Quran Inaeleza Nini Kuhusu Uhusiano wa Wakristo na Waislam?
- Rev. Godwin Chilewa
- Apr 4, 2025
- 5 min read

Dunia ya leo imejaa chuki, husuda fitna na vita. Upendo umepoa, kiburi kimetamalaki na chuki imeota mizizi. Mbaya zaidi ni kuwa dini imekuwa chanzo kikubwa cha mafarakano, chuki na vita. Sasa ikiwa Mungu ndiye aliyeleta dini duniani kama njia au muongozo wa kiroho kwa wanadamu, kwanini dini hizo zimekuwa chanzo cha chuki, vita na mafarakano? Inawezekana kuna mahali waumini au viongozi wa dini wa leo wamepotoka?
Tuanze kwa kutafakari uhusiano wa dini mbili maarufu zaidi duniani, Ukristo na uislam. Dini hizi zenye msingi wa imani ya Ibrahim leo hii zimejenga mfarakano mkubwa miongoni mwa waumini wake. Lakini je, wajua kwamba mtume Muhammad (s.a.w) aliuheshimu sana ukriso na kuwaheshimu waumini wake? Wajua kwamba mtume Muhammad (s.a.w) alibashiriwa utume na kasisi (padre) wa Kikristo aitwae Waraqah bin Nawfal?
Ilikuwa hivi: Baada ya tukio la kwanza la wahyi (ufunuo) ambapo mtume Muhammad (s.a.w) alitokewa na Jibril katika pango la la Hira, Muhammad alirudi nyumbani akiwa amejaa hofu na mshangao mshangao mkubwa. Mkewe, bi Khadija alimtuliza na kisha akampeleka kwa binamu yake (Bi Khadija) aitwae Waraqah bin Nawfal aliyekuwa kasisi (padri) Mkristo, msomi wa Torati na Injili, na mmoja wa Wakristo waliokuwa wakipinga ibada ya sanamu na kuhimiza imani kwa Mungu mmoja.
Padri Waraqah bin Nawfal baada ya kusikia maelezo ya Muhammad kuhusu kile kilichotokea, alimwambia "Huyo aliyekutokea ni Namus (Jibril), ambaye alimtokea Musa. Laiti ningekuwa kijana bado! Laiti ningekuwa hai siku watu wako watakapokutoa (Makkah)". Mtume Muhammad (s.a.w) alishangazwa na jibu hilo na akauliza: "Je, watu wangu watanikataa?" Waraqah akajibu "Hakika, hakuna mtu aliyewahi kuja na kitu kama hiki bila kukabiliwa na uadui. Ikiwa nitakuwa hai wakati huo, nitakusaidia kwa nguvu zangu" (Soma Sahih Bukhari, Kitabu cha Mwanzo wa Wahyi - Kitab Bad' al Wahy - hadithi ya kwanza, au kitabu cha kiswahili Maisha ya Mtume Muhammad)
Zingatia kwamba maneno ya padri huyu Mkristo, Waraqah ulikuwa ndio uthibitisho wa kwanza wa nje kwa mtume Muhammad (s.a.w) kuhusu utume wake, na yalionyesha uelewa kuhusu ujumbe wa Mungu na changamoto ambazo mitume hukumbana nazo. Ni kwa sababu hii Mtume Muhammad katika maisha yake ya awali hakuwahi kuukana ukristo kwamba si dini ya mwenyezi Mungu au ni ukafiri kama zinavyoeleza sura na hadithi zinazofuata:
Surat Al-Ma’idah (5:82)
“Hakika utawakuta wale walio karibu mno kwa upendo kwa Waumini ni wale wanaosema: Sisi ni Wakristo. Hayo ni kwa sababu miongoni mwao wamo makasisi na watawa, nao hawatakabari.”
Aya hii inaonyesha kuwa Wakristo wana sifa za unyenyekevu na wana uhusiano wa karibu na Waislamu kwa sababu ya imani yao katika Mungu.
————————————————
Surat Al-Baqara (2:62)
“Hakika wale walioamini, na Mayahudi, na Wakristo, na Wasabai, yeyote miongoni mwao atakayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akatenda mema, basi watapata malipo yao kwa Mola wao, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika.” Hii inaonyesha kuwa Wakristo wanaweza kupata wokovu kwa kumwamini Mungu na kutenda matendo mema.
————————————————
2. Qur’an Inavyothibitisha Ubora wa Wakristo
Surat Al-Ma’idah (5:46)
“Na tukawafuatishia Isa bin Maryamu, akiitimiza Taurati iliyokuwa kabla yake. Na tukampa Injili yenye uwongozi na nuru na inayo sadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na uwongofu na mawaidha kwa wachamungu.” Hii inathibitisha kuwa Injili ilitoka kwa Mungu na ilikuwa mwongozo wa kweli.
————————————————
Surat Al-Imran (3:55)
“Mwenyezi Mungu alipo sema: Ewe Isa! Mimi nitakufisha na nitakupandisha kwangu, na nitakutakasa na wale waliokufuru, na nitawaweka wale waliokufuata juu ya wale waliokufuru mpaka Siku ya Kiyama…”Hapa, Qur’an inathibitisha kuwa wafuasi wa Yesu watakuwa juu ya wasiomwamini mpaka Siku ya Kiyama, jambo linaloashiria nafasi ya kipekee ya Ukristo.
————————————————-
KWA UJUMLA….
Qur’an inakubali kuwa Wakristo wana nafasi ya pekee kama watu wa Kitabu, na pia inaonyesha kuwa kuna uhusiano mzuri kati ya Waislamu na Wakristo. Ingawa kuna tofauti za kiimani, Qur’an inawahimiza Waislamu kuwa na uhusiano wa amani na Wakristo, hasa wale wanaoishi kwa haki na unyenyekevu.
——————————————————
Qur’an Surat Al-Ma’idah (5:5):
“Leo mmehalalishiwa vitu vizuri. Na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao…” Aya hii inaeleza kuwa Waislamu wanaruhusiwa kula chakula cha “Watu wa Kitabu”, yaani Mayahudi na Wakristo, ikiwemo wanyama waliowachinja, mradi tu mchakato wa uchinjaji unazingatia kumtaja Mungu (Allah).
—————————————————
HADITHI Kuhusu Ukarimu wa Wakristo
Mtume Muhammad (SAW) alisema:
“Hakika mtawakuta watu wenye huruma zaidi kwa Waislamu ni wale wanaosema: ‘Sisi ni Wakristo.’ Hii ni kwa sababu miongoni mwao wamo makasisi na watawa, na wao hawatakabari.”
(Imepokelewa na Imam Ahmad, (Tafsiri ya Qur’an 5:82) Hadithi hii inathibitisha kwamba Wakristo wana tabia ya unyenyekevu, huruma, na ukarimu kwa Waislamu.
——————————————————
2. Hadithi Kuhusu Ulinzi wa Wakristo wa Najran
Mtume Muhammad (SAW) aliwapatia Wakristo wa Najran (Yemen ya sasa) mkataba wa ulinzi, akisema: “Najran na wakazi wake wako chini ya ulinzi wa Mwenyezi Mungu na ahadi ya Mtume wake. Mali yao, dini yao, makanisa yao, na watawa wao wako salama. Hakuna mtu atakayelazimishwa kubadili dini yake.” (Mkataba wa Najran, Ibn Sa’d, Kitab al-Tabaqat al-Kabir) Hii inaonyesha jinsi Mtume Muhammad (SAW) alivyowaheshimu Wakristo na kuwapa uhuru wa dini.
———————————————————
3. Hadithi Kuhusu Urafiki wa Waislamu na Wakristo
Mtume Muhammad (SAW) aliwahi kusema:
“Acha Wakristo wa Habasha wakiwa katika amani, kama wao wanavyotuacha sisi.”
(Sunan Abu Dawood, 4309) Hii inahusiana na wakati Mtume alipowatuma baadhi ya Waislamu kuhifadhiwa na Mfalme wa Kikiristo wa Habasha (Najashi) wakati wa mateso huko Makka.
———————————————
(Qur’an, Surat Aal-Imran 3:64)
“Enyi watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lililo sawa baina yetu na nyinyi, ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote, wala tusifanye baadhi yetu kuwa miungu badala ya Mwenyezi Mungu.” Aya hii inahimiza maelewano, mshikamano, na kuheshimiana kati ya Waislamu na Wakristo kwa msingi wa kumwabudu Mungu mmoja. ZINGATIA:
“Neno lililo sawa baina yetu na nyinyi” maana yake TUNAMWAMINI Mungu mmoja.
Maneno hayo yanalingana na
yale ya Nabii Issa bin Mariam (Masihi, Yesu Kristo) katika INJILI aliyesema “Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.” (Yohana 10:16)
————————————————
KWA UJUMLA:
Hadithi hizi zinaonyesha kuwa Mtume Muhammad (SAW) aliwaheshimu Wakristo na alihimiza uhusiano wa amani na undugu kati ya Waislamu na Wakristo. Alisisitiza haki zao za kidini, akawapa hifadhi, na kutambua tabia zao njema kama huruma na unyenyekevu. Hii ni dalili kwamba Uislamu unahimiza kuheshimu na kushirikiana na Wakristo kwa msingi wa haki, amani, na uadilifu.
———————————————————
TATIZO LILOPO:
Baadhi ya viongozi wa dini, wameacha kuhubiri ukweli huu na kufundisha fitna na uchonganishi unaotangaza uadui kati ya wakristo na waislam. wakiwajumuisha WAKRISTO na WAPAGANI (Makafir) jambo ambalo si kweli. Mafundisho hayo ni kinyume na kweli ya mwenyezi Mungu, kama inavyoelezwa katika Quran na hadithi. Mbaya zaidi baadhi ya waislam na wakristo wanafurahia na kushabikia mafundisho ya chuki kuliko yanayohimiza upendo na amani kama alivyohimiza mtume (S.A.W) Jifunze ukweli ili usiyumbishwe.
Mwenyezi Mungu atupe mwongozo na taufiq katika haki na uadilifu.
Rev. Godwin Chilewa






Comments