TISS Isifanye Kosa Lililofanywa na CIA
- Rev. Godwin Chilewa
- 2 days ago
- 6 min read

Katika ulimwengu wa intelijensia, makosa makubwa hayaanzi na kutopatikana kwa taarifa bali kwa namna taarifa hizo zinavyotafsiriwa. Hivyo miongoni mwa makosa hatari zaidi ya kiitelijensia ni kile kinachoitwa confirmation bias. Hili ni tatizo la kisaikolojia linaloweza kuyumbisha maamuzi ya kitaifa na hata kusababisha majanga ya kisiasa, umwagaji damu, na migogoro ya kidiplomasia.
Confirmation bias ni hali ambapo mchambuzi wa idara ya usalama au taasisi huchagua, kuamini, au kutoa uzito mkubwa kwa taarifa zinazothibitisha imani au msimamo uliopo tayari huku akipuuza au kudharau ushahidi unaopingana na mtazamo huo. Kwa lugha rahisi, ni “kuona unachotaka kuona, na kupuuza usichotaka kuona.” Katika idara za usalama, hili ni kosa hatari sana. Kwa sababu intelijensia bora si ile inayothibitisha matarajio ya viongozi, bali ile inayowaambia ukweli hata kama ukweli huo haupendezi.
Mfano maarufu zaidi wa confirmation bias ni ule wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kabla ya Vita vya Yom Kippur mwaka 1973. Katika kipindi hicho CIA ilikuwa na imani thabiti kwamba Misri haiwezi kuivamia Israel. Hoja yao ilikuwa kwamba Misri haina uwezo wa kijeshi wa kushinda vita dhidi ya Israel. Hivyo ingawa taarifa nyingi za kiintelijensia zilikuwepo zikionyesha maandalizi ya kijeshi ya Misri.
Lakini badala ya kuzichukua kwa uzito taarifa hizo zilipuuzwa au kutafsiriwa kwa namna ya kuendana na imani iliyokuwepo.
Mbaya zaidi ni kwamba Wachambuzi wa CIA waliona maandalizi ya kijeshi ya Misri kama “mazoezi ya kawaida ya kijeshi” badala ya maandalizi ya vita dhidi ya Israeli. Matokeo yake Misri ilianzisha mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya Israel na CIA ikashindwa kutabiri tukio hilo pamoja na kuwa na resources zote zilizohitajika kufanya hivyo.
Baada ya aibu hiyo, CIA ilifanya mageuzi muhimu, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mfumo wa Red Teaming ambapo timu maalum hupewa jukumu la kupitia taarifa zilizofanyiwa uchambuzi wa kiitelijensia kwa lengo la kupinga na kuhoji tathmini rasmi, yaani kuangalia kwa jicho tofauti na wachambuzi wa awali na kutafuta ushahidi au vipengele muhimu vilivyosahauliwa au kupuuzwa.
Tatizo la confirmation bias hazikuikumba CIA mwaka 1973 pekee. Mwaka 2003 wakati wa vita kati ya Marekani na Iraq kulikuwa na mgogoro mkubwa kuhusu taarifa za silaha za maangamizi (WMDs). Upo ushahidi kwamba taarifa zilichujwa kwa mtazamo uliolenga kuthibitisha kwamba Iraq ilikuwa na silaha hizo na kila ushahidi uliopingana na imani hiyo ulipuuzwa.
Mwaka 2023 kabla ya shambulio la Hamas MOSSAD iliangukia katika mtego huohuo. Ripoti kadhaa zilionyesha dalili za maandalizi ya mashambulizi, lakini zilipuuzwa kwa sababu ya imani kwamba Hamas haikuwa tayari kwa vita kubwa. Matokeo yake Israel ilishambuliwa kwa namna isiyotarajia hata kidogo.
Urusi nayo ilipata hasara kubwa kwa sababu ya kosa hilohilo. Mwaka 2022 kabla ya vita vya Ukraine, KGB ilikuwa na taarifa nyingi kuhusu nchi iliyopanga kuivamia. Hata hivyo baadhi ya wachambuzi waliathiriwa na dhana kwamba Ukraine ingeanguka haraka, wakapuuza ushahidi wa wazi uliokuwepo kuhusu uwezo wa upinzani wa Ukraine. Matokeo yake Urusi ikajikuta kwenye vita ya hasara na isiyokwisha.
Mifano hii inaonyesha jambo mojja muhimu. Kwamba hata idara na taasisi zenye nguvu na uzoefu mkubwa zinaweza kuanguka kwenye mtego wa confirmation bias.
Katika muktadha wa Tanzania, inaonekana mwaka 2025 Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) nayo ilikumbwa na janga hilohilo la confirmation bias. Kabla ya uchaguzi mkuu zilikuwepo taarifa nyingi zilizoonesha upinzani mkubwa uliokuwa ukimkabili Rais Samia Suluhu Hassan ndani na nje ya chama chake.
Ndani ya CCM baadhi ya wajumbe walikuwa wakitaka kiongozi huyo asipewe nafasi ya kugombea na badala yake kifanyike kile kilichokuja kufahamika baadae kama “kumwaga oil” yaani kubadili timu nzima ya serikali kali kwa kuweka wagombea wapya. Ingawa taarifa zilionesha waziwazi uzito wa suala hilo, idara iliishauri CCM kuendelea na mgombea huyo jambo lililofanya apitishwe kwa “Azimio” badala ya utaratibu wa kawaida.
Si hivyo tu, lakini pia TISS ilikuwa na taarifa za uhakika kuhusu nguvu ya upinzani, na jinsi ambavyo CHADEMA ingeweza kushinda uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge wa mwaka 2025. Hii ilitokana na ukweli kwamba wananchi walikuwa wamekichoka Chama Cha Mapinduzi kutokana na hali ngumu ya maisha, tuhuma za ufisadi na kukosa uwajibikaji.
TISS haikupuuzia taarifa hii. Iliichukulia kwa uzito mkubwa, na kuitaarifu serikali pamoja na chama tawala juu ya hatari iliyokuwepo. Lakini badala ya viongozi wa chama hicho kutafakari kwa makini wapi walipopotoka, wao wakaja na wazo la kuua upinzani kwa kuwadhibiti wagombea wote walioonekana kuwa tishio. Mpango huu badala ya kukisaidia chama kupata ushindi ukachochea hasira ya wananchi na kuongeza nguvu ya upinzani.
TISS pia ilijikwaa kwenye suala la uchaguzi mkuu na maandamano ya Oktoba 29. Vuguvugu lililokuwepo kabla ya uchaguzi mkuu lilionesha wazi kwamba wananchi, na hasa wanachama wa vyama vya upinzani walikuwa hawana imani na tume ya uchaguzi na walikuwa wakijiandaa kuzuia kufanyika kwa uchaguzi na au kupinga matokeo ya uchaguzi kwa nguvu zote ikiwa pamoja na maandamano.
Pamoja na kuwa na taarifa za kina, TISS ikafanya kosa lilelile lililofanywa na CIA mwaka 1973. Ikapuuza ukweli huo kwa kuamini watanzania hawatathubutu kufanya hivyo, na wachache watakaojaribu watadhibitiwa. Hili lilikuwa kosa kubwa la kimkakati.
Katika hili zipo pia taarifa kwamba TISS ilikuwa na taarifa za hatari iliyokuwa ikija, na iliitahadharisha serikali mapema, na kutoa mapendekezo ya kuepusha balaa hilo. Hata hivyo uongozi wa juu ulikataa ushauri huo, na kutaka njia mbadala zitumike ikiwa pamoja na nguvu ya hali ya juu katika kuwadhibiti wale watakaojaribu kuandamana.
Taarifa zinadai kuwa hili ndilo lilofanya kuvujishwa kwa taarifa nyeti zilizomfanya askofu Josephat Gwajima kuieleza dunia kwamba Rais alikuwa hakubali ushauri wa wataalam wake na kwamba hiyo ndiyo sababu inayomfanya kuwabadilisha kila wakati. Tuhuma ambazo Rais alizijibu kwa namna yake.
Jambo la kutia shaka ni kwamba miezi tisa sasa baada ya matukio ya Oktoba 29, bado ipo hatari kubwa kwamba TISS inaweza kuendelea kukabiliwa na tatizo lilelile lililoifanya nchi ikaingia katika matatizo. Si kwasababu uongozi wa TISS umeshindwa kazi, bali kwa sababu nyinginezo. Kiuhalisia ni kwamba DGIS aliyepo sasa Bw. Sulemani Abubakar Mombo ni jasusi wa hali ya juu, mwenye weledi na sifa zote anazopaswa kuwanazo mkurugenzi wa idara.
Baadhi ya maafisa wa TISS wanadai kwamba ukiondoa mapungufu yake binafsi, kiutendaji Mombo anaweza kuwekwa kwenye nafasi moja na marehemu Emilio Mzena, na Colnel Apson Mwang’onda wakurugenzi wanaoheshimika katika idara. Hata hivyo heshima ya DGIS Mombo imewekwa kwenye mizani baada ya matukio ya Oktoba 29 kwani wengi wanaamini ndiye aliyemshauri Rais kutoa amri ya “shoot to kill” jambo ambalo halijathibitishwa.
Sababu ya kwanza inayoweza kufanya TISS irudie kosa la confirmation bias ni msukumo mkubwa wa kisiasa kutoka juu. Ni ukweli usiopingika kwamba Chama tawala na serikali yake imejaa viongozi wenye mtazamo fulani usiobadilika (mfano: maandamano ni tishio la usalama badala ya dalili ya changamoto za kijamii, Gen Z wanafadhiliwa na mabeberu, na kwamba nchi za Magharibi zinatuonea wivu).
Msukumo wa viongozi hawa unaweza kuifanya TISS kuanza kutafuta taarifa zinazothibitisha mtazamo huo na kupuuza taarifa sahihi zinazopinga mtazamo wa viongozi. Hii ni hatari kubwa na inaweza kusababisha janga la kitaifa au mgogoro mkubwa wa kidiplomasia.
Maafisa wa idara, hasa wachambuzi wanaposukumwa kuwaza tofauti na taaluma zao wanaweza kushawishika kuvujisha siri za serikali, kurubuniwa na vyombo vya ki jasusi vya nchi nyingine, na kupoteza weledi wao.
Mbaya zaidi ni pale mfumo unapoonekana kutowalinda wachambuzi kiasi cha kutishiwa kufukuzwa kazi, kushushwa cheo au kuhamishwa kwa sababu ya kutoa ushauri inaopingana na wanasiasa, au kiongozi wa nchi. Hii itafanya maafisa (wachambuzi) kuogopa kutoa tathmini inayopingana na matarajio ya viongozi. Badala yake, watatoa taarifa “salama” kisiasa lakini zisizo sahihi kiintelijensia.
Uwepo wa mawazo jumuishi (group think) pia ni sababu nyingine inayoweza kuleta balaa. Wachambuzi wanapokuwa na mtazamo mmoja bila changamoto hukosa mawazo mbadala, na au kupanga aiba ya taarifa anayopaswa kupewa kiongozi hata kama haina ukweli au haijitoshelezi. Hii hufanya makosa kujirudia bila kugundulika.
Kosa lingine kubwa ambalo idara imekuwa ikilifanya ni kuchanganya usalama na siasa. Taarifa za kiintelijensia zinapochanganywa na maslahi ya kisiasa uhalisia hupotoshwa na ushauri kwa viongozi unakuwa dhaifu. Hili pia husababishwa na baadhi ya viongozi wa kitaifa kujiteulia washauri (kwa kuangalia urafiki) na kupuuza wataalam wa fani husika.
Kwa hali ilivyo sasa, na kama tahadhari haitachukuliwa, TISS inaweza kurudia makosa yanayoonekana kama ya kawaida lakini yenye madhara makubwa mno. Makosa hayo ni pamoja na kudharau ukubwa wa malalamiko ya wananchi, kutoa tathmini zisizo sahihi kuhusu mwenendo wa maandamano na uhalisia wa muelekeo na nguvu ya vyama vya siasa. na kushauri hatua kali zisizoendana na hali halisi.
Kosa lingine kubwa ni kushindwa kuona hatari zinazokuja kwa sababu hazilingani na simulizi rasmi. Hili linaweza kusababisha migogoro ya kijamii kuongezeka, hasara ya kidiplomasia na kupoteza imani ya wananchi kwa taasisi za dola.
Ili kuepuka tatizo hili kubwa (confirmation bias) TISS inapaswa kuwa na timu huru yenye nguvu ya kuchambua na kupinga mapendekezo au ushauri wenye mwelekeo wa kisiasa badala ya kiitelijensia, kabla haujapelekwa kwa kiongozi mkuu, wizara au idara husika.
Timu hii inapaswa kuundwa na maafisa wenye uwezo wa hali yajuu katika uchambuzi, timu ipewe ridhaa na nguvu ya kutoa mawazo mbadala (kupinga) na ilindwe dhidi ya adhabu inayoweza kutolewa na viongozi wenye hasira, au wasioelewa uzito wa kazi ya TISS.
Idara pia inapaswa kudumisha utamaduni wa kusema ukweli (Speak truth to power) ili kujenga hesima yake na kuliponya taifa. Maafisa wa idara na hasa Wachambuzi wahimizwe kutoa ukweli bila kujali unampendeza nani, na kupimwa kwa ubora wa uchambuzi, si utii pekee.
Aidha ni muhimu sana Wachambuzi wote wafundishwe saikolojia ya uchambuzi ili waweze kutambua biases zao, na kutumia mbinu za structured analytic techniques.
Zaidi ya yote TISS itenganishe Intelijensia na Siasa. Taarifa zitolewe kwa misingi ya ushahidi na sio kwa matarajio ya kisiasa. Hii itasaidia kulinda uhuru wa Kitaaluma wa maafisa wa idara na hasa wachambuzi. Mfumo tasmi uwepo kulinda wachambuzi dhidi ya “kutumbuliwa”
Historia imeonyesha wazi: mataifa hayashindwi kwa sababu ya kukosa taarifa, bali kwa sababu ya kupotosha taarifa. Confirmation bias ni adui wa kimya ndani ya taasisi za usalama. Kwa ujumla janga hili ni hatari zaidi kuliko adui wa nje kwa sababu huvaa sura ya “uhakika”.
Kwa TISS, huu ni wakati wa kujifunza kutoka kwa makosa ya wengine hasa CIA mwaka 1973. Kinyume chake, historia inaweza kujirudia.
Na mara zote, gharama ya makosa ya intelijensia hulipwa na taifa zima.
Uwe na amani.






Comments