Kukamatwa Kwa Wakili Madeleka ni Dalili ya Kuporomoka Kwa Utawala wa Sheria Nchini
- Rev. Godwin Chilewa
- 12 minutes ago
- 3 min read
Na Rev. Godwin Chilewa

Kukamatwa kwa Wakili Peter Madeleka kwa tuhuma za “kudharau amri ya mahakama kunaibua maswali mazito kuhusu mustakabali wa utawala wa sheria Tanzania. Wakili Madeleka, msomi aliyejijengea heshima kubwa alikamatwa akiwa katika mazingira ya utekelezaji wa wajibu wake wa kisheria jambo linalosababisha maswali mengi. Mbaya zaidi ni pale inapoonekana kwamba chombo kinachopaswa kulinda sheria kinatumika kama chombo cha kuzima sauti za kisheria ukizingatia kwamba amri yenyewe ya mahakama (iliyomtia matatani) inaibua shaka ya uhalali wake wa kikatiba.
1. Mgongano wa Kikatiba: Sheria dhidi ya Katiba
Katika mfumo wowote wa kisheria, Katiba ndiyo sheria mama (supremacy of the constitution). Hakuna amri ya mahakama, hakuna sheria ndogo, wala mamlaka ya kiutendaji inayoweza kusimama juu yake. Kwa msingi huo kama amri iliyodaiwa kudharauliwa ilikuwa kinyume na Katiba kama Wakili Madeleka alivyodai, basi uhalali wa amri hiyo unakuwa na shaka, utekelezaji wake unakuwa ni matumizi mabaya ya mamlaka, na adhabu kwa anayeipinga inaweza kuwa ni ukandamizaji wa haki.
Kwa mantiki hiyo, kumkamata wakili kwa kusimamia tafsiri ya Katiba ni sawa na kuiadhibu taaluma ya sheria yenyewe.
Hii ni hatari ya kimuundo (structural risk).
2. Uhalifu wa Kitaaluma (Criminalization of Professional Duty)
Wakili anapotekeleza wajibu wake, hana hiari ya kisiasa bali ana wajibu wa kikatiba kutetea haki, kutafsiri sheria, na kupinga ukiukwaji wa Katiba.
Kumkamata wakili akiwa katika utekelezaji wa jukumu hilo kunatengeneza mazingira ya hofu ya ndani ya taaluma ya sheria, kujiziba midomo kwa mawakili (self-censorship) na kuporomoka kwa ubora wa utetezi mahakamani. Hii inazalisha kile kinachoitwa chilling effect ambapo mawakili wanaacha kusema au kufanya haki kwa sababu ya hofu. Na hapa ndipo kauli ya Yesu inapata uzito wake wa kiroho na kisiasa:
“Kama mambo haya yanafanyika kwa mti mkavu, je itakuwaje kwa mti mbichi?”
3. Precedent Hatari: Kutoka Kwa Wakili hadi Kwa Raia wa Kawaida
Katika taratibu za kimahakama kesi moja hujenga precedent. Iwapo wakili aliyefundishwa sheria, anayejua haki zake, na mwenye uwezo wa kujitetea anaweza kukamatwa katika mazingira ya utata wa kikatiba, basi raia wa kawaida hana kinga yoyote, ulinzi wa kisheria unakuwa wa kinadharia tu, na mfumo wa haki unageuka kuwa chombo cha mamlaka, si kinga ya wananchi. Hii ndiyo maana ya “mti mbichi” katika mantiki ya Yesu. Wakili ni mti mkavu kwani anaijua haki na sheria, wakati raia wa kawaida ni mti mbichi kwani hana ulinzi wa kisheria wa kutosha. Ikiwa mti mkavu unachunywa magamba, basi mbichi utaangamia kabisa.
4. Kuyeyuka kwa Utawala wa Sheria (Erosion of Rule of Law)
Utawala wa sheria una misingi mitatu: Usawa mbele ya sheria, Uhuru wa mahakama na Ulinzi wa haki za msingi. Vitendo vya aina hii vinaathiri nguzo zote tatu. Usawa unapotea kwani sheria inatumika kwa kuchagua nani aadhibiwe. Mahakama zinadhoofika na zinapoteza uhalali wa kimaadili, na haki za msingi zinavunjwa kwa sababu uhuru wa kujieleza na haki ya utetezi vinabanwa. Matokeo yake ni hali ya legal uncertainty ambapo sheria haieleweki, na haki haitabiriki.
5. Taifa Linaelekea Wapi?
Kwa mtazamo wa kiusalama wa taifa (national stability analysis), matukio ya aina hii huzaa madhara makubwa. Kwanza ni kupungua kwa imani ya wananchi kwa taasisi za dola. Pili ni kuongezeka kwa hasira ya kimya (silent resentment), tatu ni hatari ya migogoro ya kijamii na kisiasa. Nne ni kujengeka kwa mazingira ya “rule by fear” badala ya “rule of law”
Mambo haya yakiachwa kuendelea kwa muda mrefu, yanaweza kusababisha kudhofika kwa uchumi (kwa sababu ya ukosefu wa uhakika wa sheria), kupungua kwa uwekezaji, na kuibuka kwa migawanyiko ya kitaifa. Kwa Tanzania hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa kuzingatia kuwa nchi bado haijapona toka majeraha mabaya ya matukio ya Oktoba 29, 2025.
Tahadhari kwa Taifa
Kukamatwa kwa Wakili Peter Madeleka si tukio la mtu mmoja. Ni ishara ishara ya mwelekeo wa mfumo wa haki, kipimo cha afya ya utawala wa sheria, na onyo kwa jamii. Ikiwa wale walioko mstari wa mbele kulinda Katiba wanaanza kuadhibiwa, basi raia wa kawaida hawana pa kujificha. Kama haya yanafanyika kwa mti mkavu, basi mti mbichi hauko salama tena.
Taifa linapaswa kuchagua kuheshimu Katiba au kuhalalisha nguvu. Kwa sababu mwisho wa safari hizi mbili ni tofauti kabisa.
Tathmini ya kiintelijensia:
Risk Level: HIGH
Institutional Integrity: DECLINING
Civil Liberties Outlook: THREATENED
Uwe na Amani






Comments