Deogratius Ndejembi vs Emmanuel Nchimbi: Uchambuzi wa Kiintelijensia Kuhusu Mabadiliko ya Uongozi wa Juu
Updated: Aug 28
Na Rev. Godwin Chilewa

Mabadiliko ya ghafla katika nafasi ya Makamu wa Rais nchini Tanzania yamefungua ukurasa mpya wenye maswali mazito ya kisiasa, kiutawala na hata kimkakati. Kujiuzuru kwa Emmanuel Nchimbi ambaye amehudumu chini ya mwaka mmoja tangu aingie madarakani si tukio la kawaida katika mfumo wa siasa za Tanzana.
Ni katika mazingira hayo, uteuzi wa Deogratius Ndejembi, kiongozi kijana na mwenye elimu ya sheria na asili ya kiufundi zaidi kuliko diplomasia unaibua mjadala mkubwa: Wengi wanajiuliza kama Tanzania inaingia awamu ya “technocratic governance” au ni mkakati wa kudhibiti nguvu za kisiasa ndani ya dola?
Asili ya Mgogoro.
Ili kuelewa uzito wa uteuzi wa Ndejembi, ni muhimu kwanza kutazama mazingira yaliyosababisha kuondoka kwa mhe. Emmanuel Nchimbi. Ripoti mbalimbali na taarifa za vikao vya CCM zinaeleza kuwa kulikuwa na dalili za kutokubaliana kati yake na Mhe. Rais Samia Suluhu juu ya masuala ya utawala, hasa baada ya uchaguzi uliogubikwa na ukosoaji na vurugu zilizosababisha vifo vya mamia ya watu.
Pamoja na hilo, kauli za Nchimbi kuhusu haja ya kupambania katiba mpya zilionekana kugusa mizizi ya mamlaka ya kisiasa ndani ya chama tawala. Katika mifumo ya chama kimoja chenye nguvu kama CCM, kauli kama hizo ni ishara ya mgeuko wa kimkakati. Ingawa suala la katiba mpya limewekwa katika ilani ya CCM dalili zinaonesha bado chama hicho hakijawa tayari kuendelea na ajenda hiyo kwa sasa.
Kwa mtazamo wa kiintelijensia, hatua ya kujiuzuru kwa Nchimbi inaweza kutafsiriwa katika sura mbili. Kwanza kama kukua kwa mgogoro wa ndani ya uongozi wa juu, na pili kama mkakati maalum wa kuondolewa kwa nguvu ya kisiasa inayoweza kuleta changamoto kwa mamlaka ya Rais.
Tofauti ya Ndejembi na Nchimbi:
Wasifu wa Ndejembi unaonyesha tofauti kubwa na mtangulizi wake, Emmanuel Nchimbi. Ndejembi amezaliwa mwaka 1983 na amekulia ndani ya mfumo wa CCM hadi kufikia ngazi za juu za uamuzi. Ki taaluma ni mwanasheria mwenye shahada ya uzamili. Hata hivyo amejikita zaidi katika sekta za maendeleo kama nishati na ardhi, akihudumu kama waziri katika maeneo hayo.
Nchimbi yeye ana uzoefu zaidi kwani amepitia ngazi zote za chama, usalama wa taifa na diplomasia. Kielimu ana shahada ya Uzamili na amehudumu kwenye nafasi za juu zaidi katika chama kwanza akiwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, na baadae Katibu mkuu wa CCM. Hivyo ukiwalinganisha utaona kuwa Mhe. Ndejembi anaonekana zaidi kama mtaalamu wa sera na utekelezaji (Technocrat), msimamizi wa miradi ya maendeleo, na Kiongozi asiye na historia nzito ya makundi ya kisiasa.
Hii inaashiria mabadiliko ya wazi: kutoka kwa “power politics” kwenda “policy execution”. Kwa lugha ya kiintelijensia Mhe. Nchimbi alikuwa “node ya nguvu ndani ya mfumo”Alikuwa na sauti ya kuweza kutikisa chama, na uwezo wa kutoa maoni bila woga. Ndejembi yeye ni “instrument ya utekelezaji ndani ya mfumo.” Ana uzoefu mkubwa wa kusimamia miradi mikubwa na kufuatilia utekelezaji.
Mlinganisho wa Kiutendaji:
Katika utawala wa kisasa, Makamu wa Rais ni kiongozi wa pili katika safu ya uongozi, ni mrithi wa Rais na pia ni “shock absorber” wa migogoro ya kisiasa. Nchimbi akiwa na uzoefu wa wizara ya mambo ya ndani na diplomasia, alikuwa na uwezo wa kushughulikia migogoro ya ndani ya chama, shinikizo la kimataifa, mahusiano na vyama vingine vya siasa, na masuala ya usalama wa taifa. Ndejembi kwa upande wake ameonyesha nguvu katika kusimamia sekta za kiuchumi, kusukuma miradi ya maendeleo na utekelezaji wa sera za serikali. Hii inaacha swali la kimkakati kama katika kipindi hiki Tanzania inahitaji zaidi “manager” au “political stabilizer?
Mahusiano na Rais:
Kihistoria, mahusiano kati ya Rais na Makamu wake yamekuwa kipimo cha uthabiti wa dola. Katiba ya Tanzania inampa Makamu wa Rais nafasi ya pili kwa nguvu na mrithi wa moja kwa moja wa urais. Katika muktadha huu, uteuzi wa Ndejembi unaweza kutafsiriwa kwa njia mbili: Kwanza kama ushirikiano rahisi (Controlled Alignment)
Kwa kifupi Mhe. Ndejembi hana mtandao mkubwa wa kisiasa unaoweza kumpa nguvu ya kujitegemea Hii inamfanya kuwa rahisi kufanya kazi na Rais, kutii maagizo yake, na pia si tishio kwa mamlaka ya juu. Ikumbukwe kwamba Mhe. Nchimbi alikuwa na sifa pamoja na mtandao mkubwa uliomfanya kuwa tishio kwa mamlaka ya juu. Hii ilimfanya (Nchimbi) kutoa ahadi ya kutomfunika rais, jambo lililomwia ugumu kulitekeleza.
Udhaifu wa Kimuundo
Kwa upande mwingine kutokuwa na mtandao mkubwa na nguvu ya kidiplomasia inaweza kuwa udhaifu. Mhe. Ndejembi anaweza kushindwa kusimamia migogoro mikubwa ya kisiasa, anaweza kushindwa kumshauri Rais kwa uwazi na hivyo kutegemea maamuzi ya Rais kwa kiwango kikubwa. Kwa maneno mengine anaweza kuwa “loyal deputy” lakini si lazima awe “power center.” Hili ni jambo zuri kwa utii na usalama wa mamlaka, lakini ni hatari kwa mustakabali wa taifa
Athari za Kistratejia: Ndani na Nje ya Tanzania
Uteuzi huu una athari pana zaidi kuliko mtu mmoja: Ndani ya nchi utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza mvutano wa ndani ya CCM. Mhe. Ndejembi ni mtu anayekubalika. Lakini unaweza pia kuonyesha kuwa mfumo unapendelea utii kuliko mjadala, utekelezaji wa maagizo kuliko ushauri mgumu. Kimataifa Tanzania inaweza kuonekana kama inaimarishs udhibiti wa kisiasa, au inajaribu kurejesha taswira ya utulivu baada ya migogoro.
Tanzania Inaelekea Wapi?
Kwa mtazamo wa kiintelijensia, kujiuzuru kwa Emmanuel Nchimbi na kuteuliwa kwa Deogratius Ndejembi si tukio la kawaida bali ni ishara wazi ya mabadiliko ya kimkakati ndani ya dola ya Tanzania. Ni dalili ya kupungua nguvu za “political heavyweights” Kuimarisha viongozi wa utekelezaji na kuweka udhibiti mkali wa mamlaka ya juu. Hata hivyo, mafanikio ya mkakati huu yatategemea kama Tanzania iko katika awamu ya maendeleo ya kiuchumi au bado iko katika awamu ya usimamizi wa migogoro ya kisiasa.
Kama ikiwa awamu ya maendeleo ya kiuchumi, Ndejembi atafanikiwa kwa kiasi kikubwa. Lakini kama itakuwa awamu ya kushughulika na migogoro ya kisiasa na diplomasia, pengo la kisiasa linaweza kuonekana haraka. Kumbe jambo la muhimu ambalo watanzania wanapaswa kuangalia si suala la “mtu gani bora,” bali ni mfumo gani Tanzania imechagua kwa kipindi hiki cha historia yake ambapo migogoro ya kisiasa na kidiplomasia inakwenda sambamba na hali mbaya ya uchumi.
Uwe na amani.






Comments