Tanzania Kwenye Mizani ya Jumuia ya Madola na Aibu ya Kidiplomasia
- Rev. Godwin Chilewa
- 3 hours ago
- 3 min read
Rev. Godwin Chilewa

Tamko la Commonwealth Ministerial Action Group (CMAG) la tarehe 10 Julai 2026 ni waraka mzito wenye lugha ya tahadhari, ishara za adhabu zinazotunyemelea, na ujumbe wa wazi kwamba Tanzania imeanza kupoteza uaminifu katika misingi ya utawala bora, haki za binadamu, na demokrasia, misingi ambayo ni uti wa mgongo wa Jumuiya ya Madola.
Baada ya matukio ya umwagaji damu tarehe 29 Oktoba 2025, tamko hili halipaswi kusomwa kama maneno ya kawaida ya “diplomasia laini”, bali kama onyo la hatua za kimfumo dhidi ya taifa ambalo linaonekana kuacha njia ya maadili ya kimataifa.
Ukisoma kwa juu juu, tamko hili linaonekana kama la kirafiki: linapongeza ushirikiano wa serikali ya Tanzania na mapokezi ya mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola. Lakini ndani yake kuna ujumbe mzito uliofichwa kwa ustadi:
Kwanza linaeleza “Concern that the situation has deteriorated.” Hii ni lugha ya kidiplomasia inayomaanisha hali imezidi kuwa mbaya, si bora. Pili tamko linasema nchi ina “Restrictions on political activities” kwa maana serikali imeanza kudhibiti siasa kwa nguvu.
Tatu, tamko linaeleza “Atmosphere of fear among the opposition” Uwepo wa mazingira ya hofu, ambayo kimsingi ni ishara ya ukandamizaji wa kisiasa. Hizi si kauli nyepesi. Katika diplomasia, maneno haya hutumika pale ambapo hatua kali zinaanza kufikiriwa.
Maelezo haya yanaonesha kuwa uamuzi wa CMAG “kuibakiza Tanzania kwenye ajenda rasmi” ni hatua kubwa sana kisiasa.
Hii ina maana gani? Tanzania sasa iko kwenye orodha ya nchi zinazofuatiliwa kwa karibu. Hii ni hatua ya awali kabla ya vikwazo vya kidiplomasia, kusimamishwa uanachama na au shinikizo la kimataifa la kufanya mageuzi.
Kwa historia ya Jumuiya ya Madola, nchi zinazofika hatua hii huwa zimeanza safari ya kuelekea kwenye adhabu isipokuwa kama zinakubali kubadili mwelekeo haraka.
Zingatia kwamba tamko linatambua kuwa serikali iliruhusu uchunguzi na kutoa ushirikiano. Hili ni jambo chanya.
Lakini tatizo ni kwamba ushirikiano haujageuka kuwa mabadiliko ya kweli.
CMAG inaeleza wazi kwamba katika masharti manne yaliyotolewa awali moja limetekelezwa, moja limetekelezwa nusu, na mawili hayajaguswa kabisa. Hii ina maana kuwa serikali imechagua kuchelewesha mageuzi muhimu. Katika macho ya jumuiya ya kimataifa, hii hutafsiriwa kama ukosefu wa nia ya dhati.
Tamko hili pia linagusia “detention and legal proceedings of the principal opposition leader”.
Hii ni pointi nyeti sana. Kimsingi Jumuia ya Madola inaona upinzani ni sehemu ya demokrasia, na kukamatwa kwa kiongozi wa chama cha upinzani kumefanywa kisiasa si kisheria. Hapa Tanzania imeingia kwenye eneo hatari kwani picha inayoonekana ni kuwa taifa linalotumia vyombo vya dola kukandamiza wapinzani.
Kwa ujumla tamko la Jumuia ya Madola limeivua nguo Tanzania. Hata hivyo baadhi ya wanasiasa na hasa machawa wanaweza kupuuzia tamko hili, na au kumdanganya kiongozi wa nchi kwamba “hali ni shwari” na kuwa “Jumuia hiyo haipaswi kuingilia mambo yetu ya ndani” kitu ambacho si kweli.
Tamko hili lina madhara makubwa na linaongeza hatari ya hadhi ya nchi kimataifa kuporomoka. Tanzania iliyowahi kuheshimika kama taifa la amani sasa inaonekana nchi yenye migogoro ya kisiasa na inayoshukiwa kukiuka haki za binadamu. Hii inaweza kusababisha uwekezaji kupungua jambo litakaloporomosha uchumi wa nchi.
Si hivyo tu, bali pia Tanzania inaweza kukabiliwa na ugumu wa kupata misaada, misaada yenye masharti na shinikizo kutoka nchi wanachama. Tanzania inaweza kujikuta ikifuatiliwa kwa karibu na taasisi au mashirika ya haki za binadamu. Ikiwa hali ya kisiasa iliyopo sasa nchini itaachwa iendelee, si ajabu Tanzania ikasimamishwa uanachama kama historia inavyotuonesha yaliyotokea Zimbabwe.
Kwa ujumla tamko lote linaweza kufupishwa kwa sentensi moja: “Tunawapa nafasi ya kujirekebisha haraka kabla CMAG haijachukua hatua kali ingawa tayari imeweka msingi wa kuzichukua.
Kumbe Tanzania bado ina nafasi ya kurekebisha mwelekeo wake. Lakini ishara zote zinaonyesha kuwa muda unazidi kututupa mkono. Ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa, taifa linaweza kujikuta likitengwa kimataifa si kwa sababu ya chuki au wivu wa mabeberu, bali kwa sababu ya maamuzi yake yenyewe.
Uwe na amani






Comments