Dalili za Mpasuko wa Ndani CHADEMA: Agizo la Lissu Lafungua Nyufa za Kimfumo
Na Rev. Godwin Chilewa

Katika siasa za ushindani, migogoro mikubwa huanza kwa tafsiri tofauti za tukio moja. Hiki ndicho kinachoonekana ndani ya CHADEMA leo, kufuatia hatua ya Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, kuruhusu ujumbe wa pole kupelekwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Kilichoonekana kwa nje kama ishara ya utu wa kawaida, ndani na nje ya chama kimegeuka kuwa mjadala mzito wa kimkakati unaogusa msingi wa mapambano yenyewe.
Kwa mtazamo wa juu juu, huu ni mjadala wa kimaadili unaohoji kama kutoa pole kwa kiongozi anayetuhumiwa kuhusika na mauaji na ukandamizaji ni sahihi au la! Lakini kwa jicho la uchambuzi wa kiintelijensia, hili ni suala pana zaidi linaloashiria mgongano kati ya mikakati miwili ya kisiasa: mapambano ya haki (justice-driven resistance) dhidi ya ujenzi wa uhalali wa kisiasa (political legitimacy building).
Ni vigumu kuelewa uzito wa mjadala huu bila kurejea mazingira yaliyoutengeneza. Uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 uligeuka kuwa chanzo cha mgogoro mkubwa wa kitaifa. Maandamano ya kupinga uchaguzi yalijibiwa kwa nguvu kubwa za dola, hali iliyosababisha mamia kama si maelfu kupoteza maisha au kutoweka Tukio hilo limepasua taswira ya Tanzania kama nchi tulivu na kuibua kile kinachoelezwa kama “national catastrophe” inayohitaji suluhisho la juu kabisa la kisiasa .
Katika mazingira haya viongozi wa upinzani wamekamatwa au kufunguliwa kesi nzito. CHADEMA imebanwa kufanya shughuli zake za kisiasa kwa uhuru, na nchi ipo chini ya uangalizi wa kimataifa kuhusu haki za binadamu huku nchi kama Marekani zikitangaza kuangalia upya uhusiano wake na Tanzania. Kwa hiyo , kila hatua ya kisiasa, hata kama ni ndogo ina tafsiri pana ya ndani na nje ya nchi.
Mvutano ulioibuka hivi karibuni ndani ya CHADEMA, kufuatia hoja ya kutoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan si wa mtu dhidi ya mtu, bali ni wa maono dhidi ya maono. Kundi moja likiongozwa na makamu mwenyekiti John Heche, na wanaharakati Mange Kimambi, Maria Sarungi na wengineo linaona kutoa pole kwa Rais Samia ni kama ishara ya kulegea kwa msimamo, na kumpa uhalali wa kisiasa kiongozi anayehusishwa na vifo vya wananchi.
Kwamba kufanya hivyo ni kudhoofisha hoja ya kimataifa kwamba Tanzania ina tatizo la haki za binadamu na kutonesha vidonda (kusababisha maumivu ya kisaikolojia) kwa waathirika wa mauaji ya Oktoba 2029 na familia zao. Kwa lugha ya kiintelijensia, hii ni hofu ya kile kinachoitwa “legitimacy leakage” yaani, kumpa adui uhalali kupitia ishara ndogo zisizo na nia ya moja kwa moja ya kisiasa.
Lakini upande mwingine ndani ya chama baadhi ya watu akiwemo Godbless Lema wanatazama jambo hili kwa jicho tofauti kabisa. Kwao, kutoa pole si usaliti, bali ni mbinu ya kidiplomasia ya kudhihirisha maono ya chama. Wanahoji kwamba siasa za kisasa zinahitaji moral high ground kwa sababu ulimwengu wa kimataifa unaangalia si tu hoja, bali pia mwenendo wa viongozi. Chama kinachotaka kuongoza nchi lazima kionyeshe utu hata kwa wapinzani wake na kuepuka siasa za visasi. Hapa tunakutana na mkakati unaoitwa “strategic moderation”yaani kupunguza makali ya lugha bila kuacha lengo la msingi.
Hatari halisi: Mgawanyiko wa kimfumo
Kwa nje, mjadala huu unaweza kuonekana kama kawaida katika vyama vya siasa. Lakini kwa ndani, una dalili za hatari kubwa zaidi inayojulikana kitaalam kama narrative fragmentation. Hii hutokea pale ambapo:wanachama hawashiriki tafsiri moja ya mapambano, au uongozi unachukua hatua bila maelezo ya kina kwa msingi na sauti za nje (hasa mitandao na diaspora) zinachochea tafsiri kali zaidi.
Ikiwa hali hii itaachwa iendelee CHADEMA inaweza kujikuta na makundi mawili yasiyo rasmi, yenye maono na misimamo tofauti. Imani ya wanachama kwa uongozi inaweza kuyumba na mwelekeo wa pamoja wa kisiasa unaweza kupotea. Historia ya vyama vingi barani Afrika inaonyesha kuwa migawanyiko mingi huanza kwa tofauti ya tafsiri, siyo tofauti ya ajenda.
Kwa ujumla CHADEMA kwa sasa inakabiliwa na mtihani mgumu kuliko yote ambao utaonesha uimara wa chama. Mtihani huo unahusisha kusimamia kwa wakati mmoja vitu viwili vinavyoonekana kupingana lakini vyote ni muhimu: Kwanza, kusimamia mapambano ya haki. Kueleza kwa msisitizo ukweli wa yaliyotokea, kudai uwajibikaji wa wahusika na kulinda heshima ya waliopoteza maisha
Pili, ni kujenga uhalali wa kisiasa wa muda mrefu. Kujionyesha kama chama kinachoweza kuongoza taifa, kujenga uhusiano wa kimataifa, na kuepuka taswira ya siasa za chuki au visasi. Kushindwa kusawazisha haya mawili kuna madhara makubwa kwani ukali ukizidi unaweza kuashiria udikteta na hivyo kuweza kusababisha hofu na kutokubalika kimataifa. Lakini pia upole ukizidi unapoteza uungwaji mkono wa msingi ukizingatia kuwa wananchi wengi wana maumivu, hasira kutokana na kumbukumbu za matukio ya Oktoba 2025 na wamechoka.
Njia ya kuokoa chama:
Ili kuzuia mgogoro huu usigeuke kuwa mpasuko, hatua za haraka na za kimkakati zinahitajika. Kwanza, uongozi wa CHADEMA unapaswa kutoa msimamo rasmi ulio wazi na usioacha tafsiri nyingi. Kwakuwa mwenyekiti ameonesha nia ya kutoa pole ni muhimu kueleza kuwa kutoa pole hakufuti madai ya haki wala hakubadilishi msimamo wa chama kuhusu matukio ya Oktoba 29. Bila kauli hii, simulizi itaendelea kuandikwa na mitandao, siyo na chama chenyewe.
Pili, uongozi unapaswa kuanzisha mawasiliano ya ndani yenye uwazi, ukieleza sababu za maamuzi makubwa ya kisiasa. Wanachama wanapokosa taarifa, hujaza pengo hilo kwa hisia, na hisia mara nyingi huleta mgawanyiko. Ni muhimunpia chama kutambua makundi ya nje lakini yenye ushawishi mkubwa hususan diaspora na kwenye mitandao ya kijamii.
Tatu, chama kinahitaji kuruhusu mjadala lakini kwa mipaka ya nidhamu ya kisiasa. Tofauti ya mawazo ni afya, lakini mashambulizi ya ndani ni sumu. Dalili zozote za kushambuliana au utengenezwaji wa makundi zidhibitiwe mapema kwa njia zinazoleta maelewano.
Nne, ni muhimu kuweka wazi mgawanyo kati ya diplomasia na mapambano ya haki ili wanachama waelewe kuwa hatua za kisiasa hazimaanishi kusahau misingi ya harakati. Uongozi wa juu, hususan Makamu Mwenyekiti, anapaswa kutoa mwelekeo unaounganisha pande zote, lugha inayokubali maumivu ya walioumia lakini pia inaelezea mkakati wa muda mrefu wa kisiasa.
Kwa mtazamo wa kiintelijensia, mgogoro huu siyo ishara ya udhaifu bali ni dalili kwamba CHADEMA iko kwenye hatua ya mpito: kutoka majeraha ya uchaguzi wa 2025 kwenda taasisi inayojipanga upya kushika dola. Lakini hatua hii ya mpito huwa hatari zaidi. Kama itaachwa bila usimamizi inaweza kuzaa mgawanyiko, kupunguza nguvu ya chama na kupoteza mwelekeo wa mapambano. Lakini kama ikiendeshwa kwa busara unaweza kuimarisha chama, kuongeza ubora wa mikakati na kujenga upinzani wenye sura ya kitaifa na kimataifa.
Uwe na amani
Rev. Godwin Chilewa






Comments