top of page

Jilinde na Wahalifu Wenye Mikakati - MAJAMBAZI na MAGAIDI

Updated: Jul 10, 2023



Dunia ya leo imegubikwa na uhalifu wa kila namna. Makundi ya majambazi, magaidi, maharamia, na wahalifu wengine wenye mikakati yameongezeka mno kiasi cha kuwapa wakati mgumu polisi, na watumishi wengine wa vyombo vya dola. Kwa ujumla hakuna mahali popote duniani unapoweza kusema uko salama kwa asilimia mia moja, au kutembea pasipo hofu ya kuvamiwa na wahalifu.

Mbaya zaidi ni kuwa kadri unavyojitahidi kujishughulisha kwa bidii ili kuboresha hali ya maisha yako ndivyo unavyokuwa kivutio kikubwa zaidi kwa wezi na majambazi. Kwa kifupi kila senti inayoongezeka mfukoni mwako, au katika akaunti yako ya benki hukufanya kuwa windo bora zaidi kwa wahalifu.

Tena kila unaponunua pikipiki au gari nzuri, huitangazia dunia kuwa kipato chako kimeongezeka, na hivyo kuwa kivutio kwa majambazi. Kwa hiyo, kama usipochukua tahadhari mafanikio yako yanaweza kuwa sababu ya kufupisha uhai wako, badala ya kuurefusha. Kwa ujumla unaweza kushambuliwa wakati wowote na mahali popote.

Pengine unaweza kufikiri wewe humo katika kundi la walio hatarini kwa sababu huna mali, magari au fedha nyingi kiasi cha kuvutia majambazi. Unaweza kujiaminisha hivyo kwa sababu pengine maisha yako ni ya kawaida sana, wewe ni mkulima tu, mmachinga, au labda mwanafunzi tu katika chuo kikuu au shule ya upili. Kama hayo ndiyo mawazo yako nakuhakikishia unajidanganya sana. Wewe pia uko katika hatari ya kuvamiwa, kuporwa kidogo ulichonacho, na hata kuuawa kama mtu mwingine yeyote. Tena katika muda na mahali usipojua unaweza kuangukia mikononi mwa magaidi; wahalifu ambao hawahitaji fedha wala mali ya mtu yeyote, bali kumwaga damu.

Si hivyo tu, unaweza kuangukia mikononi mwa mwendawazimu mwenye silaha aliyeamua kuua bila sababu yoyote. Katika miaka ya karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la matukio ya mashambulizi ya risasi katika mashule, sehemu za kazi na hata mabarabarani. Mara nyingi mashambulizi ya aina hii hufanywa na raia wa kawaida wanaofikia maamuzi ya kuua watu wasiokuwa na hatia kwa sababu zao binafsi. Wauaji hawa huwa hawajali umri wala jinsia ya mtu. Huua yeyote anayeonekana mbele yao.

Miaka ya nyuma matukio ya aina hii yalikuwa yakitokea katika nchi zilizoendelea tu, hususan Ulaya na Marekani. Lakini kutokana na maendeleo ya teknolojia na sababu nyinginezo yameongezeka na kusambaa kila mahali. Hivi sasa imekuwa kitu cha kawaida hata katika nchi za kiafrika ikiwa pamoja na nchini Tanzania kuona watu wakiuana. Mfano halisi ni tukio lililotokea jijini Dar es Salaam tarehe 25 August 2021 ambapo kijana aitwae Hamza aliwashambulia kwa risasi polisi na wapita njia na kufanikiwa kuua askari wawili na raia mmoja kabla naye kuuawa na maafisa wa jeshi la polisi.

Ni kwa sababu hii unapaswa kuwekeza katika ulinzi na usalama wako binafsi, kama vile unavyowekeza katika kulinda afya ya mwili wako. Kitabu hiki kitakusaidia kwa kiasi kikubwa kujifunza mbinu mbalimbali za kujilinda na wahalifu katika mazingira yote.




Comments


bottom of page