top of page

DIPLOMASIA YA NDANI: Je, Kikao cha Rais Samia na TEC ni Maridhiano au Mkakati wa Kisiasa?

Na Rev. Godwin Chilewa



Katika mazingira ya mvutano wa kisiasa uliodumu kwa miezi kadhaa nchini Tanzania, kikao kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kimeibua mjadala mpana wa kitaifa na kimkakati. Kikao hicho, kilichofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, kimeelezwa rasmi kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano, amani, na mshikamano wa kitaifa. Hata hivyo, kwa mtazamo wa kiintelijensia, tukio hili linahitaji kuchambuliwa zaidi ya maelezo rasmi likiangaliwa kama sehemu ya mchakato mpana wa usimamizi wa mgogoro wa kisiasa nchini.


Muktadha wa Kisiasa: Chanzo cha Kikao

Kikao hiki hakikutokea kwa bahati mbaya. Kimekuja katika kipindi ambacho uhusiano kati ya serikali na Kanisa Katoliki ulikuwa umeingia katika mvutano mkubwa kufuatia matukio ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025. Kanisa, kupitia TEC, lilijitokeza wazi kulaani mauaji ya waandamanaji na kuomba uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu vurugu hizo.


Kwa upande wa serikali, maelezo rasmi yanaonyesha kuwa kikao hicho kilijikita katika kujadili masuala ya kitaifa ikiwemo siasa, imani, maendeleo, na mustakabali wa amani nchini Hata hivyo, lugha ya kidiplomasia inayotumika katika taarifa hizo haifuti ukweli kwamba kulikuwa na ufa mkubwa wa kimahusiano uliotokana na mgogoro huo. Kwa mantiki ya kiintelijensia, kikao hiki kinaweza kutafsiriwa kama hatua ya juu ya “strategic engagement” kati ya dola na taasisi yenye ushawishi mkubwa wa kijamii, yenye uwezo wa kuathiri mwelekeo wa maoni ya umma.


Uchambuzi wa Nia: Kujisafisha au Maridhiano?

Mjadala mkubwa unaoendelea hivi sasa ni kama Rais Samia anajaribu kujisafisha kisiasa au ana nia ya dhati ya kuleta maridhiano ya kitaifa.

Kwa upande mmoja, kuna dalili za wazi za mkakati wa kisiasa (political image management). Shinikizo la ndani na la kimataifa baada ya matukio ya 2025 linaifanya serikali kuwa katika nafasi ya kutafuta njia za kurejesha uhalali wake mbele ya wananchi na jumuiya ya kimataifa. Kwahiyo kukutana na TEC taasisi yenye uhalali mkubwa wa kimaadili ni hatua inayoweza kusaidia kupunguza shinikizo hilo.


Kwa upande mwingine, kuna viashiria vinavyoonyesha uwezekano wa nia ya dhati ya kupunguza mvutano. Kukubali kukutana na wakosoaji, kuzungumzia masuala ya kitaifa kwa uwazi, na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano ni dalili za “strategic de-escalation” yaani juhudi za makusudi za kushusha joto la kisiasa.

Kwa tathmini ya kiintelijensia, ukweli uko katikati ya pande hizi mbili. Hii ni hali ya “hybrid intent,” ambapo hatua za kisiasa zinaweza kuwa na malengo ya muda mfupi ya kujisafisha na kujenga taswira, lakini pia kufungua uwezekano wa utulivu wa muda mrefu.


Je, Kikao Hiki Kimemnufaisha Nani?

Kikao hiki kinaweza kuchambuliwa kwa mizani ya faida za kimkakati kwa kila upande.

Kwa serikali, faida kuu ni ya muda mfupi. Kikao kimejenga picha ya uongozi unaosikiliza, kinapunguza ukosoaji, na kinaweza kusaidia kurejesha imani kwa kiwango fulani. Aidha, kinadhibiti simulizi (narrative) ya kwamba serikali imefungwa kwa ukosoaji.


Kwa TEC, faida ni kubwa na ya muda mrefu zaidi. Kwa kukubaliwa kukutana na Rais, kanisa limeimarisha nafasi yake kama mdau halali wa kitaifa katika masuala ya siasa na haki za kijamii. Hii inalipa TEC uwezo mkubwa wa kushinikiza ajenda ya uwajibikaji na maridhiano ndani ya mfumo rasmi. Kwa lugha ya kiintelijensia, TEC imepata “strategic leverage,” wakati serikali imepata “tactical image gain.”


Mitazamo ya Wananchi Ukoje?

Tathmini ya hisia za wananchi inaonyesha mgawanyiko wa wazi. Kundi moja linaona kikao hiki kama mwanzo wa matumaini, na ishara kwamba mazungumzo yanaweza kurejea na mgogoro unaweza kutatuliwa kwa njia ya amani.


Kundi la pili lina mashaka makubwa. Linaona kikao hiki kama mbinu ya kisiasa ya kupunguza presha bila dhamira ya kufanya mageuzi halisi. Hoja kuu ni: kwa nini hatua hii ichukuliwe sasa, baada ya muda mrefu wa mvutano? Tena baada ya Rais Samia Suluhu kutoa mfululizo wa vijembe, kauli za kejeli na dhihaka dhidi ya TEC.


Kundi la tatu lina msimamo mkali zaidi, likisisitiza kuwa bila haki kwa waathirika na uwajibikaji wa vyombo vya dola, mazungumzo yoyote hayana maana ya msingi. Kwa mtazamo wa kiintelijensia, ishara kuu hapa ni kuwepo kwa “trust deficit” yaani pengo la imani kati ya serikali na wananchi. Ukweli ni kwamba kikao kimepunguza joto la kisiasa, lakini hakijajenga imani ya kudumu.


Mtazamo wa Mbele: Nini Kinaweza Kutokea?

Kikao hiki ni mwanzo, si mwisho wa mchakato. Uhalisia wa nia ya serikali utaamuliwa na hatua zitakazochukuliwa baadae. Mambo muhimu yatakayobeba uzito wa kimkakati ni pamoja na suala la uchunguzi huru na wa kuaminika kuhusu matukio ya 2025, uwezekano wa uhuru wa kisiasa na haki za kiraia kuruhusiwa kwa kiwango kikubwa zaidi, na kama TEC itaendelea kuwa sauti huru bila kuzuiwa kimkakati. Kimsingi mambo haya ndiyo yataamua kama kikao hiki kitakuwa historia ya mabadiliko au kumbukumbu ya hatua ya kisiasa isiyo na matokeo ya kudumu.


Kwa jumla, kikao kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na TEC kina uzito mkubwa wa kisiasa na kijamii. Kinaashiria mabadiliko ya mbinu kutoka msuguano wa moja kwa moja kwenda kwenye mazungumzo. Hata hivyo, kwa tathmini ya kiintelijensia, kikao hiki kinaonekana zaidi kama “pressure-release mechanism” tu, njia ya kupunguza shinikizo la kisiasa kuliko suluhisho kamili la mgogoro uliopo.


Pamoja na hayo, ikiwa kitapata ufuatiliaji wa hatua halisi na za dhati, kinaweza kuwa mwanzo wa safari ya kuelekea maridhiano ya kweli ya kitaifa. Kwa sasa, Tanzania ipo katika hatua ya mpito kati ya kurejesha imani au kuendeleza sintofahamu ya kisiasa. Hatua za serikali na muitikio wa wananchi ndizo zitakazoamua hatima hiyo.


Uwe na amani

 
 
 

Comments


bottom of page