Barua ya Kujiuzuru Mhe. Emmanuel Nchimbi Imeficha Nini?
- Rev. Godwin Chilewa
- 2 hours ago
- 4 min read
Na Rev. Godwin Chilewa

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Emmanuel John Nchimbi, ametangaza kujiuzulu na kustaafu kabisa siasa na utumishi wa umma. Katika barua yake ya tarehe 25 August 2025 iliyosambazwa na vyombo mbalimbali vya habari, mheshimiwa Nchimbi ameeleza kuwa ataondoka madarakani tarehe 4 Septemba 2026 .
Kwa mtazamo wa kawaida, barua ya Mhe. Emmanuel Nchimbi inaonekana ya heshima, utulivu, na kufuata taratibu za kikatiba. Hata hivyo, katika uchambuzi wa kiintelijensia, maandiko ya aina hii hutazamwa kwa maana ya juu na pia kama mawasiliano ya kisiasa yenye tabaka mbili, yaani rasmi na fiche (surface vs subtext).
Barua ya Nchimbi imejengwa kwa ustadi mkubwa wa kisiasa. Lugha yake ina sifa tatu kuu. Sifa ya kwanza ikiwa uhalalishaji wa uamuzi wake. Mhe. Nchimbi ameanza kwa kutaja vifungu vya Katiba hususan ibara ya 50(2)(c) na 149(2). Hii ni mbinu ya kuonyesha kuwa hatua yake ni ya kisheria na si ya ghafla. Kisheria, vifungu hivi vinatoa mwanya wa Makamu wa Rais kujiuzulu na kuruhusu Rais kuteua mrithi .
Kwa tafsiri ya kiintelijensia, hii si hatua ya dharura bali ni operesheni iliyopangwa ndani ya mfumo wa dola kwa maana ya simulizi ya kuondoka kwa udhibiti” (controlled exit narrative).
Pili, Mhe. Nchimbi anasema “nimeamua kustaafu siasa na utumishi wa umma.” Haya ni maneno yanayopaswa kuangaliwa kwa umakini. Kwa kawaida, viongozi wa kariba hii huwa hawaondoki ghafla bila sababu kubwa ya kisiasa au binafsi. Kwa tafsiri ya ndani hii ni lugha ya aidha kuficha ukweli wa shinikizo la kisiasa , mabadiliko ya nguvu (power reconfiguration). au kuyumba kwa uaminifu kwa mamlaka ya juu (Loyalty Framing)
Zingatia kwamba Mhe. Nchimbi anakumbusha kuwa alitoa ahadi kwa Rais kwamba angemtumikia kwa uaminifu, na angeondoka pale ambapo mabadiliko yangehitajika. Kwa tafsiri ya ndani hapa tunaona wazi kuwa mamlaka halisi iko kwa Samia Suluhu Hassan, na uamuzi huu unatokana na mapenzi ya kisiasa ya kiongozi mkuu wa dola.
Katika kufafanua hili Makamu wa Rais ameongeza sentensi muhimu isemayo “Nimeridhika bila shaka kuwa Rais anatamani mabadiliko.” Hii ndiyo kiini cha uchambuzi wote.
Katika taaluma ya kiintelijensia, kauli kama hii huangaliwa kama signal ya moja kwa moja kutoka kwa mamlaka ya juu ambayo imefungwa katika lugha ya heshima ili kuepuka mgogoro wa wazi.
Kwa tafsiri halisi Makamu wa Rais ameondolewa kwa njia ya kidiplomasia.
Hii inaungwa mkono pia na taarifa za nje zinazoonyesha kuwa kujiuzulu kwake kulihusishwa na hitaji la Rais kufanya mabadiliko ya uongozi . Aidha kwa mawiki kadhaa kulikuwepo na mashinikizo ya wazi kumtaka Makamu wa Rais kujiuzuru hasa baada ya “kuwahimiza Watanzania kupambania katiba mpya”
Ni muhimu kuelewa kuwa Makamu wa Rais ni nafasi ya pili kwa nguvu nchini Tanzania na ni mrithi wa moja kwa moja wa Rais iwapo lolote litatokea. Kwa hiyo, kuondoka kwa mtu kwenye nafasi hii si tukio la kawaida, ni tukio la kimkakati. Zaidi ya hapo, Mhe. Nchimbi alikuwa madarakani chini ya mwaka mmoja tangu uchaguzi wa 2025. Tafsiri ya kiintelijensia inaashiria kuwa ama kulikuwa na misalignment ya kisiasa ndani ya uongozi au kwa sasa kuna mabadiliko ya mkakati wa serikali ambayo hayakuendana na msimamo wake
Nchimbi amehitimisha barua yake kwa kusema “Nitaendelea kuwa raia mwema” Kauli hii inaonekana ya kawaida, lakini katika uchambuzi wa kisiasa ina maana nzito. Zingatia kwamba hasemi “nitaendelea kulitumikia taifa” bali “nitaendelea kuwa raia mwema.” Kwa tafsiri ya kiitelijensia ni kwamba anaondoka kwenye power structure kabisa, angalau kwa sasa.
Hii ni tofauti na viongozi wengi wanaoacha nafasi lakini hubaki ndani ya mfumo.
NINI KINAENDELEA NYUMA YA PAZIA?
Kwa kuchanganya vipengele vyote, uchambuzi wa kiintelijensia unaonyesha uwezekano wa mambo yafuatayo mgogoro wa ndani ya uongozi unaosukuma mabadiliko na upangaji upya wa nguvu na mamlaka katika chama na serikali yake. Kuondoka kwa Nchimbi kunaweza kuwa sehemu ya kupanga upya uongozi, kuweka watu wanaoendana zaidi na dira ya sasa ya Rais au wanaomuunga mkono bila kuhoji.
Hii nadhihirisha pia dalili zilizoanza kujionesha muda mrefu kwamba kulikuwa na tofauti za mtazamo kuhusu mwelekeo wa nchi hasa kwenye masuala nyeti kama mageuzi ya kisiasa au utawala. Kimsingi haya ni maandalizi ya jambo kubwa na la kushitua au kushangaza litakalokuja baadae. Katika siasa za Afrika, mabadiliko ya ghafla kwenye nafasi za juu mara nyingi huashiria kutokubaliana au kuyumba kwa uaminifu, maandalizi ya sera mpya, au hatua kubwa ya kisiasa inayokuja
MUSTAKABALI WA TANZANIA
Kwa nje, Tanzania itaendelea kuonekana tulivu. lakini kwa ndani, kuna fukuto la hali ya juu. Wananchi wanadai katiba mpya na mabadiliko ya kimfum pamoja na ujenzi wa muundo mpya wa nguvu. Hili ni vuguvugu ambalo haliwezi kupoa kwa urahisi kwani linasukumwa na mageuzi ya dunia nzima.
Kwa upande mwingine hatua hii inaimarisha zaidi nafasi ya Rais kama kitovu cha maamuzi yote makubwa na imepunguza kwa kiasi kikubwa plurality ya ndani ya serikali. Nchimbi alikuwa na mtazamo tofauti na kuondoka kwake kunaweza kupunguza sauti mbadala ndani ya mfumo. Aidha hii inaonesha kuibuka kwa kizazi kipya cha utawala kwani mrithi wake atakuwa mtu aliyechaguliwa na Rais mwenyewe, kwa uangalifu mkubwa, akiwakilisha “direction mpya” ya dola inayofuata maelekezo ya Rais.
Kwa kumalizia, kujiuzuru kwa Emmanuel John Nchimbi hakupaswi kutafsiriwa kama tukio la kawaida la kisiasa. Ni ishara ya mabadiliko ya kimkakati ndani ya dola, yanayompa Rais nguvu ya maamuzi isiyopingwa, lakini yaliyofungwa kwa lugha ya heshima na utulivu ili kulinda taswira ya utawala.
Kwa mtazamo wa kiintelijensia hii ni operesheni ya kisiasa iliyopangwa kwa uangalifu na wala si ajali ya kisiasa. Ni reconfiguration ya nguvu, si kuondoka kwa mtu mmoja tu. Kwa lugha nyepesi lakini yenye uzito ni kuwa Tanzania iko kwenye mgogoro wa wazi, unaofichwa na mchakato wa kujipanga upya kisiasa.
Uwe na amani.






Comments