Kesi ya Uhaini Dhidi ya Tundu Lissu: Mwelekeo wa Hukumu na Hatima ya Lissu
Na Rev Godwin Chilewa

Kesi ya Tundu Antipasi Lissu ni uwanja wa mapambano ya kimkakati kati ya dola na upinzani hivyo kwa mtazamo wa kiintelijensia, haiwezi kuchambuliwa kwa kutumia mizani ya sheria pekee; bali inahitaji uelewa wa kina unaounganisha ushahidi wa mahakamani, mwenendo wa taasisi za dola, na mienendo ya kisiasa ya ndani na kimataifa.
Kisheria, msingi wa mashtaka dhidi ya Lissu unatokana na hotuba aliyotoa akidaiwa kuhamasisha kuvurugwa kwa uchaguzi, akitumia lugha ambayo upande wa mashtaka umetafsiri kama wito wa uasi dhidi ya mamlaka halali ya serikali. Hapa ndipo hoja ya msingi kisheria inayopaswa kuangaliwa kwa umakini: je, kauli ya kisiasa inaweza kufikia kiwango cha “uhaini” au inabaki katika wigo wa “uchochezi”?
Kwa mujibu wa misingi ya sheria ya jinai, kosa la uhaini kwa kawaida huhitaji ushahidi wa vitendo vinavyoonyesha dhamira ya wazi ya kuipindua serikali, si tafsiri ya maneno pekee. Hivyo basi, utegemezi mkubwa wa upande wa mashtaka katika tafsiri ya hotuba unaonyesha uwepo wa udhaifu wa kimuundo katika kesi yenyewe.
Udhaifu huu unaonekana zaidi kupitia mwenendo wa mahakama katika hatua za awali za shauri. Kumbukumbu zinaonyesha kuwa upande wa mashtaka umejaribu kuwasilisha ushahidi mpya katika hatua za baadaye, hali inayotafsiriwa kitaalamu kama jaribio la kuziba mapengo ya ushahidi uliopo.
Katika mantiki ya kiintelijensia ya uchunguzi wa kesi, hatua kama hii mara nyingi huashiria kuwa jalada la awali halikuwa na uzito wa kutosha kuthibitisha kosa linalodaiwa. Aidha, jitihada za kutumia mashahidi wa siri na kuzuia uwazi wa mwenendo wa kesi zimeibua maswali makubwa kuhusu uadilifu wa mchakato mzima wa haki.
Sambamba na hilo kitendo cha viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama kukataa au kushindwa kufika nafasi kusimama mahakamani kutoa ushahidi kumemuweka Tundulisu katika nafasi nzuri zaidi ya utetezi. Aidha kauli ya DCI Kingai kwamba yeye na viongozi wengine watasherehekea Tundu Lissu akitiwa hatiani inathibitisha chuki, uadui na mateso aliyodai Tundulisu kuwa amekuwa akifanyiwa na vyombo vya dola. Katika kesi ambayo adhabu ya kosa husika ni kifo, mahakama inabeba wajibu wa kulinda haki za msingi za pande zote.
Kwa upande mwingine, mwenendo wa kesi umeathiriwa kwa kiasi kikubwa na mazingira ya kisiasa yaliyotangulia kukamatwa kwa Lissu. Uchaguzi wa mwaka 2025 ulifanyika katika mazingira yaliyokuwa na ushindani mdogo, huku vyama vikuu vya upinzani vikiondolewa au kujiondoa kwenye mchakato na wakati wa uchaguzi huo, kulitokea maandamano yaliyoambatana na vifo na ukamataji wa raia wengi, hali iliyoongeza shinikizo la kisiasa na kijamii dhidi ya serikali Katika muktadha huu, kesi dhidi ya Lissu inaonekana kama njia ya kimkakati ya kudhibiti nguvu ya upinzani na kudumisha uthabiti wa dola.
Kwa mtazamo wa kiintelijensia, kesi hii inaingia katika kundi la “high-value political trials,” ambapo matokeo yake hayaamuliwi tu na uzito wa ushahidi bali pia na tathmini ya athari zake kwa utulivu wa nchi na taswira ya kimataifa. Ni muhimu kuzingatia kuwa kosa la uhaini nchini Tanzania ni miongoni mwa makosa mazito zaidi kisheria, likiwa na uwezekano wa adhabu kali ikiwemo kifo. Hii inaifanya kesi hii kuwa na uzito wa kipekee, na hivyo kuongeza uwezekano wa kuingiliwa na maamuzi ya kimkakati ya kisiasa.
Katika kuchambua mwelekeo wa kesi hii, kuna matokeo matatu yanayoweza kujitokeza. Kwanza ni uwezekano wa Tundulisu kuachiwa huru kwa msingi wa udhaifu wa ushahidi, hasa kama mahakama itazingatia tafsiri finyu ya sheria ya uhaini kama ilivyowasilishwa na upande wa mashitaka. Shitaka la uhaini linahitaji ushahidi wa vitendo vya moja kwa moja na kuthibitishwa pasipo shaka yoyote. Upande wa mashitaka ungekuwa na nguvu kama mashitaka dhidi ya Tundu Lissu yangekuwa ya uzandiki kulingana na aina ya ushahidi uliowasilishwa.
Lakini pia upo uwezekano wa Tundu Lissu kutiwa hatiani, hasa ikiwa tafsiri pana ya kauli za kisiasa itatumika na mazingira ya kisiasa yataendelea kuwa na msukumo wa kulinda mamlaka ya dola. Endapo mahakama itaamua kufanya hivyo basi haitamuhukumu adhabu ya kifo. Badala yake itamhukumu kifungo kati ya miaka mitano hadi kumi na tano kwa makosa mengine. Hili litafanyika ili kupunguza “Reaction” ya wananchi na jumuia ya kimataifa.
Adhabu ya kifungo itakuwa sahihi zaidi kwa sababu itafanya mambo mengine mawili ya muhimu. Itampa nafasi Rais Samia Suluhu kuweza kumtoa gerezani kwa msamaha wa rais, lakini pia itakuwa imemuondolea Tundu Lissu haki ya kugombea urais katika chaguzi zijazo. Zingatia kuwa kwa mujibu Ibara ya 67(2)(c) ya Katiba :mtu aliyepatikana na hatia ya makosa ya jinai harihusiwi kugombea nafasi ya juu ya uongozi ikiwa pamoja na ubunge au urais.
Uchambuzi wa kiintelijensia, unaonesha pia uwezekano wa tatu ambao ni suluhu ya kisiasa. Hii ndiyo inaonekana kuwa na urahisi mkubwa zaidi. Suluhu ya kisiasa inaweza kujitokeza kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na makubaliano ya kisiasa yasiyo rasmi yanayoweza kumfanya DPP afute kesi. Historia ya kesi zenye mchanganyiko wa siasa na sheria katika kanda ya Afrika Mashariki inaonyesha kuwa njia hii hutumika pale ambapo kuendelea kwa kesi kunaweza kuleta madhara makubwa ya kisiasa au kidiplomasia kwa taifa. Hata hivyo kwa mahali kesi hii ilipofikia njia hii si rahisi tena.
Kwa ujumla uchambuzi unaonesha kuwa kesi ya uhaini dhidi ya Tundu Lissu ipo katika makutano ya sheria na siasa. Kisheria, kuna dalili za udhaifu wa ushahidi unaotegemea tafsiri ya kauli badala ya vitendo. Kisiasa, kuna nguvu zinazoathiri mwelekeo wa kesi ambazo haziwezi kupuuzwa. Hivyo basi, mustakabali wa kesi hii hauwezi kutabiriwa kwa uhakika kwa kutumia vigezo vya kisheria pekee; bali unategemea mizania ya nguvu kati ya sheria, siasa, na maslahi ya taifa katika jukwaa la ndani na kimataifa.
Kwa mtazamo wa kiintelijensia, kesi hii inaweza kuelezwa kama “controlled legal process within a politically sensitive environment,” ambapo mwisho wake hautokani na hoja au kile kinachothibitishwa mahakamani, bali na kile kinachoonekana kuwa salama zaidi kwa uthabiti wa dola. Hata hivyo, hatua hii endapo itatekelezwa itaporomosha kwa kiasi kikubwa heshima ya mahakama kama chombo cha utoaji haki.
Uwe na Amani






Comments