top of page

Georgia Guidestones: Jiwe la Siri, Ajenda ya Dunia, au Tafsiri Iliyopotoshwa?



Je, umewahi kusikia habari za Georgia Guidestones, mnara wa mawe uliosimama kwa miongo kadhaa katika jimbo la Georgia, nchini Marekani? Wengi wa walioujua waliuita “Stonehenge ya Marekani,” wakiufananisha na ule mnara wa kale wa mawe uliopo nchini Uingereza. Lakini kwa wengine ulikuwa zaidi ya sanaa, ulikuwa ujumbe wa siri, ajenda ya dunia mpya, na mwongozo wa kizazi kijacho baada ya maangamizi.


Mnara huu ulijengwa mwaka 1980 katika eneo la Elbert County. Jambo lililozua utata mkubwa ni kwamba mtu aliyeagiza ujenzi wake hakujulikana kwa jina halisi. Alitumia jina la bandia R. C. Christian ambalo wengi wanaamini lilikuwa ishara ya kihistoria au kidini huku likihusishwa na harakati za zamani kama Rosicrucians. Kwa kifupi mpaka sasa hakuna anayejua kwa uhakika utambulisho wake wa kweli na au yuko wapi.


Georgia Guidestones liliundwa kwa mawe makubwa ya granite sita yaliyopangwa kwa umbo maalum, yakielekeza jua, mwezi, na nyota kuashiria maarifa ya hali ya juu ya anga. Maandishi yalichongwa kwa lugha nane kuu, Kiingereza, Kihispania, Kiswahili, Kiarabu, Kichina, Kirusi, Kihindi, na Kiebrania. Uwepo wa Kiswahili miongoni mwa lugha hizi kulizua mjadala mkubwa. Wengi walijiuliza je, Afrika nayo ni sehemu ya ujumbe huu wa kimataifa?


Jambo lililoshangaza zaidi ni kuwa mawe hayo yalibeba kanuni 10 zilizolenga “kuongoza wanadamu.” Baadhi ya ujumbe huo ulikuwa kudhibiti idadi ya watu duniani isizidi milioni 500, kuongoza uzazi kwa hekima ili kuboresha ubinadamu, kuunda lugha moja ya dunia, kusawazisha haki za mtu binafsi na wajibu kwa jamii, na kulinda mazingira.


Kwa baadhi ya watu, haya yalionekana kama mwongozo wa amani na ustawi. Lakini kwa wengine, yalikuwa ishara ya ajenda ya siri ya kudhibiti dunia hasa wazo la kupunguza idadi ya watu lililozua hofu na nadharia za njama.



Pengine utajiuliza "kwanini mnara huu ulijengwa?" Kwa ujumla sababu rasmi hazikuwahi kuthibitishwa wazi. Hata hivyo, kuna nadharia tatu zinazoaminika au kuhusishwa na ujenzi wake. Kwanza ni kuwa "mwongozo baada ya maangamizi." Wengi wanaamini ulikuwa umeandaliwa kwa ajili ya manusura wa tukio kubwa, janga la kimataifa au vita vya nyuklia.


Wako pia wanaoamini kwamba mnara huo ulikuwa sehemu ya ajenda ya "New World Order" mfumo mpya unaoundwa ili kuiongoza dunia chini ya mamlaka moja. Hata hivyo asilimia kubwa ya watu waliamini ni "mradi wa kifalsafa na kibinadamu" unaohamasisha maadili ya kimataifa.


Pamoja na kazi kubwa ya ubunifu katika ujenzi wa mnara huo ujumbe wake haukuwafurahisha watu wengi. Baadhi waliuona ni ujumbe wa makufuru na au ishara za mpinga Kristo. Mnamo tarege 6 Julai 2022, sehemu ya mnara huo ililipuliwa kwa bomu. Baadaye, mabaki yaliyosalia yalibomolewa kabisa kwa sababu za kiusalama. Tukio hili lilifanyika karibu na eneo la Georgia na lilizua mjadala mpya duniani. Maelfu walijiuliza kama huo ulikuwa ni uharibifu wa kihistoria au kuondolewa kwa “ishara hatari”?


Mojawapo ya mambo yaliyofanya mjadala wa mnara huu kuwa wa kina zaidi ni kuhusishwa kwa Afrika hususan lugha ya Kiswahili. Uwepo wake unaonyesha Afrika Mashariki ilitambuliwa kama sehemu muhimu ya dunia ya baadaye. Wengine wanaamini bara hili lina nafasi kubwa katika mipango ya kimataifa kutokana na utajiri wake wa maliasili.


Pamoja na hilo, Afrika ina kasi kubwa ya ongezeko la idadi ya watu hivyo mijadala ya “population control” mara nyingi huigusa moja kwa moja. Hata hivyo, hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaoonyesha Afrika ilihusika katika kuanzishwa kwa mradi huu.



Licha ya nadharia nyingi, ukweli unabaki kuwa mnara huu ulikuwa kitandawili. Hakuna ushahidi rasmi wa ajenda ya siri ya kimataifa, utambulisho wa R. C. Christian umebaki kuwa siri, na mbaya zaidi ni kuwa maandishi yake yanaweza kutafsiriwa kwa mitazamo tofauti aidha ya matumaini au ya hofu kutegemea imani, wahusika, na mazingira.


Ukweli unabaki kwamba Georgia Guidestones haukuwa mnara wa mawe yaliyochongwa ki sanaa tu. ulikuwa kioo cha hofu, matumaini, na fikra za binadamu kuhusu mustakabali wa dunia. Kwa sasa swali kuu linabaki kuwa "Je, hili lilikuwa onyo la hekima kwa kizazi kijacho au jaribio la wachache kuandika sheria za dunia nzima?


Uwe na amani

 
 
 

Comments


bottom of page