top of page

NAFASI ZA UONGOZI ZIZINGATIE TAALUMA


Nianze kwa kuweka bayana kwamba naiheshimu katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa mhe. rais mamlaka ya kuteua viongozi na wasaidizi anaowataka au kuona wanafaa. Naheshimu majukumu ya viongozi na nafasi walizopewa na kwa namna yoyote si nia yangu kumshambulia au kumkebehi mtu kwa chuki au sababu binafsi. Lengo langu ni kutoa maoni yenye nia ya kujenga.

Nimeshawishika kuandika makala hii baada ya kuona picha ya waziri wa ulinzi mheshimiwa Stergomena Lawrence Tax akiwa na mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwenye shughuli ya mafunzo ya kijeshi kati ya Tanzania na China. Picha hiyo iliyojipatia umaarufu mkubwa inamuonesha mheshimiwa Stergomena Tax akiwa anaangalia mazoezi hayo akiwa amegeuza kiona mbali (darubini) iliyopaswa kumuwezesha kuona vizuri na kwa ukaribu. Ni dhahiri mheshimiwa huyo alikuwa hajui kifaa hicho huwa kinatumiwaje. Natamani angeuliza.

Swali ambalo wadau wengi wanajiuliza ni kama mheshimiwa huyo alifanikiwa kufuatilia mazoezi hayo ipasavyo, na baadae kuweza kutoa maoni yake, kuwapongeza, na au kubadilishana mawazo na makamanda au mheshimiwa rais kuhusu yale aliyoyaona. Hilo ni swali tusilohitaji majibu maana halituhusu.

Binafsi simlaumu mheshimiwa Tax kwa kugeuza kiona mbali, maana mtu yeyote ambaye hajawahi kutumia kifaa hicho angeweza kufanya hivyo. Hata hivyo ninasikitika kwamba huyu ndiye waziri anayeshughulika na makamanda na wapiganaji wetu. Ni dhahiri baada ya shughuli hii kuisha makamanda waliokuwepo walicheka sana kwa kioja hiki. Ni aibu!

Tena kwa uzoefu wangu jeshini sio ajabu baadae makuruta watakapokuwa wakifundishwa kushika kiona mbali, wale watakaokosea wakapachikwa jina “Stergomena” kama watu fulani walivyowahi kubandikwa jina “Kihiyo.”

Ni kwa sababu hii nadhani kuna haja kubwa mheshimiwa rais akaangalia kwa makini nafasi anazowapa wateule wake kama zinaendana na taaluma zao hata kama watu hao wana elimu ya juu au uzoefu wa mambo mengine.

Nifafanue tena kwamba sina shaka hata kidogo kuhusu elimu na uzoefu wa uongozi wa mheshimiwa Stergomena Tax. Nafahamu ana shahada toka chuo kikuu cha Dar es Salaam, na shahada ya juu toka chuo kikuu cha Tsukuba. Si hivyo tu mheshimiwa huyu anao uzoefu wa kutosha wa mambo ya utawala na diplomasia. Kwa kifupi anafaa sana kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje, au wizara nyingine laini lakini sio wizara ya Ulinzi. Hii inahitaji mwanajeshi.

Nisisitize hapa kwamba wizara ya ulinzi ni mojawapo ya wizara nyeti kabisa inayohusisha usalama wa mipaka, ustawi wa makamanda na wapiganaji, silaha na mafunzo. Mambo haya yanaweza kufanywa kwa weredi zaidi na mtu mwenye uzoefu na jeshi hususan jenerali mstaafu au aliyepo madarakani.

Kwa kuwa hatuna wanajeshi wastaafu kwenye siasa, hii ni mojawapo ya nafasi ambazo mheshimiwa rais anapaswa kuzijaza kwa kumteua jenerali au kanali mstaafu (au aliyeko kazini) kuwa mbunge na kisha kumkabidhi wizara ya ulinzi. Naamini utendaji wake utakuwa na manufaa makubwa zaidi kwa taifa kuliko kumpa nafasi hiyo mtu asiye mwanajeshi.

Pengine utauliza swali “mbona mheshimiwa Mwinyi alishikilia nafasi hiyo muda mrefu na kwa umakini?” Jibu ni kuwa makamanda walimvumilia na kumsaidia tu si kwamba alikuwa mkamilifu. Utawezaje kujadili mambo ya ndani ya sera na utendaji wa jeshi kama hujawahi kuwa afisa wa jeshi? Utakuwaje imam kama hujui kudhika msahafu?

Mara nyingi tunajidanganya kwamba uwaziri ni nafasi ya kibutawala na usimamizi wa sera tu. Sivyo! Kuna zaidi ya hilo. Wenzetu kwenye nchi zilizoendelea huthamini sana taaluma, na ni nadra kuona wizara kama ya ulinzi anapewa mtu ambaye hajawahi kuwa afisa wa juu wa jeshi. Hili hufanyika kwa kujua tabia na utamaduni wa jeshi.

Suala hili linapaswa kuzingatiwa pia kwa wizara nyingine za kipekee. Kwa mfano, itakuwa kichekesho kukabidhi wizara ya sheria kwa mtu mwenye shahada ya uhandisi majengo, na wizara ya mipango na uchumi kwa daktari wa mifupa. Hizi ni wizara zinazohitaji elimu, na weledi wa ndani katika usimamizi na utekelezaji wa shughuli zake.

Kumbe ni muhimu tujifunze kutokana na makosa. Tumshukuru Mungu kwamba mheshimiwa Stergomena aligeuza kiona mbali cha kuangalilia mazoezi ya kijeshi tu. Imagine tunapokuwa na waziri wa fedha asiyejua kutumia kiona mbali cha uchumi wetu. Si ajabu tukajikuta tukiwa na tozo juu ya tozo juu ya tozo.


Rev. Godwin Chilewa

Comments


bottom of page