top of page

URITHI WA MADARAKA AU DEMOKRASIA?

Na Rev. Godwin Chilewa



Kifo cha ghafla cha Seneta mashuhuri wa Marekani, Lindsey Graham, kimeacha gumzo kubwa kisiasa kwa sababu ya pengo la uongozi wake, Hata hivyo hatua ya dada yake, Darline Graham Nordone, kuchukua nafasi yake katika Seneti imewaacha hoi hata wale waliozoea kupora madaraka! Wengi wanajiuliza kama huu ni urithi wa kisiasa? Au ni utekelezaji halali wa sheria? na kama ni utaratibu wa kisheria nini athari zake kwa mustakabali wa demokrasia, hasa kwa nchi za Afrika.


Ukweli ni kwamba Katiba ya Marekani hairuhusu urithi wa madaraka. Badala yake, kupitia Marekebisho ya 17, gavana wa jimbo ana mamlaka ya kuteua mtu yeyote kuwa seneta mbadala wa muda pale seneta anapofariki au kuacha nafasi kabla ya kipindi cha uchaguzi. Mamlaka haya ni ya kisheria na hayaingiliwi na serikali kuu. Hivyo basi, Darline hakurithi kiti hicho kama mali ya kifamilia, bali aliteuliwa kisiasa .


Hata hivyo, ukweli huu haujazuia mjadala mkali kuhusu maadili ya uamuzi huo. Wanasiasa na wanaharakati wengi wanasema wazi huu ni mfano wa wazi wa nepotism yaani upendeleo wa kifamilia ndani ya siasa. “Ni vigumu kuamini kwamba kati ya maelfu ya watu wenye uwezo, ndugu wa karibu ndiye chaguo bora zaidi.” Mwanasiasa mmoja alilalamika. Wengine wanaona kuwa uteuzi huo unadhoofisha misingi ya demokrasia kwa kuweka hisia za kifamilia juu ya ushindani wa wazi, kupunguza imani ya wananchi katika mfumo, kuleta taswira ya siasa kuwa mali ya familia chache.


Ukiacha Marekani, suala hili limezia mjadala mkubwa nchini Tanzania hasa baada ya kauli ya aliyekuwa mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bw. Zito Zuberi Kabwe kutoa kauli inayoonesha kuunga mkono kitendo hicho (nepotism ). Kabwe ametoa kauli hii wakati Tanzania ikikabiliwa na malalamiko mengi yabuwepo wa nepotism katika serikali kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya taifa.


Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, nafasi ya kisiasa inapokuwa wazi, wananchi ndio wenye mamlaka ya mwisho kupitia uchaguzi mdogo. Hakuna kifungu kinachoruhusu mtu kuteuliwa moja kwa moja kwa misingi ya uhusiano wa kifamilia. Mfumo huu unalinda usawa wa kisiasa, ushindani wa haki, na uhalali wa viongozi wanaochaguliwa. Hata hivyo kwa sasa sheria na kanuni hizi zinaelekea kuyeyuka kama samli kwenye kikaango.


Wasiwasi unaowakumba wengi nchini ni uwezekano wa viongozi wetu kuweza kubadilisha sheria kuiga mfumo huu wa kimarekani kwa manufaa yao binafsi. Ukweli ni kuwa ingawa mfumo wa Marekani una faida ya kuzuia pengo la uongozi, una hatari kubwa kwa mazingira ya Afrika.


Kwa ujumla mfumo huu unaweza kuhalalisha “familia za kisiasa” utafungua mlango wa urithi wa madaraka, na kudhofisha imani ya wananchi katika uchaguzi. Katika bara ambalo tayari linakabiliwa na changamoto za utawala, hatua kama hizi zinaweza kuwa kichocheo cha migogoro ya kisiasa, na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.


Kwa wachambuzi wa kisiasa kesi ya Darline Graham si suala la sheria pekee, ni suala la maadili ya uongozi. Ingawa ni kweli kwamba, gavana aliyefanya uteuzi amefuata Katiba na hakuvunja sheria yoyote., bado kuna haja ya kujiuliza kama kila kilicho halali kisheria ni sahihi kisiasa na kimaadili?


Kwa Afrika, jibu linaonekana wazi, demokrasia haiwezi kuruhusu kivuli cha urithi wa kifamilia kuingia katika uongozi wa umma vinginevyo siasa itageuka kuwa mali ya wachache, badala ya sauti ya wengi.


Uwe na Amani.

 
 
 

Comments


bottom of page