top of page

Uamuzi wa Mahakama Kuu Dhidi ya Tundu Lissu na Athari Zake Kwa Siasa na Diplomasia

Na Rev. Godwin Chilewa



Tarehe 21 Agosti 2026, Mahakama Kuu ya Tanzania ilitoa uamuzi wenye uzito mkubwa wa kisheria na kisiasa kwa kumkuta mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kuwa ana kesi ya kujibu katika shtaka la uhaini. Uamuzi huu umetolewa na jopo la majaji watatu baada ya kuridhika kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka unatosha kuanzisha wajibu wa utetezi kwa mshtakiwa.


Kwa mujibu wa kanuni za mwenendo wa mashauri ya jinai, hatua hii si hukumu ya mwisho bali ni kiashiria kwamba kesi imeingia katika hatua ya msingi ya usikilizwaji wa utetezi. Hata hivyo, kwa kuzingatia hadhi ya mshtakiwa pamoja na uzito wa shtaka la uhaini, uamuzi huu una athari pana zinazovuka mipaka ya ukumbi wa mahakama na kuingia katika nyanja za siasa za ndani na diplomasia ya kimataifa.


Maana ya Kisheria ya “Kesi ya Kujibu”

Katika taaluma ya sheria ya jinai, kauli ya mahakama kuwa mshtakiwa “ana kesi ya kujibu” (prima facie case established) ina maana kuu tatu: Kwanza ni kuwa upande wa mashtaka umefanikiwa kuwasilisha ushahidi wa awali unaoonyesha uwezekano wa kutendeka kwa kosa linalodaiwa. Pili, mahakama imejiridhisha kuwa endapo ushahidi huo hautapingwa au kukanushwa, unaweza kupelekea hatia kuthibitishwa. Tatu, mzigo wa ushahidi (evidential burden) unahamia kwa mshtakiwa, ambaye sasa anatakiwa kuwasilisha utetezi wake iwe kwa ushahidi wa mashahidi, vielelezo, au hoja za kisheria.


Kwa mantiki hii, uamuzi huu hauleti hitimisho la moja kwa moja kwamba mshitakiwa ana hatia, bali unathibitisha tu kuwa hoja za mashtaka hazijaporomoka katika hatua ya awali. Kwa mujibu wa taarifa za kesi husika, mahakama iliona kuwa ushahidi uliotolewa unatosha kuendelea na kesi ya uhaini, hivyo kumtaka Tundu Lissu kuanza kujitetea.


Ni muhimu kuzingatia kwamba katika sheria ya Tanzania, kosa la uhaini ni miongoni mwa makosa mazito zaidi, likiwa na adhabu kali inayoweza kufikia kifungo cha maisha au hata kifo. Kwa msingi huo upande wa mashitaka unapaswa kuthibitisha pasipo shaka yoyote kwamba mtuhumiwa ametenda kosa husika. Aidha, mtuhumiwa katika utetezi wake anachopaswa ni kutoa hoja zinazotengua ushahidi au hata kutia shaka tu uwezekano wa kosa hilo kutendeka.


Hoja mojawapo nzito ambayo imekuwa ikitajwa mara nyingi ni ule uwezekano wa mtu mmoja kuweza kupanga na kutekeleza kosa la uhaini peke yake. Hoja hii inapata uzito mkubwa sana ukizingatia kuwa mamia ya watu wengine waliokamatwa na kufunguliwa kesi ya uhaini baada ya matukio ya tarehe 29 Oktoba 2025 waliachiwa huru bila masharti yoyote jambo linalotia shaka kwamba mashitaka hayo yalikuwa ya kisiasa.


Muktadha wa Kisiasa wa Shauri

Kesi dhidi ya Tundu Lissu haiwezi kutenganishwa na muktadha mpana wa kisiasa nchini Tanzania ukizingatia kuwa mshitakiwa ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, ambacho kihistoria kimekuwa na mvutano wa kisiasa na dola, hasa katika kipindi cha uchaguzi wa mwaka 2025.


Aidha, mazingira ya kisiasa kabla na baada ya uchaguzi huo yaligubikwa na malalamiko ya ukandamizaji wa kisiasa, ukosefu wa usawa wa kisiasa, pamoja na matukio ya vurugu na vifo vya raia, hali iliyozua mjadala mpana kuhusu mustakabali wa demokrasia nchini. Katika mazingira haya, hatua yoyote ya kisheria dhidi ya kiongozi wa upinzani, hususan inayohusisha shtaka la uhaini, hupata tafsiri ya ziada ya kisiasa, iwe kwa haki au kwa dhana ya kisiasa.


Athari kwa Mchakato wa Maridhiano ya Kitaifa

Katika muktadha wa maridhiano ya kisiasa, uamuzi huu una athari zenye sura mbili zinazopingana. Kwa upande mmoja, serikali inaweza kuwasilisha uamuzi huu kama ushahidi wa utawala wa sheria (rule of law), ikisisitiza kuwa migogoro inapaswa kushughulikiwa kupitia vyombo halali vya kisheria.

Hata hivyo, kwa upande mwingine, uwepo wa kesi nzito ya jinai dhidi ya kiongozi wa upinzani una uwezo wa kudhoofisha imani kati ya pande hasimu za kisiasa. ya kweli yanahitaji mazingira ya kuaminiana, na kesi ya aina hii inaweza kutafsiriwa kama kikwazo kinachozuia mazungumzo ya dhati.


Zaidi ya hayo, historia ya madai ya ukandamizaji wa kisiasa na hatua kali za dola dhidi ya wapinzani inaweza kufanya uamuzi huu kuonekana kama sehemu ya mkakati mpana wa kisiasa badala ya mchakato huru wa kisheria. Hali hii inaweza kuchelewesha au hata kuvuruga juhudi zozote za maridhiano ya kitaifa.


Uwezekano wa Kutumika Kama Chombo cha Shinikizo la Kisiasa

Katika uchambuzi wa kiintelijensia wa kisiasa, hatua za kisheria wakati mwingine hutumika kama zana za kuathiri mienendo ya kisiasa.

Kesi ya uhaini dhidi ya kiongozi wa juu wa upinzani inaweza kuwa na athari ya: kuweka shinikizo kwa chama husika ili kuingia katika mazungumzo ya kisiasa, kudhibiti au kupunguza nguvu ya uhamasishaji wa kisiasa wa upinzani, kuunda mazingira ambayo upande wa upinzani unalazimika kufanya maamuzi ya kimkakati ili kulinda uhai wa chama au viongozi wake.


Hata hivyo, mkakati wa aina hii una hatari ya kurudisha nyuma matokeo yaliyokusudiwa. Badala ya kulazimisha mazungumzo, unaweza kuimarisha misimamo mikali ya kisiasa na kuongeza mgawanyiko.


Athari kwa Diplomasia ya Kimataifa

Katika nyanja ya kimataifa, kesi hii tayari imeanza kuvutia uangalizi wa wadau mbalimbali, ikiwemo mataifa ya Magharibi, taasisi za haki za binadamu, na mashirika ya kimataifa. Kwanza, kesi dhidi ya kiongozi wa upinzani kwa shtaka la uhaini mara nyingi huchukuliwa kama kipimo cha uhuru wa kisiasa na uhuru wa mahakama. Hali hii inaweza kuathiri taswira ya Tanzania katika jamii ya kimataifa.


Pili, tayari kumekuwepo na ishara za wasiwasi wa kimataifa kuhusu hali ya haki za binadamu nchini, ikiwemo hatua za vikwazo dhidi ya maafisa wa usalama (polisi) mmojawapo akiwa Mafwele, na tathmini upya ya mahusiano ya kidiplomasia. Tatu, mazingira ya kisiasa yenye migogoro yanaweza kuathiri imani ya wawekezaji wa kimataifa, ambao kwa kawaida hutegemea utulivu wa kisiasa na uhakika wa kisheria katika kufanya maamuzi ya uwekezaji.


Si hivyo tu, bali pia mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika mara nyingi huhimiza nchi wanachama kuhakikisha utawala wa sheria unaendana na kulinda haki za msingi za kisiasa, hivyo kuongeza shinikizo la kidiplomasia kwa njia ya mazungumzo ya kimya (quiet diplomacy).


Kwa kumalizia nisisitize kwamba kwa pmtazamo wa kisheria, uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba Tundu Lissu ana kesi ya kujibu ni hatua ya kawaida katika mwenendo wa mashauri ya jinai, unaothibitisha tu uwepo wa ushahidi wa awali unaohitaji kujibiwa na mshtakiwa. Hata hivyo, kwa mtazamo mpana zaidi, uamuzi huu una uzito mkubwa wa kisiasa na kidiplomasia. Unaweza ama kuimarisha hoja ya utawala wa sheria au kudhoofisha juhudi za maridhiano, kutegemeana na namna unavyotafsiriwa na wadau mbalimbali.


Katika mazingira ya sasa ya kisiasa nchini Tanzania, ambapo kuna historia ya mvutano wa kisiasa na uangalizi wa kimataifa, kesi hii ina uwezekano mkubwa wa kuendelea kuwa kiini cha mjadala mpana kuhusu mustakabali wa demokrasia, haki za binadamu, na uhusiano wa Tanzania na jumuiya ya kimataifa. Kwa hiyo, maendeleo ya hatua zinazofuata katika kesi hii yatakuwa na umuhimu mkubwa kwa mwelekeo wa kisiasa na kisheria wa taifa kwa ujumla.


Uwe na amani.

 
 
 

Comments


bottom of page