Tujifunze Toka kwa Wenzetu - Botswana na Namibia.
- Rev. Godwin Chilewa
- Oct 4, 2024
- 7 min read

Kama umewahi kuishi Marekani au Ulaya bila shaka utakuwa unafahamu kwamba nchi hizo zina idadi ndogo sana ya wahamiaji toka Botswana na Namibia. Raia wa nchi hizo za Afrika huona kama laana kuziacha nchi zao walizozaliwa kwenda kuishi ughaibuni. Kwao ni aibu na fedheha kubwa. Pengine utajiuliza kwanini? Jibu ni kwamba nchi zao zina kila kitu kinachotamanika, tena zaidi ya Ulaya na Marekani. Hapo ndipo linapokuja swali gumu zaidi. Sisi watanzania tumekosa nini na au tumepungukiwa nini?
Kwa kifupi Tanzania, Botswana, na Namibia zote zilipata uhuru katika nyakati tofauti, lakini maendeleo ya kiuchumi ya nchi za wenzetu yana mwelekeo tofauti. Botswana na Namibia wamepiga hatua kubwa mno katika kuinua uchumi wa nchi zao na kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida.
Kwa ujumla zipo sababu nyingi na za kimsingi zilizochangia kwa kiasi kikubwa wenzetu kusonga mbele na sisi kufika hapa tulipo. Hapa nitataja sababu chache tu:
1. Sera za Uchumi baada ya Uhuru
Tanzania, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere, ilichagua mfumo wa siasa na uchumi wa kijamaa (African socialism) ambao ulisisitiza usawa na umiliki wa pamoja wa rasilimali. Ingawa lengo lilikuwa zuri, sera za ujamaa kama vile "Azimio la Arusha" na "Utaifishaji" wa sekta binafsi ziliathiri uchumi kwa kusababisha udumavu wa uzalishaji na uwekezaji nchini. Ubunifu na vipawa vingi vilikufa.
Baada ya sera za ujamaa, Tanzania ilianza kurekebisha uchumi wake chini ya uongozi wa Benjamin Mkapa, ambaye alianzisha sera za ubinafsishaji na kufungua milango ya uwekezaji. Hata hivyo, uwazi na uwajibikaji wa serikali katika sekta muhimu kama madini na nishati uliendelea kuwa changamoto, na mara nyingi sera hizi zilitumiwa vibaya ili kuwanufaisha wachache. Baadae hatua za Rais Magufuli kuboresha ukusanyaji wa kodi na kuziba mianya ya ufisadi zilipata umaarufu mkubwaingawa zilikuwa na athari kwa sekta binafsi kutokana na udhibiti mkali wa biashara.
Botswana, kwa upande mwingine, ilitumia sera za soko huria, kuimarisha sekta binafsi, na kufanya kazi na makampuni ya kimataifa, hasa katika sekta ya madini (hususan almasi), jambo lililosaidia ukuaji wa kiuchumi wake. Wenzetu waliweka sera za kiuchumi zinazohamasisha uwekezaji wa nje bila kusahau sekta binafsi. Kwa kufanya hivyo serikali imeweza kudhibiti nakisi ya bajeti kwa kutoendekeza matumizi yasiyo ya lazima, huku ikihimiza uzalishaji wa ndani. Rais Mokgweetsi Masisi ameendelea na sera hizi, akisisitiza ubunifu na uchumi wa kidijitali kama njia ya kupanua uchumi wa nchi hiyo.
2. Utawala Bora
Botswana imekuwa na sifa nzuri ya kuwa na utawala bora tangu uhuru wake. Nchi hiyo imekuwa na utawala wa sheria, uwazi, na uongozi thabiti wa kisiasa. Namibia pia imepata faida kutokana na utulivu wa kisiasa na sera thabiti za kiuchumi. Tanzania, ingawa imekuwa na utulivu wa kisiasa kwa kiasi kikubwa, changamoto za rushwa na ukosefu wa uwazi katika baadhi ya awamu za uongozi kumeathiri sana kasi ya maendeleo yake ya kiuchumi.
Pamoja na hilo viongozi wa Botswana wanajulikana kwa uwajibikaji wa hali ya juu na uwazi kwenye usimamizi wa rasilimali za taifa. Rais wa kwanza wa Botswana, Seretse Khama, alianzisha msingi wa utawala bora kwa kuweka taasisi imara za kidemokrasia na uhuru wa vyombo vya habari. Serikali imekuwa ikichukulia kwa uzito sheria za kupambana na rushwa, na taasisi kama Directorate on Corruption and Economic Crime (DCEC) zimekuwa muhimu katika kudumisha uwazi. Utawala huu umeifanya Botswana kuwa moja ya nchi zenye kiwango cha chini cha rushwa barani Afrika.
Namibia: Sam Nujoma, rais wa kwanza wa nchi hiyo, alijenga msingi wa utawala wa sheria na uwazi wa kisiasa baada ya uhuru kutoka Afrika Kusini. Serikali ya Namibia imeweka mikakati madhubuti ya kupambana na rushwa, na hii imechangia kuweka mazingira ya kuaminika kwa wawekezaji wa nje na ndani.
Tanzania imekuwa na changamoto kubwa kwenye suala la uwajibikaji. Ingawa baadhi ya marais kama Julius Nyerere walikuwa na uadilifu wa hali ya juu na walionekana kama viongozi wa watu, kuna awamu za uongozi zilizoonekana kukumbwa na rushwa na ukosefu wa uwazi. Kwa mfano, katika awamu za uongozi za miaka ya 1990 na 2000, kulikitokeza ripoti nyingi za ufisadi uliosababisha baadhi ya sekta muhimu kama maliasili, utalii, madini, udhibiti wa mapato ya serikali na fedha za kigeni kuporomoka.
3. Mali Asilia na Matumizi Yake:
Botswana ilifanikiwa kusimamia vizuri utajiri wake wa madini, hasa almasi, kupitia ushirikiano na kampuni za kimataifa kama De Beers. Serikali ilianzisha mikakati ya kutumia mapato ya madini kujenga miundombinu, elimu, na huduma za afya, na hii imechangia maendeleo ya kiuchumi. Rais Ian Khama aliendeleza sera hizi kwa kuhakikisha kuwa taifa linaendelea kufaidika na rasilimali zake kwa uwazi na ustawi wa jamii. Botswana pia imejenga utamaduni wa kuheshimu utu na utumishi uliotukuka kuliko kujilimbikizia mali.
Namibia pia imefaidika na utajiri wa madini na mafuta. Serikali ilianzisha Namibia Petroleum Corporation (Namcor) kusimamia sekta ya mafuta kwa uwazi, na mapato ya rasilimali hizi yameelekezwa katika maendeleo ya jamii. Hifikepunye Pohamba, aliyekuwa rais wa Namibia, alichukua hatua madhubuti kupambana na ufisadi, na hii imechangia usimamizi bora wa rasilimali. Wanamibia kama walivyo watswana wanaheshimu utu na utumishi uliotukuka na kulaani wizi na rushwa kwa nguvu zote.
Tanzania ina utajiri mkubwa wa madini, gesi asilia, na utalii, lakini mara nyingi kumekuwa na matatizo ya usimamizi wa mapato ya rasilimali hizo. Wakati wa uongozi wa marais kama Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete, mikataba ya madini haikuwa wazi na ilisababisha malalamiko kuhusu jinsi faida zake zilivyokuwa zikitumika. Tanzania pia ilikabiliwa na ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali, kashfa za mikataba mibovu isiyo na tija kwa serikali, na kutowajibika kwa wafanyakazi. Wizi na ufisadi ukafanywa kuwa jambo la kawaida.
Rais John Magufuli alipoingia madarakani alichukua hatua kali kurekebisha mikataba ya madini na kuongeza mapato ya serikali kupitia sera za kiuchumi za kitaifa, ingawa mbinu zake ziligawanya maoni ya watu. Uwajibikaji iliongezeka na rushwa ilipungua kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo lilizuka tatizo lingine la wafanyabiashara kutishwa na kudhirumiwa mali zao. Hali hii ilipunguza kasi ya uwekezaji nchini na kuzorotesha ukuaji wa pato la taifa. Katika kipindi hiki pia kulikuwa na u siri mkubwa katika uingiaji wa mikataba ya mamilioni ya dola.
4. Elimu na Uwekezaji Rasilimali Watu:
Botswana: Viongozi wa nchi walitambua umuhimu wa kuwekeza katika rasilimali watu, hasa katika elimu na afya. Serikali ya Botswana imewekeza katika elimu ya juu na afya bora kwa kutumia mapato ya almasi. Chuo Kikuu cha Botswana kimekuwa moja ya taasisi za elimu bora, na mpango wa afya wa kitaifa umeimarisha ustawi wa raia. Mifumo ya elimu ya msingi na serikali imetengenezwa kwa namna inayowafaa wananchi, kuwawezesha kujitegemea na kujenga utaifa.
Namibia: Viongozi wake pia wameelekeza juhudi nyingi katika elimu, hasa kwa kuboresha elimu ya ufundi na taaluma. Hii imewawezesha wananchi kushiriki katika sekta muhimu kama madini na kilimo. Miaka mingi baadavya uhuru Namibia ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la wataalam hasa madaktari na wahandisi. Hata hivyo uongozi wa nchi hiyo ulifanikiwa kuziba pengo kwa kukodisha na kuajiri maelfu ya wataalam kutoka nje. Namibia ilifanya hivyo mpaka ilipofanikiwa kusomesha na kupata wataalam wa nje. Pamoja na changamoto hizo hali ya maisha ya wananchi iliendelea kuwabya kuridhisha kulinganisha na nchi nyingi za Afrika.
Tanzania ilifanikiwa sana katika kufuta ujinga wa kutojua kusoma na kuandika, na kusimamisha elimu ya msingi. Katika uongozi wake mwalimu Julius Nyerere alianzisha sera ya elimu kwa wote yenye lengo la kujitegemea (“Education for Self-Reliance”). Hata hivyo, mabadiliko yaliyofuata baadae yalisababisha changamoto kubwa kwenye sekta ya elimu ya juu na afya. Uwekezaji katika elimu ya juu bado haukidhi mahitaji ya kiuchumi ya kisasa.
Pamoja na hayo elimu inayotolewa mashuleni na vyuo vikuu bado hairidhishi au kukidhi haja na ushindani wa dunia kisayansi na teknolojia. pia imekuwa changamoto, Elimu bora na mafunzo ya ufundi ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda na kuhamasisha ubunifu na ujasiriamali. Botswana na Namibia ziliwekeza mapema katika elimu, na sekta zao za afya na ustawi wa jamii zimeimarika zaidi.
5. Amani - Utulivu wa Kisiasa na Uhuru wa Kidemokrasia:
Botswana imekuwa ikijivunia utulivu wa kisiasa na uhuru wa vyombo vya habari, jambo ambalo limechangia kuaminika kwa nchi hiyo katika kanda na duniani kwa ujumla. Uchaguzi wa kidemokrasia na mabadiliko ya madaraka umekuwa wa amani, na hii imeimarisha taasisi za kisiasa. Namibia pia imejenga mifumo imara ya kisiasa, na imekuwa na uchaguzi wa kidemokrasia kwa muda mrefu. Ingawa chama tawala, SWAPO, kimekuwa madarakani kwa muda mrefu, kumekuwa na mazingira ya kushirikisha vyama vya upinzani na jamii.
Tanzania kwa kiasi kikubwa imekuwa na utulivu wa kisiasa tangu uhuru. Hata hivyo, kumekuwa na wasiwasi kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na demokrasia katika awamu za karibuni za uongozi, hasa wakati wa John Magufuli. Ingawa alikuwa kiongozi mwenye nia ya kujenga taifa, mbinu zake za kuendesha siasa ziliathiri uhuru wa kidemokrasia, huku kukiwa na malalamiko kutoka kwa vyama vya upinzani.
Nini kifanyike kuboresha hali ya uchumi wa Tanzania na Maisha ya Wananchi?
Jibu ni lilelile nililolieleza kwenye makala zangu zilizotangulia:
1. Kuboresha Sera za Uchumi:
Tanzania inaweza kufaidika zaidi kwa kuimarisha sekta binafsi na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje. Sera zinazowezesha mazingira bora ya kibiashara, uwazi katika uwekezaji, na kupunguza urasimu zinaweza kuchochea ukuaji wa sekta muhimu kama viwanda na huduma. Serikali ione umuhimu wa kuwashirikisha wananchi katika mipango na maamuzi ya mambo yanayowahusu ili kuinua ufanisi.
2. Kupambana na Rushwa.
Hatua madhubuti za kudhibiti rushwa na kuhakikisha uwajibikaji serikalini ni muhimu. Wakati wa utawala wake Rais John Magufuli aliidhihirishia dunia kwamba rushwa inaweza kukomeshwa nchini endapo serikali itaamua kwa dhati kufanya hivyo. Utawala bora, utendaji unaozingatia sheria na uwazi vitavutia uwekezaji zaidi na kuweka misingi thabiti ya uchumi wa kisasa.
3. Kuwekeza katika Miundombinu
Tanzania imejitahidi sana kuwekeza kwenye miundo mbinu. Ujenzi wa reli ya kisasa, barabara zinazounganisha mikoa, na upanuzi wa bandari ndogo na vivuko ni muhimu kwa maendeleo. Tanzania inapaswa kuendelea kuwekeza kwenye teknolojia ya mawasiliano ili kurahisisha biashara na kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali.
4. Kuboresha Elimu na Afya:
Uwekezaji zaidi unahitajika katika elimu, hasa elimu ya ufundi na teknolojia, ili vijana wawe na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la kisasa. Afya bora pia ni muhimu kwa ajili ya maendeleo endelevu.
5. Usimamizi Bora wa Maliasili
Tanzania inaweza kufaidika zaidi kwa kuweka mikakati bora ya usimamizi wa rasilimali zake, kuhakikisha kuwa mapato yanayotokana na madini, gesi asilia, na utalii yanatumika vyema kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Wakati wa uongozi wake Raus Magufuli aliweka misingi ya kusimamia maliasili hasa madini. Ni muhimu serikali iiendelee kudhibiti uchimbaji na usafirishaji wa madini bila kukoma.
HITIMISHO
Ni dhahiri kwamba viongozi wa Botswana na Namibia wamefaulu kwa sababu ya msisitizo wa utawala bora, usimamizi wa rasilimali kwa uwazi, uwekezaji katika rasilimali watu, na sera za kiuchumi zinazohamasisha uwekezaji. Tanzania, ingawa imepiga hatua, inahitaji kuongeza uwazi, kupambana zaidi na rushwa, na kuimarisha uwekezaji katika sekta binafsi na elimu. Nchi yetu ina nafasi kubwa ya kuongeza kasi ya maendeleo yake ya kiuchumi na kuhakikisha wananchi wake wanapata ustawi wa hali ya juu kama wenzetu.
Rev. Godwin Chilewa
Comments