kazi.


Matukio haya yanathibitisha pasipo shaka yoyote kwamba uwepo wa utofauti wa mawazo, upinzani wa ndani, na hata kuhama kwa wanachama ni mambo ya kawaida katika siasa na wala hayathibitishi kwamba chama fulani ni dhaifu kama ilivyoelezwa na baadhi ya wachambuzi.


3. USALITI WA KISIASA UNATOKANA NA NINI?

Katika uchambuzi wa kiintelijensia, usaliti haupaswi kuchukuliwa kama jambo linalotokea bila sababu. Mara nyingi huwa na mazingira, vichocheo, maslahi na fursa zinazoweza kueleza kwa nini mtu anabadilisha msimamo wake au kuamua kufanya kazi kinyume na taasisi aliyokuwa akiitumikia.


Kwa ujumla Kuna sababu kuu nane.

A. Tamaa ya madaraka na nafasi za uongozi

Hii ni moja ya sababu zinazoweza kuchochea migogoro mikubwa ndani ya vyama.

Mwanasiasa anapokuwa na matarajio ya kupata nafasi fulani, lakini matarajio hayo yasipotimia, anaweza kuanza kuamini kwamba taasisi imemzuia kufikia malengo yake.


Kwa mfano, mtu aliyekuwa na matarajio ya kugombea ubunge, uenyekiti wa chama au nafasi ya juu ya uongozi anaposhindwa katika mchakato wa uteuzi anaweza kutoridhika na matokeo. Wengine hukubali uamuzi na kuendelea na chama. Wengine hujiondoa. Wengine huanzisha kundi la upinzani ndani ya chama. Na katika mazingira mengine, mtu anaweza kuamua kushirikiana na wapinzani wa chama chake. Hapa tunakutana na dhana ya political ambition yaani tamaa au msukumo wa kutafuta madaraka ya kisiasa.


B. Maslahi binafsi na manufaa yanayotarajiwa

Siasa zina nafasi ya kuhusisha maslahi ya kiuchumi, kijamii na kitaaluma. Mtu anaweza kuona kwamba kuendelea kuwa ndani ya chama fulani hakumpi tena fursa alizokuwa anatarajia.

Anaweza kuona fursa kubwa zaidi katika chama kingine, serikali au taasisi nyingine. Hali hii inahusiana na dhana ya political opportunism.

Hata hivyo, si kila mtu anayehamia chama kingine anafanya hivyo kwa sababu ya fedha au manufaa binafsi. Hilo linahitaji ushahidi wa kila tukio.


C. Kutokuwepo kwa demokrasia ya ndani ya chama

Hili ni eneo muhimu sana. Wanachama wanapohisi hawana nafasi ya kutoa maoni, kupinga maamuzi au kushiriki katika uteuzi wa viongozi, wanaweza kupoteza imani na taasisi. Hali hiyo inaweza kuzalisha uasi, kujitenga au kuondoka.


D. Kutokubaliana kwa itikadi na mikakati

Wakati mwingine mtu haondoki kwa sababu ya fedha, madaraka au kushawishiwa na chama kingine. Anaweza kuondoka kwa sababu anaamini chama chake kimeacha misingi aliyokuwa akiifuata. Kwa mfano, ndani ya CHADEMA kunaweza kuwa na tofauti kuhusu:

Kushiriki au kutoshiriki uchaguzi katika mazingira fulani. Kufanya mazungumzo na serikali. Kutumia maandamano kama njia ya shinikizo. Kutafuta maridhiano au kuendeleza msimamo wa upinzani mkali. Kuweka kipaumbele kwenye mageuzi ya mfumo au kushiriki katika mfumo uliopo. Tofauti hizi zinaweza kuwa za kweli na za kiitikadi hivyo tatizo ni kuzitafsiri zote kama usaliti.


E. Shinikizo, vitisho na mazingira ya kisiasa

Katika mazingira ambayo mwanasiasa anakabiliwa na shinikizo kubwa, vitisho, matatizo ya kiuchumi au vikwazo vya shughuli zake, anaweza kuanza kutafuta njia nyingine ya kuendelea na maisha yake ya kisiasa.

Hapa kuna tofauti kati ya mtu anayebadili msimamo kwa sababu ya ushawishi na mtu anayefanya hivyo kutokana na mazingira ya kulazimishwa.


Katika uchunguzi, jambo hili linahitaji kuangalia mazingira halisi ya mhusika, si kuishia kwenye kitendo cha kutenda tofauti au kuondoka.


F. Migogoro binafsi na uongozi

Wakati mwingine tofauti zinazohusu watu binafsi hugeuzwa kuwa tofauti za kisera.

Mwanasiasa anapokosa maelewano na mwenyekiti, katibu mkuu au kiongozi mwingine, anaweza kuanza kupinga maamuzi yote yanayotolewa na uongozi huo.

Hali hii inaweza kusababisha migogoro ya makundi. Katika mazingira hayo, chama kinaweza kupoteza uwezo wa kutofautisha kati ya kukosoa uongozi na kukisaliti chama.


G. Ushawishi wa nje na mitandao ya maslahi

Vyama vya kisiasa vinaweza kuwa na washindani wanaotaka kuvipunguza nguvu.

Katika mazingira ya ushindani, wapo watu au makundi yanayoweza kutumia fedha, ahadi za nafasi, mahusiano au ushawishi mwingine kuwavuta viongozi wa chama pinzani.

Hata hivyo, kuwepo kwa uwezekano wa aina hii hakuthibitishi kwamba kila mgawanyiko unasababishwa na operesheni ya chama kingine.


Kwahiyo Kiintelijensia, tunahitaji kutofautisha

Infiltration yaani kujipenyeza kwa watu katika taasisi kwa madhumuni ya kupata taarifa au kuathiri shughuli zake. Subversion ambalo ni jaribio la kudhoofisha taasisi kutoka ndani. Defection kwa maana ya kuondoka kwa mtu katika chama na kujiunga na chama kingine au kubadili upande wake wa kisiasa.

Dissent: Kutoa upinzani au kutokubaliana na msimamo wa uongozi na Betrayal kitendo cha kuvunja uaminifu kwa kufanya kitendo kinachokiuka wajibu au maslahi ya taasisi kwa namna inayoweza kuthibitishwa. Hizi si dhana zinazofanana.


4. KWA NINI CHADEMA INAONEKANA KUWA NA WASALITI WENGI ZAIDI?

Hapa kuna masuala ya kimuundo na kisaikolojia yanayostahili kuchunguzwa.

Kwanza, mwonekano wa migogoro.

CHADEMA ni chama kikuu cha upinzani na shughuli zake zinapata uangalizi mkubwa wa vyombo vya habari. Migogoro yake inapokuwa hadharani, inakuwa na nafasi kubwa katika mjadala wa kitaifa. Hivyo, kuna uwezekano wa wananchi kuona migogoro yake zaidi kuliko migogoro ya ndani ya vyama vingine.


Pili, tofauti ya nguvu za taasisi.

CCM ina historia ndefu ya kutawala, miundo mipana ya kitaasisi na mizizi ya kisiasa iliyojengeka katika maeneo mengi ya nchi.

CHADEMA imekuwa ikifanya kazi katika mazingira tofauti ya kisiasa na kiutawala, na imekabiliwa na changamoto za uendeshaji na ushindani. Hali hii inaweza kufanya migogoro ya CHADEMA ionekane kwa urahisi zaidi na kuwa na athari kubwa kwa shughuli zake.


Tatu, matarajio makubwa ya viongozi.

Chama kinapokuwa na matarajio makubwa ya kushika dola, ushindani wa nafasi za uongozi unaweza kuwa mkali. Viongozi wanaweza kuanza kuona nafasi za chama kama fursa za mustakabali wao binafsi.


Nne, utamaduni wa kutafsiri tofauti kama usaliti.

Hili ni eneo hatari zaidi linalopaswa kuangaliwa kwa kina. Kama kila mtu anayepinga uamuzi wa mwenyekiti anaitwa msaliti, chama kinaweza kuingia katika mazingira ya hofu na ukimya.

Wanachama wataacha kutoa mawazo mbadala kwa sababu wanaogopa kuonekana hawana uaminifu. Matokeo yake ni kwamba viongozi wanaweza kukosa taarifa muhimu za kurekebisha makosa yao.


Hii ni hali inayoweza kuelezwa kwa dhana ya groupthink , tabia ya kundi kutanguliza makubaliano na utii kuliko uchambuzi huru na mjadala wa mawazo tofauti. Kundi linaweza kuonekana lina umoja mkubwa, lakini kwa ndani likawa limepoteza uwezo wa kujikosoa.


Kwahiyo dhana kwamba CHADEMA ni chama dhaifu kwa sababu kina wasaliti wengi ni hitimisho pana lenye hisia za kipropaganda zaidi kuliko ushahidi wa kitaalam. Ni kweli kwamba CHADEMA imekabiliwa na migogoro ya ndani, na kuhama kwa baadhi ya viongozi wake. Matukio hayo yanaweza kuwa na madhara kwa mshikamano, taswira na uwezo wa chama kuendeleza ajenda zake lakini si udhaifu wa kitaasisi. Zingatia kwamba CCM imekabiliwa na migogoro mikubwa ya ndani, makundi ya kisiasa na uhamaji wa viongozi wake.

Jambo la msingi ni uwezo wa kila taasisi kuhimili migogoro hiyo na kuendelea kufanya kazi.


Uwe na Amani

Rev. Godwin Chilewa



 
 
 

Comments


bottom of page