Siasa za Vita na Uadui Zitajenga Taifa?
- Rev. Godwin Chilewa
- 2 days ago
- 3 min read
Na Rev. Godwin Chilewa

Katika katiba ya Jamhuri ya Muungano na sera, Tanzania ni taifa linalofuata mfumo wa vyama vingi. Lakini katika uhalisia wa kisiasa, mienendo yake mara nyingi hutoa taswira ya mfumo wa chama kimoja uliovaa vazi jipya. Tofauti kati ya nadharia na vitendo inajionesha bayana katika siasa za nchi, huku ushindani unaotarajiwa kuzaa hoja mbadala na uwajibikaji umegeuka kuwa uadui unaoziba milango ya mazungumzo ya kitaifa. Hiyo ndiyo Tanzania.
Mizizi ya tatizo hili inaanzia kwenye historia ya kisiasa ya nchi. Katika enzi za chama kimoja chini ya mwalimu Julius Nyerere, utamaduni wa siasa uliundwa juu ya umoja, nidhamu na utiifu kwa chama tawala. Mfumo huo uliweka msingi imara wa dola yenye chama kimoja chenye ushawishi mpana katika taasisi zote za umma.
Mwaka 1992, Tanzania iliporuhusu rasmi vyama vingi, mabadiliko hayo yalikuwa ya kisheria zaidi kuliko ya kiutamaduni. Taasisi nyingi ikiwa pamoja na vyombo vya dola ziliendelea kufanya kazi kwa mtazamo wa zamani, ambapo chama tawala kilionekana kuwa sawa na dola yenyewe.
Hali hii ilisababisha kutokuwepo kwa usawa wa kimfumo kati ya chama tawala na upinzani. Upatikanaji usio sawa wa taarifa na mahusiano na vyombo vya dola, kujengwa kwa hofu ya kisiasa: kwamba kushirikiana na mpinzani ni kusaliti
Kwa mantiki hiyo, kiongozi wa upinzani akionekana karibu na vyombo vya dola kama TISS au mkuu wa jeshi la polisi, huonekana kama msaliti, na akiwa na uhusiano wa karibu na kiongozi wa chama tawala husemwa Menunuliwa. Hii si kwa sababu ya ukweli, bali ni matokeo ya mazingira ya muda mrefu ya kutoaminiana.
Ukitazama tatizo hili kijuujuu ni rahisi kumlaumu mtu au kikundi fulani, lakini ukweli ni kwamba tatizo hili limekua kwa sababu ya mfumo mzima wa kisiasa: Chama tawala (Chama Cha Mapinduzi) kimeendelea kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya taasisi za dola. Vyama vya upinzani navyo vimejenga siasa za mapambano makali kama njia ya kujilinda na kujitambulisha wakati vyombo vya dola mara nyingi huonekana kuwa upande mmoja badala ya kuwa kwa manufaa ya kitaifa.
Kwa miaka mingi, kila upande umejenga ukuta wake: CCM ikijiona mlinzi wa utulivu wa taifa, na upinzani ukijiona sauti ya haki inayokandamizwa. Katikati ya mitazamo hii miwili, mazungumzo ya kitaifa yamekufa na badala yake limezaliwa kundi la machawa wa chama tawala walio tayari kushangilia kila linalosemwa na watawala hata kama halina manufaa kwa taifa. Uzalendo umepotea!
Hali hii ni tofauti na mifumo kama wa United States, ambapo licha ya ushindani mkali kati ya Democratic Party na Republican Party, kuna nyakati muhimu ambapo viongozi hukaa pamoja kwa maslahi ya taifa. Kwa mfano, baada ya mashambulizi ya September 11 attacks, vyama vyote viwili vilisimama pamoja kupitisha sera za usalama wa taifa.
Tena yanapofika masuala ya kiuchumi na ushindani wa kimataifa hapo uchama huwekwa pembeni kwa naskahi ya taifa. Mipango ya miundombinu, kama Infrastructure Investment and Jobs Act (2021), ilipata uungwaji mkono kutoka pande zote mbil, na katika mijadala ya bajeti na madeni ya taifa, mara nyingi hufanyika makubaliano ya pande mbili (bipartisan deals) ili kuepusha madhara makubwa kwa uchumi.
Tofauti kubwa hapa si kwamba Marekani haina migogoro ipo,, na wakati mwingine mikali sana bali ni kwamba mfumo wao unalazimisha ushirikiano katika maeneo ya msingi ya kitaifa. Kumbe tatizo la Tanzania: Kukosekana kwa “Consensus Culture” hatuthamini siasa za makubaliano ya msingi. Kila hoja kutoka upande mmoja huonekana kama tishio kwa upande mwingine. Hii ina madhara makubwa.
Licha ya kujenga uadui lakini pia sera nzuri kutoka upinzani hukataliwa kwa sababu ya nani ameitoa, si ubora wake. Serikali hupitisha maamuzi bila mjadala mpana wa kitaifa, na wananchi hukosa uwakilishi halisi wa mawazo tofauti. Badala ya wananchi kumiliki serikali, mambo huwa kinyume chake.
Ili kuvunja mzunguko huu wa uadui, hatua kadhaa za kimkakati zinahitajika. Kwanza yafanyike mageuzi makubwa ya kitaasisi. Vyombo vya dola vinapaswa kuonekana na kufanya kazi kama taasisi za taifa, si za chama. Hii itajenga imani kwa pande zote.
Pili yaanzishwe majukwaa ya mazungumzo ya Kitaifa yanayowakuranisha viongozi wa vyama vyote kujadili masuala ya msingi kama uchumi, usalama na katiba bila kujali tofauti za kichama. Kipaumbele kiwekwe kwenye masuala ya msingi tu na si propaganda.
Tatu, Vyombo vya habari na asasi za kiraia vilenge kuhimiza mjadala wa sera badala ya mashambulizi ya kisiasa. Mvutano uliopo sasa unatengeneza mazingira magumu kwa pande zote, lakini zaidi kwa wasio madarakani.
Nne wananchi wote na hasa wanachama na viongozi wa chama tawala waelimishwe maana na utendaji wa mfumo wa vyama vingi vya suasa. Watambue kwamba upinzani si adui wa taifa bali ni sehemu ya mfumo wa uwajibikaji. Kukubali hili ni hatua muhimu ya kisaikolojia na kisiasa. Aidha wananchi wafundishwe kutofautisha kati ya ushindani wa kisiasa na uadui wa kitaifa.
Kwa ujumla Tanzania Inahitaji Mageuzi ya Fikra. Changamoto ya Tanzania si ukosefu wa sheria au mifumo, bali ni ukosefu wa utamaduni wa kisiasa unaokubali tofauti bila uhasama. Bila kubadili mtazamo huu, hata mageuzi ya kisheria hayataleta matokeo ya kudumu. Huu ni wakati wa kujiuliza:m kama siasa za vita na ushindani zitatusaidia kujenga taifa au kutubomoa. Jibu la swali hili ndilo litakaloamua mustakabali wa demokrasia ya Tanzania.
Uwe na Amani






Comments