top of page

TUHUMA ZA UTEKAJI NYARA - JESHI LA POLISI LINAWEZA KUKWEPA LAWAMA?

Updated: Sep 15, 2024

Hivi karibuni, tuhuma za utekaji nyara na mauaji ya watu wasio na hatia zimekuwa kama jambo la kawaida. Kila unapofungua gazeti au kutembelea mitandao ya kijamii, utakutana na vilio vya ndugu na marafiki waliopoteza wapendwa wao, au kelele za wanaharakati wanaotetea haki za binadamu na kudai kurejeshwa kwa watu wanaodaiwa kutekwa nyara.


Mbali na akina Ben Saanane na wenzake waliopotea muda mrefu uliopita, watu wengine wanaotajwa kutekwa nyara au kupotea ni pamoja na Deusdedith Soka, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) wilaya ya Temeke, Edgar Mwakalebela, na Ali Mohammed Kibao, ambaye alishushwa kutoka kwenye basi la Tashrif na watu wanaodhaniwa kuwa maafisa wa usalama. Inasemekana kuwa zaidi ya watu 200 wametekwa nyara au kupotea katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.


Kutokana na matukio hayo, wanasiasa na wanaharakati wameilaumu serikali, hususan jeshi la polisi na idara ya usalama wa taifa, kwa kuhusika na utekaji nyara huo. Hata hivyo, lawama hizo zimekanushwa vikali na viongozi wa serikali, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na jeshi la polisi, ambao wamehusisha vitendo vya utekaji nyara na mauaji ya kishirikina.


Pengine utajiuliza kwa nini wananchi wanahusisha vyombo vya dola, hasa jeshi la polisi, na utekaji nyara unaoendelea? Kuna mambo kadhaa yanayoweza kuwa sababu ya lawama hizo, lakini hapa nitazungumzia mambo matatu tu. Kwanza, ni tabia ya ukatili na unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya askari.


Ingawa askari wengi wa sasa ni waadilifu na wenye weledi, kundi dogo la askari wakorofi linaathiri sana sifa na uaminifu wa jeshi letu. Askari hao hutumiwa na watu wenye fedha kuwatisha, kuwatesa, kulipiza kisasi, au kuwaadhibu mahasimu wao. Baadhi ya askari hawa hata hujivunia kutumia maneno kama “nitakuua” au “nitakupoteza” bila kujali athari zake.


Jambo la pili ni matumizi mabaya ya mamlaka na viongozi wa serikali, hasa wakuu wa wilaya na mikoa, kutoa maagizo kwa polisi kuwakamata au kuwatesa wapinzani wa kisiasa na watu wasio na hatia. Hili limethibitishwa na matukio ya awali yaliyofanywa na kina Sabaya na wenzake. Kwa bahati mbaya, historia haifutiki kirahisi.


Jambo la tatu ni utaratibu mbovu wa jeshi la polisi kuwaruhusu askari waliovaa kiraia kubeba hadharani silaha kubwa. Kawaida, silaha kubwa kama bunduki zinapaswa kubebwa na askari aliyevaa sare rasmi za jeshi. Askari wa CID au yeyote aliyevaa kiraia anatakiwa kubeba silaha ndogo (pistol) na kuificha chini ya mavazi yake. Utaratibu huu husaidia wananchi kuwa na uhakika kwamba mtu mwenye silaha ni askari, huku ukimpa askari aliyevaa kiraia fursa ya kujipenyeza kwa adui bila kujulikana.


Askari waliovaa kiraia wakiwa na silaha kubwa hadharani wanajitambulisha wazi na hivyo kujikuta katika hatari ya kudhaniwa kuwa ni majambazi. Ndiyo maana katika nchi zilizoendelea, polisi au maafisa wa FBI wanapokuwa na silaha huku wakiwa wamevaa kiraia, hufuatwa utaratibu ufuatao: (a) Kuvaa beji inayotambulisha kazi yao; (b) Kuvaa fulana au vest iliyoandikwa POLICE au FBI; na (c) Kuning'iniza kitambulisho shingoni.


Utaratibu huu hupunguza mauaji ya bahati mbaya, huku ukiwahakikishia wananchi kuwa mtu mwenye silaha ni askari. Kwa bahati mbaya, askari wetu hawafuati taratibu hizi, hali inayopelekea kuibua mashaka. Hivi sasa, ni vigumu kuthibitisha kama watu waliomteka nyara Soka na Ali Mohammed Kibao walikuwa askari halisi au majambazi waliovaa silaha hadharani. Hakika, leo hii hakuna mwananchi anayeweza kutofautisha askari na jambazi; mtu yeyote anayeonekana na silaha hadharani huchukuliwa kuwa ni askari.


Ni vyema sasa kwa jeshi la polisi kujisafisha kwa vitendo. Ni wakati muafaka kuhakikisha askari wanaovaa kiraia wanakuwa na vitambulisho vinavyoonekana wazi, pamoja na fulana au vizibao vilivyoandikwa POLICE au CID.


Mch. Godwin Chilewa

Comments


bottom of page