HUKUMU YA MTU MMOJA AU TASWIRA YA MFUMO MZIMA?
Na Rev. Godwin Chilewa

Tundu Lissu amehukumiwa kifungo cha miaka minne kwa kosa la uchochezi. Mamilioni ya watanzania wanalia na kuomboleza huku wengine wakifanya sherehe za kujipongeza. Wako wanaosema mwanasiasa huyo ameonewa huku wengine wakipaza sauti kusema alistahili adhabu kubwa zaidi. Kwa miongo kadhaa ijayo hukumu hii itabaki kuwa kumbukumbu na simulizi ya kusisimua kama ile iliyotokea miaka 2000 iliyopita kule Yerusalemu.
Kimsingi hukumu ya Tundu Lissu inapaswa kuchunguzwa zaidi ya mipaka ya kesi ya mtu mmoja. Ni tukio lenye uzito wa kisiasa, kisheria na kijamii ambalo linazua maswali mapana kuhusu hali ya demokrasia nchini Tanzania, uhusiano kati ya dola na vyama vya upinzani, uhuru wa kujieleza na uwezo wa taasisi za nchi kusimamia tofauti za kisiasa kwa misingi ya sheria.
Labda nianze kwa kutahadharisha kwamba katika uchambuzi wa kiintelijensia, tukio kubwa halichunguzwi kwa kuangalia tukio lenyewe pekee bali pia mazingira yaliyolizalisha, wahusika wenye maslahi, mifumo inayoliendeleza, sababu za msingi na matokeo yanayoweza kujitokeza.
Kwa hiyo, hiyo pamoja na kuangalia kwa nini Tundu Lissu amehukumiwa, makala hii pia itachunguza kwa nini Tanzania imeendelea kukumbwa na migogoro ya kisiasa ambayo mara kwa mara huibua mvutano kati ya serikali, chama tawala, vyama vya upinzani na wananchi. Je, tatizo liko katika mwenendo wa serikali? Je, vyama vya upinzani vina udhaifu wa ndani? Je, wananchi wana uelewa wa kutosha kuhusu haki zao na namna serikali inavyopaswa kuwajibika? Au tatizo ni urithi wa mfumo wa kisiasa ambao, licha ya kuruhusu vyama vingi kikatiba na kisheria, bado unaweza kuendeleza baadhi ya fikra na mazoea ya utawala wa chama kimoja?
Maswali haya yanahitaji kujibiwa kwa uchunguzi wa kina kuhusu mfumo mzima wa uongozi na siasa za Tanzania, na kwamba mjadala kuhusu Lissu na CHADEMA unapaswa kuwa fursa ya kuchunguza mfumo mzima, badala ya kugeuka kuwa vita nyingine ya propaganda za kisiasa.
1. MAANA YA KESI YA TUNDU LISSU KISIASA NA KISHERIA
Tundulisu alishitakiwa kwa kosa la uhaini, kosa kubwa zaidi kwa mujibu wa sheria za Tanzania linalobeba hukumu ya kifo. Tarehe 6 Novemba 2026 Mahakama Kuu ilimuona Lissu hana hatia katika shtaka la uhaini, lakini ikamkuta na hatia ya kosa dogo la uchochezi na kumhukumu kifungo cha miaka minne. Mahakama iliweka bayana kwamba upande wa mashtaka haukuthibitisha nia ya mshitakiwa kuitisha serikali, jambo lililokuwa sehemu muhimu ya shtaka la uhaini. Hata hivyo, iliona kuwa kauli zake kuhusu kuzuia na kuvuruga uchaguzi wa mwaka 2025 zilikidhi masharti ya kosa la uchochezi.
Hapa ndipo watetezi na baadhi ya wachambuzi wa sheria wameibua maswali kuhusu namna mahakama ilivyotumia kifungu cha kosa dogo mbadala katika kutoa hukumu hiyo, wakati kosa la uchochezi halikuwemo kwenye hati ya mashitaka. Kituo cha Haki za Binadamu cha Chama cha Wanasheria wa Marekani (ABA) kimeeleza wasiwasi kwamba Lissu hakuwa amepewa taarifa ya kutosha kuhusu shtaka la uchochezi na hivyo hakuwa na nafasi halisi ya kujiandaa kulitetea. Zingatia kuwa haya ni maoni ya tathmini ya kisheria, ya American Bar Association na si hukumu ya mwisho kuhusu uhalali wa uamuzi wa mahakama.
Kwa mtazamo wa kiintelijensia, kuna masuala manne yanayopaswa kutenganishwa: Kwanza, wajibu wa kisheria wa mwanasiasa. Uhuru wa kujieleza hauondoi wajibu wa mwanasiasa kuzingatia sheria. Wito wa mageuzi, maandamano na kutokubaliana na serikali ni sehemu ya siasa za kidemokrasia. Lakini wito unaovuka mpaka na kuhamasisha vitendo vya vurugu unaweza kuibua wajibu wa kisheria.
Pili, wajibu wa serikali. Serikali ina wajibu wa kulinda usalama na utulivu wa nchi. Hata hivyo, jukumu hilo halipaswi kutumiwa kuondoa nafasi ya wananchi kukosoa sera, kupinga maamuzi, ukiukwaji wa haki za msingi au kudai mageuzi ya kisiasa.
Tatu, uhuru na uaminifu wa mahakama. Katika demokrasia, mahakama inapaswa kutoa haki bila kuathiriwa na shinikizo la uongozi wa juu au mamlaka ya uteuzi, msimamo wa chama tawala, na pia nafasi ya kisiasa ya mshtakiwa. Hata pale ambapo uamuzi wa mahakama hauwaridhishi viongozi wa nchi au baadhi ya wananchi wa kawaida. Aidha, hoja kuhusu haki ya kusikilizwa, shtaka lililofunguliwa, ushahidi na mwenendo wa shauri lazima zichunguzwe kwa uzito.
Nne, athari za kisiasa. Hukumu dhidi ya kiongozi mkuu wa upinzani inaweza kuwa na athari zaidi ya mhusika mwenyewe. Inaweza kuathiri ari ya wanachama, mikakati ya chama, imani ya wananchi katika taasisi na mtazamo wa jumuiya ya kimataifa kuhusu mazingira ya kisiasa nchini.
Kwa hiyo, kuachiwa huru kwa shtaka la uhaini hakumaanishi kuwa maswali yote kuhusu kesi yameondoka. Hoja ya ukandamizaji wa wapinzani bado inasimama.
Lakini pia, hukumu ya kosa la uchochezi haithibitishi kwamba mfumo mzima wa mahakama umefeli. Upo uwezekano kwamba mfumo wa mahakama unafanya kazi nzuri kwa nyakati na mazingira fulani, lakini unayumba katika mazingira au aina ya kesi fulani. Uthibitisho wa masuala haya unahitaji tathmini tofauti na ushahidi wake.
2. MABADILIKO YA MFUMO WA SIASA, TANZANIA ILIBADILI SHERIA PEKEE AU ILIBADILI UTAMADUNI WA KISIASA?
Hii ni mojawapo ya hoja muhimu zaidi katika kuelewa changamoto za demokrasia ya nchini. Tanzania ilitoka katika mfumo wa chama kimoja na kuingia katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Hata hivyo, kubadilisha mfumo wa kisheria hakumaanishi kwamba fikra, miundo, mahusiano na mazoea yote yaliyojengwa katika kipindi cha chama kimoja nayo yalibadilika mara moja.
Mfumo wa chama kimoja ulijenga utamaduni wa kisiasa ambao chama tawala na dola vilikuwa na uhusiano wa karibu sana katika uendeshaji wa shughuli za nchi. Kwa kipindi kirefu, chama kilikuwa kitovu cha uhamasishaji, utekelezaji wa sera na usimamizi wa maisha ya kisiasa. Baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, vyama vingine vilipata nafasi ya kisheria kushiriki katika siasa. Lakini taasisi zote, taratibu za kiutawala na utamaduni wa kisiasa havikujengwa upya ili kutoa ushindani ulio sawa.
Hapa ndipo tunapopaswa kutofautisha kati ya demokrasia ya kikatiba na demokrasia inayotekelezwa kwa vitendo.
Demokrasia ya kikatiba inatambua haki ya kuanzisha chama, kutoa maoni, kushiriki katika uchaguzi na kuwania uongozi. Demokrasia inayotekelezwa kwa vitendo inahitaji haki hizo ziweze kutumiwa bila vikwazo visivyo vya lazima, vitisho, upendeleo au matumizi yasiyo sawia ya mamlaka na nguvu ya dola.
CCM imeendelea kuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 60, huku vyama vya upinzani vikikabiliwa na vikwazo vya ushiriki wa kisiasa. Chama tawala kimekuwa kikiendesha propaganda zisizo sahihi ikiwa pamoja na kuwa Lebo viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani kama wasaliti, wapinga maendeleo, na watu wanaotumiwa na mabebelu.
Ingawa propaganda ni kitu cha kawaida na kinachokubalika kisiasa, matumizi mabaya au yaliyokithiri ya njia hii huweza kujenga uadui mkubwa kwa wananchi, kuligawanya taifa, na polepole kuliingiza katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Matatizo ya uchaguzi wa mwaka 2025 na mauaji yaliyoambatana na uchaguzi huo ni ushahidi tosha wa chuki iliyojengwa.
Zingatia kwamba chama tawala kilmeweka msingi usiotaka kutikiswa kwamba chenyewe ndicho kwa asili kina haki yakuongoza, na kwamba vyama vya upinzani ni wasaliti. Imani hii inaungwa mkono na majeshi ya ulinzi na usalama kwa sababu yana imani na chama hicho, na au yana taarifa hasi kuhusu viongozi na au utendaji wa vyama vya upinzani.
Vyama vya upinzani navyo vinajikuta vikitumia nguvu nyingi ya kupambana na chama tawala ili kudai haki, kujilinda na kutafuta nafasi ya kujipanua na kuingia ikulu. Katika kufanya hivi vinalazimika kujibu mapigo ya propaganda, kuwa Lebo viongozi na wanachama wa chama tawala, na kufanya siasa za chuki zinazofanana na chama tawala lakini bila kuungwa mkono au kusaidiwa na vyombo vya dola jambo linalowatia matatani. Hali hii ndiyo inayozua maswali kuhusu usawa wa ushindani hasa majeshi na vyombo vya dola vinaporuhusu chama tawala kuvunja sheria waziwazi huku vikidhibiti upinzani kwa makosa yaleyale.
Lipo pia tatizo la chama tawala kuwa na faida ya kimfumo. Kwa kawaida chama kinachokaa madarakani kwa muda mrefu kama ilivyo CCM kinaweza kujenga mtandao mpana wa kisiasa, kiutawala na kijamii. Kinaweza kuwa na rasilimali, uzoefu, miundombinu na ushawishi ambao chama kipya hakiwezi kuupata kwa urahisi. katika hali ya kawaida hilo si kosa la kisheria. Chama kinachopata uungwaji mkono wa wananchi kina haki ya kuendelea kushinda uchaguzi. Tatizo ni pale faida ya kuwa madarakani inapochanganywa na matumizi ya taasisi za umma kwa namna inayodhoofisha ushindani wa vyama vingine.
Kwa mfano hivi sasa mikutano ya chama tawala inakuwa na nafasi pana zaidi kuliko ya upinzani. Vyombo vya dola vinachukuliwa kuwa sehemu ya kulinda maslahi ya chama fulani badala ya kulinda sheria na wananchi wote. Taasisi zinazosimamia uchaguzi hazionekani kuwa huru vya kutosha badala yake zinamilikiwa na chama tawala. Wanaharakati na wakosoaji wa serikali wanakabiliwa na vikwazo visivyo sawia. Na rasilimali za umma zinachanganywa na shughuli za kisiasa za chama. Haya ni maeneo yanayohitaji tathmini zaidi, si tuhuma zinazopaswa kuchukuliwa kuwa zimethibitishwa
Kwa ujumla uchambuzi wa kiintelijensia unaonesha kuwa urithi wa chama kimoja unaweza kuendelea kuwepo hata baada ya sheria kuruhusu vyama vingi. Unaweza kuishi katika namna viongozi wanavyofikiri kuhusu upinzani, namna taasisi zinavyotekeleza majukumu yao na namna wananchi wanavyotafsiri mamlaka ya kisiasa.
Hivyo, tatizo si historia ya CCM pekee. Ni suala la kujenga taasisi zinazoweza kufanya kazi kwa usawa hata pale chama kingine kinaposhika dola.
3. JE, CHADEMA INA MATATIZO?
Kuna dhana inayosikika katika mijadala ya kisiasa kwamba CHADEMA ni chama dhaifu kwa sababu kina wasaliti wengi, migogoro ya viongozi na watu wanaotuhumiwa kufanya kazi kwa maslahi ya chama tawala. Dhana hii inahitaji kuchunguzwa kwa kina. Kwanza, ni muhimu kuelewa kwamba chama cha siasa si taasisi inayoundwa na watu wenye maslahi yanayofanana kwa kila jambo. Ni muungano wa watu wenye mitazamo, matarajio, tamaa, mikakati na maslahi mbalimbali.
Kwa hiyo, migogoro ndani ya chama si jambo la kipekee kwa CHADEMA. Inapatikana katika vyama vingi duniani, ikiwemo vyama vilivyokaa madarakani kwa muda mrefu. Hata hivyo, si sahihi kutumia ukweli huo kufunika matatizo halisi yanayoweza kuathiri uwezo wa chama kutekeleza majukumu yake.
A. Changamoto ya utegemezi wa viongozi binafsi
Chama kinapokuwa kinategemea sana ushawishi, umaarufu na uwezo wa mtu mmoja au watu wachache, kinaweza kukumbwa na tatizo la urithi wa uongozi. Kiongozi anapokosekana kwa sababu yoyote ile, chama kinaweza kupoteza mwelekeo ikiwa hakijajenga mifumo imara ya uongozi na maamuzi. Kwa mtazamo wa kiintelijensia, hiki ni kitu kinachoweza kuitwa leadership dependency risk yaani hatari ya taasisi kutegemea mno watu binafsi. Chama imara kinapaswa kuwa na uwezo wa kuendelea kufanya kazi hata mwenyekiti wake anapokuwa mahabusu, anapokuwa nje ya nchi, anapostaafu au anaposhindwa kutekeleza majukumu yake. CHADEMA kimeweza kufanya hivyo.
B. Tatizo la kutokubaliana kuhusu mkakati
Katika vyama vya upinzani, mara nyingi kunakuwa na mitazamo tofauti kuhusu namna ya kuikabili serikali. Baadhi ya viongozi wanaweza kuamini katika mazungumzo na ushirikiano. Wengine wanaweza kusisitiza maandamano, shinikizo la kisiasa na kutokubali kushiriki katika mfumo ambao wanaamini hauna haki. Tofauti hizo si usaliti moja kwa moja.
Tatizo linatokea pale chama kinaposhindwa kuwa na utaratibu wa kujadili tofauti hizo, kufanya maamuzi na kuyasimamia kwa nidhamu ya pamoja. Matokeo yake ni migawanyiko, tuhuma, makundi ya ndani na kupungua kwa imani ya wanachama.
C. Propaganda ya usaliti na lebo za kisiasa
Neno msaliti ni silaha yenye nguvu sana katika siasa. Mwanachama anayekosoa uongozi anaweza kuitwa msaliti. Kiongozi anayependekeza mazungumzo anaweza kuitwa pandikizi. Anayesisitiza msimamo mkali anaweza kuitwa mchochezi au mtu asiye na busara. Lebo hizi zinapotumiwa bila ushahidi zinaweza kuua mjadala wa ndani na kuifanya taasisi ishindwe kujirekebisha. Kwa upande mwingine, haiwezekani kupuuza uwezekano wa watu kutumia nafasi za uongozi kwa manufaa binafsi au kushirikiana na wapinzani wa chama kwa maslahi yao. Lakini madai ya aina hiyo yanahitaji ushahidi, si hisia wala umaarufu wa mtuhumiwa.
D. Tatizo la kujenga chama badala ya kujenga taasisi
Vyama vinapokuwa na viongozi wanaotanguliza mamlaka yao kuliko mifumo ya chama, huanza kudhoofika. Demokrasia ya ndani inahitaji uchaguzi wa viongozi ulio wazi na unaokubalika. Uwazi wa mapato na matumizi ya chama. Uwajibikaji wa viongozi kwa wanachama. Utaratibu wa kutatua migogoro. Nafasi ya vijana na wanawake kushiriki katika maamuzi. Mafunzo ya sera, uongozi na utawala kwa viongozi.
Kwa hiyo, CHADEMA ina haki ya kukosoa mazingira ya kisiasa na kudai usawa wa ushindani. Lakini pia ina wajibu wa kujichunguza na kuimarisha taasisi yake.
Hoja ya msingi hapa ni kuwa upinzani hauwezi kuwa imara kwa kutegemea makosa ya serikali pekee. Lazima ujenge uwezo wa ndani, uaminifu, sera, nidhamu na mifumo ya uwajibikaji. Lakini, hata kama CHADEMA ina udhaifu wowote hauwezi kutumika kama sababu ya kuhalalisha vikwazo visivyo halali dhidi yake au dhidi ya wananchi wanaounga mkono chama hicho.
4. PROPAGANDA, LEBO NA VITA YA KISAIKOLOJIA KATI YA VYAMA
Moja ya matatizo makubwa yanayodhoofisha demokrasia ya Tanzania ni matumizi ya propaganda kama mbinu ya kushinda ushindani wa kisiasa. Katika siasa, propaganda si lazima iwe taarifa ya uongo. Inaweza kuwa taarifa ya kweli iliyochaguliwa, kupangwa na kuwasilishwa kwa namna inayolenga kuunda mtazamo fulani kwa wananchi.Tatizo hujitokeza pale ukweli unapopotoshwa, taarifa zinapofichwa au wananchi wanapopewa lebo badala ya hoja.
Kwa mfano, katika mazingira ya kisiasa tuliyo nayo sasa tunaweza kukutana na lebo kama msaliti, pandikizi la chama tawala, mchochezi, mpinzani wa maendeleo, mtu anayepinga serikali kwa kila jambo, adui wa taifa, au mtu anayehujumu amani. Lebo hizi zinapotumiwa bila ushahidi zinaweza kuathiri namna wananchi wanavyowatazama viongozi na taasisi.
Vita ya kutengeneza taswira
Kila chama kinaweza kujaribu kujenga taswira nzuri kuhusu viongozi wake na taswira mbaya kuhusu wapinzani wake. Chama tawala kinaweza kutumia mafanikio ya serikali kujenga hoja kwamba upinzani hauna mchango katika maendeleo. Upinzani nao unaweza kuonyesha kila changamoto ya serikali kama ushahidi kwamba mfumo mzima umeshindwa. Katika mazingira hayo, ukweli unaweza kupotea katikati ya ushindani wa kutengeneza muonekano.
Hapa kuna aina tatu za propaganda zinazopaswa kuangaliwa kwa makini. Kwanza ni Propaganda ya uhalalishaji ambapo kila upande hutengeneza hoja za kuhalalisha matendo yake hata pale yanapokuwa na mapungufu. Pili ni propaganda ya kumdhalilisha mpinzani: Badala ya kujibu hoja za mpinzani, nguvu kubwa hutumika kushambulia tabia, historia, familia au uaminifu wake. Tatu ni propaganda ya hofu ambapo wananchi huambiwa kwamba bila chama fulani nchi itavurugika, uchumi utaporomoka au amani itapotea. Kwa upande mwingine, wananchi wanaweza kuambiwa kwamba serikali ikibaki madarakani hakuna haki wala uhuru utakaopatikana. Hizi ni mbinu zinazoweza kutumiwa na wahusika mbalimbali katika mazingila tofauti.
Matokeo ya vita hii ni wananchi kuanza kujitambulisha kwa misingi ya vyama badala ya misingi ya utaifa. Mtu anaweza kuunga mkono ukiukwaji wa haki kwa sababu mtuhumiwa anatoka chama asichokipenda. Vilevile, anaweza kupinga hata jambo zuri kwa sababu limependekezwa na chama anachokipinga.
Huu ni mtego wa kisaikolojia unaojulikana kama partisan bias yaani upendeleo wa kisiasa unaomfanya mtu kutafsiri taarifa kwa kuzingatia uaminifu wake kwa chama, badala ya kupima ushahidi uliopo.
Katika mfumo au utaratibu huu demokrasia haiwezi kustawi ikiwa wananchi wanaanza kuamini kwamba haki ni haki pale tu inapowasaidia watu wa upande wao. Taifa linapaswa kuwa kubwa kuliko chama. Haki inapaswa kuwa kubwa kuliko uaminifu wa kisiasa.
5. UBINAFSI, TAMAA YA MADARAKA NA KUKOSEKANA KWA UZALENDO
Tatizo jingine linalopaswa kuangaliwa kwa makini ni namna maslahi binafsi yanavyoathiri maamuzi ya kisiasa. Si kila mtu anayeingia katika siasa anaingia kwa lengo la kutumikia wananchi. Wapo wanaoingia kwa sababu ya kutafuta mamlaka, heshima, utajiri, fursa za kiuchumi au ushawishi. Hali hii inaweza kuathiri chama tawala na vyama vya upinzani.
Katika chama tawala, tamaa ya madaraka inaweza kusababisha watu kutumia nafasi zao kulinda vyeo, mitandao ya kiuchumi na manufaa yanayotokana na kuwa karibu na mamlaka.
Katika upinzani, tamaa hiyo hiyo inaweza kujitokeza katika mapambano ya kugombea nafasi za uongozi, kudhibiti rasilimali za chama, kutafuta umaarufu au kuhamia upande mwingine kwa matarajio ya kupata manufaa binafsi. Kwa hiyo, siasa inaweza kugeuka kutoka katika mfumo wa kutafuta suluhisho la matatizo ya wananchi na kuwa mfumo wa kugombea fursa.
Demokrasia inapokuwa na taasisi dhaifu za uwajibikaji, kuna hatari ya viongozi kuona madaraka kama njia ya kujitajirisha. Hili linahusiana na dhana ya rent-seeking au kutumia nafasi, mamlaka au ushawishi wa kisiasa kupata manufaa ya kiuchumi ambayo hayatokani na ushindani wa haki au uzalishaji wenye tija.
Madhara makubwa ya utaratibu huu ni pamoja na rasilimali za umma kutumika kwa maslahi ya watu wachache. Uwekezaji katika huduma za jamii unaweza kudhoofika. Uteuzi wa viongozi wa nafasi nyeti unaweza kuathiriwa na ukaribu badala ya uwezo. Rushwa inaweza kugeuka kuwa sehemu ya mtandao wa kulindana jambo linaloweza kuwasukuma wananchi kupoteza imani katika taasisi za serikali. Mbaya zaidi ni kwamba tatizo hili halina mipaka ya chama. Linahitaji mifumo ya uwazi, ukaguzi huru, sheria zinazotekelezwa kwa usawa na ulinzi wa watu wanaofichua vitendo vya rushwa.
Kukosekana kwa uzalendo wa kitaasisi
Uzalendo si kupiga kelele za kuipenda Tanzania, kuvaa nguo, tai au skafu zenye bendera ya taifa. Uzalendo ni kukubali kwamba maslahi ya taifa yanaweza kulazimu mtu kupoteza nafasi, umaarufu au manufaa binafsi. Kiongozi mwenye uzalendo anatambua kwamba serikali ni ya wananchi wote, hata wale wasio wa chama chake au ambao hawakumpigia kura. Mwanasiasa mwenye uzalendo anatambua kwamba kushindwa kwake katika uchaguzi si kushindwa kwa taifa. Na mwananchi mwenye uzalendo anatambua kwamba kukosoa serikali si lazima kumaanishe kuichukia nchi.
Hapa ndipo tunapopaswa kutenganisha dhana mbili: kuipenda serikali iliyopo na kuipenda nchi. Hizi si dhana zinazofanana. Unaweza kuipenda Tanzania na ukapinga sera za serikali. Unaweza kuikosoa CHADEMA na wakati huohuo ukatetea haki yake ya kisiasa. Unaweza kuunga mkono CCM katika uchaguzi lakini ukapinga matumizi mabaya ya mamlaka na mwanachama wake. Huo ndiyo msingi wa uzalendo unaojenga taifa.
6. ELIMU YA URAIA NA UFAHAMU MDOGO WA WANANCHI KUHUSU SERIKALI
Demokrasia ya vyama vingi inahitaji uwepo wa vyama na wananchi wanaoelewa mamlaka yao, haki zao na wajibu wa taasisi mbalimbali. Changamoto kubwa katika jamii nyingi ni kwamba wananchi wanaweza kujua majina ya viongozi, lakini wasielewe vizuri mipaka ya mamlaka yao.
Kwa mfano, mwananchi wa kawaida anaweza kuwa mpiga kura mzuri. Lakini je, anaelewa tofauti kati ya serikali, chama tawala, Bunge, mahakama na mamlaka za serikali za mitaa?
Je, anajua ni nani anayepaswa kuwajibika kuhusu huduma za afya, elimu, barabara, usalama na matumizi ya fedha za umma?
Je, anaelewa kwamba mbunge si mtumishi wa chama pekee, bali ni mwakilishi wa wananchi?
Je, anaelewa tofauti kati ya kupinga serikali, kuvunja sheria na kutekeleza haki ya kikatiba ya kukosoa mamlaka?
Kutokuwepo kwa uelewa wa kutosha katika maeneo haya kunaweza kufanya wananchi wawe rahisi kushawishiwa na propaganda.
Mwananchi asiyefahamu mamlaka yake anaweza kudhibitiwa kwa taarifa
Mwananchi anapokosa elimu ya uraia, anaweza kuamini kwamba kila kitu kinachofanywa na serikali ni sahihi kwa sababu tu serikali ina mamlaka. Vilevile, anaweza kuamini kila anachosema mwanasiasa wa upinzani kwa sababu tu anapinga serikali. Haya ni mazingira yanayodhoofisha uwezo wa wananchi kufanya maamuzi huru.
Elimu ya uraia inapaswa kuwafundisha wananchi Katiba na haki za msingi, mipaka ya mamlaka ya viongozi, mfumo wa kutunga sheria, majukumu ya Bunge na mahakama, wajibu wa serikali za mitaa, Namna ya kufuatilia matumizi ya fedha za umma, tofauti kati ya taarifa, maoni, propaganda na ushahidi, namna ya kudai haki bila kutumia vurugu. Lengo hapa si kuzalisha wananchi wanaopinga serikali bali kuzalisha wananchi wanaoweza kuhoji, kuchambua na kuisimamia serikali yoyote itakayokuwa madarakani.
7. VITA KATI YA CHAMA TAWALA NA UPINZANI: NANI ANAPOTEZA?
Katika mfumo wa kidemokrasia, chama tawala na upinzani vinapaswa kuwa na ushindani wa kisera, hoja na uwezo wa kuongoza. Lakini Tanzania imekuwa ikikumbwa na mazingira ambayo ushindani wa kisiasa unaweza kugeuka kuwa mapambano ya kutafuta ushindi wa upande mmoja kwa gharama ya mwingine.
Chama tawala kinaona upinzani wenye nguvu kama tishio kwa utulivu na mwendelezo wa utawala wake. Upinzani nao unaona kila hatua ya serikali kama jaribio la kuudhoofisha au kuufuta. Matokeo yake ni kuingia katika mzunguko wa kutoaminiana.
Kwa mfano hivi sasa Chama tawala kinaogopa kupoteza mamlaka huku upinzani nao unakabiliwa na vikwazo na mazingira ya kutokuaminiana. Kila upinzani unapoongeza shinikizo na uhamasishaji, serikali nayo inaongeza hatua za kiusalama na udhibiti. Hii inasababisha Kutoaminiana kuzidi na wananchi kupoteza imani ya taasisi sa erikali. Hii ni political security dilemma ambapo hatua ambazo upande mmoja unaziona kama kujilinda zinaweza kutafsiriwa na upande mwingine kama tishio, na hivyo kuzalisha mwitikio unaoongeza mvutano.
Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba wajibu wa kila upande ni sawa katika kila tukio. Serikali ina mamlaka na wajibu wa ziada kwa sababu inamiliki vyombo vya dola na ina wajibu wa kikatiba wa kulinda haki za wananchi ambao kimsingi ndio wanaobeba gharama. Mvutano wa kisiasa unapozalisha machafuko kama yale ya Oktoba 29, 2026 biashara zinaweza kufungwa, uwekezaji unaweza kusita, huduma za kijamii kuathirika na familia kupoteza wapendwa wao.
8. NGUVU YA WANAHARAKATI NA UMUHIMU WA MAPAMBANO DHIDI YA SERIKALI
Katika demokrasia, wanaharakati wana nafasi muhimu ya kusimamia uwajibikaji wa mamlaka.
Kwa mtazamo wa makala hii mwanaharakati ni watu au makundi yanayotumia mbinu mbalimbali za kijamii, kisheria, kitaaluma na kisiasa kutetea haki, kupinga ukosefu wa haki na kushinikiza mabadiliko. Hawa wanaweza kuwa wanasheria, waandishi wa habari, wanazuoni, mashirika ya kiraia, wanaharakati wa haki za binadamu, vijana, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida.
Ni muhimu kuelewa kwamba uanaharakati si lazima uwe sehemu ya chama cha siasa. Mwanaharakati anaweza kuwa mwanachama wa CCM, CHADEMA, ACT-Wazalendo au asiwe mwanachama wa chama chochote. Aidha si kila mtu anayeongea, kutoa hoja au kutukana mtandaoni ni mwanaharakati. Hili ni jambo la kuzingatia kwa sababu hivi sasa hata watu wanaojulikana kuwa wagonjwa wa akili, wanapoongea maneno ya kupinga au kuunga mkono upande fulani hupewa Lebo ya uanaharakati. Jambo ambalo si sahihi.
Kwa nini wanaharakati ni muhimu?
Wanaharakati ni muhimu kwa sababu wanasaidia kuweka mamlaka chini ya uangalizi.
Serikali inapokuwa na mamlaka makubwa bila uangalizi wa kutosha, kuna hatari ya matumizi mabaya ya madaraka. Wanaharakati wanaweza kufichua matatizo, kuhoji maamuzi na kudai uwajibikaji hata pale ambapo viongozi wa vyama vya siasa wanaogopa au kushindwa kufanya hivyo kwa sababu mbalimbali.
Pili, wanaharakati wanatoa sauti kwa watu wasio na uwezo wa kujitetea. Kila mahali kuna wananchi ambao hawawezi kufikia mahakama, vyombo vya habari au viongozi wenye mamlaka. Mashirika ya kiraia na wanaharakati wanaweza kusaidia kuwasilisha matatizo yao katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa.
Tatu, wanaharakati wana nguvu ya kuchochea mageuzi ya kisheria na kitaasisi. Mabadiliko mengi katika jamii huanza kwa watu wanaohoji hali iliyopo. Haki za wafanyakazi, usawa wa kijinsia, uwajibikaji wa serikali na uhuru wa habari ni maeneo ambayo yamefaidika na juhudi za utetezi wa kijamii.
Nne, wanaharakati wanawezakuzuia ukimya wa kijamii. Katika jamii ambayo watu wanaogopa kuzungumza kuhusu matatizo yao inaweza kuonekana kuwa na utulivu, lakini ndani yake kukawa na malalamiko makubwa yasiyopata nafasi ya kushughulikiwa.
Je, kupambana na serikali ni kosa?
Hapa kuna umuhimu wa kutofautisha mambo mawili. Kuna kupambana na serikali kwa maana ya kisiasa na kiraia kwa kukosoa sera, kufanya maandamano ya amani, kuandika, kufungua kesi, kuandaa mijadala na kudai mabadiliko.
Na kuna vitendo vya kutumia vurugu, vitisho, uharibifu wa mali au kushambulia watu.
Jambo la kwanza ni sehemu muhimu ya demokrasia na uwajibikaji wa mamlaka. Jambo la pili linaweza kuleta wajibu wa kisheria. Kwahiyo serikali haipaswi kuchukulia kila ukosoaji kama tishio la usalama wa taifa au uchochezi. Vilevile, wanaharakati hawapaswi kutumia jina la haki za binadamu kuhalalisha vitendo vya vurugu.
Serikali inayokubali kukosolewa ina nafasi kubwa zaidi ya kujenga uaminifu kuliko serikali inayotaka kusifiwa pekee. Kwa upande mwingine, uanaharakati unaopima mafanikio yake kwa ukubwa wa hasira au idadi ya watu wanaokabiliana na vyombo vya dola unaweza kupoteza lengo lake la msingi ambalo ni kuboresha mfumo wa haki, si kuunda vurugu nyingine.
9. TANZANIA INAHITAJI MAGEUZI YA MFUMO, SI MABADILIKO YA VIONGOZI PEKEE
Kama kweli tunataka kutatua changamoto za demokrasia ya Tanzania basi tunapaswa kutafakari upya mifumo yetu.. Kwa kifupi hatuwezi kutegemea kubadilisha viongozi huku tukiacha mifumo ileile inayozalisha migogoro halafu tukadhani tutakuwa na amani. Tunahitaji mageuzi ya kitaasisi, kisheria, kisiasa na kijamii.
A. Katiba mpya yenye misingi imara ya uwajibikaji
Tanzania inahitaji mchakato jumuishi wa kupata katiba inayoweka wazi mipaka ya mamlaka ya serikali, haki za wananchi na uhuru wa taasisi.
Mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa ni pamoja na uhuru na uwajibikaji wa mihimili ya dola. Uundwaji wa Tume huru ya uchaguzi yenye mfumo wa uteuzi unaoaminika, ulinzi wa haki za vyama vya siasa, uhuru wa kujieleza, kukusanyika na kuandamana kwa amani, uundwaji wa mifumo ya kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka nabuwajibikaji wa viongozi wa kisiasa na watumishi wa umma. Katiba haipaswi kuwa chombo cha kulinda maslahi ya chama kilicho madarakani. Inapaswa kuwa mkataba wa wananchi wote.
B. Kujenga taasisi huru zisizoegemea chama
Taasisi za umma zinapaswa kufanya kazi kwa misingi ya sheria, si kwa matarajio ya viongozi wa kisiasa. Hili linahusu Tume ya uchaguzi, Mahakama, Polisi, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka, na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Taasisi za kupambana na rushwa na Vyombo vya habari vya umma. Uhuru wa taasisi haupaswi kuwa uhuru wa kutowajibika. Taasisi huru pia zinapaswa kuwa wazi, kupimwa kwa utendaji na kuwajibika kwa sheria.
C. Kufanya mageuzi ya sheria za uchaguzi na vyama vya siasa
Sheria zinapaswa kuweka mazingira yanayohakikisha vyama vyote vinapata nafasi ya kushiriki katika ushindani wa kisiasa.
Ni muhimu kupitia upya masharti ya usajili na uendeshaji wa vyama, usawa wa mikutano ya kisiasa, mifumo wa ruzuku kwa vyama, matumizi ya rasilimali za umma katika kampeni, utatuzi wa malalamiko ya uchaguzi, mamlaka ya wasimamizi wa uchaguzi na haki ya wagombea na vyama kukata rufaa. Lengo kuu hapa ni kuhakikisha wananchi wanaweza kuchagua viongozi bila vikwazo visivyo halali.
D. Kuanzisha mfumo wa kitaifa wa mazungumzo ya kisiasa
Tanzania inahitaji utamaduni wa viongozi kukutana na kutatua tofauti zao kabla hazijawa migogoro mikubwa. Mazungumzo hayo yanapaswa kuwa na ajenda, ratiba, wajumbe wanaoaminika na mfumo wa kufuatilia utekelezaji wa makubaliano. Mazungumzo haya hayapaswi kutumika kunyamazisha madai ya haki. Yanapaswa kujenga makubaliano ya kitaifa kuhusu misingi ya ushindani wa kisiasa.
F. Elimu ya uraia iwe ajenda ya kitaifa
Elimu ya uraia isiwe somo la wakati wa uchaguzi pekee bali shule zote, vyuo, vyombo vya habari na asasi za kiraia zinapaswa kusaidia wananchi kuelewa Katiba, haki zao, wajibu wa serikali na mifumo ya uwajibikaji. Wananchi wafundishwe pia kutambua habari za uongo, propaganda na upotoshaji wa kisiasa.
G. Kujenga mfumo wa uwajibikaji wa kiuchumi
Mojawapo ya njia za kupunguza tamaa ya madaraka ni kufanya madaraka yasitumike kama njia rahisi ya kujilimbikizia mali. Hili linahitaji uwazi wa mali na maslahi ya viongozi, ufuatiliaji wa mikataba ya umma, ulinzi wa wanaofichua rushwa, ukaguzi wa matumizi ya fedha, adhabu zinazotekelezwa bila upendeleo, na kuzuia migongano ya maslahi katika maamuzi ya serikali. Uongozi unapaswa kuwa dhamana ya kutumikia wananchi, si uwekezaji wa kupata utajiri.
H. Haki kwa waathirika wa vurugu za kisiasa
Matukio ya Oktoba 2025 yanahitaji kushughulikiwa kwa misingi ya ukweli, haki na uwajibikaji. Kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na uchunguzi huru na wa kuaminika kuhusu vifo, majeruhi, uharibifu wa mali, madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi na ukiukwaji mwingine wa haki. Familia zilizoathirika zinahitaji kupata ukweli kuhusu yaliyowapata wapendwa wao.
Hakuna taifa linaloweza kujenga maridhiano ya kweli kwa kufunika maumivu ya wananchi wake.
12. HITIMISHO: TANZANIA INAHITAJI KUTOKA KATIKA SIASA ZA KUISHINDA KWA GHARAMA ZOTE
Tanzania imefika katika wakati ambao inahitaji kujitathmini kwa kina kuhusu maana ya demokrasia, uongozi na uzalendo. Hukumu ya Tundu Lissu si tukio linalopaswa kutazamwa kwa mtazamo wa CHADEMA pekee. Ni sehemu ya mjadala mpana kuhusu nafasi ya upinzani, matumizi ya sheria, uhuru wa taasisi na haki za wananchi.
Lakini pia hatupaswi kufanya kosa la kuamini kwamba matatizo yote ya demokrasia yatatatuliwa kwa kuondoa chama kimoja na kukiweka kingine madarakani. Chama kipya kinaweza kuingia madarakani na kuendeleza tabia zilezile ikiwa taasisi hazitabadilika.
Vilevile, chama kilichokaa madarakani kwa muda mrefu kinaweza kuendelea kutawala kwa ridhaa ya wananchi ikiwa ushindani ni wa haki, taasisi ni huru na haki za wote zinalindwa.
Kwa hiyo, mjadala wa Tanzania usisimamie ajenda ya nani anastahili kushinda vita ya kisiasa, bali ni mfumo gani utahakikisha kwamba mshindi wa uchaguzi hawezi kujiona kuwa mmiliki wa nchi na mshindwa hawezi kunyimwa haki zake za uraia. Viongozi na wananchi wote wanapaswa kuzingatia kwamba serikali si adui wa upinzani, na upinzani si adui wa serikali. Wote ni sehemu ya mfumo mmoja wa taifa.
Serikali inahitaji upinzani imara kwa sababu upinzani una uwezo wa kuhoji maamuzi, kuibua mapungufu na kuwasilisha sera mbadala. Upinzani nao unahitaji serikali inayoheshimu sheria kwa sababu bila taasisi zinazofanya kazi kwa haki, ushindani wa kisiasa hauwezi kuwa na maana.
Wanaharakati wanahitaji uhuru wa kuhoji. Serikali inahitaji wananchi wanaowajibika. Mahakama zinahitaji uhuru wa kutoa haki. Vyama vinahitaji demokrasia ya ndani. Na wananchi wanahitaji elimu inayowawezesha kutofautisha maslahi ya chama na maslahi ya taifa.
Tanzania haihitaji chama tawala chenye uwezo wa kuondoa upinzani. Haihitaji upinzani wenye lengo la kuondoa serikali kwa gharama yoyote. Inahitaji mfumo ambao chama tawala kinaweza kushindwa uchaguzi bila kuogopa, na upinzani unaweza kushinda uchaguzi bila kuogopwa.
Huo ndiyo msingi wa demokrasia inayokomaa.
Na pengine ujumbe muhimu zaidi kwa viongozi wote wa kisiasa ni huu: Madaraka ni dhamana ya muda, lakini taifa ni urithi wa vizazi. Hakuna kiongozi, chama wala serikali inayopaswa kujiona kuwa kubwa kuliko taifa inalopaswa kulitumikia.
Uwe na amani
Rev. Godwin Chilewa






Comments