top of page

Kesi ya Tundu Lissu, TISS na Mustakabali wa Mgogoro wa Kisiasa Tanzania

Na Rev. Godwin Chilewa



Kesi ya Tundu Lissu inaashiria mgogoro wa kisiasa uliobadili umbo na si asili yake. Baada ya matukio ya damu ya Oktoba 29, 2025, wengi walidhani Tanzania imeingia katika kipindi cha “utulivu japo wa kulazimishwa.” Lakini kwa mtazamo wa kiintelijensia, hali iliyopo sasa ni dhahiri kwamba si utulivu, bali ni mgogoro uliobadilika sura (mutated political conflict).


Hivi sasa mapambano si kati ya waandamanaji na polisi, na hayapo tena mitaani; badala yake yamehamia mahakamani, katika taasisi za dola, na katika uwanja wa diplomasia na siasa za kimataifa. Katikati ya mabadiliko haya, kesi ya kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu, imegeuka kuwa kitovu cha mvutano wa kisiasa na kiusalama nchini.


KESI YA LISSU SI KESI YA MTU MMOJA

Kisheria, kesi ya uhaini inayomkabili Lissu ilitokana na hotuba yake ya kisiasa akidai mageuzi ya uchaguzi kabla ya uchaguzi wa 2025. Lakini kwa mtazamo wa kiintelijensia, kesi hii imevuka mipaka ya mahakama na kuwa:

“strategic political instrument”


Tundu Lissu, ambaye ni mwenyekiti wa CHADEMA na mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani nchini, amekuwa mahabusu tangu Aprili 2025 bila dhamana kutokana na uzito wa kosa la uhaini . Kesi yake imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara na kugubikwa na mijadala kuhusu ushahidi wa siri, uwazi wa mahakama na haki ya utetezi. Katika mazingira ya kisiasa yenye mgawanyiko, kesi ya aina hii haiwezi kubaki kuwa ya kisheria tu, hugeuka kuwa kipimo cha uhalali wa mfumo wa haki, alama ya mvutano kati ya dola na upinzani na kichocheo cha hisia za umma


MCHAKATO WA KESI NA ATHARI ZAKE

Kesi ya Lissu imeonyesha dalili kadhaa za kimkakati:

1. “Judicialization of Political Conflict”

Mgogoro umehamia mahakamani badala ya mitaani. Hata hivyo changamoto ni kwamba Mahakama zinapoonekana kuhusishwa na siasa, au kupokea mashinikizo ya viongozi wa juu hukumu hupoteza uaminifu kwa wananchi. Hali hii huunda kile kinachoitwa “legitimacy deficit within institutions”


2. “Delay Dynamics” kama Chanzo cha Mvutano

Kesi hii imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara kitu ambacho kimeongeza hali ya sintofahamu na hasira ya kisiasa . Uchambuzi wa kiitelijensia unaonesha kwamba ucheleweshaji wa kesi nyeti kama hii huongeza hisia za kunyimwa haki, huimarisha simulizi za ukandamizaji, na huongeza uwezekano wa mobilization ya kisiasa.


3. “Opacity Risk” (Hatari ya Ukosefu wa Uwazi)

Hatua zilizochukuliwa na mahakama kama kuficha mashahidi, na kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya kesi zimeibua maswali kuhusu uwazi wa mchakato. Kwa taaluma ya ujasusi, ukosefu wa uwazi huongeza information vacuum” ambapo nafasi hiyo hujazwa na uvumi, propaganda na polarization..


MGOGORO WA SASA: NINI KINAENDELEA CHINI KWA CHINI?

Kwa mtazamo mpana, Tanzania sasa ipo katika hatua hatari inayojulikana kama: “controlled tension environment” Hii ina maana: hakuna maandamano makubwa ya wazi lakini kuna mkusanyiko wa hasira ya kimfumo. Dalili zake ni: pamoja na kukamatwa kwa wanachama wa upinzani na kesi za ugaidi au uchochezi, shinikizi la kimataifa kuhusu haki za binadamu na utawala wa sheria, tofauti kubwa ya tafsiri ya matukio kati ya serikali na upinzani. Hali hii hujenga mazingira ya utulivu unaoonekana lakini uliojaa hatari  “latent instability”


TISS: KATI YA USALAMA NA SIASA

Katika mazingira haya, jukumu la TISS linakuwa nyeti zaidi kuliko wakati wowote. Tatizo kuu lililojitokeza tangu 2025 ni mfumo kuelemea zaidi kwenye usalama wa dola (state security) kuliko usalama wa kisiasa (political stability).

Kwa lugha ya kiintelijensia, hii ni over securitization of political space” Matokeo yake ni upinzani kuonekana kama tishio badala ya mshindani wa kisiasa, Taarifa kuchujwa ili kuendana na matarajio ya kisiasa na hatari za kweli kutoonekana kwa uhalisia wake


NAFASI YA KESI YA LISSU KATIKA MUSTAKABALI WA TAIFA

Kesi ya Lissu sasa ni inflection point” yaani sehemu ya mabadiliko ambayo inaweza kuelekeza taifa katika mojawapo ya njia mbili:

Njia ya Kwanza: ni urejeshaji wa uhalali hasa kama mchakato utaonekana kuwa: huru, wazi na wa haki kiasi cha kuweza kupunguza mvutano, kujenga imani ya ndani na nje na kufungua njia ya maridhiano ya kisiasa.


Njia ya Pili ni kuongezeka kwa mgogoro

Ikiwa mchakato utaonekana kuwa: wa kisiasa, usio wa haki na uliodhibitiwa. Hii itasababisha kuimarika kwa hisia za ukandamizaji, kuchochea maandamano mapya na kuongeza shinikizo la kimataifa


TISS INAPASWA KUFANYA NINI SASA?

Kwa mtazamo wa kitaaluma, Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) inaoaswa kufanya mageuzi ya haraka ya kimkakati:

1. Kuhama kutoka “Reactive Intelligence” kwenda “Predictive Intelligence”

Badala ya kusubiri matukio, inapaswa kuchambua mienendo ya kisiasa, na kutabiri hatari kabla hazijatokea


2. Kutoa Ushauri Huru kwa Uongozi

Katika kutekeleza wajibu huu taarifa lazima ziwe: kamili, za kweli, bila kupunguzwa na bila kupotoshwa kisiasa. Hi ndiyo njia ya kuepuka:

strategic surprise failure”


3. Kujenga Mfumo wa “Conflict De-escalation”

TISS isiwe chombo cha kukandamiza wapinzani au makundi ya aina fulani, bali:kiwe chombo cha kushauri namna ya kupunguza mvutano na kiungo kati ya usalama na siasa


4. Kuepuka “Echo Chamber”

Hili ni jambo linalopaswa kuangaliwa kwa umakini wa hali ya juu. Hatari kubwa kwa sasa ni mfumo kusikia:kile unachotaka kusikia, si kile kinachotokea.


UKIMYA AU DHORUBA?

Tanzania ipo katika hatua ambayo si rahisi kuitafsiri kwa macho ya kawaida. Kuna utulivu juu ya uso, lakini chini yake kuna mvutano unaoendelea kujengeka. Kesi ya Tundu Lissu si tukio la kawaida, ni kipimo cha mwelekeo wa taifa. Ikiwa itasimamiwa kwa haki, inaweza kuwa mwanzo wa kurejesha uhalali. Lakini ikiwa itasimamiwa kisiasa, inaweza kuwa kichocheo cha mgogoro mpya.


Katika siasa za kisasa, nguvu inaweza kunyamazisha sauti, lakini haki ndiyo huondoa sababu ya kupaza sauti. Na katika mazingira ya Tanzania ya sasa mabadiliko hayo yatakuja aidha kwa utulivu au kwa dhoruba kubwa.


Uwe na amani

 
 
 

Comments


bottom of page